Agostino wa Hippo

(Elekezwa kutoka Augustino)

Agostino wa Hippo (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Picha ya kale zaidi (karne ya 6) ya Agostino katika kanisa la Laterani, Roma (Italia).
Agostino wa Hippo akibatizwa na Ambrosi, mwaka 387.

Ndiye aliyekuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5.

Baada ya ujana uliovurugika kinadharia na kimaadili, aliongokea imani Katoliki, akabatizwa na Ambrosi huko Milano, Italia. Kisha kurudi Afrika Kaskazini, alishi kitawa na marafiki kadhaa, akimtumikia Mungu na kusoma Maandiko Matakatifu. Askofu kwa miaka 34, akilisha kundi lake kwa hotuba na maandishi mengi ambamo alifafanua kwa hekima imani sahihi na kupinga kwa nguvu aina mbalimbali za uzushi za wakati ule[1].

Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake bora, tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe aliyoaga dunia[2].

Maisha yake

hariri

Katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini wenyeji walikuwa Waberberi kama mama yake, lakini watu wa mjini, kama baba yake, na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Ulaya wakitumia hasa lugha ya Kilatini. Kwa jumla sehemu hii ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi.

Mama yake (Monika, anayeheshimiwa kama mtakatifu) alikuwa Mkristo, kumbe baba (Patrisi) alifuata dini ya jadi ya kuabudu miungu mingi kabla hajabatizwa mwishoni mwa maisha yake.

Agostino alizaliwa tarehe 13 Novemba 354 mjini Thagaste katika mkoa wa Numidia. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Aurelius Augustinus. Wakati ule Ukristo ulikuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma; dhuluma dhidi ya Wakristo zilikuwa zimekwisha rasmi mwaka 313 kwa Hati ya Milano iliyotolewa na Konstantino Mkuu ili kuruhusu uhuru wa dini.

Alikuwa na wadogo wawili, mmoja mwanamume, Naviji, na mwingine wa kike, ambaye hatujui jina lake, ila kwamba baada ya kufiwa mume wake akawa mmonaki na abesi.

Monika alimuathiri sana Augustino na kumlea katika imani ya Kikristo. Mwanae aliweza kuandika kwamba alipokuwa ananyonya maziwa ya mama, alifyonza pia upendo kwa jina la Yesu. Akiwa mtoto alipokea chumvi kama ishara ya kuingia ukatekumeni akabaki daima anavutiwa na Yesu, hata alipozidi kusogea mbali na Kanisa lake.

Wakati wote wa ujana wake alifuata anasa na uzushi, bila kujali machozi ya mama yake.

Alipata elimu yake nzuri ya lugha na ya ufasaha wa kuhubiri huko Thagaste, Madaura na hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis) ingawa hakuwa daima mwanafunzi mzuri, mbali ya kuwa na akili ya pekee. Alimudu kikamilifu Kilatini, lakini si sana Kigiriki.

Akiwa huko Karthago, mwaka 373 alisoma kitabu cha maadili cha Sisero ambacho kilibadilisha hisia zake hivi kwamba “matumaini yote ya bure yakawa hayana maana kwangu, nikatamani hekima isiyokufa kwa ari isiyosemeka moyoni mwangu”.

Lakini kwa kuamini ukweli haupatikani pasipo Yesu, ambaye hatajwi katika kitabu hicho, alianza kusoma Biblia, ila hakupenda tafsiri ya Kilatini wala yaliyomo, akiyaona tofauti na mtindo wa falsafa inayotafuta ukweli. Hivyo alisogea mbali na dini iliyoonekana kutotia maanani hoja za akili ambayo pamoja na imani ndizo “nguvu mbili zinazotuongoza kwenye ujuzi”. Ndivyo alivyoandika baadaye, akitoa pia kauli mbili za msingi kuhusu kulenga ukweli: “Usadiki ili uelewe”, halafu “uelewe ili usadiki”.

