Ubatizo ni sakramenti ya kwanza ya Ukristo. Unaitwa "mlango wa sakramenti", kwa sababu ni lazima kuupokea kabla ya kupokea nyingine yoyote, hasa ekaristi.

Mchoro wa kale wa Ubatizo huko Roma, Italia.
Ubatizo wa mkatekumeni huko Benin.
Ubatizo wa mtoto mchanga huko Odessa, Ukraina.

Sakramenti ya kwanza

hariri

Sakramenti ya kwanza daima ni ubatizo, kwa kuwa ndio kupata uzima mpya kwa kushiriki kifo na ufufuko wa Yesu, inavyodokezwa wazi zaidi mtu akizamishwa na kutolewa majini. “Je, hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kuunganika naye; tukijua nano hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena” (Rom 6:3-6).

Sakramenti nyingine zote ama zinastawisha ama zinafufua uzima huo wa Kimungu ambao ni sharti la kuingia mbinguni. “Amin, Amin, nakuambia: Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu” (Yoh 3:5).

Kwa hiyo kubatizwa ni kuzika utu wa kale "maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo" (Gal 3:27).

Ubatizo huonyesha mambo muhimu matatu:

  1. Kuifia dhambi.
  2. Kuzaliwa upya katika Kristo.
  3. Kumpokea Kristo milele.

Ubatizo ni lazima uendane na imani ya kweli. Maana wote wenye imani ya kweli ni watoto wa Mungu: “Kwa maana kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huko ndiko kuushinda ulimwengu, hiyo imani yetu” (1Yoh. 5:4).

Jina la Kiswahili na la lugha nyingine nyingi linatokana na kitenzi cha Kigiriki βαπτίζω (baptizo, maana yake nazamisha (nazika, nafunika) majini, naosha, lakini pia nanawa).

Maana ya kwanza inadokeza lengo la kumzika mtu ili afufuke pamoja na Yesu Kristo katika uzima mpya.

Maana ya pili na ya tatu zinadokeza lengo la kumtakasa mtu kutoka dhambi zake.

Ibada zinazotumia maji zinapatikana katika dini nyingi, kutokana na kitu hicho kumaanisha wazi uzima na usafi.

Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27). “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo” (Ufu 22:1).

Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo wa Kanisa. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, si tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Mtume Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18). Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame. “Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).

Ubatizo wa Yohane

hariri

Yohane Mbatizaji alipotikisa Wayahudi wenzake kwa kuhubiri toba kandokando ya mto Yordani aliwadai wapokee "ubatizo wa maji" kama ishara ya kuongoka na ya kuwa tayari kumpokea Masiya ajaye, atakayebatiza "kwa Roho Mtakatifu na moto" (Math 3:11).

Ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote. “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11). Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5).

Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake. “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27). Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho. Kumbe ubatizo unaotuokoa “siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu” (1Pet 3:21).

Ubatizo alioupokea Yesu

hariri

Yesu alibatizwa na Yohane akiwa na umri wa miaka 30 hivi akithibitisha ubora wa kazi ya mtangulizi wake na utayari wa kubeba dhambi za ulimwengu kama mwanakondoo wa sadaka ya upatanisho.

Hapo Roho Mtakatifu alimshukia kwa sura ya njiwa na Mungu Baba alimshuhudia kuwa ndiye Mwana wake mpendwa, aliyempendeza kwa utiifu wake (Mk 1:11).

Ubatizo uliotolewa na Yesu

hariri

Injili ya Yohane inashuhudia kwamba Yesu pia alianza kubatiza, tena watu wengi kuliko Yohane, ingawa kwa njia ya wanafunzi wake (Yoh 3:22; 4:1-2). Ubatizo huo ulifanana kabisa na ule wa Yohane na kulenga Wayahudi.

Ubatizo ulioagizwa na Yesu

hariri

Kumbe baada ya kufufuka aliwaagiza wanafunzi wake wakabatize mataifa yote akifafanua watumie maneno yapi katika ibada hiyo: "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu" (Math 28:19).

Mambo muhimu kabla ya mtu mzima kubatizwa

hariri
  1. Mtu mzima huanza kwa kulisikia neno la Mungu; kwa maana "imani huja kwa kusikia" (Rum 10:17).
  2. Ni lazima kujifunza mambo unayopaswa kuyafanya ili kuikuza imani hiyo. "Enendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza ... na kuwafundisha kuyashika yote niliyoyaamuru mimi" (Math 28:19,20).
  3. Kisha fanya uamuzi sahihi wa kumfuata Kristo kimaisha.
  4. Ni lazima kupata toba na msamaha wa dhambi. “Tubuni mkabatizwe kila mtu kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi” (Mdo 2:38).

Ubatizo wa watoto wachanga

hariri

Kadiri ya madhehebu mengi, watoto wachanga wanaweza kubatizwa kwa sababu hawakatai neema ya Mungu. Wanafunzi wa Yesu walipotaka kuwazuia wasiletwe kwake “alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa” (Mk 10:14-15). Yeremia aliambiwa, “Kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5). Yohane Mbatizaji alitabiriwa “atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye” (Lk 1:15).

