Wilaya ya Mbozi
Wilaya ya Mbozi ni wilaya mojawapo kati ya 5 za Mkoa wa Songwe.
Eneo la wilaya ni kilomita za mraba 3440.
Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 515,270. Baada ya kutenga maeneo ya wilaya mpya ya Momba na Halmashauri ya mji wa Tunduma mnamo 2012/13, Mbozi kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya 2022 ina jumla ya watu 510,599, hii ikiwa sawa na asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa wa Songwe ambao kwa takwimu hizo ni 1,344,687 [1]..
Wakazi
haririWakazi ni hasa Wanyiha, Wakinga, Wanyakyusa, Wandali na Wanyamwanga. Wanyiha ni takriban nusu ya wakazi wa wilaya wakikalia nyanda za juu. Wanyamwanga ni takriban asilimia 10 za wakazi wakikaa kwenye ukanda wa chini kata za Nambinzo, Isalalo na Ipunga.
Makabila mengine ni pamoja na Wawanda, Walambya, Wamalila na Wasafwa. Katika miaka ya mwisho Wamasai na Wasukuma wamehamia wilayani.
Pato la wananchi wa mkoa wa Songwe kwa sehemu kubwa linabebwa na Halmashauri ya Mbozi kupitia zao la kahawa ambalo kwa mwaka huuingizia mkoa zaidi ya trilioni 1.3 na pato kwa mtu mmojammoja kwa mkoa wa Songwe ni milioni 2.23 ukiwa mkoa wa 19 kitaifa, kwa wilaya ya Mbozi pato lake ni wastani wa milioni 2.5.
Eneo
haririEneo la wilaya liko katika kimo cha mita 1,500-2,750 juu ya usawa wa bahari. Nyanda za juu ni maeneo ya Iyula, Vwawa, Igamba na Ndalambo, yana ardhi nyekundu.
Kimondo cha Mbozi, ambacho ni maarufu duniani kama kimondo kikubwa cha chuma, si mbali na misioni ya Mbozi. Kimondo hicho kina uzito unaokadiriwa kuwa tani 12.
Mbozi Mission ndipo mche wa kwanza wa zao la kahawa ulipopandwa mwaka 1902 na wamisionari Wamoravian kutoka Ujerumani na baadaye kuenea katika maeneo mengi ya nyanda za juu za wilaya ya Mbozi, kituo cha kwanza cha ununuzi wa kahawa kilijengwa eneo la Igamba jirani na ilipo mahakama ya Mjerumani kwenye eneo la mwene Nzowa.
Maliasili na visukuku katika eneo la Magamba
haririKatika kijiji cha Magamba, kilichopo kata ya Isansa, kumegunduliwa makaa ya mawe hazina ya zaidi ya tani milioni 52, ambapo wakoloni Waingereza walifanya majaribio ya makaa hayo mwaka 1934 kuendeshea garimoshi na katika kufua umeme kwenye kituo cha umeme Mombasa mwaka 1935.
Eneo hilo limepata umaarufu zaidi baada ya kupatikana kwa visukuku vya mifupa ya mijusi mikubwa ya kale (dinosauri) kando ya kijito Mahoma. Profesa Patrick O'Connor wa Chuo kikuu cha Ohio nchini Marekani amekuwa akifanya utafiti tangu mwaka 2002 ambapo ameweza kugundua mabaki hayo.
O'Connor anasema baadhi ya mifupa aliyogundua inadhihirisha kuwepo kwa dinosauri wadogo chini ya futi moja walioishi duniani hapa miaka milioni 100 iliyopita. Mifupa ya dinosauri inaonesha mnyama huyo alikuwa mkubwa na uzito wa zaidi ya tani 40. (Hayo yamo katika mahojiano kati ya Kenneth Mwazembe na Prof. O'Connor yaliyofanyika Julai 2008 kijijini Magamba)
Katika kijiji cha Nkangamo kata ya Nkangamo tarafa ya Ndalambo kuna miamba yenye michoro ya kale inayokadiriwa kuchorwa miaka 3000 iliyopita. Katika eneo hilo pia kuna jiwe au mwamba wenye wayo wa binadamu unaoonekana kukanyagwa kabla jiwe halijawa gumu. Kwa bahati mbaya Idara ya Mambo ya Kale haijafuatilia habari hizo.