Hapo, kusudi asiishi bila Mungu, alijitafutia dini ya kuridhisha hamu yake ya kujua ukweli na ya kuwa karibu na Yesu, akajiunga kwa karibu miaka 10 na Umani. Dini hiyo ilidai kufuata akili na kufafanua sababu ya mabaya kuwepo duniani kutokana na chanzo cha pili cha ulimwengu kilicho kinyume cha Mungu, ikikataa Agano la Kale ili kufuata Ukristo wa kiroho.

Augustino alipenda pia maadili ya dini hiyo kwa sababu yalikuwa yanawadai sana baadhi ya waumini tu, yakiwaacha wengine wote wasijali zaidi. Hatimaye Wamani walikuwa wanasaidiana kupanda chati katika jamii. Lakini alipokutana na askofu wao Fausto, alikosa imani nao kwa kuona alivyoshindwa kujibu maswali yake.

Kazi baada ya masomo

hariri

Baada ya kuhitimu masomo, alifundisha Kilatini huko Thagaste (374), halafu namna ya kuhubiri huko Kartago (375-383), akaendelea kufanya hivyo nchini Italia, kwanza Roma (384), halafu Milano (384-386), makao makuu ya Dola, alipopata kazi ya heshima sana.

Wakati huo wote aliendelea kuishi bila ndoa na mwanamke aliyemzalia mtoto wa kiume mwenye akili sana, Adeodatus.

Akiwa Milano alikutana na watu, hasa Ambrosi askofu wa Milano, waliomvuta awe Mkristo Mkatoliki.

Mahubiri bora ya Ambrosi aliyokwenda kuyasikiliza kwanza ili kuzidi kupata mbinu za kutoa hotuba, yalizidi kumgusa moyoni na kumfanya asadiki mamlaka ya Biblia nzima inavyosomwa rasmi na Kanisa. Aliona uzuri na udhati wa masimulizi ya Agano la Kale yakifafanuliwa kiroho kama mifano ya mambo ya Agano Jipya inayomuelekea Kristo, kiini cha yote. Katika barua za Mtume Paulo, Augustino alimtambua Kristo kama mwokozi, si mwalimu tu.

Hasa aliguswa na maneno ya Rom 13:13-14 aliyoyasoma kwa kufungua tu kitabu kisha kumsikia mtoto wa jirani akiimba kwa kukariri, “Chukua usome, chukua usome”. Alitambua ameambiwa mwenyewe na Mungu maneno hayo yakimdai aachane na matendo ya mwili akamvae Kristo.

Wongofu na ubatizo

hariri

Kisha kuongoka hivyo tarehe 15 Agosti 386, akiwa na umri wa miaka 32, aliacha kufundisha na hata kuishi na mama mtoto, akatawa kwa muda Cassiciaco karibu na ziwa la Como, akiwa na Monika, Adeodatus na marafiki wachache, akarudi Milano alipobatizwa na Ambrosi pamoja na mwanae na rafiki yake Alipio usiku wa Pasaka ya mwaka 387.

Mmonaki

hariri

Baada ya kubatizwa na kunuia akaishi kitawa Thagaste, alirudi Afrika; njiani, huko Ostia, bandari ya Roma, alifiwa mamaye. Ndoto yake ilikuwa kujitosa katika maisha ya sala na masomo pamoja na marafiki wake. Lakini hiyo ilidumu miaka mitatu tu.

Padri na askofu

hariri

Mwaka 391 bila kutarajia alipewa daraja ya upadri huko Hippo, alipoanzisha monasteri, akigawa muda wake kati ya sala, masomo na mahubiri, halafu mwaka 395 akachaguliwa kuwa askofu msaidizi wa mji huo na mwaka 397 akawa askofu wa jimbo hilo.

Ilimbidi akubali matakwa ya Mungu kwake, kwamba ajitoe kwa wengine na kuwashirikisha ujuzi wake ili kuishi kweli kwa ajili ya Kristo. “Kuhubiri mfululizo, kujadili, kusisitiza, kujenga, kuwa tayari kwa yeyote ni jukumu kubwa sana, ni mzigo mzito, ni juhudi ya ajabu”. Ilikuwa kama wongofu wake wa pili.

