Nigeria
| |||||
Kaulimbiu ya taifa: Unity and Faith, Peace and Progress (Umoja na Imani, Amani na Maendeleo) | |||||
Wimbo wa taifa: Arise O Compatriots, Nigeria's Call Obey (Amkeni wananchi, mtieni wito la Nigeria) | |||||
Mji mkuu | Abuja | ||||
Mji mkubwa nchini | Lagos | ||||
Lugha rasmi | Kiingereza | ||||
Serikali Rais
Makamu wa Rais |
Shirikisho la Jamhuri Muhammadu Buhari Yemi Osinbajo | ||||
Uhuru kutoka Uingereza |
1 Oktoba 1960 | ||||
Eneo - Jumla - Maji (%) |
923,768 km² (ya 32) 1.4% | ||||
Idadi ya watu - 2015 kadirio - 2006 sensa - Msongamano wa watu |
182,202,000 (ya 7) 140,431,790 188.9/km² (ya 71) | ||||
Fedha | Naira (₦) (NGN )
| ||||
Saa za eneo - Kiangazi (DST) |
(UTC+1) (UTC+2) | ||||
Intaneti TLD | .ng | ||||
Kodi ya simu | +234
- |
Nigeria (kwa Kiswahili pia: Nijeria au Naijeria) ni nchi ya Afrika ya Magharibi kwenye pwani ya Bahari Atlantiki.
Imepakana na Benin, Niger, Chad na Kamerun.
Mji mkuu ni Abuja ikitanguliwa na Lagos hadi mwaka 1991.
Nigeria imepata uhuru wake tarehe 1 Oktoba 1960, ikiunganisha maeneo ya koloni la Nigeria na sehemu ya kaskazini ya eneo lindwa la Kamerun ya Kiingereza.
Kwa sasa ni nchi ya Afrika yenye watu wengi na uchumi mkubwa kuliko zote. Kimataifa, ni ya 7 kwa idadi ya watu na ya 20 kwa uchumi.
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]Nigeria inaunganisha maeneo tofauti sana ikiwa na msitu wa mvua upande wa kusini kupitia nchi ya savana hadi kanda ya Sahel na mwanzo wa jangwa la Sahara kaskazini kabisa.
Mlima wa juu ni Chappal Waddi yenye m 2,419 juu ya UB.
Hali ya hewa ni ya kitropiki. Kusini kuna mvua mwaka wote lakini kaskazini mwa nchi kuna ukame kati ya Novemba na Aprili.
Mito mikubwa ni mto Niger na mto Benue; yote miwili inakutana na kuishia katika delta ya Niger ambayo ni kati ya delta kubwa zaidi duniani.
Mji mkubwa zaidi ni Lagos (mji mkuu wa zamani) ukiwa na wakazi 15,000,000. Kati ya miji mingine kuna Abuja, Kano, Ibadan, Oshogbo, Ilorin, Abeokuta, Ogbomosho na Port Harcourt.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Historia ya kale (hadi waka 1500)
[hariri | hariri chanzo]Tangu mnamo 500 KK kulikuwa na Utamaduni wa Nok kaskazini mwa Nigeria. Unajulikana tu kutokana na sanamu kubwa za watu zilizotengenezwa kwa terakota (udongo wa kuchomwa) ambazo zilitengenezwa kati ya 500 KK na 200 BK kufuatana na vipimo vya rediokaboni. [1][2][3][4]
Kumbukumbu ya mji wa Kano inaanza katika mwaka 999 BK.
Katika kusini milki ya Nri kati ya Waigbo ilianza kabla ya karne ya 10 BK ikaendelea hadi kumezwa na koloni la Uingereza mwaka 1911.[5][6] Nri ilitawaliwa na mfalme (Eze Nri) na mji wa Nri huangaliwa kama chanzo cha utamaduni wa Waigbo.[7]
Tangu karne ya 12 kuna habari za falme za Ife na Oyo katika kusini magharibi zilizoundwa na Wayoruba. [8][9] and 14th[10] Ife ilianza kukaliwa na watu tangu karne ya 9 na utamaduni wake ulitengeneza sanamu mashuhuri za terakota na bronzi. [8].
Karne za kati
[hariri | hariri chanzo]Mnamo mwaka 1500 kulikuwa na falme kubwa katika eneo la Nigeria ya leo. Katika kusini ni milki ya Benin (tofauti na nchi ya leo) na Onitsa ya Waigbo, katika kaskazini falme za Wahausa na Songhai ambazo zilitawaliwa na wafalme au masultani Waislamu. Falme za kaskazini zilishiriki katika biashara ya ng'ambo ya Sahara ambako hasa chumvi, dhahabu na watumwa walipelekwa kwa njia ya misafara hadi nchi za Waislamu karibu na Bahari Mediteranea. [11], [12]
Wakati huohuo wapelelezi Wareno na Wahispania walianza kufika kwenye pwani za Afrika ya Magharibi na pia katika delta ya Niger. Walianza kujenga vituo vya biashara kwa vibali vya watawala wa sehemu za pwani kama huko Lagos na Calabar. Wazungu walifanya biashara ya bidhaa mbalimbali na watu wa pwani na hii ilikuwa pia chanzo cha biashara ya watumwa ya kuvukia Atlantiki. [13] Bandari ya Calabar kwenye Hori ya Biafra (leo hii inajulikana zaidi kwa jina la "Bight of Bonny") iliendelea kuwa moja kati ya vituo vya biashara ya watumwa vikubwa zaidi kwenye pwani ya Afrika ya Magharibi. Vituo vingine vya biashara ya watumwa kwenye pwani ya Nigeria vilikuwa Lagos na Badagry, [13][14] Wangi waliouzwa hapo walifukuwa wafungwa wa vita vya watawala wenyeji kati yao au walikamatwa katika kampeni zilizoendeshwa kwa shabaha za kupata watumwa wa kuuzwa. [15]
Watendaji wakuu walioleta watumwa pwani walitoka katika milki ya Oyo kwenye kusini magharibi na Ukhalifa wa Sokoto katika kaskazini. [13][14]
Utumwa katika maeneo ya Nigeria ya leo haukuanzishwa na watu kutoka Ulaya, ulikuwepo tayari pia biashara ya watumwa.[16] Lakini soko jipya kwenye pwani lililoanzishwa na Wazungu lilibadilisha uwiano katika jamii nyingi za Kiafrika na pia uhusiano kati ya jamii za Kiafrika. Watawala karibu na pwani waliweza kupata faida kwa kuuza watumwa moja kwa moja kwa Wazungu na waliweza kununua silaha za moto; wenye silaha za moto waliweza kushinda vita, kupata wafungwa wengi na kuuza wafungwa wengi zaidi. Hivyo mahitaji makubwa ya soko la watumwa la Atlantiki yalilisha ufuatano wa vita na mashindano ya kukamata wafungwa zaidi.[17]
Idadi ya watumwa ndani ya Nigeria ilizidi kukua katika karne ya 19 ambako biashara ya watumwa kwenye Atlantiki ilikwisha. Manmo 1890 mkusanyiko mkubwa wa watumwa katika Afrika walikuwa watumwa katika milki ya Khalifa wa Sokoto, takriban watu milioni 2. [18]
Karne ya 19 na ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Tangu mnamo 1860 Uingereza ilianza kupanua athira yake katika Nigeria. Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza kuwa na viwanda vingi; viwanda vyake vilihitaji mafuta kwa matumizi ya grisi kwa kulainisha mwendo wa mashine. Delta ya mto Niger ilikuwa na idadi kubwa ya michikichi inayozalisha mafuta.[19] Hapo shirika kama Royal Niger Company zilipata maeneo makubwa chini ya mamlaka yao kwa njia ya mapatano na mikataba na watawala wenyeji, malipo na matishio na maeneo haya yaliwekwa baadaye chini ya serikali ya Uingereza.
Kwenye mkutano wa Berlin madai ya Uingereza juu ya pwani ya Nigeria yalikubaliwa na mataifa mengine ya Ulaya. Baadaye Waingereza waliendelea haraka kuhakikisha mamlaka yao juu ya maeneo ya kaskazini ama kwa mapatano au kwa vita kwa kusudi la kuzuia upanuzi wa Ufaransa.
