Ukristo katika karne za kwanza
Ukristo katika karne za kwanza ni sehemu ya historia ya Kanisa hadi mwaka 325 BK, mwaka ulipofanyika mtaguso mkuu wa kwanza huko Nisea, leo nchini Uturuki.
Kwa kawaida karne hizo tatu zinagawiwa pande mbili: wakati wa Mitume wa Yesu (hadi mwaka 100 hivi) na baada ya kifo chao wote.
Wakati wa Mitume
haririHabari kuu za kipindi cha kwanza, kama ile ya siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu kuwashukia wafuasi wa Yesu, zinapatikana hasa katika Matendo ya Mitume, kitabu kilichoandikwa na mwinjili Luka kwenye miaka ya 80. Humo unasimuliwa hasa uenezi wa Ukristo katika maeneo ya upande wa kaskazini wa Bahari ya Kati.
Tukio lingine muhimu linalosimuliwa na Luka ni uongofu wa Mtume Paulo, mwenezi mkuu wa Ukristo na mfafanuzi bora wa imani hiyo mpya.[1]
Pamoja na uenezi, linajitokeza badiliko kubwa la Wakristo: awali walikuwa wote Wayahudi ama kwa kuzaliwa ama kwa kuongoka,[2] nao wanaitwa Wakristo wa Kiyahudi. Lakini katika karne ya 1 idadi yao ilizidiwa na ile ya Wakristo wa mataifa mengine.
Sambamba na hilo lugha ya kimataifa ya Kigiriki ilizidi kutumika badala ya Kiaramu, lugha mama ya Yesu na mitume wake.[3] Ndiyo sababu Agano Jipya limeandikwa lote kwa Kigiriki. Vitabu 27 vinavyoliunda vilianza kulinganishwa na vile vya Agano la Kale kama vitakatifu.
Tena Yerusalemu uliokuwa mji mkuu wa Wayahudi na wa Wakristo wa kwanza, ulizidi kukosa umuhimu, hasa baada ya Mtume Petro na wenzake kuuhama au kuuawa. Wakati wa vita vya kwanza vya Kiyahudi hata waumini wa kawaida walihama, na waliporudi hakukuwa tena na hekalu, kwa kuwa lilibomolewa mwaka 70. Mbali ya hayo, uhusiano na Wayahudi ulizidi kuharibika, na hatimaye Wakristo walikatazwa wasishiriki tena ibada sinagogini.
Jumuia ya Roma, makao makuu ya dola, ilizidi kuwa muhimu, hasa baada ya kufikiwa na Petro na Paulo, ambao walimalizia huko kazi yao kwa kufia dini katika dhuluma ambayo ilianzishwa na Kaisari Nero mwaka 64 na kuendelea kwa kwikwi hadi mwaka 313.
Wakati wa watetezi wa dini
haririBila kujali dhuluma hiyo ya nyingine, Ukristo ulizidi kuenea ndani na nje ya Dola la Roma.
Ushujaa wa umati wa wafiadini na upendo kati ya Wakristo vinafikiriwa kuwa sababu kuu ya uenezi. Kutoka kwenye miji, imani ilizidi kuenea vijijini pia.
Pamoja na hayo, walianza kujitokeza waandishi mbalimbali kutetea Kanisa mbele ya serikali, na wengine kuchambua imani dhidi ya uzushi uliozidi kupata nguvu hasa kwa namna ya Gnosis. Waandishi hao ni kati ya wale wanaoitwa mababu wa Kanisa au walau waandishi wa Kikanisa.
Wakati huohuo matumizi ya vitabu vya Agano Jipya katika ibada yalizidi kujadiliwa na kutungiwa orodha rasmi (Kanuni ya Biblia).
Tanbihi
hariri- ↑ Oxford Dictionary of the Christian Church ed. F.L. Lucas (Oxford) entry on Paul
- ↑ Catholic Encyclopedia: Proselyte: "The English term "proselyte" occurs only in the New Testament where it signifies a convert to the Jewish religion (Matthew 23:15; Acts 2:11; Acts 6:5; etc.), though the same Greek word is commonly used in the Septuagint to designate a foreign sojourner in Palestine. Thus the term seems to have passed from an original local and chiefly political sense, in which it was used as early as 300 B.C., to a technical and religious meaning in the Judaism of the New Testament epoch."
- ↑ Ehrman, Bart D. (2012). Did Jesus Exist?: The Historical Argument for Jesus of Nazareth. HarperCollins, pp 87- 90.