Ally Sykes
Ally Sykes | |
Ally Sykes na Mwalimu Julius Nyerere 1958 | |
Amekufa | 19 Mei 2013 |
---|---|
Nchi | Tanzania |
Kazi yake | Mwanaharakati |
Ally Kleist Sykes (Gerezani, Dar es Salaam, 10 Oktoba 1926 - Nairobi, Kenya, 19 Mei 2013) alikuwa mzalendo muasisi wa TANU na moja kati ya wapigania uhuru wakubwa wa Tanganyika katika miaka ya 1950. Ally Sykes ndiye aliyemwandikia na Kumkabidhi Mwalimu Julius Nyerere kadi ya TANU Na. 1. Historia ina kawaida ya kujirudia. Ally Sykes mmoja wa waasisi wa TANU, mmoja wa wale watu wasiozidi takriban saba walikuwa katika kamati ya ndani ya TAA iliyounda TANU, mmoja wa wafadhili wakuu wa TANU, mmoja wa askari kwa maana yake halisi kwa kuwa ni Ally Syke ndiye TAA hadi TANU ikimtegemea kwa kutekeleza mambo ya hatari dhidi ya Waingereza. Pia alikuwa mwanajeshi, mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu. [1]
Ally Sykes ndiye alikuwa akipewa kazi za hatari za kumwaga ‘’sumu na upupu’’ dhidi ya serikali. Sumu na upupu huu yalikuwa makaratasi aliyokuwa akichapa nyumbani kwake usiku makaratasi ambayo Waingereza waliyaita makaratasi ya ‘’uchochezi.’’ Waingereza na makachero wake walikuwa wanamjua Ally Sykes vizuri. Waingereza walikuwa wakijua kuwa alikuwa na medali ya mlenga shabaha bingwa aliyopata Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Huyu ndiye Ally Sykes mzalendo muasisi wa TANU ambaye sahihi yake ndiyo iko katika kadi ya TANU ya Baba wa Taifa.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Wasifu
[hariri | hariri chanzo]Ally Sykes alikuwa mtu maarufu kupita kiasi. Alikuwa kwanza ana umaarufu wa kuzaliwa. Kazaliwa Dar es Salaam Gerezani, mtoto wa mjini. Kisha alikuwa maarufu kwa nasaba. Baba yake Kleist Sykes alikuwa mmoja wa watu mashuhuri katika siasa zote za Dar es Salaam katika miaka ya ya mwanzo ya 1900 hadi alipofariki mwaka 1949. Baba yake alilelewa na Afande Plantan askari kiongozi katika jeshi la Schutztruppe la Wajerumani lilokuja Tanganyika na Herrman von Wissman wakati Wajerumani walipoingia kuitawala Tanganyika.
Kleist alikuwa ndiye katibu muasisi wa Tanganyika African Association TAA mwaka 1929 chama kilichokuja baadae kujibadili na kuwa TANU Ally Sykes akiwa mmoja wa hao waasisi. Baba yake Kleist aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) na kupitia jumuia hii akajenga shule ya kwanza ya Kiiislam Dar es Salaam, shule ambayo ilisomesha Qur’an pamoja na masomo ya kisekula. Hii Al Jamiatul Islamiyya ndiyo iliyotoa viongozi wa kwanza kuiendesha TAA na baadaye TANU katika harakati za kudai uhuru.
Harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika na usaibu na Nyerere
[hariri | hariri chanzo]Inajulikana na wengi Ally Sykes na kaka yake Abdulwahid Sykes ndio watu wa mwanzo kumpokea Julius Nyerere alipokuja Dar es Salaam mwaka 1952. Nyerere alifika nyumbani kwa akina Sykes kwa utambulisho na hii ilijenga urafiki ambao ulipitiliza na kuwa udugu mkubwa wa mapenzi ya dhati si baina yao tu bali hata kwa wake na mama zao. Mama yake Nyerere Bi Mugaya hakuwa akipungua nyumbani kwa Mama Abdu Bi Mrurguru biti Mussa Mtaa wa Kirk. Halikadhalika Maria Nyerere hakuwa akipungua nyumbani kwa aidha kwa Bi Zainab mkewe Ally Sykes Mtaa wa Kipata au kwa Bi Mwamvua mkewe Abdulwahid Sykes Mtaa wa Aggrey.
Wakati huu Abdulwahid ndiye akiwa rais wa TAA na harakati za kuanzisha TANU zimepamba moto achilia mbali hila na fitna za Waingereza kuwatokomeza viongozi shupavu wa TAA kama Hamza Mwapachu, Dk. Vedast Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi nje ya Dar es Salaam kukivunja nguvu chama. Ndiyo maana TANU ilipokuja asisiwa mwaka 1954 Ally Sykes kadi yake ya TANU ikawa namba 2, Nyerere namba 1, Abdulwahid Sykes kadi yake namba 3, Dossa Aziz kadi namba 4, John Rupia kadi yake namba 7.
Kipindi hiki Ally Sykes alikuwa Katibu wa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA) na vilevile alikuwa mwakilishi wa chama hicho katika Kamati ya Uajiri ya Serikali (Government Establishment Committee). Thomas Marealle ndiye alikuwa rais wa TAGSA na Rashid Kawawa alikuwa mwanakamati. Wanasiasa hawa vijana Ally Sykes akiwa mmoja wao wenyewe walijipa jina, ‘’Wednesday Tea Club’’ wakikutana kila siku ya Jumatano kunywa chai pamoja na kutumia wakati ule kupanga mikakati ya kuwang’oa Waingereza katika ardhi ya Tanganyika. Kupitia Ally, Abdulwahid na Dossa Aziz Nyerere akaweza kujuana na wenyeji wa Dar es Salaam maarufu katika hao ni Sheikh Hassan bin Amir, Mshume Kiyate, [[[Jumbe Tambaza]], Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mtamila, Bi. Titi Mohamed, Tatu biti Mzee na wengineo.
Kifo chake na kutojaliwa mchango wake katika vyombo vya habari
[hariri | hariri chanzo]Historia huwa inajirudia. Kifo cha Ally Sykes kimepuuzwa na vyombo vya habari kama ilivyokuwa awali kuwa hata kifo cha kaka yake Abdulwahid Sykes alipofariki mwaka 1968 magazeti ya TANU (wakati ule ‘’The Nationalist’’ na ‘’Uhuru’’) chama alichokiasisi kwa jasho, damu na fedha zake magazeti haya yalipuuza kifo hicho. Kuna watu katika TANU katika kipindi kile walikuwa wanajaribu kuifuta historia ya kupigania uhuru wakitaka kuondoa mchango wa Abdulwahid na Ally Sykes katika historia ya uhuru. Hata hivyo ‘’Tanganyika Standard’’ gazeti ambalo ndilo liliokuwa likilinda maslahi ya ukoloni Tanganyika, ndilo lililoandika taazia ya Abdulwahid Sykes. Mhariri wa Tanganyika Standard Brendon Grimshaw hakuweza kustahamili fedheha ile, aliandika taazia ambayo itaishi zaidi ya miaka miaka mia moja na zaidi. Taazia ile ilitikisa fikra Makao Mkuu ya TANU Mtaa wa Lumumba na ikawakera wengi. Grimshaw alisema katika taazia yake kuwa TANU imeundwa pakubwa kwa mchango wa ukoo wa Sykes.
Mwaka wa 1968 wakati Abdulwahid anafariki Waislam walikuwa wako katika taharuki kubwa ya kile kilichokujajulikana kama ‘’mgogoro wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) taharuki iliyojaa simanzi kwa kuwa Mufti wa wakati ule Sheikh Hassan bin Amir mmoja wa masheikh viongozi katika TANU alikuwa kakamatwa na kufukuzwa nchini kwa amri ya Nyerere. Wakati haya yakijiri, Tewa Said Tewa na Bi.Titi Mohamed viongozi wa juu wa EAMWS walikuwa wakiandamwa na Nyerere na hapakuwa na uelewano mzuri baina yao. Ajabu ni kuwa umauti umemkuta Ally Sykes katika hali kama ile ile iliyokuwapo wakati kaka yake alipofariki dunia mwaka 1968 wakati nchi ikiwa katika mgogoro wa EAMWS kishindo ambacho kilidumu takriban miezi mitatu.
