Elizabeth I wa Uingereza

Malkia wa Uingereza na Ireland kutoka 1558 hadi 1603
Kuhusu malkia mwingine mwenye jina hili ona Elizabeth II wa Uingereza

Elizabeth I wa Uingereza (7 Septemba 1533 - 24 Machi 1603) alikuwa malkia wa Uingereza kuanzia 1558 hadi kifo chake. Alikuwa mwanamke wa tatu kutawala Uingereza kama malkia.

Malkia Elizabeth mnamo 1585.

Aliitwa mara nyingi "malkia bikira" kwa sababu hakuolewa wala kuzaa watoto. Kutokana na neno la Kiingereza kwa bikira ("virgin") koloni la kwanza la Uingereza likaitwa "Virginia".

Wakati wake ulikuwa kipindi cha kustawi kwa utamaduni na uchumi katika Uingereza ambako William Shakespeare alitunga maigizo na tamthiliya zake, Francis Bacon aliandika falsafa yake na Francis Drake aliweka misingi ya upanuzi wa ukoloni wa Uingereza duniani. Elizabeth alihakikisha pia kipaumbele cha Kanisa Anglikana kama dini rasmi ya taifa na kulitenganisha moja kwa moja na usimamizi wa Papa wa Roma[1].

Alizaliwa katika nasaba ya Tudor kama mtoto wa mfalme Henry VIII wa Uingereza na mke wake wa pili Anne Boleyn. Hakumkumbuka mama yake aliyeuawa na mumewe akiwa mdogo wa miaka mitatu.

Alipata elimu nzuri akajua lugha sita za Kiingereza, Kifaransa, Kiitalia, Kihispania, Kigiriki na Kilatini.

Kwa miaka mingi hali ya cheo chake ilikuwa mashakani. Babake Henry VIII hakumtaka kama mrithi baada ya kumchukia mamake aliyemwua. Lakini mke wa mwisho wa Henry VIII alimshawishi mfalme kuwaingiza mabinti zake katika orodha ya ufuatano wa warithi wa cheo chake lililothibitishwa na bunge.

Malkia

hariri

Elizabeth alikuwa malkia baada ya kifo cha dada yake Maria Tudor. Mwenyewe alilelewa kama Mkristo wa Kiprotestanti akahakikisha ya kwamba ibada za Kikatoliki zilizopewa nafasi kubwa na dadake aliyekuwa Mkatoliki ziwe zimekomeshwa kwa nguvu zote[2]. Kwa kusudi hili alitangaza sheria kuwa ibada zote zilipaswa kufuata liturujia ya Common Book of Prayer na kumfanya mfalme au malkia kuwa gavana mkuu wa kanisa la Uingereza.

Alimaliza vita dhidi ya Ufaransa vilivyowahi kudhoofisha nguvu za taifa kwa miaka mingi.

Matatizo ya Mary Stuart

hariri

Mwaka 1568 malkia wa Uskoti, Mary Stuart, alikimbilia Uingereza kwa sababu alikuwa katika hatari ya kuuawa kwake nyumbani, hivyo aliomba msaada wa Elizabeth. Mary Stuart alionekana kama hatari kwa utawala wa Elizabeth kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa na haki za kushika taji la Uingereza.

Elizabeth aliamua kumkamata na kumfunga akiendesha utafiti juu ya mashtaka dhidi yake. Mary Stuart alikaa mafungoni kwa kipindi cha miaka 18; mwishowe alishtakiwa kutokana na kushiriki katika mipango ya kumwua Elizabeth akapewa hukumu ya mauti na kuuawa mwaka 1587.

Upanuzi wa enzi ya Uingereza

hariri

Elizabeth alikuwa amepanua uwezo wa Uingereza baharini akishirikiana na Francis Drake na Walter Raleigh. Drake alizunguka dunia yote kama mtu wa pili baada ya Ferdinand Magellan. Baadaye alipewa kibali cha malkia cha kuendesha vita vya baharini dhidi ya meli za Hispania iliyokuwa taifa kubwa la Wakatoliki. Drake na wenzake walishambulia mara kwa mara meli za Wahispania zilizobeba fedha kutoa makoloni ya Amerika na kiasi kikubwa cha fedha hii kilifika kwenye mifuko ya kifalme ya London.

Vita na Hispania

hariri

Baada ya kuuawa kwa malkia Mkatoliki Mary Stuart mfalme Filipo II wa Hispania aliamua kushambulia Uingereza. Alitengeneza kundi kubwa la jahazi manowari lililowahi kupatikana hadi wakati ule. Lakini wanamaji Waingereza waliweza kuwazuia wasipeleke askari zao kwa nchi kavu. Dhoruba iliharibu baadaye meli nyingi za Wahispania. Ushindi huu ulikuwa msingi wa nafasi kubwa ya Uingereza baharini iliyoendelea kuwepo hadi karne ya 20.

Miaka ya mwisho

hariri

Hali ya vita na Hispania iliendelea. Kuanzia mwaka 1593 Waeire, waliokuwa Wakatoliki vilevile, walianza kuasi utawala wa Uingereza na vita hivyo vilihitaji nguvu zote za ufalme; askari wengi walikufa na malkia alipaswa kuongeza mzigo wa kodi kwa raia wa ufalme. Wengi walisikitikia vita hivyo. Gharama kubwa za vita ya Ueire zilimlazimisha malkia kuomba mara kadhaa kibali cha bunge ili kuongeza kodi. Kwa njia hii nafasi ya bunge la Uingereza likaongezeka nguvu.

Elizabeth aliaga dunia mwaka 1603 akiwa na umri wa miaka 69.

Tanbihi

hariri
  1. Cfr. Bishop Challoner, Memoirs of Missionary Priests and other Catholics of both sexes that have suffered death in England on religious accounts from the year 1577 to 1684 (Manchester 1803)
  2. 13 Eliz. c.1 made it high treason to affirm that the queen ought not to enjoy the Crown, or to declare her to be a heretic. "An act against Jesuits, seminary priests, and such other like disobedient persons", (27 Eliz.1, c. 2), the statute under which most of the English martyrs suffered, made it high treason for any Jesuit or any seminary priest to be in England at all, and a felony for any person to harbor or aid them. Cfr.Burton, Edwin, Edward D'Alton, and Jarvis Kelley. "Penal Laws." The Catholic Encyclopedia Vol. 11. New York: Robert Appleton Company, 1911. 3 February 2019

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
 
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu: