Nenda kwa yaliyomo

Vita ya miaka 30

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
The printable version is no longer supported and may have rendering errors. Please update your browser bookmarks and please use the default browser print function instead.
Jeshi la Kaisari mbele ya Stralsund
Mapigano kwenye daraja la Prague 1648
Ulaya baada ya Amani ya Westfalia

Vita ya miaka 30 ilipigwa kati ya miaka 1618 hadi 1648. Ilikuwa vita ya Kiulaya lakini mapigano yake yalitokea hasa katika Ujerumani kwenye eneo la Dola Takatifu la Kiroma.

Madola ya Ujerumani yalipigana kati yao, na nchi za nje zilishiriki zikiwemo Hispania, Ufaransa, Uswidi, Uholanzi na Denmark.

Vita ilileta uharibifu kupita kiasi kwa ajili ya Ujerumani kushinda vita zote zilizofuata katika historia. Hukumbukwa hadi leo.

Hali ya kisiasa kabla ya vita

Ujerumani ilikuwa sehemu kubwa ya Dola Takatifu la Kiroma pamoja na majimbo ambayo leo ni Ucheki, Uholanzi, Uswisi, Ufaransa ya magharibi, Italia ya kaskazini na Austria. Dola Takatifu ilikuwa kama maungano ya madola madogo zaidi chini ya Kaisari.

Mkuu alikuwa Kaisari aliyetoka katika nasaba ya Habsburg akiwa mtawala wa Austria hasa na madaraka yake juu ya Dola Takatifu kwa jumla yalikuwa madogo. Maeneo mengine yalijitegemea kwa kiasi kikubwa chini ya watawala wao wa kikabaila.

Miaka 100 kabla ya vita matengenezo ya Kiprotestanti yalienea katika Ujerumani na sehemu ya madola ilipokea madhehebu mapya, lakini wengine walibaki Wakatoliki. Madola mengi yalisisitiza ya kwamba wananchi wote wafuate dhehebu moja tu, ama Ukatoliki ama Ulutheri; hapakuwa na uhuru wa dini kwa kila raia.

Uhusiano kati ya madhehebu ya Kikristo ulikuwa mbaya kwa muda mrefu. Karibu katika kila nchi Wakristo walilazimishwa kufuata madhehebu rasmi. Ikiwa mtawala fulani aliona vema kukubali mawazo ya Martin Luther mapadri wote walipewa chaguo la kufuata Ulutheri au kuhama nchi. Vilevile baada ya kifo chake ikiwa mtawala aliyefuata alikuwa na msimamo tofauti, mapadri wakarudi na wachungaji wa Kiinjili wakafukuzwa.

Raia hawakuulizwa wenyewe wanasadiki nini, isipokuwa katika miji iliyojitawala na kuwa na utaratibu wa kidemokrasia. Lakini hata mijini huko haikuwa kawaida kuruhusu madhehebu mawili mahali pamoja.

Mafundisho ambayo kwetu leo yanaonekana kuwa na tofauti ndogo yaliweza kumfikisha mtu gerezani au hata kifoni.

Uhusiano mbaya ulikuwepo vilevile kati ya wafuasi wa Luther na Wareformati. Katekisimu zao zilitumika kama bendera. Walishutumiana kuwa wazushi wasioelewa vizuri kiini cha imani.

Fitina ya kidini katika Bohemia

Vita ilianza kama fitina kati ya Kaisari aliyekuwa Mkatoliki Mwaustria na maungano ya madola ya Kiprotestanti ndani ya Dola Takatifu. Chanzo kilikuwa uasi wa makabaila wa Kiprotestanti katika jimbo la Bohemia dhidi ya siasa ya Kaisari Ferdinand II aliyechaguliwa pia kuwa mfalme wa Bohemia.

Ferdinand alikataa kukubali uhuru wa dini ulioahidiwa na mtangulizi wake kwa ajili ya Bohemia. Fitina hii ilikuwa vita baada ya gavana wa Kaisari kutupwa nje ya dirisha la chumba cha mkutano mjini Praha tarehe 23 Mei 1618. Wakubwa wa Bohemia waliendela kutamka ya kwamba Ferdinand si mfalme wao tena, wakamchagua kabaila wa Palentino kama mfalme mpya.