Ally Sykes kafa wakati nchi ipo katika taharuki kwa kile kinachodaiwa ‘’uadui baiana ya Waislam na Wakristo.’’ Kwa hiki kifo cha Ally Sykes bila shaka wahariri wa magazeti walikuwa wameshughulishwa katika kutafuta habari mpya za ‘’kuchomwa makanisa’’ na ‘’ugomvi wa kuchinja,’’ hawakuwa na muda wa kufuatilia msiba wa muasisi wa TANU marehemu Ally Sykes. Lakini iweje hali iwe kama vile miaka saba tu baada ya uhuru kupatikana nchi iingie na taharuki ya kiasi kile na hivi sasa taharuki ile ijirejee upya tena ikishuhudiwa na waasisi wa harakati za ukombozi?
Nyaraka za historia alizoficha nyumbani pake na kumpatia Mohamed Said
[hariri | hariri chanzo]Nyaraka hizi mpaka Ally Sykes anakufa zilibaki kuwa sehemu ya malalamiko kwa Mohamed Said kwa Ally kuwa hazikustahili kuwa mikononi kwake na kazifungia katika ‘’safe’’ zake.
Nilikuwa nikamwambia mara kadhaa inagawa hakutaka kunisikiliza kuwa nyaraka hizi ni mali ya taifa la Tanzania lazima azikabidhi serikalini kwa kuhifadhiwa na kuwekwa Tanzania National Archive (TNA) kama urithi wa kizazi kijacho. Yeye siku zote akinambia, ‘’Mohamed hizi nyaraka ninaogopa nikiwapa serikali watazichoma moto.’’ Alikuwa na sababu ya kusema vile. Nyaraka za Ally Sykes zinakwenda nyuma kiasi cha miaka mia moja kuanzia siku babu yake Sykes Mbuwane alipotia mguu katika ardhi ya Tanganyika kutoka meli ya kvitia ya Wajerumani pale Pangani akitokea Msumbiji. Nyaraka zile zina barua za wanasiasa wa mwanzo katika Tanganyika achilia mbali habari za baba yake. Ukianza kufunua majalada yale hutachoka kupekua karatasi baada ya karatasi. Nyingine zimechoka kwa umri mrefu.
Katika majalada yale utakutana na wazalendo na machifu, utakutana na wasiasa wenye asili ya Kiasia na Waingereza wenyewe waliokuwa watawala. Nyaraka zile utawaona na utawasikia watu hawa wakizungumza na wewe: Dk Joseph Mutahangarwa, Chief Abdieli Shangali wa Machame, Paramount Chief Thomas Marealle wa Marangu, Chief Adam Sapi Mkwawa wa Wahehe, Chief Harun Msabila Lugusha, Dk. Wilbard Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dk Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Dossa Aziz, Ivor Bayldon, Yustino Mponda, Ivor Bayldon, Rashid Mfaume Kawawa, Bhoke Munanka, Rashid Kheri Baghdelleh, Robert Makange, Saadani Abdu Kandoro, Malkia Elizabeth, Chief Secretary Bruce Hutt, Gavana Edward Twining, Gavana Ronald Cameron, Mwalimu Thomas Plantan na ndugu zake – Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Plantan, Mwalimu Mdachi Shariff, Mwalimu Nicodemus Ubwe, Kassela Bantu, John Rupia, Hamza Kibwana Mwapachu, Othman Chande, Leonard Bakuname, Stephen Mhando, Oscar Kambona, Peter Colmore, Albert Rothschild, Ali Mwinyi Tambwe, Alexander Thobias, Japhet Kirilo, Joseph Kimalando, Ian Smith, Roy Welensky, Jim Bailey, Kenneth Kaunda, Meida Springer, John Hatch, Gretton Bailey, Brig. Scupham, Dome Okochi Budohi, Annur Kassum, Nesmo Eliufoo, Yusuf Olotu, Joseph Kimalando, Julius Nyerere na wengine wengi wakubwa kwa nyadhifa walizokuja kukamata katika Tanganyika huru na wale walioanguka njiani.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- http://www.mohammedsaid.com/2013/12/ally-kleist-sykes-1926-2013-mzalendo.html?updated-min=2013-01-01T00:00:00-08:00&updated-max=2014-01-01T00:00:00-08:00&max-results=34 Archived 19 Julai 2018 at the Wayback Machine. katika wavuti ya Mohamed Said
- Ally Sykes katika wavuti ya TanServe
- Ally Sykes katika wavuti wa the East African