Nenda kwa yaliyomo

Mita

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mita ya kimataifa, Reli ya metali ya platini iliyokuwa mfano halisi wa mita hadi mwaka 1960. (NIST)

Mita (pia: meta) ni kipimo cha urefu ambacho kimekuwa kipimo sanifu cha kimataifa.

Neno limetokana na Kigiriki μέτρον/métron (kipimo, pia chombo cha kupimia), kwa kupitia Kiingereza "metre", "meter".

Kutokana na maana hiyo "mita" inataja pia mitambo ya kupima maji, umeme na kadhalika. Hapo matumizi ya Kiswahili yanafanana na ya Kiingereza "metre", "meter".

Mita ya asili

Mita imeundwa kama kipimo wakati wa mapinduzi ya Kifaransa mwaka 1793. "Mita" iliamuliwa kuwa sehemu moja kati ya sehemu milioni 10 za meridiani ya Paris (mstari kutoka ikweta hadi ncha ya kaskazini unaopitia mjini wa Paris).

Nia ilikuwa kumaliza vipimo vya kale kutokana na viungo vya mwili kama hatua, mkono, mguu na kadhalika. Vipimo hivi asilia vilitofautiana kila mahali; Ujerumani ilikuwa na futi tofautitofauti zaidi ya kumi katika mikoa na majimbo mbalimbali.

Mita ya asili ilichongwa kama reli ya shaba na baadaye ya platini ambayo ni metali ngumu sana.

Nchi zote duniani hutumia vipimo vya mita hata kama nchi mbalimbali bado hutumia vipimo asilia kufuatana na utamaduni wao. Kwa mfano nchi za mapokeo ya Kiingereza hupenda inchi na futi.

Matumizi ya vipimo ya kale katika maisha ya kila siku si kizuizi kupeleka watu angani. Warusi bado wanapenda kipimo cha "verst" (mita 1066,8), Wamarekani huhesabu "yard" (mita 0,9144) lakini wote walifaulu kurusha makombora angani - pasipo kutumia vipimo vya mita.

Elezo ya mita leo

Tangu mwaka 1960 mita imekubaliwa kuwa umbali unaosafiriwa na nuru katika anga pasipo hewa (ombwe) katika muda wa sekonde 1/299,792,458.

Sehemu ndogo na wingi za mita

Mita 1 huwa na desimita 10, sentimita 100, milimita 1,000. Mita 1,000 ni kilomita moja.

Kiasi Jina Kifupi Kiasi Jina Kifupi
100 mita m      
10–1 desimita dm 101 dekamita dam
10–2 sentimita cm 102 hektomita hm
10–3 milimita mm 103 kilomita km
10–6 mikromita µm 106 megamita Mm
10–9 nanomita nm 109 gigamita Gm
10–12 pikomita pm 1012 teramita Tm
10–15 femtomita fm 1015 petamita Pm
10–18 atomita am 1018 eksamita Em
10–21 zeptomita zm 1021 zetamita Zm
10–24 yoktomita ym 1024 yotamita Ym
10–27 rontomita rm 1027 ronamita Rm
10–30 kwektomita qm 1030 kwetamita Qm

Vipimo vya kawaida:

Kilomita (km) : Kilomita moja ni mita 1000

Dekamita (deca): Dekamita moja ni mita 10

Sentimita (cm): Sentimita ni sehemu ya mia ya mita; mita ina sentimita 100.

Milimita (mm): Milimita ni sehemu ya kumi ya sentimita moja; sentimita ina milimita kumi, mita ina milimita elfu moja.