Nenda kwa yaliyomo

Hastings Banda

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hastings Kamuzu Banda

Sanamu ya Banda

Rais wa kanza wa Malawi
Muda wa Utawala
6 Julai 1966 – 24 Mei 1994
mtangulizi Elizabeth II
malkia wa Milki ya Britania
aliyemfuata Bakili Muluzi

Waziri Mkuu wa Malawi
Muda wa Utawala
6 Julai 1964 – 6 Julai 1966
Governor–General Sir Glyn Smallwood Jones
mtangulizi (wa kwanza)
aliyemfuata mwenyewe kama rais

tarehe ya kuzaliwa Machi au Aprili 1898
Kasungu, eneo lindwa la British Central Africa
tarehe ya kufa 25 Novemba 1997 (umri takriban miaka 99)
Afrika Kusini
chama Malawi Congress Party
dini Presbiteri

Hastings Kamuzu Banda (1898 - 25 Novemba, 1997) alikuwa daktari na mwanasiasa aliyeendelea kuwa kiongozi, rais na dikteta wa Malawi tangu mwaka 1961 hadi 1994.

Mtoto na kijana

[hariri | hariri chanzo]

Kamuzu Banda alizaliwa karibu na Kasungu, Malawi iliyokuwa wakati ule sehemu ya eneo lindwa la Afrika ya Kati ya Kiingereza (baadaye Nyasaland). Wazazi walikuwa Mphonongo Banda na Akupingamnyama Phiri. Tarehe ya kuzaliwa haijulikani ilhali wakati ule hakukuwa na utaratibu wa kuandikisha watu. Alikubali baadaye matokeo ya utafiti wa rafiki kutoka Marekani aliyekadiria ya kwamba alizaliwa mnamo Machi au Aprili 1898.[1][8]

Jina lake Kamuzu lamaanisha "mzizi mdogo" kwa sababu alizaliwa baada ya mama yake kutumia dawa ya mitishamba kwa kusudi la kupata mimba [2]. Banda lilikuwa jina la baba yake, na jina la Hastings alijiongezea baada ya kubatizwa kwa heshima ya mmisionari mmoja kutoka Uskoti aliyependwa naye.

Mnamo 19151916 Banda aliondoka kwao akisafiri kwanza Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) na mwaka 1917 aliendelea hadi Johannesburg katika Afrika Kusini alipopata kazi kwenye migodi ya Witwatersrand. Wakati ule alijiunga na kanisa la African Methodist Episcopal Church na hapo askofu wa kanisa lile aliona kipaji chake akamkubali kwa masomo. Mwaka 1925 Banda aliondoka kwenda Marekani.

Masomo Marekani na Uingereza

[hariri | hariri chanzo]
Dr Banda kijana

Alisoma kwa miaka 3 kwenye Wilberforce Institute iliyokuwa chuo cha Kanisa la A.M.E. akaendelea kwa miaka 2 Bloomington, Indiana, kwa maandalizi ya masomo ya tiba.

Kutoka huko alikaribishwa kuhamia Chuo Kikuu cha Chicago alipokuwa msaidizi wa profesa wa lugha aliyetunga kamusi na sarufi ya lugha ya Chichewa, akajisomea historia akamaliza bachelor. Kwa msaada wa wafadhili aliweza kuendelea kusoma elimu ya tiba kwenye Meharry Medical College huko Tennessee alipomaliza mwaka 1937.

Kwa kurudi kwao kama tabibu alihitaji mtihani kufuatana na mfumo wa Uingereza, hivyo alihamia Chuo Kikuu cha Edinburgh alipopokea vyeti vya tiba na upasuaji mwaka 1941. Alianza kufanya kazi ya tabibu huko Uingereza katika miaka 1941-1951.

Siasa na uhuru

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1946 Banda aliombwa kuhudhuria mkutano wa Pan-African Congress mjini Manchester (15-19 Oktoba 1945) kama mwakilishi wa Nyasaland. Tangu mkutano huu alishiriki katika siasa. Alijulikana kwake Nyasaland kama Mwafrika mwenye elimu ya juu zaidi kutoka nchi yake.

Baada ya miaka kadhaa huko Gold Coast (Ghana) aliombwa na wanasiasa Waafrika arudi Nyasaland akafika mwaka 1958. Kwenye mkutano wa chama cha Nyasaland African Congress (NAC) alichaguliwa mara moja kuwa kiongozi. Alikuta nchi yake Nyasaland kuwa sehemu ya Shirikisho la Afrika ya Kati ambako walowezi wa Rhodesia ya Kusini walikuwa na athira kubwa na kuendeleza ubaguzi wa rangi. Banda alipinga kuwepo kwa shirikisho hili.

Alizunguka nchini akiwahutubia watu na kudai uhuru wa Unyasa[3]. Kutokana na muda mrefu wa kukaa mbali na nyumbani alihitaji wafasiri maana alishindwa mwanzoni kutumia Lugha mama yake.

Wananchi wengi walimfuata na hadi mwaka 1959 harakati ya uhuru iliongezeka kiasi kwamba serikali ilitangaza hali ya dharura. Banda alikamatwa na kuwekwa jela kwa miezi 11. Chama cha NAC kilipigwa marufuku lakini wanachama nje ya gereza waliunda badala yake chama cha "Malawi Congress Party" (MCP) na kumtangaza Banda kuwa mwenyekiti ingawa bado alikaa jela.

Wakati huo wanasiasa katika Uingereza walianza kukazia uhuru kwa makoloni yake. Kwa hiyo Banda aliachishwa gerezani kwenye Aprili 1960 akapelekwa London kwa majadiliano kuhusu uhuru wa nchi.

Baada ya uchaguzi wa Agosti 1961 ulioleta kura nyingi kwa chama chake Banda alikuwa waziri wa ardhi na serikali za mitaa. Tarehe 1 Februari 1963 alikuwa waziri mkuu wa Nyasaland.

Mwaka 1964 aliongoza nchi kwenye uhuru kamili. Banda aliamua kubadilisha jina kutoka Nyasaland kuwa "Malawi".

Kuelekea udikteta

[hariri | hariri chanzo]
Rais Banda akitembezwa na Jomo Kenyatta wakati wa ziara yake huko Nairobi

Wakati wa Agosti na Septemba 1964 Banda alijikuta mara ya kwanza mbele ya upinzani wa mawaziri wengi. Walilalamika juu ya Banda kutoshauriana nao akifanya maazimio, kuendelea kwa uhusiano wa kidiplomasia na Afrika Kusini (iliyofuata siasa ya apartheid) na Ureno iliyotawala makoloni ya Msumbiji n.k.

Banda aliachisha mawaziri watatu tarehe 7 Septemba. Mawaziri wengine waliwafuata wakijiuzulu. [4] Maandamano nchini yalifuata na wafuasi wa Banda walipigana na hao wa mawaziri. Mawaziri wengi waliondoka nchini. Wawili walijaribu kuingia pamoja na wanamgambo wenye silaha kutoka Msumbiji lakini walishindwa.

Mwaka 1966 Malawi ikawa jamhuri na Hastings Banda rais wake wa kwanza na chama cha MCP kilikuwa chama pekee cha kisiasa.

Mwaka 1970 alitangazwa kuwa mwenyekiti kwa maisha yote wa chama cha MCP. Hatua hii ilifuatwa na Banda kuwa rais wa taifa kwa maisha yake yote. Umoja wa vijana wa chama cha MCP ulihakikisha kukomeshwa kwa kila upinzani nchini pamoja na vyombo vya dola.

Wote walipaswa kumtaja kwa jina la "His Excellency the Life President Ngwazi Dr. H. Kamuzu Banda" kwa kuongeza "Ngwazi" ambalo ni neno la Chichewa lenye maana ya "shujaa". Kutamka maneno ya ukosoaji dhidi ya rais ilikuwa hatari.

Alitangaza mambo mengi kuwa marufuku Malawi, kwa mfano wanawake kuvaa suruali, kuonyesha magoti, wanaume kuwa na nywele ndefu au suruali fupi. Makanisa yalipaswa kutafuta kibali cha serikali, Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku. Wamalawi wenye asili ya Uhindi walipaswa kuachana na nyumba zao na kuhamia maeneo ya pekee katika miji. Magazeti, vitabu na filamu vilichunguliwa na wakaguzi wa serikali.

Banda alifaulu kutunza amani nchini wakati wa utawala wake lakini aliongoza kama dikteta. Mwaka 1983 mawaziri watatu wa serikali yake waliuawa. Banda mwenyewe alianzisha majadiliano kuhusu kukubali vyama vingi nchini. Mawaziri watatu waliunga mkono hoja hii na mara moja rais aliachisha baraza lote la mawaziri akaita mkutano wa bunge na kuachisha wabunge wote. Mawaziri watatu walifungwa katika chumba bungeni na kupigwa. Mbunge mmoja aliingia katika chumba hiki na kuwaona wakiteswa alikamatwa pamoja nao. Wote wanne walipatikana wamekufa katika gari la Peugeot lililopinduka. Serikali ilizuia kufunguliwa kwa majeneza wakati na mazishi yaliyotokea usiku. Walitangazwa kuwa wahanga wa ajali lakini baadaye ilijulikana waliuawa kwa kupiga misumari katika vichwa vyao kabla ya kuweka maiti katika gari na kulisukuma katika korongo.[5]

Hadi mnamo 1990 nchi za magharibi zilisaidia au angalau kuvumilia serikali ya Banda kwa sababu alikuwa mpinzani wa ukomunisti, pia kati ya nchi chache za Afrika zilizoendelea kuwa na uhusiano na Afrika Kusini. Lakini kuporomoka kwa ukomunisti kulisababisha badiliko. Wafadhili wa miradi ya maendeleo walidai mabadiliko ya kuheshimu haki za binadamu. Serikali ya Uingereza ilisimamisha usaidizi wote kwa Malawi.

