Upagani
Upagani ni jina la kutaja imani za dini ambazo ama zinaabudu miungu mingi au ni dini za jadi.
Neno hili linatumiwa hasa na watu katika mapokeo ya Ukristo kutaja imani nyingine, lakini siku hizi, hasa katika nchi kadhaa za Ulaya, kuna pia vikundi vya watu ambao wanajiita hivi wenyewe.
Asili ya jina
[hariri | hariri chanzo]Asili ya neno ni lugha ya Kilatini ambaPo "pagus" ni eneo la mashambani, mbali na miji mikubwa, na "paganus" ni mtu anayeishi huko vijijini au mashambani.
Chaguo la neno hili kwa ajili ya dini kinatunza historia ya kwamba huko mwanzoni katika zamani za Roma ya Kale Ukristo ulikuwa dini ya watu wa miji lakini imani za kale za Waroma ziliendelea kwa muda mrefu vijijini.
Istilahi
[hariri | hariri chanzo]Hata kama neno "mpagani, upagani" linatoka katika mapokeo ya Kikristo, si lugha ya Biblia.
Maandiko ya Biblia ya Kiebrania kwa kawaida yanatumia neno "goi / goyyim" (גוי / גוים ) kwa kutaja watu wasio Wayahudi. Goi inamaanisha "taifa" na mara chache inaweza kutumiwa pia kwa taifa la Israeli.[1]. Lakini wingi wake "goyyim" (mataifa) unamaanisha watu wasio Wayahudi ambao pia wana imani tofauti.
Katika Agano Jipya lugha hii imetafsiriwa kwa Kigiriki na pale tunaposoma "mataifa" [2] kwa Kiswahili lugha asilia ya Kigiriki inatumia "ἔθνη, ethni"
Wapagani wapya
[hariri | hariri chanzo]Tangu karne ya 19 kumekuwa na watu katika Ulaya waliotafuta njia mbadala za kidini nje ya Ukristo; wengine wao walijaribu kufufua imani za jadi za Ulaya na hapa wengine wametumia jina la "upagani" kwa imani hizi. Hao ambao wamekadiriwa kuwa makumi elfu katika nchi mbalimbali za Ulaya wanaitwa "neo pagans" yaani "Wapagani wapya"".
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kwa kawaida Biblia ya Kiebrania inatumia neno "am" kwa ajili ya Wayahudi wenyewe; "Am" ni kama "taifa" lakini zaidi kwa maana ya ukoo ilhali "goy" ni taifa zaidi kwa maana ya kieneo na kisiasa.
- ↑ kama vile Luka 21, 24: Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |