Nenda kwa yaliyomo

Fiji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Matanitu Tu-Vaka-i-koya ko Viti
फ़िजी गणराज्य
فِجی رپبلک

Jamhuri ya Visiwa vya Fiji
Bendera ya Fiji Nembo ya Fiji
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: "Rerevaka na Kalou ka Doka na Tui"
"Umwogope Mungu na umheshimu malkia"
Wimbo wa taifa: God Bless Fiji
Lokeshen ya Fiji
Mji mkuu Suva
18°10′ S 178°27′ E
Mji mkubwa nchini Suva
Lugha rasmi Kiingereza, Kifiji na Kihindustani (Hindi/Urdu)
Serikali
Rais
Waziri Mkuu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Machifu
Jamhuri chini ya kamati ya kijeshi
Ratu Wiliame Katonivere
Sitiveni Rabuka
Ratu Ovini Bokini
Uhuru
Tarehe
10 Oktoba 1970
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
18,274 km² (ya 151)
--
Idadi ya watu
 - Julai 2018 kadirio
 - Msongamano wa watu
 
926,276 (ya 161)
46/km² (ya 148)
Fedha Fijian dollar (FJD)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
(UTC+12)
(UTC)
Intaneti TLD .fj
Kodi ya simu +679

-


Shujaa wa Mlimani kutokea Fiji

Fiji (kwa Kifiji: Matanitu ko Viti; kwa Kihindustani: फ़िजी, فِجی) ni nchi ya visiwani ndogo ya Melanesia katika Pasifiki yenye visiwa vikubwa 322 na wakazi 926,276.

Kati ya visiwa vingi kuna 106 vyenye wakazi. Visiwa vikuu ni Vanua Levu na Viti Levu wanapokaa asilimia 87 za wakazi wote, na ndipo mji mkuu, Suva ulipo.

Jiografia

[hariri | hariri chanzo]
Ramani ya Fiji

Fiji inapatikana katika latitudo 176’ 53” kusini na 178’12” magharibi, lakini pia mstari wa kimataifa wa tarehe unaipa Fiji saa sawa katika visiwa vyake vyote.

Fiji ni funguvisiwa lililoko mbali na visiwa vigine vya Pasifiki. Liko mashariki kwa Vanuatu, magharibi kwa Tonga na kusini kwa Tuvalu, na takriban km 2.100 kaskazini kwa Auckland (New Zealand).

Visiwa vyake vikubwa 322 na vingine vidogovidogo zaidi ya 500 vina eneo la ardhi kavu la km² 18,270. Hizo ni asilimia kumi tu ya eneo lote la kilomita za mraba 194,000, ambazo kwa kiasi kikubwa ni la maji ya bahari ya Pasifiki.

Visiwa hivyo vimesheheni milima, kiasi cha kufikia hadi mita 1300 kwa urefu, milima ambayo imetandwa na misitu.

Maeneo mengine katika Fiji ni Nandi ambapo kuna uwanja wa ndege wa kimataifa, na Lautoka ambako kuna viwanda na shughuli nyingi za uzalishaji hufanyika hapo.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Wakazi wa visiwa vya Fiji, wanaaminika kuwa walitokana na wavuvi wa masafa marefu ambao walifika katika visiwa hivyo zaidi ya miaka 3500 iliyopita.

Shughuli za ufinyanzi katika jamii ya watu wa kabila la Walapita zimeonekana kutawala maeneo mengi sana katika visiwa vya Fiji, nazo ni ushahidi wa kuwa Fiji imekuwa ikikaliwa na watu tangu miaka 3500 hadi 1000 kabla ya Kristo.

Japokuwa jamii ya kabila hilo ndio wanaoaminika kuwa wa kwanza kuishi katika visiwa vya Fiji, lakini hali hii inatiliwa shaka kutokana na jamii ya kabila la Wamelanesia kuwepo kwa wingi sana katika visiwa hivyo, hali inayoashiria kuwa pengine kabila hilo pia limekuwepo tangu kale.

Utamaduni katika visiwa vya Fiji umekuwa ukifanana sana na ule wa jamii ya Wamelanesia ambao hupatikana magharibi mwa bahari ya Pasifiki, lakini utamaduni huo umekuwa ukifananishwa sana na ule wa jamii za Samoa na Tonga.

Shughuli za biashara katika mataifa hayo matatu yalianza muda mrefu kabla ya kuja kwa watawala wa Ulaya ambao kwa kiasi kikubwa wanaaminika kufika katika visiwa hivyo kwa usafiri wa boti ndogo ndogo maarufu kama kanuu ambazo zinaaminika kuwa zilitengenezwa na wakazi wa visiwa hivyo.

Zana mbalimbali za kufinyangwa zimekuwa zikipatikana katika visiwa vya Samoa na hata katika visiwa vya Marquesas zaidi ya kilometa elfu moja kutoka katika makao makuu ya Fiji.

Mpelelezi wa kutoka Uholanzi aliyejulikana kama Abel Tasman, aliitembelea Fiji katika miaka ya 1643, akiwa anatafuta bara la Afrika kusini lililojulikana kama “the great Southern continent”.

Kwa muda wa karne moja hivi iliyopita, katika visiwa vya Fiji kumekuwa kukiibuka tamaduni tofautitofauti, hali iliyooashiria ubaguzi wa kikabila kuwepo, tofauti na leo, ambapo, wakazi wa Fiji wamekuwa wakiishi kwa amani na wamekuwa wakikielezea kipindi hicho kama kipindi cha “na gauna ni tevoro” yaani "wakati wa shetani".

Fiji ilijipatia uhuru wake kutoka katika utawala wa kikoloni wa Uingereza tarehe 10 Oktoba 1970.

Tangu uhuru katika visiwa vya Fiji kumekuwepo na mapinduzi ya kijeshi mara nne: mara mbili mwaka 1987, mara moja mwaka 2000, na mara moja mwaka 2006, lakini kwa ujumla, jeshi nchini humo limekuwa likishikilia madaraka ya moja kwa moja au kupitia kwa serikali iliyopo madarakani tangu mwaka 1987, hali iliyosababishwa na wakazi wa Fiji kulaumu serikali yao kutawaliwa na watu wenye asili ya Uhindi..

Mwaka 1990, katiba mpya katika utawala wa Fiji iliundwa ambayo ilichukua nafasi ya ile ya awali ambayo ilikuwa ikiegamia upande wa makabila kwa kiasi kikubwa.

Tarehe 10 Aprili 2009, Rais Iloilo, aliifuta katiba ya nchi hiyo na kufutilia mbali mamlaka ya mahakama akajitangaza kuwa rais wa visiwa hivyo, lakini baadaye alianzisha tena utawala wa kikatiba hali iliyopelekea mwenyewe kutolewa madarakani kwa kubainika alikuwa madarakani kinyume cha katiba.

Tarehe 13 Julai 2009, Fiji ilitolewa katika mkutano wa visiwa vinavopatikana katika bahari ya Pasifiki kutokana na kushindwa kwake kuendesha uchaguzi kwa njia ya kidemokrasia.

Hatimaye tarehe 17 Septemba 2014 uchaguzi huru ulifanyika na kukipa ushindi chama cha FijiFirst (59.2%).

Fiji hutawaliwa na Rais akifuatiwa na waziri mkuu, na baada ya hapo hufuatia Mwenyekitit wa Halmashauri ya Machifu.

Siasa ya Fiji hufanyika kwa mtindo wa kuchagua wawakilishi bungeni, ambapo waziri mkuu ndiye mkuu wa serikali husika, na rais ndiye mkuu wa visiwa vyote vya Fiji.

Halikadhalika uchaguzi katika Fiji huhusisha vyama vingi ambapo serikali ya Fiji hutawala maamuzi yote ya nchini humo, lakini chini ya demokrasia na utawala wa sheria.

