Hajj
Haji au Hajj (Ar. حج) ni hija ya Waislamu kwenda Makka penye jengo la Kaaba. Inafanywa wakati wa mwezi Dhul-hijja ambayo ni mwezi wa 12 wa kalenda ya Kiislamu, hasa tarehe 8 - 12 za mwezi. Katika Uislamu hija hii ni wajibu kwa kila Mwislamu mwenye uwezo wa kuifanya angalau mara moja maishani mwake.
Hajj inaanza siku ya 8 ya Dhul-hijja kwa kuingia katika hali ya ihram; hii inafanywa kwa kuoga kufuatana na masharti ya dini na kwa wanaume kwa kuvaa nguo za hajj ambazo ni vitambaa viwili vyeupe pekee. Viatu haviruhusiwi isipokuwa kandambili. Wanawake hawana masharti kuhusu mavazi isipokuwa hawaruhusiwi kufunika uso. Hapo wanaingia Makka mjini wakifanya tawaf yaani kuzunguka Kaaba mara saba. Baadaye wanaelekea kwenda bonde la Mina wanapolala katika hema zilizoandaliwa. Wengine wanatangulia kufika Mina kabla ya tarehe hii.
Siku ya 9 Dhul-hijja wanaelekea mlima wa Arafat kwa umbali wa kilomita 10 wanapokaa wakisimama na kusali hadi jioni. Baada ya machweo wanaenda Muzafila wanapolala.
Kabla ya macheo siku ya 10 Dhul-hijja wanarudi Mina ambako wanafanya ibada ya kumrushia sheitani mawe. Ishara ya sheitani inayotupiwa mawe ilikuwa nguzo ya mwamba inayoitwa jamarat lakini baada ajali nyingi ambako watu walikosa nguzo na kuwapiga wenzao kwenye upande mwingine kuna sasa ukuta. Baada ya kurusha mawe 7 wanaume wanakata nywele zote za kichwani (wanawake nywele kadhaa pekee). Halafu wanachinja sadaka maana siku hii ni sikukuu ya Idd ul Adha. Siku hizi kondoo 1 anachinjwa na wachinja wanaoajiriwa kwa kila haji. Sehemu kubwa ya nyama inawekwa katika friza na kutumwa baadaye kwa watu maskini kote duniani.
Baadaye wanarudi Makka kwa tawaf ya pili kwa kuzunguka Kaaba mara saba. Kutoka hapa wanaenda "sa'i" wanapotembea mara saba kati ya vilima vya Safa na Marwa wakifuata nyayo za Hagar aliyetafuta hapa maji kwa mtoto wake Ismail.
Siku zinazofuata wanakaa tena Mina wanarusha mara ya pili mawe kenye kuta za jamarat.
Hajj inakwisha kwa kuzunguka Kaaba mara ya tatu na mwisho.
Mahujaji wengi wanatumia nafasi kutembela mji wa Madina baada ya hajj na kuona msikiti wa mtume.
Mwislamu aliyetimiza safari hii anapewa cheo cha heshima alhaji au hajja kwa wanawake.
Safari ya kutembela Makka nje ya siku za hajj huitwa umrah haina cheo sawa na hajj yenyewe.
Idadi ya mahujaji inaelekea kuwa milioni tatu kila mwaka. Hadi mwaka 2006 ajali nyingi zilitokea kutokana msongamano mkubwa wa watu lakini baadaye serikali ya Saudia imeajiri wataalamu kutoka kote duniani kupanga njia salama kwa mahujaji hasa kwa kutenganisha watu wanaoelekea pande mbalimbali na njia za kufika na kuondoka. Siku hizi mahali ambako watu wengi wanatakiwa kuzunguka sehemu moja zimejengewa majengo ambako watu wanaweza kutembea kwenye ghorofa wakati mmoja.