Ingawa watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika, Mungu anaweza kuwamiminia rohoni mwanga wa imani. “Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu” (Zab 8:2). “Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake... kwa shangwe” (Lk 1:41,44). “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako” (Math 11:25-26).

Hata watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Mtume Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye. “Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yoh 13:7). Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu. “Je, mmeelewa na hayo niliyowatendea?... Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:12,15).

Kumbe, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto kama wengine pia. Walimletea Yesu “mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne... Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, ‘Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5). Kwa ubatizo watoto wanaunganishwa naye na kuanza kuponywa madonda ya dhambi ya asili. “Tazama, mimi naliumbwa kati hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zab 51:5). “Ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Rom 5:19).

Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu mwanzo, usipingwe na yeyote kwa miaka elfu na zaidi. Ni kwamba Wayahudi walipokea watoto katika dini yao kwa kuwatahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu” (Lk 2:21). Watu wa mataifa walipoongokea dini hiyo, walioshwa na kutahiriwa pamoja na watoto wao. Mitume pia walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu. Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33); “watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).

Ubatizo na sakramenti nyingine

hariri
Sakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi

Kadiri ya Wakatoliki na Waorthodoksi, ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula. Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu. Mitume waliwaendea Wasamaria “wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16). “Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yoh 6:53).

Marejeo

hariri
  • Canadian Council of Churches, Commission on Faith and Witness (1992). Initiation into Christ: Ecumenical Reflections and Common Teaching on Preparation for Baptism] (PDF). Winfield, B.C.: Wood Lake Books. ISBN 2-89088-527-5.
  • Chaney, James M. (2009). William the Baptist. Oakland, TN: Doulos Resources. uk. 160. ISBN 978-1-4421-8560-9. OCLC 642906193. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Julai 8, 2009.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Dallmann, Robert (2014). Baptisms - One? Many? Or Both?. ChristLife, Inc. ISBN 978-0991489107.
  • Gerfen, Ernst (1897). "Baptizein": the Voice of the Scriptures and Church History Concerning Baptism. Columbus, Ohio: Press of F.J. Heer.
  • Guelzo, Allen C (1985). Who Should Be Baptized?: a Case for the Baptism of Infants. Reformed Episcopal Pamphlets. Philadelphia, PA: Reformed Episcopal Publication Society.. 26 pp. N.B.: States the Evangelical Anglican position of the Reformed Episcopal Church.
  • Guelzo, Allen C (1985), What Does Baptism Mean?: a Brief Lesson in the Spiritual Use of Our Baptisms, Reformed Episcopal Pamphlets, Philadelphia, PA: Reformed Episcopal Publication Society
  • Jungkuntz, Richard (1968). The Gospel of Baptism. St. Louis: Concordia Publishing House. OCLC 444126.
  • Kolb, Robert W. (1997). Make Disciples, baptizing: God's gift of new life and Christian witness. St. Louis: Concordia Seminary. ISBN 0-911770-66-6. OCLC 41473438.
  • Linderman, Jim (2009). Take Me to the Water: Immersion Baptism in Vintage Music and Photography 1890–1950. Atlanta: Dust to Digital. ISBN 978-0-9817342-1-7.
  • Matzat, Don (Spring 1997). "In Defense of Infant Baptism". Issues, Etc. Journal. 2 (3). Iliwekwa mnamo Februari 26, 2009.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Root, Michael; Saarinen, Risto, whr. (1998). Baptism and the Unity of the Church. Grand Rapids, MI: W.B. Eerdmans; Geneva: W.C.C. [i.e. World Council of Churches] Publications. Also mentioned on t.p.: "Institute for Ecumenical Research, Strasbourg, France". ISBN 2-8254-1250-3.
  • Scaer, David P. (1999). Baptism. St. Louis: The Luther Academy. OCLC 41004868.
  • Schlink, Edmund (1972). The Doctrine of Baptism. St. Louis, Mo: Concordia Publishing House. ISBN 0-570-03726-3. OCLC 228096375.
  • Slade, Darren M. (Agosti 15, 2014). "The Early Church's Inconsequential View of the Mode of Baptism" (PDF). American Theological Inquiry. 7 (2): 21–34. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Septemba 3, 2014.
  • Stookey, Laurence Hull (1982). Baptism, Christ's act in the church. Nashville, TN: Abingdon. ISBN 0-687-02364-5. OCLC 7924841.
  • Torrell, Jean-Pierre (2011). A Priestly People: Baptismal Priesthood and Priestly Ministry. New York/ Mahwah, NJ: Paulist Press. ISBN 978-0-8091-4815-8.
  • Ware, Kallistos (1993). The Orthodox Church. New York: Penguin Books. ku. 277–278. ISBN 0-14-014656-3. OCLC 263544700.
  • Weigel, George (2016). "The Most Important Day of Your Life". First Things.
  • Willimon, William H. (1980). Remember who you are: baptism, a model for Christian life. Nashville: Upper Room. ISBN 0-8358-0399-6. OCLC 6485882.
  • World Council of Churches (1982). Baptism, Eucharist, and ministry. Geneva: World Council of Churches. ISBN 2-8254-0709-7. OCLC 9918640.
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ubatizo kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.