Katika Machi 1992 maaskofu Wakatoliki wa Malawi walitunga waraka kwa Wakristo walipotamka ukosoaji wa Banda na serikali. Wanafunzi wa vyuo walichukua upande wa maaskofu na kuandamana. Vyuo vikafungwa.

Hadi Oktoba 1992 Banda alipaswa kukubali kura ya wananchi kuhusu swali la kukubali vyama vingi. Kura hii ilileta asilimia 64 kwa ajili ya demokrasia ya vyama vingi. Mwaka huohuo halmashauri mpya ilitangaza katiba mpya na kuondoa "urais wa maisha". Jeshi la Malawi lilivamia vituo vya Umoja wa Vijana wa MCP na kukamata silaha zote zilizowahi kupewa kama mkono wa utawala wa chama [6]. Katika uchaguzi wa mwaka 1994 Banda aligombea tena urais lakini alishindwa na Bakili Muluzi. Chama kipya cha Muluzi kilipata wabunge wengi.

Mwaka 1995 Banda alikamatwa na kupelekwa mahakamani kwa mashtaka ya kuhusika katika mauaji ya mawaziri ya mwaka 1983[7]. Aliachishwa kutokana na upungufu wa ushahidi.

Banda aliendelea kuwaangalia Wamalawi kama "watoto wa siasa" akatabiri ya kwamba wanahitaji "mkono wa chuma".

Mwaka 1997 alingonjeka akapelekwa kwa matibabu Afrika Kusini alipofariki tarehe 25 Novemba 1997 akiwa na umri wa miaka 99 hivi.

  1. Dr Banda - Biography, uk. 4, iliangaliwa kwenye tovuti ya scribd.com mnamo Januari 2017
  2. Obituary: Dr Hastings Banda Ilihifadhiwa 5 Agosti 2018 kwenye Wayback Machine., na Richard Dowden katika gazeti la The Independent, 27 Novemba 1997, ilitazamiwa Januari 2017
  3. "History of Malawi" kwenye tovuti ya Historyworld.net. 31 December 1963. Iliangaliwa Januari 2017
  4. "History of Malawi" kwenye tovuti ya Historyworld.net. 31 December 1963. Iliangaliwa Januari 2017
  5. Mwakasungura, Kapote, Miller, Douglas: Malawi's Lost Years (1964-1994) uk. 201, Mzuni Press, 10.08.2016 ISBN 978-99960-45-19-6, ilangaliwa kupitia google books Januari 2017
  6. Reuben Chirambo, Operation Bwezani Ilihifadhiwa 23 Mei 2013 kwenye Wayback Machine., Nordic Journal of African Studies 13(2): 146–163 (2004), iliangaliwa kwenye tovuti ya Chuo kikuu cha Helsinki wakati wa Januari 2017
  7. Malawi Tries Ex-Dictator in Murder, Los Angeles Times May 21, 1995, na Bob Drogin; iliangaliwa Januari 2017

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]
  • "Banda, Hastings Kamuzu". Oxford Dictionary of National Biography (tol. la 2004).
  • Hulec, Otakar and Jaroslav Olša, jr (2008). Dějiny Zimbabwe, Zambie a Malawi (in Czech, translation of title: History of Zimbabwe, Zambia and Malawi), Nakladatelství Lidové noviny.
  • Lwanda, John Lloyd, (1993). Kamuzu Banda of Malawi: A Study in Promise, Power, and Paralysis, Dudu Nsomba Publications.
  • Meredith, Martin (2005). The Fate of Africa: From the Hopes of Freedom to the Heart of Despair, Public Affairs.
  • Muluzi, Bakili (with Yusuf M. Juwayeyi, Mercy Makhambera, Desmond D. Phiri), (1999). Democracy with a Price: The History of Malawi since 1900. Jhango Heinemann, Blantyre.
  • Mwakikagile, Godfrey, (2006). Africa After Independence: Realities of Nationhood. Johannesburg, South Africa: Continental Press.
  • Ross, Andrew C. (2009). Colonialism to cabinet crisis: a political history of Malawi, African Books Collective, 2009 ISBN 99908-87-75-6. This gives extensive biographical detail on Hastings Banda.
  • Rotberg, Robert I, (1965). The Rise of Nationalism in Central Africa. Cambridge: Harvard University Press.
  • Shaw, Karl (2005) [2004]. Power Mad! (kwa Czech). Praha: Metafora. ISBN 80-7359-002-6. {{cite book}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)
  • Short, Philip (1974). Banda. London: Routledge & Kegan Paul.
  • van Donge, Jan Kees (1995). Kamuzu's legacy: the democratisation of Malawi. African Affairs, Vol 94, No 375.
  • Williams, T. David (1978). Malawi, the Politics of Despair. Cornell University Press.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]