Idadi kubwa ya wakazi wa Fiji inajumuisha wenyeji wa Fiji ambapo watu wa kabila la Melanesia huchukua asilimia 56.8 ya wakazi wote wa Fiji, wakati wale wanaojulikana kama Wahindi wa Fiji huweza kufikia asilimia 37.5, na wengine ni wahamiaji kutoka katika mataifa ya Ulaya waliohamia nchini humo kwa wingi hususani katika karne ya 19.

Kwa ujumla kiasi cha watu wa Kihindi kimekuwa kikipungua siku hadi hadi siku kutokana na wengi kuhama katika visiwa hivyo kwa sababu tofautitofauti, lakini vilevile kumekuwa na kiasi kidogo cha watu kutoka katika visiwa vya Solomoni ambao wengi wao walikuja visiwani hapo kama wafanyakazi.

Fiji inajulikana kama visiwa vya lugha nyingi, kwani lugha tofautitofauti zimekuwa zikipatikana katika visiwa hivyo, hali kadhalika historia ya visiwa hivyo inaonesha kuwepo kwa makabila ambayo yamekuwa yakihamahama kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine.

Lugha rasmi visiwani ni Kifiji, Kiingereza na Kihindustani kinachofanana na Kihindi na Kiurdu. Pia kuna lugha nyingine saba za asili (angalia orodha ya lugha za Fiji).

Dini ni moja ya mambo ambayo hutofautisha jamii mbalimbali katika visiwa vya Fiji, hususani baina ya makabila ya Wafiji wenyewe na Wahindi waishio Fiji, ambapo asilimia kubwa ya wenyeji ni Wakristo, wakati watu kutoka India ni Wahindu (70%) AMa Waislamu (17.9%).

Kwa ujumla dini katika visiwa vya Fiji imetawaliwa na Wakristo ambao ndio wamechukua asilimia kubwa ya idadi ya watu (64.4%), japokuwa Wakristo hawa wanajumuisha madhehebu tofautitofauti kama vile Wamethodisti, Wakatoliki, Wapentekoste, Wasabato na Waanglikana. Wahindu ni 27.9% na Waislamu 6.3% za wakazi wote.

Utamaduni

[hariri | hariri chanzo]

Utamaduni katika visiwa hivi hujumuisha tamaduni kutoka makabila tofautitofauti yakiwemo ya Wafiji wenyewe, Wahindi, Wachina na Wazungu ambao kwa ujumla huwa na tamaduni tofatitofauti.

Kwa hakika utamaduni wa asili unapewa kipaumbele kama sehemu ya maisha ya kila siku kati wa wakazi wengi, lakini hivi karibuni kumekuwako na mwingiliano wa tamaduni kutoka nchi mbalimbali. Kuna shughuli tofautitofauti za kitamaduni kama sanaa, uchongaji, muziki na michezo mbalimbali, mkuu ukiwa Rugby ambao wachezaji kutoka Fiji wameshiriki mashindano mbalimbali kimataifa. .

Wakazi wa visiwa vya Fiji hujishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile uchimbaji wa madini, uvuvi, uvunaji wa mafuta, na biashara.

Chakula wanachokula wakazi wa visiwa hivi hujumuisha chakula kitokanacho na mazao ya bahari maarufu kama "sea foods".

Kwa upande wa sikukuu Fiji husherehekea sikukuu mbalimbali kama vile Mwaka mpya, Maulid, Ijumaa kuu, Pasaka, Siku ya Fiji, Krismasi n.k.

Kwa ujumla visiwa vya Fiji vimekuwa vivutio kwa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwenda kwa ajili ya mengi, lakini zaidi mapumziko, hii ni kutokana na hali tulivu iliyopo visiwani hapo, maji maangavu na pia ukarimu wa wakazi wa Fiji.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Serikali
Taarifa za jumla
Safari


Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.