Katika Wilaya ya Mbozi imegunduliwa kuwepo kwa dhahabu maeneo ya Idiwili na Shidunda, jirani na kimondo cha Mbozi. Pia eneo la Magamba inapopakana na wilaya ya Chunya ni ukanda wa dhahabu unaohitaji wataalamu kufanya utafiti zaidi ili kujua wingi wa dhahabu iliyopo katika maeneo hayo.
Kwa upande wa kijiji cha Magamba mpakani na Chunya kumeonekana dalili za kuwepo kwa mafuta ya petroli hasa kwenye machimbo ya mkaa wa mawe ambao upo kiasi cha mita moja kutoka usawa wa ardhi. Kwa sasa kampuni ya Magamba Coal Mine au Troll Mining Company inayomilikiwa na jenerali mstaafu Robert Mboma inawekeza/kuvuna makaa hayo. Hao wawekezaji wanapaswa kujenga mitambo ya kufua umeme wa makaa ili uwepo wao huko uwe kwa faida ya Watanzania wote.
Miji
haririMiji wilayani ni Mlowo, penye viwanda vya kahawa vitatu vya GDM, Mbozi MCCO na LIMA (watu 37,000-50,000). Aidha Vwawa ndiko makao makuu ya wilaya ambapo idadi ya wakazi wake ni zaidi ya 60,000. Miji mingine miwili iko kando ya barabara kuu ya TANZAM kutoka Dar es Salaam kupitia Mbeya kwenda Zambia.
Reli ya TAZARA inapita vilevile wilayani na kuna vituo huko Vwawa na Tunduma.
Utawala
haririKatika wilaya hii kuna kata 29 za Vwawa, Mlowo, Ihanda, Ukwile, Ipunga, Kilimampimbi, Isalalo, Msia, Ruanda, Mahenje, Nanyala, Iyula, Hezya na Nyimbili. Nyingine ni Ichenjezya, Ilolo, Hasanga, Igamba, Nambinzo, Itaka Halungu, Isansa, Itumpi, Shiwinga, Mlowo, Magamba, Mlangali na Bara.
Misheni ya Moravian Mbozi
haririKitovu cha kihistoria kilikuwa kijiji cha Mbozi penye kituo cha misheni cha Moravian pamoja na hospitali na shule ya sekondari. Kituo kilianzishwa mwaka 1899 na mmisionari Mjerumani, Traugott Bachmann. Bachmann aliyejipa jina la wenyeji la Mwalwizi alichagua mahali pa misioni kwa sababu palikuwa mpakani wa maeneo ya Nzova na Mwasenga waliokuwa machifu muhimu wa Wanyiha.
Asili ya jina la Mbozi
haririAsili ya jina Mbozi linatokana na dawa za asili zilizotengenezwa yaani majani ya miti yanachumwa kisha hutwanga kwenye kinu na kuongezewa maji kidogo kisha huchujwa na kupewa mgonjwa. Wanyiha huita dawa hiyo Mbozyo lakini Wazungu walishindwa kutamka Mbozyo wakasema Mbozi.
Tanbihi
haririViungo vya Nje
hariri- [1]
- Tanzanian Government Directory Database
- [2] Ilihifadhiwa 3 Machi 2016 kwenye Wayback Machine.
Kata za Wilaya ya Mbozi - Mkoa wa Songwe - Tanzania | ||
---|---|---|
Bara | Halungu | Hasamba | Hasanga | Hezya | Ichenjezya | Idiwili | Igamba | Ihanda | Ilolo | Ipunga | Isalalo | Isansa | Itaka | Itumpi | Iyula | Kilimampimbi | Magamba | Mahenje | Mlangali | Mlowo | Msia | Nambinzo | Nanyala | Nyimbili | Ruanda | Shiwinga | Ukwile | Vwawa |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Songwe bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Wilaya ya Mbozi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari . Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno |