Tanganyika African National Union
Tanganyika African National Union (TANU) kilikuwa chama kilichotawala Tanganyika na Tanzania hadi muungano wa chama hiki na Chama cha Afro-Shirazi cha Zanzibar ulipounda Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.
TANU ilianzishwa 7 Julai 1954 kutokana na Tanganyika African Association (TAA). TAA ilikuwa na mwelekeo wa kitamaduni zaidi ya siasa. Mwenyekiti wa kwanza wa TANU alikuwa Julius Kambarage Nyerere.
TANU ilishinda kila uchaguzi chini ya utawala wa kikoloni ikawa chama cha kuongoza Tanganyika hadi ilipopata uhuru wake mwaka 1961. Katiba ya Taifa ya mwaka 1962 ilifanya TANU kuwa chama cha pekee nchini ikifuata mfano wa nchi za kijamaa zenye muundo wa siasa ya chama kimoja.
Mtiririko wa upatikanaji uhuru
[hariri | hariri chanzo]Mtiririko wa kupigania uhuru wa Tanganyika na mchango wa Mwalimu katika kupigania uhuru:
1929: TAA yaundwa ikiwa na wajumbe wafuatao:
- Kleist Sykes
- Mzee bin Sudi
- Ibrahim Hamis
- Zibe Kidasi
- Ali Said Mpima
- Suleiman Majisu
- Raikes Kusi
- Rawson Watts
- Cecil Matola
1950: TAA yawasiliana na KAU; Abdulwahid alikwenda Nairobi kukutana na Jomo Kenyatta ili kujenga mawasiliano na chama cha Kenya African Union (KAU).
1951: Kuundwa kwa tawi la siasa la TAA; likiwa na wajumbe wafuatao:
- Abdulwahid Sykes (Katibu)
- Sheikh Hassan bin Amir
- Hamza Kibwana Mwapachu
- Said Chaurembo
- Dk. Kyaruzi
- John Rupia
- Stephen Mhando
1951: Kenyatta akutana tena na viongozi wa TAA. Safari hii mkutano huo ulifanyika Arusha. Wajumbe wa TAA walikuwa Abdulwahid Kleist Sykes, Dossa Aziz na Stephen Mhando.
1952: Abdulwahid alichaguliwa kuwa Rais wa TAA.
1952: Mwalimu Nyerere atambulishwa kwa Abdulwahid na Kasela Bantu. Baada ya utambulisho huo ikawa kila Jumamosi Mwalimu Nyerere akawa anakutana na akina Dossa Azizi, Ally Sykes, Abdulwahid Sykes, Dustan Omar na Mhando kujadili mustakbali wa nchi ya Tanganyika.
Mikutano hiyo ama ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Dossa Azizi mtaa wa Congo au mtaa wa Stanley nyumbani kwa Abdulwahid.
Alikuwa ni Dossa Azizi ambaye mara nyingi alikuwa akimrudisha Mwalimu Nyerere kwa gari lake Pugu (St. Francis College) baada ya mkutano.
1953: Mwalimu achaguliwa kuwa Rais wa TAA. Wazee waliompa nguvu ya kisiasa Mwalimu mara baada ya kuingia katika TAA/TANU.
Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Mohammed Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate na Mwinjuma Mwinyikambi. Wengine walikuwa Rajab Diwani, Makisi Mbwana, Sheikh Haidar Mwinyimvua na Idd Faiz Mafongo. Aidha walikuwepo Idd Tosiri, Sheikh Mohamed Ramia na Mashado Ramadhani Plantan.
Oktoba 10, 1953 Mwalimu Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia walikutana kujadili namna ya kuibadili TAA kuwa chama kamili cha siasa.
1954: TANU yaanzishwa. Wajumbe wa mkutano uliojadili kuibadili katiba ya TAA kuwa TANU walikuwa Abdulwahid Sykes, Julius Nyerere, Tewa Said Tewa, Dossa Aziz, Ally Sykes, Kasela Bantu, Abubakar Ilanga na Saadan Abdu Kandoro. Wengine walikuwa Suleiman M. Kitwala, C.O. Milinga, Patrick Kunambi, Gerimano Pacha, Japhet Kirilo na L.M. Makaranga. Walikuwa pia Joseph Kimalando na John Rupia.
Mkutano wa kuizindua rasmi TANU ulihudhuriwa na wajumbe wafuatao: Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia na Mshume Kiyate. Wengine walikuwa Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajab Diwani, Suleiman.M. Kitwala, Schneider Plantan na Marsha Bilali. Walikuwepo pia Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Idd Faiz Mafongo, Idd Tulio, Denis Phombeah na wengine.
Julius Nyerere alipewa kadi ya TANU Na. 1, kadi Na. 2 ikaenda kwa Ally Sykes na Abdulwahid akachukua kadi ya TANU Na. 3, Dossa Azizi alichukua kadi Na. 4, kadi Na. 5 ikaenda kwa Phombeah. Dome Okochi alipata kadi Na. 6, John Rupia Na. 7, Bibi Titi Mohamed kadi Na. 16 na Idd Tosiri kadi Na. 25.