Hapo alitegemeza maskini na mayatima, alisimamia malezi ya wakleri, akiwadai waishi pamoja, akaeneza monasteri za kiume na za kike. Alifanya adhimisho la ekaristi kuwa kiini cha maisha ya jumuia zake.

Mahubiri yake mengi yanaonyesha alivyojua kujadiliana na umati akitumia maneno rahisi na ya kawaida na hata ucheshi katika kulinganisha Neno la Mungu na mazingira yao.

Kwa tabia yake karimu na pendevu, hisia zake, uvumilivu na utayari wa kusamehe alifanya hata maadui kadhaa kuwa marafiki.

Maisha yake ya Kiroho yaliyoongoza uandishi wa kanuni yake kwa watawa yamefuatwa na mashirika mengi ya kiume na ya kike hadi leo.

Kwa miaka 35 mpaka kifo chake, mbali na kutimiza majukumu yake mengi, aliendelea kueleza na kutetea imani sahihi ya Kikristo kwa mahubiri, maandishi na vitabu vingi sana (hata vya mitindo mipya) dhidi ya aina zote za uzushi za wakati ule: Wamani, Wadonati, Wapelaji na Waario. Hivyo tangu alipokuwa hai, hakuongoza Kanisa la Afrika Kaskazini tu, bali alitegemeza imani kila mahali.

Kwa njia hiyo amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo, hasa wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na katika Uprotestanti uliotokea katika Kanisa hilo. Kwa mfano Martin Luther alimtaja kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mtume Paulo). Augustino alijilisha tunu za Kikristo na kutokeza utajiri wake wa dhati, akibuni mawazo na mifumo ya kulisha vizazi vijavyo. Hata nakala za vitabu vyake ni nyingi sana, zikithibitisha vilivyopendwa na kuenea.

Hivyo aliathiri sana ustaarabu wa Magharibi unaozidi kuenea leo duniani kote. Mawazo yote yaliyomtangulia yanakutana katika maandishi yake na kuwa chemchemi ya mafundisho kwa nyakati zilizofuata.

Miaka ya mwisho

hariri

Tarehe 26 Septemba 426 alikusanya waamini ili kuwatambulisha padri Eraklio aliyemchagua kama mwandamizi wake naye aweze kutumia miaka yake ya mwisho katika kusoma kwa dhati zaidi Maandiko matakatifu. Watu walimkubalia kwa shangwe.

Miaka minne iliyofuata Augustino alifanya kazi kubwa kwa kumaliza vitabu mbalimbali na kuanza kuandika vingine. Kati ya vile vya wakati huo kuna “Retractationes” (yaani “Kupitia Upya” vile vilivyotangulia), ambamo tunaona unyofu wake kwa kuwa tayari kurekebisha baadhi ya mafundisho aliyowahi kuyatoa. Hivyo mpaka mwisho alionyesha alivyolenga ukweli kuliko yote.

Pia miaka hiyo alijadiliana na wazushi hadharani na kurudisha amani iliyohatarishwa na makabila ya kusini yakifaidika na matatizo kati ya Kaisari na jemadari wake Bonifasi.

Alimuandikia mpatanishi: “Ni utukufu mkubwa zaidi kuzuia vita vyenyewe kwa neno moja, kuliko kuangamiza watu kwa upanga, na vilevile kusababisha au kudumisha amani kwa amani kuliko kwa vita. Kwa sababu wanaopigana, ikiwa ni watu wema, bila shaka wanalenga amani, ila kupitia damu. Kumbe kazi yako ni kuzuia umwagaji damu”.

Hata hivyo, tumaini lilitoweka Bonifasi alipoalika kwa hasira washenzi wa Kijerumani walioitwa Wavandali kutoka Hispania wavamie Afrika.

Agostino aliaga dunia akiwa Hippo tarehe 28 Agosti 430, wakati Wavandali walipokaribia kuteka mji wake baada ya kuuzingira miezi mitatu, huku wakibomoa makanisa na nyumba za vijijini na kuua au kukimbiza wakazi, wakiwemo watawa. Baadhi waliteswa na kuchinjwa, wengine walibakwa au kufanywa watumwa.

Mbele ya maovu hayo yaliyokomesha ustaarabu wa Kirumi, Augustino alizidi kutafakari fumbo la Maongozi ya Mungu ili kujifariji na kuwatuliza wengine kama alivyofanya miaka 20 ya nyuma, Roma ilipotekwa kwa mara ya kwanza na Wagoti. Aliona ustaarabu huo ulikuwa umechakaa, kumbe Kristo tu hazeeki kamwe na ni wa kutegemewa.

Hapo awali, alidhani mtu akiongoka na kubatizwa atafikia kwa urahisi ukamilifu unaoelekezwa na Hotuba ya Mlimani. Miaka ya mwisho alikiri kwamba Yesu tu alitekeleza sawasawa hotuba yake hiyo. Waamini wanahitaji daima kuongoka na kutakaswa naye ili kufanywa wapya. “Nimeelewa kwamba mmoja tu ni mkamilifu kweli… Kumbe Kanisa lote - sisi sote, tukiwa pamoja na Mitume - tunapaswa kusali kila siku: ‘Utusamehe dhambi zetu kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea’”. Ndio wongofu wake wa tatu, uliomfanya amalizie maisha yake kwa unyenyekevu wa hali ya juu.

Katika ugonjwa wa mwisho aliomba Zaburi za toba ziandikwe kwa herufi kubwa na kubandikwa ukutani aweze kuzisoma kutoka kitandani huku akijiaminisha kwa Mungu kwa machozi mengi usiku na mchana.

Ili kujiandaa zaidi kufa, siku 10 za mwisho hakuruhusu mtu kumtembelea, ila waliomletea chakula na dawa.

 
Kaburi la Agostino katika basilika la San Pietro in Ciel d'Oro, Pavia (Italia).

Kazi na mafundisho yake

hariri

Katika historia yote Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.

Kati ya mababu wa Kanisa, ndiye aliyetuachia maandishi mengi zaidi, kuanzia yale maarufu sana yanayoitwa "Maungamo", kwa kuwa humo miaka 397-400 aliungama sifa za Mungu na ukosefu wake mwenyewe kwa kusimulia alivyoishi hadi miaka ya kwanza baada ya kuongoka.

Kila wakati ulifurahia zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika kujichunguza na kutoa siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.

Uzingatifu wake wa fumbo la nafsi yake ambamo fumbo la Mungu limefichama, ni mzuri ajabu kiasi cha kubaki hata leo kilele cha kujitafiti kiroho. Aliandika: “Usiende nje, rudi ndani mwako; ukweli unakaa katika utu wa ndani; na ukiona umbile lako ni geugeu, panda juu yako. Lakini kumbuka, unapopanda juu yako, unapanda juu ya roho inayofikiri. Basi, ufikie pale mwanga wa akili unapowaka”. Tena: “Naona ni lazima wanadamu warudishiwe tumaini la kupata ukweli”.

Posidi, mtu wa kwanza kuandika habari za maisha ya Augustino (kwa Kilatini, “Vita Augustini”), alisema “waamini wanamkuta daima hai” katika vitabu vyake. Kweli havionyeshi imepita miaka 1600 tangu viandikwe: humo anaonekana kama rafiki yetu wa wakati huu anayesema nasi kwa imani isiyozeeka.

Augustino mwenyewe aliviorodhesha 1,030, ambavyo si vyote.

Kazi yake kubwa haikuwa kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali na kutoa majibu yaliyo muhimu mpaka leo.

Akilinganisha imani na akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu (Ukweli mkuu na Upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wa Mungu). Huyo katika roho yake isiyokufa, bado ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu, ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.

Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya mapokeo na kuathiri Kanisa lote la Magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi). Kitabu muhimu zaidi kuhusu Utatu (kwa Kilatini kinaitwa “De Trinitate”) alikiandika miaka 399-420. Kilichukua muda mrefu kwa kuwa alisimamisha uandishi wake miaka minane “kwa sababu ni kigumu mno na nadhani wachache tu wanaweza kukielewa; basi kuna haraka zaidi ya kuwa na vitabu vingine tunavyotumaini vitafaidisha wengi”.

Hivyo alielekeza nguvu zake kutunga vitabu vya katekesi kwa wasio na elimu (hasa “De Catechizandis Rudibus”). Akijibu hoja za Wadonati, ambao walitaka Kanisa la Kiafrika na kuchukia mambo ya Kilatini, alikubali kurahisisha lugha hata kufanya makosa ya kisarufi kusudi wamuelewe zaidi akifafanua umoja wa Kanisa ulivyo muhimu kwa mahusiano na Mungu na kwa amani duniani.

Hasa hotuba zake, zilizoandikwa na wengine wakati alipokuwa anazitoa kwa watu akiongea nao kirahisi, zimechangia kueneza ujumbe wake. Tunazo bado karibu 600, lakini zilikuwa zaidi ya 3,000.

Pia alifafanua upya imani kuhusu umwilisho wa Mwana wa Mungu, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451): uwepo wa hali mbili (ya Kimungu na ya kibinadamu) katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”.

Dhambi na neema

hariri

Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao.

Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.

Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa.

Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho.

Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu.

Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki.

Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki.

Mji wa Mungu

hariri

Juu ya uhusiano kati ya serikali na kanisa Augustino katika miaka 413-426 aliandika kitabu "De Civitate Dei" (maana yake kwa Kilatini ni: Mji wa Mungu. Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala").

Alieleza kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au Kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa.

Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Agostino alifahamu taratibu za Waroma Wapagani waliotazama Makaisari wao kuwa miungu, na vilevile habari za demokrasia ya Kigiriki ya kale. Akafahamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwa moto na maadui katika siku zake jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babeli na Yerusalemu.

Pamoja na "mji" huo alisema upo "mji" wa pili ndio mji wa Mungu ambao ni mji wa upendo na undugu wenye neema yake.

Miji yote miwili iko pamoja ingawa zina taratibu tofauti. Mkristo ni raia wa miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu pande zote mbili. Lakini ajue kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Kumbe mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashiriki enzi ya Mungu.

Ndiyo sababu inafaa serikali isikie mawazo ya Kanisa, kwani ni kwa njia ya Kanisa kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu tu.

Ni kutokana na mafundisho hayo pia kwamba Kanisa la Magharibi lilijifunza umuhimu wa kuwa na msimamo imara mbele ya serikali mbalimbali kama ulivyojitokeza katika historia ndefu ya Kanisa, ingawa Agostino alijua jinsi Kaisari Theodosi alivyotubu kanisani baada ya askofu Ambrosi wa Milano kumtenga kwa sababu aliwatuza wanajeshi wa serikali yake walioua watu wengi ovyo walipotuliza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Watu wengi pamoja na Askofu walisikitikia tendo hilo. Baadaye Theodosi alipotaka kuingia katika ibada, Askofu huyo alimtangaza ametengwa kwa sababu ya kumwaga damu ya Wathesalonike, hivyo hawezi kushiriki meza ya Bwana. Kaisari akakubali kosa mbele ya umati. Hata baadaye viongozi wa Kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano wa Ambrosio na mafundisho ya Agostino.

Mafundisho hayo yaliathiri mawazo na fikra za Wakristo kwa karne nyingi za baadaye.

Tunaweza kuona aina mbili za matokeo ya urithi huo.

Kwa upande mmoja Kanisa lilijaribu kutawala jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za Kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na wale wa Kanisa. Hoja hiyo huitwa "Uklerikali" (clericalism).

Nguvu ya kisiasa ya Kanisa ilifikia kilele chake mwanzoni mwa karne ya 13 wakati wa Papa Inosenti III, halafu ilizidi kupungua hadi kupingwa kabisa na mapinduzi mbalimbali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789).

Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu tofauti na ya mtawala, na hata vita vya kidini.

Agostino aliingiza pia hoja ya "vita halali" katika Ukristo uliowahi kukataa ukatili na vita kama dhambi dhidi ya Mungu. Agostino alieleza kwamba wakati mwingine vita ni halali, na kama ni halali ni wajibu wa Mkristo pia. Maelezo hayo yalitumiwa baadaye na watawala na wanasiasa Wakristo kwa kutetea vita vya kila aina.

Lakini sehemu nyingine ya urithi huo imebaki: kazi ya Kanisa ya kuzitetea haki za binadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kuzigandamiza. Kwa mfano makanisa ndiyo yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika ya Kusini, hata dhidi ya serikali zilizoutetea. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka mzigo wa kupokea wageni maskini kutoka nchi jirani.

Mwishoni tusifiche sehemu ya urithi wa Agostino iliyokuwa ngumu zaidi mpaka leo. Katika mikoa ya Afrika Kaskazini walikuwepo Wakristo wengi waliojitenga na Kanisa kubwa na kuanzisha madhehebu ya Wadonato. Agostino alijadiliana nao miaka mingi akijaribu kuwavuta warudi tena.

Mwaka 411 B.K. serikali ya Kiroma ilitafuta shauri la Agostino katika suala la Wadonato kule Karthago na Numidia (Tunisia na Algeria). Serikali ilitaka kuwe na umoja wa kidini kati ya wananchi. Pia wapinzani wa utawala wa Roma huko Afrika Kaskazini walijiunga na Kanisa la Wadonato.

Basi Agostino aliona kwamba Wadonato wameshika mafundisho ya uongo, akaogopa wataongoza waumini wao jehanamu. Akaona Kanisa lisiache wafundishe uongo (alivyoelewa mwenyewe), akaona vema kutumia nguvu ya serikali walazimishwe kurudi katika Kanisa kubwa.

Mwenyewe hakukubali adhabu ya kifo kwa "wazushi" hao, lakini serikali ilichukua kibali chake cha kuingilia kati kama msingi wa kuwatesa vikali na kuwaua wengi. Wadonato walipoteswa hivi na serikali, Agostino akanyamaza, hakupinga.

Mateso hayo ya Wakristo Wadonato chini ya serikali ya Kikristo mbele ya macho ya Kanisa Katoliki yaliendelea muda mrefu yakawa mwanzo wa mwisho wa Ukristo Afrika Kaskazini. Miaka mia mbili baadaye wanajeshi wa Waarabu Waislamu wakaingia huko, wakakuta Ukristo uliodhoofishwa (pia kutokana na dhuluma za Wavandali Waario dhidi ya Wakatoliki). Baada ya muda mfupi wenyeji wengi sana wa sehemu hizo wakaacha Ukristo wakajiunga na Uislamu.

Tukiangalia hali ya Misri tunaona tofauti: huko Wakristo wakashika imani yao katika karne zote ingawa kwa matatizo makubwa chini ya serikali ya Kiislamu. Lakini katika sehemu ya Afrika Kaskazini-Magharibi nguvu za ndani za Ukristo zilivunjika wakati wa mateso hayo makali ya Wadonato (halafu ya Wakatoliki) kwa mikono ya Wakristo wenzao.

Tatizo halikuishia Afrika Kaskazini. Agostino katika kitabu chake kimojawapo alitetea siasa ya ugandamizaji wa wazushi bila kuruhusu wauawe. Katika karne zilizofuata maandiko hayo yaliongoza sera ya Kanisa la magharibi dhidi ya wazushi kote Ulaya.

Kanisa lilikubali wazo la kwamba wazushi wanapaswa kugandamizwa. Basi kwa karne nyingi Kanisa la magharibi likaendelea kuwagandamiza na kuwatesa Wakristo wasiokubali mafundisho yake au uongozi wake. Watu wakateswa, kuchomwa moto na kufungwa gerezani, yote hayo kwa idhini ya Kanisa.

Hata madhehebu ya Uprotestanti kama Walutheri, Waanglikana na Wareformati yalitenda hivihivi baada ya kuwa dini rasmi ya serikali katika maeneo yao. Walifuata mfano uliowekwa wakati wa mgongano kati ya Kanisa kubwa na Wadonato huko Afrika Kaskazini katika karne ya 5.

Bila shaka Agostino hakutegemea matokeo hayo lakini hata habari hizi za kuhuzunisha ni sehemu ya urithi wa mtu huyo ambaye kwa mengine tunamkumbuka kama mwalimu mkubwa wa Ukristo mzima.

Sala zake

hariri

Wewe Bwana ni mkuu na unastahili kabisa sifa. Uweza wake ni mkuu na hekima yako haina mipaka. Mtu anataka kukusifu, yeye aliye sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, yeye anayetembea akielekea kifo, ushahidi wa dhambi yake, wa kwamba wewe unapinga wenye kiburi. Hata hivyo mtu, sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, anataka kukusifu. Wewe unamchochea aonje furaha ya kukusifu, kwa kuwa umetuumba kwa ajili yako, na moyo wetu hautulii mpaka ustarehe ndani mwako.

Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto!

Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia. Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako.

Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.

Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka.

Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako.

Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako.

Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako.

Maandishi yake makuu

hariri

Maandishi kuhusu maisha yake

hariri
  • Confessiones (Maungamo) 397-398 - anamoeleza maisha yake pamoja na njia yake ya imani. Ni kitabu ambacho baada ya Biblia kilisomwa zaidi katika Karne za Kati
  • Retractationes (Masahihisho) 426-428 - anamopitia maandiko yake ya awali akitaja mifano jinsi alivyobadilisha mawazo na hoja zake

Maandishi juu ya falsafa na teolojia

hariri
  • De Musica (kuhusu muziki)
  • De civitate Dei (Mji wa Mungu) 413 - 426
  • De Trinitate (Kuhusu Utatu) 400-416 - andiko lake kubwa lenye vitabu 15
  • De doctrina christiana (kuhusu mafundisho ya kikristo) 397-426
  • De libero arbitrio (kuhusu nia huru)
  • De beata vita (kuhusu maisha mema) -- kuhusu raha na kumjua Mungu
  • De magistro (juuy a mwalimu) -- mafundisho kuhusu umuhimu wa lugha
  • De vera religione (kuhusu dini ya kweli) -- kuhusu imani ya kikristo
  • Soliloquia (mazungumzo na nafsi) -- kuhusu uwezo wa akili ya kujijua
  • De immortalitate animae(kuhusu roho isiyokufa)

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo kwa Kiswahili

hariri
  • MT. AUGUSTINO, Kanuni– tafsiri ya Mapadri Waaugustino – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1992 – ISBN 9976-67-059-1
  • M. CULLEN, O.S.A., Maungamo ya Mtakatifu Augustino kwa Muhtasari – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda – ISBN 9976-63-643-1
  • M. CULLEN, O.S.A., Mtakatifu Monika: Mlinzi wa Akina Mama Wakristu – tafsiri ya E. Msigala, O.S.A. - ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Ndanda 2002 – ISBN 9976-63-641-5
  • U. D. KINYERO, O.S.A., Mt. Agustino wa Hippo - Wasifu
  • M. CULLEN, O.S.A., Watakatifu Monika na Augustino - ed. Shirika la Mt. Augustino Tanzania, 2013

Vyanzo vingine

hariri
  • Magee, Bryan (1998). The Story of Thought. London: The Quality Paperback Bookclub. ISBN 0789444550.
  • Magee, Bryan (1998). The Story of Philosophy: The Essential Guide to the History of Western Philosophy. New York: DK Pub. ISBN 078947994X.
g Saint Augustine, pages 30, 144; City of God 51, 52, 53 and The Confessions 50, 51, 52

Viungo vya nje

hariri