Jumba la Sultani, Zanzibar
Jumba la Sultani ni jengo la kihistoria kwenye Mji Mkongwe wa Zanzibar. Linapatikana kando ya mtaa wa Mizingani likitizamana na bahari, na Jumba la Maajabu lililoko jirani. Lilikuwa makazi ya Sultani wa Zanzibar kuanzia mwaka 1911 hadi mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964. Leo hii ni jumba la makumbusho[1].
Jumba la ukingoni
[hariri | hariri chanzo]Jengo hili lilijengwa mahali pa jumba lililotangulia kuwa makazi ya masultani. Jumba hilo lilijulikana kwa jina la Kiarabu "Bait as-Sahel" (Kiarabu: بيت الساحل bait as-sahel, au "Jumba la Ukingoni"). Bait as Sahel ilijengwa kwenye miaka 1827-1834 kwa ajili ya Sultani Said[2]. Mpelelezi Mwingereza Richard Burton aliiona mwaka 1872 akaandika lilikuwa jengo refu la ghorofa mbili, lenye kuta nyeupe na paa la vigae vya rangi ya kijani[3].
Burton aliandika kwamba mizinga 8 ilikaa mbele ya jumba kando ya bahari[4]. Kuwepo kwa mizinga hiyo moja kwa moja mbele ya jengo kulisababisha pia kuharibika kwa jumba katika vita ya Uingereza dhidi Zanzibar mwaka 1896 ambako manowari za Waingereza walilenga kwanza kunyamazisha sehemu zote zenye mizinga na askari.
Jumba jipya baada ya 1896
[hariri | hariri chanzo]Nyumba mpya ilijengwa mahali pa mtangulizi wake kwa kutumia ukuta uliokuwa umebaki. Jumba la Sultani ni jengo lenye ghorofa tatu na kuta nyeupe. Mwanzoni lilikaliwa na familia ya Sultani, na mnamo mwaka 1911sultani mpya Khalifa bin Harub aliingia hapa akikaa hadi kifo chake mwaka 1960. Mwanawe sultani Abdullah bin Khalifa aliishi pia hapa hadi mapinduzi ya mwaka 1964.
Baadaye jina likabadilishwa kuwa Jumba la Wananchi (People's Palace) nalo likatumiwa kama ofisi za serikali. Mwaka 1994 likabadilishwa kuwa jumba la makumbusho.
Jumba la makumbusho
[hariri | hariri chanzo]Ghorofa moja la jumba la makumbusho limewekwa wakfu kwa Sultani Khalifa bin Harub; nyingine kwa Sayyida Salme, anayejulikana kama Emily Ruete, aliyekuwa binti mmojawapo wa sultani aliyetoroka na mpenzi wake Mjerumani akawa mke wake na kuishi Ulaya. Maonyesho ni pamoja na vitabu na barua zake, nguo na vifaa vya maisha ya kila siku. Vitu kadhaa vya fenicha na mali nyingine kwa familia ya sultani viko kwenye maonyesho ili kuwapa wageni picha ya maisha ya kifalme Zanzibar wakati wa karne ya 19.[5][6][7][8]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ The palace museum, tovuti ya Bradt travel guide Zanzibar, ISBN 978-1841622880
- ↑ Sultan's Palace Zanzibar, Tanzania, tovuti ya archnet (elimu ya usanifu wa jamii za Kiislamu ínayoendeshwa na Taasisi ya Agha Khan), iliangaliwa Machi 2021
- ↑ Richard F. Burton: Zanzibar; City, Island, And Coast, Vol. I., uk 256, London 1872. (online via archive.org)
- ↑ "The palace lies east of, and close to, the fort. It is fronted by a wharf, and defended by a stuccoed platform mounting eight or nine brass guns en barbette, intended more for show than use. " (Burton 1872)
- ↑ "The Palace Museum". Zanzibar Travel. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-04-21. Iliwekwa mnamo Novemba 29, 2018.
{{cite web}}
: More than one of|accessdate=
na|access-date=
specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Palace Museum". Lonely Planet. Iliwekwa mnamo Novemba 29, 2018.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "The palace museum". Zanzibar travel guide. Iliwekwa mnamo Novemba 29, 2018.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Museums - Palace Museum". Zanzibar Tourism. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-04-11. Iliwekwa mnamo Novemba 29, 2018.
{{cite web}}
: More than one of|accessdate=
na|access-date=
specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)