Tim Walz
Timothy James Walz - (amezaliwa Aprili 6, 1964) ni mwanasiasa wa Marekani, mwalimu wa zamani, na mstaafu wa Jeshi la Marekani ambaye amekuwa Gavana wa 41 wa Minnesota tangu mwaka 2019.
Yeye alikuwa Mwakilishi katika Nyumba ya Wawakilishi ya Marekani kutoka 2007 hadi 2019. Walz ni mgombea mwenza wa Makamu wa Rais wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2024.
Tim Walz alizaliwa katika Jiji la West Point, Nebraska. Baada ya shule ya upili, alijiunga na Walinzi wa Kitaifa wa Marekani. Alihitimu kutoka Chuo cha Jimbo la Chadron katika Jimbo la Nebraska. Baada ya kumaliza chuo, Walz alihamia Minnesota mwaka 1996. Hapo awali, alikuwa mwalimu wa historia na mkufunzi wa mpira wa miguu wa Marekani kabla ya kuingia katika siasa na kufanya kazi katika Congress. Alichaguliwa kuwa mjumbe wa Nyumba ya Wawakilishi ya Marekani kutoka Minnesota.
Walz alihudumu katika Nyumba ya Wawakilishi ya Marekani kwa mihula mitano kabla ya kuchaguliwa kuwa Gavana wa Minnesota mwaka 2018.
Mnamo Agosti 6, 2024, Makamu wa Rais wa sasa, Kamala Harris, alimtangaza Walz kama mgombea mwenza katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2024.
Maisha ya Mapema
[hariri | hariri chanzo]Timothy James Walz alizaliwa Aprili 6, 1964, katika West Point, Nebraska, katika Hospitali ya Memorial. Mama yake, Darlene Rose Reiman, alikuwa mfanyakazi wa nyumbani na alikulia shambani. Baba yake, James Frederick Walz, alikuwa mwalimu na mwalimu mkuu ambaye alihudumu katika Jeshi la Marekani wakati wa Vita vya Korea, na alifanya kazi katika bucha ya familia akiwa mtoto. Walz ana asili ya Kijerumani, Kiswidi, na Kiireland.
Walz na kaka zake watatu walikulia katika kijiji kidogo kaskazini mwa Nebraska kinachoitwa Valentine. Shuleni, alicheza mpira wa miguu, mpira wa kikapu, na kushiriki katika riadha. Wakati wa kiangazi, Walz alifanya kazi kwenye shamba la familia. Alimaliza shule katika Shule ya Upili ya Butte mwaka 1982 katika darasa la wanafunzi 25, na baadaye akaenda Chadron, Nebraska, kwa masomo ya chuo kikuu.
Baba yake Walz alikufa Januari 1984[1], na familia yake ikapata changamoto za kifedha, hivyo Walz alihamia Texas na kujiunga na Walinzi wa Kitaifa. Baadaye alirudi Nebraska mwaka 1987 na kuanza shule katika Chuo cha Jimbo la Chadron. Mwaka 1989, alihitimu na shahada ya Sayansi katika Elimu ya Sayansi ya Jamii.
Kazi
[hariri | hariri chanzo]Mwalimu
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kuhitimu kutoka Chuo cha Jimbo la Chadron, Walz alifanya kazi kama mwalimu na mkufunzi huko Nebraska[2]. Wakati akifundisha, alikutana na mke wake, Gwen Whipple, mwalimu, na mwaka 1994 wawili hao walifunga ndoa. Miaka miwili baadaye, walihamia Mankato, Minnesota, jimbo la nyumbani kwa Gwen. Walz alifanya kazi kama mwalimu wa jiografia na mkufunzi wa mpira wa miguu katika Shule ya Upili ya Mankato West.
Nyumba la Wawakilishi la Marekani
[hariri | hariri chanzo]Tim Walz alihudumu kama mjumbe wa Nyumba ya Wawakilishi ya Marekani kutoka 2007 hadi 2019, akiwakilisha Wilaya ya 1 ya Minnesota. Walz alijikita katika kusaidia maveterani,[3] kilimo, na maendeleo ya vijijini. Alifanya kazi ili kuboresha huduma za afya kwa maveterani. Walz aliacha Nyumba ya Wawakilishi ili kugombea Ugavana wa Minnesota mwaka 2018.
Gavana
[hariri | hariri chanzo]Tim Walz alichaguliwa kuwa Gavana wa Minnesota na kuanza kutumikia Januari 2019. Katika uongozi wake kama gavana, alijikita katika masuala ya elimu, huduma za afya, na maendeleo ya miundombinu. Walz aliiongoza Minnesota wakati wa janga la COVID-19, akitekeleza mikakati kama barakoa na vikwazo vya biashara. Pia alijitolea kushughulikia masuala ya dhuluma za rangi kufuatia kifo cha George Floyd[4] mwaka 2020.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Tim Walz Opens Up About Losing His Father at 19 in Unreleased Conversation with Kamala Harris (Exclusive Clip)". People.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-12-09.
- ↑ "Tim Walz was named 'most inspiring teacher' — and other memories from former students". NBC News (kwa Kiingereza). 2024-08-06. Iliwekwa mnamo 2024-12-09.
- ↑ George Fabe Russell. "Tim Walz's military record: What to know about potential VP's National Guard service". USA TODAY (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2024-12-09.
- ↑ Alayna Treene, Michael Williams, Kristen Holmes (2024-08-07). "Trump in 2020 praised Tim Walz's handling of George Floyd protests | CNN Politics". CNN (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-12-09.
{{cite web}}
: CS1 maint: multiple names: authors list (link)