Sirili wa Aleksandria
Sirili wa Aleksandria (Theodosios, Misri, 370 hivi - Aleksandria wa Misri, 444) alikuwa Patriarki wa Aleksandria, Misri (kuanzia tarehe 18 Oktoba 412 hadi kifo chake) na mwanateolojia.
Alishiriki mabishano ya karne ya 4 kuhusu imani juu ya Yesu Kristo akitetea dogma ya umoja wa Nafsi yake ya Kimungu kwa kutegemea daima mapokeo ya Kanisa na mamlaka ya mababu waliomtangulia, hasa Atanasi. Kwa ajili hiyo aliitwa “mlinzi wa usahihi” (wa imani).
Mtu wa hamaki na mwenye uwezo wa kufanikisha mambo yoyote, ni maarufu hasa kwa kumkomesha Nestori wa Konstantinopoli katika Mtaguso wa Efeso (431) uliomtangaza Bikira Maria kuwa Mama wa Mungu. Vilevile alikuwa mkali dhidi ya wazushi wengine, Wayahudi na Wapagani, na hata dhidi ya Yohane Krisostomo.
Kwa kweli ulikuwa wakati mgumu ambapo ukweli uliweza kushinda uzushi kutokana tu na wachungaji wenye msimamo mkali katika kulinda kundi la waamini walilokabidhiwa[1].
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1883 Papa Leo XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Juni[2].
Asili na ujana
[hariri | hariri chanzo]Sirili alizaliwa katika kijiji cha Theodosios, Misri, karibu na El-Mahalla El-Kubra ya leo, mwaka 370 hivi.
Miaka michache baadaye mjomba wake Theofilo wa Aleksandria alipata kuwa Patriarki wa Aleksandria. Mama yake alibaki karibu na kaka yake, hivyo mtoto alipata malezi mazuri na elimu sanifu ya wakati ule: lugha (390-392), fasihi (393-397) hatimaye teolojia na Biblia (398-402).
Mwaka 403 alitumwa Konstantinopoli kushiriki “Sinodi ya Mwaloni” iliyomuondosha Patriarki wa mji huo, Yohane Krisostomo, na kulipatia Kanisa la Aleksandria kwa mpigo mmoja ushindi dhidi ya wapinzani wake wote wawili, Antiokia na Konstantinopoli.
Patriarki
[hariri | hariri chanzo]Theofilos alipofariki tarehe 15 Oktoba 412, kisha kuongoza Kanisa la Misri kwa nguvu sana miaka 27, Sirili alichaguliwa Patriarki wa Aleksandria baada ya siku tatu.
Akitumia mamlaka yake katika jiji hilo lenye ushindani na fujo, alifaulu kufunga makanisa ya Wanovasyani na kufukuza Wayahudi wengi.
Pia alitetea kwa nguvu msimamo wa teolojia ya Shule ya Aleksandria dhidi ya ile ya Antiokia na haki ya Kanisa la Aleksandria kuwa la pili duniani (baada ya Kanisa la Roma) na la kwanza Mashariki kote dhidi ya Kanisa la Konstantinopoli lililopendelewa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381). Hata hivyo mwaka 417 au 418 alikubali kurudhisha ushirika nalo ulilovunjika mwaka 406, Yohane Krisostomo alipofukuzwa moja kwa moja.
Ushindani huo ulikomaa tena mwaka 428 alipochaguliwa kuwa Patriarki wa Konstantinopoli mmonaki mkali Nestori, mwenyeji wa Antiokia kama Yohane huyo.
Sirili alipata nguvu dhidi yake pale ambapo padri wa Antiokia alianza kuhubiri huko Konstantinopoli kwamba Bikira Maria hastahili kuitwa "Mama wa Mungu," ila “Mama wa Kristo". Waamini walipomshtaki kwa Nestori, huyo akamtetea kwa msingi wa teolojia ya Antiokia iliyosisitiza ukweli wa ubinadamu wa Yesu.
Kwenye Pasaka 429, Sirili aliwaandikia wamonaki barua dhidi ya Nestori ikitetea teolojia ya Aleksandria iliyosisitiza ukweli wa umungu wa Yesu. Nakala ilipofika Konstantinopoli, Nestori alihubiri dhidi yake. Ndio mwanzo wa mawasiliano makali kwa njia ya barua yaliyozidisha ushindani kati ya wanateolojia wa miji hiyo miwili.
Hali hiyo iliwafanya wote wawili wamuombe Papa Selestini I aingilie kati. Hapo sinodi iliyofanyika Roma mwaka 430 ilikubali hoja za Sirili dhidi ya Nestori.
Ili kumaliza mabishano hayo ya hatari, Kaisari Theodosius II aliitisha mtaguso mkuu huko Efeso, palipokuwa upande wa Sirili, ambaye alifungua na kufunga Mtaguso wa Efeso (431) kabla Nestori na wafuasi wake hawajafika; hivyo, mtaguso uliagiza Nestori aondoshwe madarakani na kupelekwa uhamishoni.
Lakini Yohane wa Antiokia na wengine wa upande wa Nestori walipofika Efeso siku nne baadaye, walifanya mtaguso wa kwao wakimhukumu Sirili kuwa mzushi, wakidai aondoshwe madarakani.
Hapo Theodosius II aliamua kuwaondosha na kuwafunga wote wawili; hivyo alimkamata Sirili, lakini huyo alikimbilia Misri akaleta fujo hadi kwenye ikulu, hata Kaisari alikubali kumfukuza Nestori arudi monasterini Antiokia.
Matukio hayo ndiyo chanzo cha farakano la Waashuru linalodumu hadi leo.
Ili azidi kudhoofisha uzushi huo, Sirili alipata itolewe hukumu dhidi ya Teodori wa Mopsuestia, aliyewahi kuwa mwalimu wa Nestori, lakini baadaye mwenyewe akailaumu hukumu hiyo.
Hivyo, mwaka 433 alikubali kuafikiana na wafuasi wa teolojia ya Antiokia na kupatana nao.
Sirili aliandika sana: kwanza dhidi ya Waario, ila baada ya mwaka 428 alilenga Unestori. Aliandika vitabu mbalimbali vya ufafanuzi wa Agano la Kale (Torati nzima, Kitabu cha Isaya na Zaburi) na Agano Jipya (Injili ya Yohane na ile ya Luka) na vya teolojia, pamoja na nyaraka rasmi kwa ajili ya Pasaka, hotuba na barua. Vitabu hivyo vilienea mapema wakati wa maisha yake hata katika tafsiri mbalimbali.
Katika kutetea msimamo wake, pamoja na shuhuda za Biblia, alitumia kuliko wote waliomtangulia zile za mababu wa Kanisa, na hata hoja za akili.
Pamoja na hayo, aliona imani ya Taifa la Mungu, yaani waamini wa kawaida, kama tokeo la mapokeo na hakika ya mafundisho sahihi: “Ni lazima tufafanue kwa watu mafundisho na maelezo ya imani namna isiyolaumika kabisa, na tukumbuke kwamba anayekwaza hata mmoja tu kati ya wadogo wanaomuamini Kristo atapatwa na adhabu isiyovumilika”.
Mwanzoni alifundisha juu ya Yesu kwa kumuiga Atanasi, lakini alipozidi kubishana na Nestori alilazimika kutumia misamiati mipya iliyoelekea kukiri uwemo wa hali mbili ndani ya Kristo. Kwa hiyo katika barua yake ya pili kwa Nestori, iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451), aliweka wazi: “Hivyo sisi tunatamka kwamba hali zilizounganika katika umoja wa kweli ni tofauti, bali kutoka zote mbili amepatikana Kristo na Mwana mmoja tu; si kwa sababu tofauti za hali hizo zimefutwa na umoja wake, bali kwa sababu umungu na ubinadamu, vilivyounganika katika umoja usiosemeka wala kufafanulika, vimetupatia Bwana, Kristo na Mwana mmoja”.
Katika barua nyingine aliandika, “Mwana ni mmoja tu, Bwana Yesu Kristo ni mmoja tu, kabla ya umwilisho wake na baada ya umwilisho vilevile. Kwa kuwa Neno aliyezaliwa na Mungu Baba hakuwa Mwana mmoja na aliyezaliwa na Bikira Maria mwingine; bali tunasadiki kwamba yuleyule aliyezaliwa kabla ya nyakati ndiye aliyezaliwa pia kimwili na mwanamke”.
Sirili alifariki Aleksandria mwaka 444 hivi, lakini mashindano yaliendelea hadi Mtaguso wa Kalsedonia na mbele zaidi.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
- Mababu wa Kanisa
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- McGuckin, John A. St. Cyril of Alexandria and the Christological Controversy. Crestwood, NY: St. Vladimir’s Seminary Press, 2004. ISBN 0-88141-259-7
- Wessel, Susan. Cyril of Alexandria and the Nestorian Controversy:The Making of a Saint and a Heretic. Oxford 2004. ISBN 0-19-926846-0
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Maandishi yake
[hariri | hariri chanzo]- Maandishi yake yote katika magombo kumi (PG 68-77) Patrologia Graeca ya Jacques Paul Migne pamoja na faharasa
- Becoming Temples of God (in Greek original and English
- Second Epistle of Cyril to Nestorius Ilihifadhiwa 12 Septemba 2006 kwenye Wayback Machine.
- Third Epistle of Cyril to Nestorius (containing the twelve anathemas) Ilihifadhiwa 4 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- Formula of Reunion: In Brief (A summation of the reunion between Cyril and John of Antioch) Ilihifadhiwa 10 Septemba 2006 kwenye Wayback Machine.
- The 'Formula of Reunion' between Cyril and John of Antioch Ilihifadhiwa 20 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- Five tomes against Nestorius (Adversus Nestorii blasphemias)
- That Christ is One (Quod unus sit Christus)
- Scholia on the incarnation of the Only-Begotten (Scholia de incarnatione Unigeniti)
- Against Diodore of Tarsus and Theodore of Mopsuestia (fragments)
- Against the synousiasts (fragments)
- Commentary on the Gospel of Luke
- Commentary on the Gospel of John
- Against Julian the Apostate
Vinginevyo
[hariri | hariri chanzo]- [1]
- "The Life and Writings of Cyril of Alexandria" Ilihifadhiwa 11 Oktoba 2008 kwenye Wayback Machine. as it relates to the Christological Controversy
- Early Church Fathers Includes text written by Cyril of Alexandria
- St Cyril the Archbishop of Alexandria Eastern Orthodox icon and synaxarion
Kwa Kiswahili
[hariri | hariri chanzo]- Masomo ya Breviari - ed. Ndanda Mission Press - Ndanda 1978
- Maisha ya Watakatifu – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1989
- MAURICE SOSELEJE – Kalendari Yetu Maisha ya Watakatifu – Toleo la Pili – ed. Benedictine Publications Ndanda-Peramiho – Ndanda 1986 - ISBN 9976-63-112-X