Kaisari alichukua silaha na kwenye mapigano ya kwanza tarehe 8 Novemba 1619 karibu na mji wa Praha waasi wa Bohemia walishindwa. Makabaila wengi wa Kiprotestanti kutoka madola mengine ya Ujerumani waliamua kuwasaidia wenzao wa Bohemia. Vita hii ilielekea kwisha kwa ushindi wa Kaisari mnamo 1623.

Uswidi kusaidia Waprotestanti

Hapo nchi jirani zilijiunga na vita. Nchi za Skandinavia zilifuata Uprotestanti na watawala wao waliamua kuwasaidia wenzao Wajerumani. Wadenmark kwanza halafu Waswidi walifika kwa wanajeshi wengi. Mfalme Gustav Adolf wa Uswidi alishinda jeshi la Kaisari mara kadhaa hadi alipouawa kwenye mapigano ya Lützen tarehe 16 Novemba 1632.

Kuingilia kwa Ufaransa

Baada ya kuona ya kwamba Kaisari aliendelea kusogea mbele, mfalme wa Ufaransa alijiunga na Uswidi akashiriki katika vita tangu mwaka 1635. Nia yake ilikuwa hasa kuzuia enzi ya nasaba ya Habsburg iliyotawala Hispania ikashika pia Austria pamoja na cheo cha Kaisari wa Dola Takatifu la Kiroma.

Hivyo vita iliyoanza kama mapigano ya kidini katika dola moja la Ujerumani iliendelea kuwa vita ya Kiulaya ambako nchi ya Wakatoliki kama Ufaransa ilishikamana na Uswidi ya Kiprotestanti dhidi ya Kaisari Mkatoliki.

Vita ilileta uharibifu mkubwa mno katika Ujerumani. Kuna makadirio ya kwamba karibu theluthi moja ya wakazi wote walikufa kutokana na mauaji, njaa na magonjwa. Katika maeneo ya Ujerumani ya Kusini zaidi ya nusu ya watu walipotea.

Wanajeshi walikuwa askari wa kukodiwa ambao mara nyingi hawakulipwa bali walipewa uhuru wa kutwaa kwa mabavu chochote walichotaka.

Amani ya Westfalia

Uchofu ulileta majadiliano juu ya amani. Mwaka 1648 wawakilishi wa wafalme walipatana katika amani ya Westfalia kanuni za amani.

  • Madhehebu matatu yaliyokubaliwa Ulaya ni Wakatoliki, Walutheri na Wareformed.
  • Kila mtawala aliamua kwa dola lake ni dini ipi itafuatwa lakini raia walikuwa na haki ya kutoka katika nchi kama mtawala alikataa dini yao. Sheria ilikuwa: "Cuius regio, eius religio" (mwenye nchi ni mwenye kuamua dini)
  • Uholanzi na Uswisi zilitoka katika Dola Takatifu la Kiroma kama nchi huru za pekee.
  • Mfalme wa Uswidi alitwaa maeneo makubwa katika Ujerumani ya Kaskazini

Mapatano hayo yaliunda ramani ya kimadhehebu kule Ulaya yenye maeneo ya Wakatoliki, Walutheri au Wareformati watupu.

Jumuiya ndogo ziliendelea kugandamizwa wakapata ustahimilivu mahali pachache. Hivyo wafuasi wa madhehebu madogo walilazimika kuficha imani yao au kuhamahama katika Ulaya.

Wakati ule nafasi mpya ilitokea: Mfalme wa Uingereza alikuwa na makoloni Marekani lakini alikosa watu. Akatafuta walowezi kwa ajili ya makoloni yake akiwaahidia wote kwamba watapata shamba pamoja na uhuru wa dini. Hivyo watu kutoka nchi nyingi za Ulaya walianza kuhamia Marekani, hasa wale waliokosa uhuru huo.

Mpaka leo nchi mbalimbali za Ulaya zinafuata hasa madhehebu moja, na Marekani ina madhehebu makubwa ambayo hayana wafuasi wengi Ulaya, k.mf. Wabatisti.