Demokrasia
Demokrasia (kutoka neno la Kigiriki δημοκρατία, dēmokratía, maana yake utawala wa watu: δῆμος, dêmos, maana yake "watu" na κράτος, krátos, maana yake "utawala") ni aina ya serikali.
Neno hilo lilitumika kuanzia karne ya 5 KK kuelezea mtindo wa utawala uliotumika katika Athene na miji mingine kadhaa ya Ugiriki, kinyume cha ἀριστοκρατία, aristokratía, "utawala wa masharifu".
Kwenye demokrasia watu fulani wa jamii wanamchagua kiongozi wao.
Kuna njia nyingi za kufanya hivi, lakini mchakato kamili kwa kawaida huitwa kushikilia uchaguzi.
Vyama vya siasa huhusika na masuala ya siasa. Yaonekana kwamba yaweza kuwa rahisi kuwa na chama cha kisiasa. Chama kitakachoshinda uchaguzi kitamchagua kiongozi kinayemtaka.
Demokrasia ni nini?
[hariri | hariri chanzo]Demokrasia ni mfumo wa serikali ambapo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya umma. Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile sheria na katika chaguzi. Wakati mwingine huwakilishwa na viongozi wao waliowachagua.
Ni utawala wa watu, na watawala hutawala kwa ridhaa ya watu.
Kwa hiyo kwa kifupi Demokrasia ni mfumo unatoa fursa ya madaraka kwa umma moja kwa moja au kutokana na uwakilishi.
Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani, alisema Demokrasia ni serikali ya watu/mfumo wa utawala wa watu, kwa ajili ya watu na unaotokana na watu. Watu wanaunda serikali.
Aina za demokrasia
[hariri | hariri chanzo]- Demokrasia ya moja kwa moja (kwa Kiingereza "Direct Democracy") ni aina ya demokrasia ambayo wananchi wote wanaweza kushiriki katika kuamua masuala ya kisiasa, ya kijamii, ya kisheria na ya kiuchumi bila kutumia chombo cha uwakilishi kama vile bunge. Uwezo huu wa wananchi kutoa maamuzi unaweza kuwapa hata uwezo wa kimahakama, ingawa mara nyingi wananchi hupewa uwezo wa kutunga au kupitisha sheria tu. Demokrasia ya moja kwa moja ni tofauti na demokrasia inayofuatwa katika nchi nyingi duniani hivi sasa, ambapo wananchi huchagua wawakilishi wao katika uchaguzi. Nchi ya Uswisi ni maarufu kwa mfumo wake wa demokrasia ya moja kwa moja ambako sheria nyingi zinaamuliwa na wananchi wote kwa njia ya kura.
- Demokrasia shirikishi ("Representative Democracy"): hapo wachache hupewa na wengi dhamana katika uwakilishi wa jamii katika maamuzi. Wachache huchaguliwa na wengi kwa njia ya demokrasia huru na ya haki kwa kufuata Katiba ya nchi hiyo. Mfano: Wabunge huwakilisha wananchi wao katika kuleta maendeleo na kuishauri serikali juu ya maendeleo ya nchi yao.
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |