Atomu
Atomu au atomi (kutoka Kigiriki átomos yaani "isiyogawika") ni sehemu ndogo ya maada yenye tabia ya kikemia kama elementi. Kila kitu duniani hujengwa kwa atomu.
Kuna aina nyingi za atomu na idadi za aina hizi tofauti ni sawa na elementi zilizopo duniani.
Muundo wa atomu
Lakini atomu yenyewe hufanywa na chembe ndogo zaidi hasa sehemu 3 ambazo ni: protoni, neutroni na elektroni. Sehemu hizi ndogo zaidi hazina tabia ya elementi fulani ila tu atomu yote ni elementi. Atomu zinatofautiana kutokana na idadi tofauti ya chembe hizi ndogo ndani yao.
Atomu ni ndogo kiasi ya kwamba hazionekani kwa macho wala kwa hadubini za kawaida. Kwa sababu hiyo wataalamu waliunda vielelezo mbalimbali vinavyojaribu kuunganisha tabia mbalimbali za atomu zinazopimiwa.
Kielelezo cha Ernest Rutherford kinasema kwamba katikati ya atomu kuna kiini chenye sehemu kubwa ya maada ya atomu yote. Kiini cha atomu hufanywa na protoni na neutroni. Atomu za elementi ileile zinaweza kutofautiana katika idadi ya neutron ndani ya kiini na hali hizi tofauti huitwa Isotopi za elementi. Isotopi tofauti ya elementi moja zinapangwa kwenye nafasi ileile ya jedwali la elementi. Isotopi kadhaa si thabiti lakini [nururifu] yaani zinaweza kutoa chembe au nururisho na kuhamia elementi nyingine.
Kiini huzungukwa na ganda ambalo ni si dutu imara lakini nafasi ya njia ambako elektroni huzunguka kiini. Nafasi hizi huitwa mizingo elektroni. Kielezo hiki kimekuwa msingi wa vielelezo vingine kama kile cha Bohr.
Kiini huitwa kwa lugha ya Kilatini (pia kwa Kiingereza) "nucleus" na hapa lugha ya Kiswahili imepokea neno "nyuklia". "Nucleas" kwa ajili ya mambo yanayohusu matumizi ya nguvu ya atomu, kwa mfano nishati ya nyuklia.
Chaji na ioni
Protoni zina chaji ya chanya, neutroni hazina chaji na elektroni zina chaji ya hasi. Kiini inafanywa na protoni zenye chaji chanya pamoja na neutroni zisizo na chaji hivyo kiini cha kila atomu kina chaji chanya. Elektroni zenye chaji hasi zinazunguka kiini.
Kwa jumla chaji hizo husawazishana na atomu yote ni batili yaani haionyeshi chaji maalumu.
Atomu inaweza kuingia katika hali ya kuwa na chaji kama elektroni moja inaongezwa au kuondolewa katika ganda lake halafu atomu hiyo huitwa "ioni".
Kama idadi ya elektroni imepungua chini ya kiwango cha kawaida atomu yote ina chaji chanya na kuitwa "kationi". Kama elektroni imeongezwa chaji ya atomu yote huwa hasi na kuitwa "anioni".
Njia za elektroni
Kufuatana na kielezo cha Niels Bohr kiini huzungukwa na mizingo elektroni mbalimbali kama kitunguu. Idadi ya mizingo hutegemeana na idadi ya elektroni au ukubwa wa atomu kwa jumla.
Ukubwa wa atomu yote hutegemeana na umbali wa mzingo elektroni wa nje. Ieleweke ya kwamba mizingo hii yote si dutu au mada lakini nafasi ambako elektroni zinazunguka kiini kwa mkasi mkubwa.
Tovuti za nje
- General information on atomuc structure Archived 23 Desemba 2012 at the Wayback Machine.
- Atomuc structure timeline Archived 26 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Atomu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Atomu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |