Nenda kwa yaliyomo

Tukuyu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Tukuyu
Tukuyu is located in Tanzania
Tukuyu
Tukuyu

Mahali pa mji wa Tukuyu katika Tanzania

Majiranukta: 9°15′0″S 33°38′24″E / 9.25000°S 33.64000°E / -9.25000; 33.64000
Nchi Tanzania
Mkoa Mbeya
Wilaya Rungwe

Tukuyu ni mji mdogo na makao makuu ya wilaya ya Rungwe katika mkoa wa Mbeya, Tanzania.

Iko mita 1300 juu ya UB, karibu na mlima wa Rungwe ikitazama beseni la Ziwa Nyasa.

Historia

[hariri | hariri chanzo]
Langenburg (Lumbila) na Neu Langenburg (Tukuyu)

Tukuyu ilianzishwa mnamo 1901 wakati wa ukoloni wa Kijerumani. Wajerumani waliwahi kuunda kituo cha kwanza pale Lumbila ya leo, kando ya Ziwa Nyasa wakakiita "Langenburg"[1] kwa heshima ya kabaila na mwanasiasa Mjerumani. Langenburg iliendelea kuwa makao makuu ya Mkoa wa Langenburg lakini ilikuwa na matatizo machoni pa Wajerumani walioona tabianchi haifai kwao kiafya. Mwaka 1900 waliamua kuhamisha makao makuu sehemu iliyokuwa baridi zaidi na kujulikana kwa jina Tukuyu wakaiita "Neu Langenburg" ("Langenburg mpya"). Boma jipya lilijengwa mwaka 1901. Hadi leo jina la hoteli "Langiboss" linakumbusha jina la zamani. Neu Langenburg iliendelea kuwa mji mdogo; mnamo 1913 ilikuwa na maduka 10 na kituo cha polisi chenye askari 66.

Neu Langenburg ilikuwa mji mkuu wa Mkoa wa Langenburg (takriban mikoa ya Mbeya na Songwe ya leo).

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waingereza walivamia Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kutoka Nyasaland (Malawi) na Wajerumani waliondoka mjini mwaka 1916; Waingereza walianzisha serikali yao ya kimkoa. Mwaka 1919 iliamuliwa katika Mkataba wa Versailles kwamba koloni la Kijerumani litawekwa mikononi mwa Waingereza waliobadilisha jina rasmi kuwa Tukuyu kuanzia mwaka 1920.

Tukuyu iko katika eneo lenye mvua nyingi na rutuba; ni kitovu cha kilimo cha chai nchini Tanzania.

Pia ni kitovu cha kilimo cha ndizi za kuiva: takribani mkoa wote wa Mbeya hutegemea ndizi kutoka Tukuyu.

Kwa miaka mingi Tukuyu ilikuwa na tatizo la mawasiliano mabaya kutokana na uharibifu wa barabara pamoja na matatizo ya kisiasa kati ya Malawi na Tanzania.

Siku hizi barabara ni nzuri kuelekea Malawi, pia kwenda Mbeya na Daressalaam.

Kuna nafasi nzuri ya utalii kwa sababu ya uzuri wa mazingira, lakini huduma bado ni chache.

Tukuyu ni eneo la Konde au Wanyakyusa. Mji wenyewe umekuwa kituo cha dayosisi ya Konde ya Walutheri pia dayosisi ya Wakatoliki. Makao makuu ya Moravian bado yako Rungwe misioni.

Tukuyu ina shule za msingi na sekondari, chuo cha ualimu na taasisi ya utafiti wa tiba, pia kuna ofisi za serikali ambayo ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Rungwe (halmashauri) au umma pamoja na mashirika binafsi au taasisi binafsi, pia kuna huduma za posta, smu, hospitali ya wilaya na huduma za benki mbalimbali.

  1. de:Langenburg ni pia mji mdogo katika kusini mwa Ujerumani; maana ya jina ni "boma ndefu"
Kata za Wilaya ya Rungwe - Mkoa wa Mbeya - Tanzania

Bagamoyo | Bujela | Bulyaga | Ibighi | Ikuti | Ilima | Iponjola | Isongole | Itagata | Kawetele | Kinyala | Kisiba | Kisondela | Kiwira | Kyimo | Lufingo | Lupepo | Makandana | Malindo | Masebe | Masoko | Masukulu | Matwebe | Mpuguso | Msasani | Ndanto | Nkunga | Suma | Swaya


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mbeya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Tukuyu kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.