Nenda kwa yaliyomo

Marie Antoinette

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Marie Antoinette mnamo mwaka 1775, akiwa na umri wa miaka 20.

Marie Antoinette (2 Novemba 1755 - 16 Oktoba 1793) alikuwa malkia wa mwisho wa Ufaransa kabla ya ufalme kufutwa katika Mapinduzi ya Ufaransa. Alizaliwa kama Maria Antonia akiwa mtoto wa malkia wa Austria Maria Theresia. [1]

Aliolewa na mwana wa mfalme wa Ufaransa mnamo 1770, wakati alipokuwa na miaka 14. Miaka minne baada ya arusi mume wake alipata kuwa mfalme Louis XVI wa Ufaransa na Marie alikuwa malkia. Mwanzoni mume na mke hawakuwa karibu kati yao, wakawa na matatizo kuzaa watoto. [2] Baada ya miaka saba ya ndoa, Marie alimzaa binti, na baadaye alizaa watoto wengine watatu.

Watu wengi nchini Ufaransa hawakutaka nchi hiyo iwe na malkia kutoka Austria. Ushirikiano wa Ufaransa na Austria haukupendwa maana nchi hizo mbili zilikuwa maadui hadi mwaka 1756, na wengi waliona Austria iliwahi kusababisha kushindwa kwa Ufaransa katika Vita vya Miaka Saba.

Wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa malkia huyu alilaumiwa kama ishara ya mfumo wa ufalme katika Ufaransa. Kulikuwa na uvumi kwamba alitumia pesa nyingi, alikuwa na wapenzi na aliunga mkono maadui wa Ufaransa. Kulikuwa na uvumi kwamba wakati maskini wa Paris waliaandamana na kulalamikia njaa wakidai hawana mkate, Marie Antoinette alijibu "Wacha wale keki kama hawana mkate" lakini hakuna ushahidi kuwa alisema hayo kweli.

Alishiriki katika mipango ya familia ya kifalme kutoroka Paris mnamo 1791. Hii ilisababisha watu wengi kufikiria kwamba familia ya kifalme, haswa Marie Antoinette, walikuwa wakipanga njama dhidi ya mapinduzi na kushirikiana na serikali za kigeni kuipindua serikali iliyochaguliwa.

Familia ya kifalme ilikamatwa mnamo 1792 na ufalme ulifutwa. Malkia aliuawa kwa kukatwa kichwa mnamo 1793, miezi tisa baada ya mumewe kuuawa.

  1. "Marie-Antoinette (queen of France) -- Britannica Online Encyclopedia". britannica.com. Iliwekwa mnamo 23 Julai 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. "Marie Antoinette — FactMonster.com". factmonster.com. Iliwekwa mnamo 23 Julai 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]