Hivyo zilitokea maeneo ya "Southern Nigeria Protectorate" na "Northern Nigeria Protectorate". Hali halisi sehemu hizi haziwahi kuwa na umoja katika historia lakini hatimaye Uingereza iliamua kutawala maeneo yote kama koloni moja.
Baada ya uhuru
[hariri | hariri chanzo]Nigeria ilipata uhuru wake tarehe 1 Oktoba 1960 kutoka kwa Uingereza ikiunganisha maeneo ya koloni la Nigeria na sehemu ya kaskazini ya eneo lindwa la Kamerun ya Kiingereza.
Kati ya miaka 1967-1970 nchi iliona vita ya wenyewe kwa wenyewe; magharibi ya nchi, inayokaliwa na Waigbo hasa, ilijaribu kujitenga kwa jina la Biafra, ikipinga utawala wa wanajeshi Waislamu. Takriban watu milioni 2 walikufa kwa njaa wakati ule.
Nigeria iliendelea kuvurugika na mapinduzi ya kijeshi.
Tangu miaka ya 1970 Nigeria ilikuwa na mapato makubwa kutokana na mafuta yaliyotolewa kutoka ardhi yake, hasa katika delta ya mto Niger.
Ulaji rushwa na ufisadi wa watawala wa kijeshi ulizuia maendeleo ya nchi jinsi ilivyoonekana katika nchi nyingine yenye mafuta.
Tangu mwaka 1999 nchi imerudi kwenye utawala wa kisheria ikapata katiba mpya na kumchagua rais Olusegun Obasanjo aliyerudishwa madarakani mara moja.
Majaribio ya wafuasi wake wa kubadilisha katiba na kumpa kipindi cha tatu yalishindikana bungeni.
Katika uchaguzi wa mwaka 2007 Umaru Yar’Adua alishinda kwa asilimia 70 za kura.
Baada ya kungonjeka kwake, makamu wa rais Goodluck Jonathan alichukua madaraka ya urais kuanzia mwaka 2010 akachaguliwa kuwa rais kwenye kura ya mwaka 2011.
Mwaka 2015 alishindwa katika uchaguzi mkuu na mgombea mwenzake, Muhammadu Buhari.
Ni kwamba tangu mwaka 2009 hadi Septemba 2015 uasi wa kundi la Boko Haram ulivuruga amani na usalama nchini Nigeria. Wanamgambo wa kundi hilo wanaotazamwa na Wanigeria wengi kuwa magaidi walianza kutwaa mamlaka juu ya sehemu za nchi hasa katika mazingira ya jimbo la Borno, kuua wananchi wengi, kuchukua watu mateka na kupigana na jeshi la Nigeria na ya nchi jirani.
Kutofaulu kwa jeshi la taifa kumaliza ghasia hizo ndiyo sababu muhimu ya kushindwa kwa rais Jonathan kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. Kufuata na ahadi zake kwa wapiga kura, Muhammadu Buhari alijitahidi kukomesha kundi hilo.
Jeshi
[hariri | hariri chanzo]Jeshi la Nigeria lina jukumu la kulinda Jamhuri ya Shirikisho ya Nigeria, kukuza maslahi ya usalama wa kimataifa ya Nigeria, na kuunga mkono juhudi za kulinda amani hasa katika Afrika Magharibi.
Jeshi la Nigeria linaundwa na Jeshi la Ardhi, ni Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Anga. Jeshi nchini Nigeria limecheza jukumu kubwa katika historia ya nchi tangu uhuru. Junta mbalimbali zilikamata udhibiti wa nchi na zilitawala kupitia wengi wa historia yake.
Kipindi cha mwisho cha utawala wake kilimalizika mwaka 1999 kufuatia kifo cha ghafla cha dikteta wa zamani Sani Abacha mwaka 1998, na mrithi wake, Abdulsalam Abubakar, kumpa mamlaka ya serikali Olusegun Obasanjo aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka wa 1999.
Ikichukua faida ya jukumu lake kama nchi yenye wakazi wengi wa Afrika, Nigeria imeweka jeshi lake kama kikosi cha kulinda amani Afrika. Tangu mwaka 1995, jeshi la Nigeria, kupitia mamlaka ya ECOMOG, limetumwa kulinda amani katika Liberia (1997), Ivory Coast (1997-1999), Sierra Leone 1997-1999, na kwa sasa katika mkoa wa Darfur huko Sudan chini ya Umoja wa Afrika.
