Kipindi cha kawaida
Mwaka wa liturujia |
---|
Magharibi |
Mashariki |
Kipindi cha kawaida ni kipindi cha liturujia katika mwaka wa Kanisa. Maelezo yafuatayo yanatokana na utaratibu wa Kanisa Katoliki, lakini kwa kiasi kikubwa yanahusu pia madhehebu mengine, kama vile Anglikana.
Baada ya kila mfululizo wa vipindi viwili vya pekee (Majilio na Noeli, Kwaresima na Pasaka), tunarudia Kipindi cha Kawaida, kinachochukua muda mrefu kuliko vingine vyote pamoja. Hapo sherehe kuu hizo zinapisha maadhimisho manyofu lakini motomoto: ndio wakati murua wa kung’amua upya utajiri wote wa Dominika kama siku ya kukutana na Bwana mfufuka kila wiki ili kwenda ulimwenguni kote kutangaza ushindi wake; kama siku ambayo inaendesha mwaka mzima ikitukumbusha kwa nguvu tunavyohitaji uwiano mzuri wa kazi na pumziko; kama siku inayodai tusimamishe shughuli zetu nyingi za kujitafutia mapato ili kupata nafasi ya kuadhimisha bure upendo wa Mungu anayetuokoa; kama siku inayokumbusha mwanzo wa uumbaji wa ulimwengu, mwanzo wa uumbaji mpya katika ufufuko wa Yesu na hatua nyingine ya safari yetu duniani.
Ekaristi ya Dominika ndiyo chakula cha safari hiyo kinachotutia nguvu mpya daima tuzidi kumuelea Bwana. Katika kutimiza agizo lake la kufanya ukumbusho wake, tunapokea upya toleo kamili la nafsi yake na tunakubali kujitoa kama alivyojitoa kwetu kwa upendo upeo. Si amri ya Kanisa tu, bali ni haja ya moyo wetu. Ndiyo sababu mwaka 304 wafiadini wa Abitene walikiri mbele ya watesi wao: “Hatuwezi kuishi bila ya Siku ya Bwana”. Ni siku ya Kanisa, yaani mkusanyiko: viungo vyake vikikutana, mwili huo wa Bwana unatimia na kudhihirika mbele ya wote. Ni siku ya furaha na amani ambayo inaambukiza kuanzia yeye na inazidi kutufanya ndugu.
Ikiwa vipindi vya pekee vya mwaka vinaadhimisha matukio makuu ya Kristo, hiki cha kawaida kinaadhimisha ushiriki wetu katika fumbo lake ndani ya Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kristo ameshatimiza kazi ya ukombozi, lakini upande mwingine mambo bado, hadi huo uwafikie watu wote, na kila mmoja apate kuwa mwana huru wa Mungu ndani ya Kanisa, mwili wa Kristo unaoendelea kuishi na kutenda ulimwenguni karne hadi karne. Moyo wa Yesu unazidi kudunda katika kifua cha Kanisa, ambalo ni Kristo ndani yetu, anayezidi kuenea duniani kote. Humo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu neno lake linazidi kuwa hai na kupiga mbio, huku Kanisa likilifafanua na kulitekeleza katika mazingira mapya daima.
Kanisa linaalika wanae wakomae katika maisha ya Kiroho kwa kushuka vilele vya Pasaka na Noeli ili kufaidika na malisho mapana ya Kipindi cha Kawaida kwa kutafakari katika mwanga wa ufufuko wake yale yote aliyoyasema na wa kutekeleza yale yote yaliyoyaagiza. Kuadhimisha na kuishi fumbo la Kristo katika hali ya kawaida ni kukubali uwajibikaji mwaminifu wa kila siku ili kumtambua kama Mwalimu anayeongozana nasi katika safari ya maisha, na hivyo kung’amua kwamba Mungu anatuinamia na kutuokoa katika maisha yetu ya kila siku. Ndiyo sababu kipindi hicho kinakazia pia utume wa Kiinjili wa Kanisa ulimwenguni na wajibu wa kuutimiza.
Kipindi hiki ni cha kawaida kwa maana kinaadhimisha fumbo la Kristo kwa jumla, kufuatana na Dominika na siku nyingine za wiki. Kwa ajili hiyo tunasaidiwa na somo la karibu mfululizo la mojawapo kati ya Injili Ndugu ili kutafakari maisha na mafundisho ya Yesu kadiri ya kila mwinjili (kwa zamu: Marko, Mathayo halafu Luka siku za kazi; Mathayo mwaka A, Marko mwaka B na Luka mwaka C siku za Jumapili). Humo, mbali na mafumbo makuu tuliyoadhimisha katika vipindi vya pekee vya mwaka wa Kanisa, tunakutana na Yesu katika maneno na matendo yake ya kawaida zaidi, katika mafungamano yake na watu, kuanzia urafiki na wanafunzi wake hadi malezi kwa watu wote. Lengo si tu kukumbuka alivyofanya wakati ule, bali hasa kutambua anavyozidi kufanya kila leo kupitia Kanisa lake.
