Kitunda (sataranji)
Kitunda (Kiing. pawn) ni kete kwenye mchezo wa shataranji ambayo inapatikana mara nane kila upande. Inajaza mstari wa mbele katika mpangilio wa jeshi la shataranji, hivyo inawakilisha askari wa kawaida. Hutazamwa kama kete dhaifu . Hata hivyo mchezaji hodari anaweza kushinda akijua kutumia vitunda vyake kwa busara. Kama kete inafika mstari wa mwisho upande wa kinyume wa ubao inabadilika kuwa kete ya juu kama malkia au ngome.
Nafasi ya kitunda ni kama askari wa mguu katika jeshi; maafisa wa juu na askari wenye silaha za pekee wanakaa nyuma yake.
Mwanzo wa mchezo
Vitunda hukaa kwenye mstari wa pili kila upande. Hii inafanana na utaratibu wa mapigano katika jeshi za kale ambako mara nyingi askari wa kawaida walikuwa mstari wa mbele na nyuma yao mfalme, maafisa au majenerali, wanajeshi wenye farasi, wapiga mishale au mashine za kurusha mikuki walikaa nyuma yao.
Mstari wa vitunda unalinda kete za juu zilizopo nyuma lakini unazibana pia kwa sababu ni farasi pekee inayoweza kuruka juu ya kete nyingine.
Kwa hiyo namna ya kufungua mstari wa vitunda ni kipindi cha kwanza katika mchezo wa shataranji.
Mwendo
Kitunda kina mwendo wa pekee. Tofauti na kete za juu hutembea mbele tu hakiwezi kurudi nyuma. Mwendo ni hatua za mraba 1-1 isipokuwa hatua ya kwanza inayoweza kuwa mraba 1 au miraba miwili.
Kama kitunda kinafikia mstari wa mwisho wa ubao kinaondolewa na kubadilishwa kwa kete nyingine yoyote isipokuwa kete kuu ya shaha. Badiliko la kitunda huwa ni uamuzi wa mchezaji wake.
Kukamata
Kitunda hukamata kete za adui kama ziko upande wa kushoto au kulia wa mraba mbele yake. Hakina uwezo wa kukamata kete zilizopo mbele yake moja kwa moja.
Jambo la pekee ni nafasi ya "kukamata kwa kupita". Hii inaweza kutokea kama kitunda kinakanyaga hatua kubwa ya kwanza kwa umbali wa miraba miwili. Kama kinapita mraba unaotishiwa na kitunda cha adui kinaweza kuondolewa. Sababu yake ni ya kwamba kama kingetembea hatua ndogo ya mraba 1 tu adui kingekuwa na nafasi ya kuishambulia. Kama mchezaji adui anaamua hivyo anaweza kuondoa kitunda na kuweka chake kwenye mraba uliotishiwa naye awali.