Majimbo ya shirikisho
[hariri | hariri chanzo]Muundo wa Nigeria ni Jamhuri ya Shirikisho. Katiba ya nchi imefuata mfano wa katiba ya Marekani.
Rais huchaguliwa na wananchi wote: ndiye mkuu wa serikali. Anawajibika mbele ya bunge lenye vitengo viwili: Senati na Baraza la Wawakilishi.
Wakazi
[hariri | hariri chanzo]Nigeria hukadiriwa kuwa na wakazi takriban milioni 180. Inasemekana nusu ya wakazi wote wana umri wa chini ya miaka 14. Hata hivyo ni vigumu kupata namba halisi kwa sababu ya umuhimu wake katika siasa.
Vikundi vikubwa katika jumla la makabila 300 ni Wahausa na Wafula kaskazini (jumla 20-30%), Waigbo (Waibo) kusini (14-18%), Wayoruba katika sehemu za magharibi (20-27%).
Katika miji mikubwa watu kukaa kwa mchanganyiko wa makabila.
Nigeria iliona mara kadhaa vurugu na mapambano kati ya makabila yaliyoongezewa ukali kwa sababu mara nyingi ukabila unaendelea sambamba na udini. Watu wa Kaskazini ni Waislamu zaidi na watu wa kusini Wakristo zaidi.
Dini
[hariri | hariri chanzo]Kuthibitisha idadi ya wafuasi wa dini mbalimbali ni vigumu vilevile. Kwa ujumla kaskazini ya nchi ina historia ndefu ya Uislamu na wakazi ni Waislamu, hasa Wahausa. Kusini kuna Wakristo wengi, Waigbo ni zaidi Wakatoliki na Wayoruba zaidi Waprotestanti.
Wengi wanasema ya kwamba idadi za Wakristo na za Waislamu zinalingana - wengine wanaona Waislamu ni wengi kidogo labda 50%, Wakristo 40% na wafuasi wa dini asilia za Kiafrika takriban 10%, lakini hawa wa mwisho kwa sasa wamepungua sana, labda wamebaki 1.4%.
Kati ya Waislamu, wengi ni Wasuni. Kati ya Wakristo, 74% ni Waprotestanti na 25% ni Wakatoliki.
Tangu mwaka 1999 suala la sharia au sheria za Kiislamu limeleta utata na mapambano katika majimbo kadhaa. Jimbo la Zamfara linalokaliwa hasa na Wahausa ambao ni Waislamu liliamua kuwa na sharia kama sheria ya kijimbo mwaka 1999 na majimbo mengine yalifuata. Kwa sasa ni Kano, Katsina, Niger, Bauchi, Borno, Kaduna, Gombe, Sokoto, Jigawa, Yobe na Kebbi. Kanuni za sharia hazitumiwi kwa namna moja kati ya majimbo haya; mapambano yalitokea juu ya jinsi gani sharia inaathiri raia wasio Waislamu.
Lugha rasmi ya nchi ni Kiingereza, ingawa wakazi wengi wanatumia zaidi lugha za makabila yao, ambayo ni zaidi ya 500. Muhimu zaidi ni Kihausa, Kiigbo na Kiyoruba.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Orodha ya nchi kufuatana na wakazi
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na idadi ya watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na msongamano wa watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na pato la taifa
- Demografia ya Afrika
- Orodha ya lugha za Nigeria
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Nicole Rupp, Peter Breunig & Stefanie Kahlheber, "Exploring the Nok Enigma", Antiquity 82.316, June 2008.
- ↑ B. E. B. Fagg, "The Nok Culture in Prehistory", Journal of the Historical Society of Nigeria 1.4, December 1959.
- ↑ Kleiner, Fred S.; Christin J. Mamiya (2009). Gardner's Art Through the Ages: Non-Western Perspectives (tol. la 13, revised). Cengage Learning. uk. 194. ISBN 0-495-57367-1.
- ↑ "Nok Terracottas (500 B.C.–200 A.D.) | Thematic Essay | Heilbrunn Timeline of Art History | The Metropolitan Museum of Art". Metmuseum.org. 2014-06-02. Iliwekwa mnamo 2014-07-16.