Kwa Kiingereza, kipindi hicho kinaitwa “Ordinary Time”, yaani “muda ambao unafuata utaratibu”, hivyo unalingana kabisa na mpango wa upendo wa Mungu na unaleta amani, ambao ni “utulivu wa utaratibu” (Thoma wa Akwino). Muda huo una pande mbili: kuanzia siku inayofuata Ubatizo wa Bwana hadi siku inayotangulia Jumatano ya Majivu, halafu kuanzia Jumatatu baada ya Pentekoste hadi mchana wa Jumamosi ya tarehe yanapoanza kuadhimishwa Majilio. Katikati ya hizo sehemu mbili za kipindi cha kawaida, mfululizo wa Pasaka unaadhimisha yale Yesu aliyoyafanya katika maisha yake ya hadhara (Kwaresima: kuanzia vishawishi jangwani hadi kifo msalabani) na ushindi wake kamili (Pasaka: kufufuka, kupaa na kumtuma Roho Mtakatifu).
Kwa Kilatini siku ya kazi inaitwa na Kanisa "feria" (wingi wake unamaanisha likizo, starehe), kwa sababu kwa Mkristo kila siku ni sikukuu. Hivyo hata Kipindi cha Kawaida ni cha pekee, kwa kuwa maisha yake yamegeuzwa na kufichika pamoja na Kristo ndani ya Mungu. Kwa mtazamo wa imani hata muda wa kawaida unaweza ukawa na utajiri mkubwa ajabu.
Mapokeo ya Roma yanaadhimisha wakati huo sherehe kadhaa (Utatu Mtakatifu, Mwili na Damu ya Kristo, Moyo Mtakatifu wa Yesu), lakini hizo haziadhimishi tukio fulani, bali ukweli uliobainishwa na mitaguso mikuu kuhusu nafsi tatu za Kimungu, uwepo wa Yesu katika Kanisa kupitia maumbo ya mkate na divai, upendo wake unaowakilishwa na moyo uliotobolewa ili utokwe na chemchemi za neema zinazosababisha Kanisa lizaliwe na sakramenti. Dominika ya mwisho inamshangilia Kristo kama Mfalme wa ulimwengu atakavyodhihirika siku ya kiyama, na hivyo inaturudisha kwenye mada ya kwanza ya Majilio, mwanzo wa mwaka mpya wa Kanisa.
Pia sikukuu nyingi za watakatifu zinapatikana wakati huo, bila ya kuzuiwa na vipindi vya pekee: k.mf. Yohane Mbatizaji, Petro na Paulo, Malaika Wakuu, na hasa Mama Maria. Hata ndani mwao tunazidi kumuadhimisha Kristo, kwa kuwa ni mashahidi wa ushindi wake dhidi ya dhambi na ni ufafanuzi hai wa utakatifu wake unaoendelea kudhihirika ndani ya Kanisa linalohuishwa na Roho Mtakatifu.
Mwishoni mwa kipindi hicho, mwezi Novemba unaadhimishwa Kanisa Shindi la mbinguni (tarehe 1), Kanisa Toharani (tarehe 2) na Kanisa Safiri duniani (tarehe 9). Ni kwamba katika wiki 33 au 34 za Kipindi cha Kawaida (kati yake 5 hadi 9 zinatangulia Kwaresima, halafu 23 hadi 28 zinafuata Pentekoste), Kanisa likihiji kati ya dhuluma za ulimwengu na faraja za Mungu, linazidi kutangaza mateso na mauti ya Bwana mpaka arudi, likielekea uzima wa milele. Wakati huo ufalme wa Mungu unazidi kujengeka na kukua taratibu kuelekea utimilifu wake.
Ndiyo maana rangi ni ya kijani, ambayo tangu zamani inahusishwa na uzima mpya na ustawi. Katika Kiebrania jina la rangi hiyo lina maana ya “kijana” pia. Katika Ukristo, rangi hiyo inamaanisha uzima mpya unaotumainiwa katika ufufuko na ule wa Kanisa baada ya Roho Mtakatifu kulijaza Pentekoste ili azidi kummwilisha Kristo katika viungo vyake.