Benjamin Disraeli
Benjamin Disraeli (21 Desemba 1804 – 19 Aprili 1881) alikuwa mwanasiasa wa Uingereza na waziri mkuu wa Ufalme wa Muungano mwaka 1868 tena kati ya miaka 1874 hadi 1880. Aliwahi kuwa waziri wa fedha na uchumi (Chancellor of the Exchequer) mnamo 1852, katika miaka 1858-1859 na 1866-1868. Alikuwa mwanachama cha Chama cha Conservative. Mpinzani wake mkuu alikuwa William Ewart Gladstone. Disraeli pia alikuwa mwandishi wa riwaya na wasifu .
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Disraeli alizaliwa katika familia ya Kiyahudi iliyogeukia Ukristo wa Kianglikana. Yeye ndiye waziri mkuu pekee mwenye asili ya Kiyahudi katika historia ya Uingereza. [1]
Disraeli alibuni wazo la uhafidhina wa "Taifa Moja", lililoundwa kuvuta matabaka yote katika jamii. Uhafidhina wake ulizingatia pia mahitaji ya matabaka ya chini na kutafuta suluhisho bila kujali itikadi. Disraeli alilenga kuvuta watu wa tabaka jipya la wafanyakazi wa viwandani ili wakubali mfumo wa jamii na siasa yake. Kwa njia hiyo alitaka kupunguza migawanyiko katika jamii iliyoanza kuzidi wakati wake.
Msimamo wake ulipingwa na Waliberali (au "Whigs") waliotetea maslahi ya wasomi wa mijini na watu wenye pesa na wenye elimu nzuri.
Disraeli alibadilisha siasa ya Chama cha Conservative kuunga mkono upanuzi wa Milki ya Uingereza na makoloni yake, pamoja na gharama kwa matumizi ya jeshi zilizokuja nayo. Disraeli alihisi kwamba siasa hiyo itakubaliwa na watu wengi.
Mafanikio ya Disraeli
[hariri | hariri chanzo]Katika kipindi kifupi cha kwanza cha Disraeli kama waziri mkuu, serikali yake ilipitisha sheria ambazo ziliungwa mkono na watu wengi. Alikomesha hukumu ya kunyongwa hadharani. Alipitisha sheria ya kubana matumizi ya rushwa wakati wa uchaguzi na kuwapa wanaume wote wenye familia haki ya kupiga kura bila kujali utajiri. Serikali yake ilinunua makampuni ya telegrafu na kuweka huduma hiyo mikononi mwa posta. Kulikuwa na mabadiliko ya sheria ya shule, mfumo wa kisheria wa Uskoti, na sheria za reli. [2]
Mwaka 1878 serikali ya Disraeli ilipitisha sheria iliyozuia kazi ya watoto wadogo na kuweka mipaka kwa saa za kazi. Sheria nyingine iliruhusu wafanyakazi kuandamana mbele ya viwanda na kushtaki waajiri mahakamani.
Katika siasa ya nje Disraeli alimpa Malkia Viktoria cheo cha Kaizari wa Uhindi.
Wakati wa utawala wake, jeshi la Uingereza lilishinda Afghanistan na vita dhidi ya Wazulu chini ya mfalme Cetshwayo.
Disraeli alifaulu kununua Mfereji wa Suez kwa Ufalme wa Muungano. Awali ulikuwa mali ya kampuni ya binafsi. Mfereji huo ulikuwa muhimu kwa Uingereza kwa sababu ulikuwa njia fupi kati ya Uingereza na Uhindi ya Kiingereza. Alitumia nafasi ya Mkutano wa Berlin wa mwaka 1878 kupata utawala wa Uingereza juu ya kisiwa cha Kupro kilichokuwa muhimu kama kituo cha jeshi la majini la kulinda Mfereji wa Suez.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Benjamin Disraeli". Kigezo:Ill. 2011. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 26 Mei 2012. Iliwekwa mnamo 9 Aprili 2011.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Blake, Robert (1966). Disraeli. St Martin's Press. uk. 495.