- ↑ Juang, Richard M. (2008). Africa and the Americas: culture, politics, and history : a multidisciplinary encyclopedia, Volume 2. ABC-CLIO. uk. 597. ISBN 1-85109-441-5.
- ↑ Hrbek, Ivan (1992). Africa from the seventh to the eleventh Century. James Currey Publishers. uk. 254. ISBN 0-85255-093-6.
- ↑ Uzukwu, E. Elochukwu (1997). Worship as Body Language. Liturgical Press. uk. 93. ISBN 0-8146-6151-3.
- ↑ 8.0 8.1 Falola, Toyin; Heaton, Matthew M. (2008). A history of Nigeria. Cambridge University Press. uk. 23. ISBN 0-521-68157-X.
- ↑ Laitin, David D. (1986). Hegemony and culture: politics and religious change among the Yoruba. University of Chicago Press. uk. 111. ISBN 0-226-46790-2.
- ↑ MacDonald, Fiona; Paren, Elizabeth; Shillington, Kevin; Stacey, Gillian; Steele, Philip (2000). Peoples of Africa, Volume 1. Marshall Cavendish. uk. 385. ISBN 0-7614-7158-8.
- ↑ Ralph A. Austen, Trans-Saharan Africa in World History, Oxford University Press, 2010 , uk. 26 (imeangaliwa kupitia google books, tar. 3-12-2016
- ↑ Ghislaine Lydon, On Trans-Saharan Trails: Islamic Law, Trade Networks, and Cross-Cultural Exchange in Nineteenth-Century Western Africa uk. 85f; Cambridge University Press, 2009 ; imeangaliwa kupitia google books 3-12-2016
- ↑ 13.0 13.1 13.2 Gordon, April A. (2003). Nigeria's Diverse Peoples: A Reference Sourcebook. ABC-CLIO. ku. 44–54. ISBN 1576076822. Iliwekwa mnamo 2015-03-29.
- ↑ 14.0 14.1 Falola, Toyin; Genova, Ann (2009). Historical Dictionary of Nigeria. Scarecrow Press. uk. 328. ISBN 0810863162. Iliwekwa mnamo 2015-03-29.
- ↑ Falola, Toyin; Paddock, Adam (2012). Environment and Economics in Nigeria. Routledge. uk. 78. ISBN 1136662472. Iliwekwa mnamo 2015-03-29.
- ↑ "Slavery – Historical survey – Slave societies". Encyclopædia Britannica's Guide to Black History. Encyclopædia Britannica. 2011. Iliwekwa mnamo 28 Mei 2011.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Nigeria's Diverse Peoples: A Reference Sourcebook von April A. Gordon, uk. 49
- ↑ "It is estimated that by the 1890s the largest slave population of the world, about 2 million people, was concentrated in the territories of the Sokoto Caliphate. The use of slave labor was extensive, especially in agriculture."Kevin Shillington (2005). Encyclopedia of African History. Michigan University Press. p. 1401. ISBN 1-57958-455-1
- ↑ S.O. Aghalino, British colonial policies and the oil palm industry in the Niger delta region of Nigeria Archived 16 Januari 2013 at the Wayback Machine., African Study Monographs, 21(1): 19-33, January 2000, tovuti ya Chuo Kikuu cha Kyoto, iliangaliwa 3-12-2016
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Official website
- Wikimedia Atlas of Nigeria
- media kuhusu Banknotes of Nigeria pa Wikimedia Commons
- Nigeria entry at The World Factbook
Abia | Abuja Federal Capital Territory | Adamawa | Akwa Ibom | Anambra | Bauchi | Bayelsa | Benue | Borno | Cross River | Delta | Ebonyi | Edo | Ekiti | Enugu | Gombe | Imo | Jigawa | Kaduna | Kano | Katsina | Kebbi | Kogi | Kwara | Lagos | Nasarawa | Niger | Ogun | Ondo | Osun | Oyo | Plateau | Rivers | Sokoto | Taraba | Yobe | Zamfara |
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira |
Makala hii kuhusu maeneo ya Nigeria bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Nigeria kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |