Nenda kwa yaliyomo

Mwandishi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 14:24, 30 Machi 2024 na Riccardo Riccioni (majadiliano | michango) (Waandishi wa leo)
(tofauti) ← Pitio lililotangulia | Toleo la sasa (tofauti) | Pitio linalofuata → (tofauti)
Sanamu ya mwandishi wa Misri ya Kale; kalamu imepotea
Mwandishi Mfaransa Jean Miélot katika ofisi yake akinakili kitabu, mnamo 1456
Waandishi wa taipureta wanaosubiri wateja huko Puducherry, Uhindi
Mwandishi wa kaligrafia mbele ya hekalu huko Vietnam

Mwandishi kwa maana ya kimsingi ni mtu anayeandika.

Jina hilo linaweza kumtaja mtu aliyeweka matini kwenye karatasi tunayosoma. Linaweza pia kumtaja mtungaji wa andiko hata kama hatuna uhakika kama aliliandika mwenyewe kwa mkono wake, kwa hiyo ni karibu na maana ya "mtungaji".

Tangu uenezaji wa elimu ya shule kwa watu wengi tendo la kuandika si jambo la ajabu tena. Lakini kwa kipindi kirefu cha historia ya binadamu walikuwepo watu wachache tu waliojua kusoma na kuandika na kwa vipindi vile kazi ya "mwandishi" ilikuwa muhimu katika jamii.

Waandishi katika historia

[hariri | hariri chanzo]

Kubuni uwezo wa kutunza habari kwa alama ya kimaandishi kulikuwa maendeleo makubwa katika historia ya binadamu. Chanzo cha maandishi kilikuwa katika kutunza kumbukumbu ya kodi na mapato. Watawala wa kwanza waliweza kushika hivi ni kiasi gani cha nafaka au mifugo kinachochangiwa na kijiji au mkoa fulani.

Kutunza kumbukumbu hii kulihitaji watu waliojua kutumia alama gani kwa maana gani na walioweza kuzitambua tena baada ya muda. Watu hao walikuwa waandishi wa kwanza. Kulingana na maendeleo ya mwandiko idadi ya alama iliongezeka zilizotaja pia mambo yasiyoonekana kama dhana za kijamii au kidini.

Waandishi walikuwa mara nyingi maafisa wa mfalme au mtawala waliokuwa karibu naye kwa sababu elimu yao ilikuwa muhimu kwa utawala. Tangu uenezaji wa biashara wafanyabiashara walitumia pia maandishi, hivyo walijifunza wenyewe kuandika au waliajiri waandishi.

Katika eneo la Mesopotamia walimwabudu mungu mlinzi wa waandishi kwa jina Nabu. Katika maktaba ya matofali ya kikabari ya Niniveh kuna matini inayosifu kazi ya mwandishi: "Onyesha bidii katika sanaa ya kuandika, maana itakupatia utajiri kwa wingi"[1]

Katika Misri ya Kale kazi ya mwandishi iliheshimiwa sana. Waandishi walionyeshwa mara nyingi kwa sanamu za kuchongwa zilizohifadhiwa hadi leo. Mwandishi Imhotep aliyekuwa afisa mtendaji mkuu wa farao Djoser alipewa heshima ya kimungu baada ya kifo chake. [2] Wana wa waandishi walifundishwa katika nyumba za baba halafu kupelekwa shule wakaingia katika huduma ya serikali na wakati mwingine kurithi nafasi ya baba.[3]

Hao waandishi walitimiza shughuli zinazotekelezwa leo na karani, mhasibu au katibu.

Waandishi katika Israeli

[hariri | hariri chanzo]

Katika Agano la Kale "mwandishi" alikuwa mtu aliyenakili sheria ya Mungu kwa watu waliotaka kuisoma, lakini baada ya uhamisho wa Babeli alizidi kuwa mtu wa maana kama mtaalamu ambaye uamuzi wake katika mambo ya dini uliheshimiwa sana. Katika miaka ya baadaye tena waandishi walizidi kupata nguvu na ushawishi katika Israeli, wakati ambapo manabii walipungua kwa idadi na umuhimu.

Waandishi wa leo

[hariri | hariri chanzo]

Kando na kuandika, waandishi wa leo wana vipawa vingine tofauti kama vile kuigiza, kuripoti katika vyombo vya habari na kusanii kwa sauti (voice artists) kama vile Raheel Farooq. Kando na kuandika vitabu vya chapa waandishi mamboleo wanafanya vitabu elektroniki yaani ebooks. Wengine waandika kwa wavuti zao. Kati ya waandishi bingwa hapa Afrika wa mambo leo ni kama Wallah bin Wallah, Mohamed Said, Ken Walibora na Yericko Y. Nyerere.

Kuna waandishi wengine ambao kazi yao ni kuwaandikia wengine. Katika dunia ya leo, ambayo kazi nyingi zafanyika kwa mtandao, waandishi hao huenda wakapewa kazi ya kuwafanyia wengine maandishi ya wavuti zao (freelance website content writers) au kuwafanyia maandishi waliyopewa chuoni.

Waandishi kama wanakili

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kupatikana kwa uchapaji njia pekee ya kupata nakala za hati, sheria, matangazo na vitabu ilikuwa kunakili matini hizi kwa mkono. Jamii zilizoendelea katika historia zilikuwa na maelfu ya watu ambao kazi yao ilikuwa kunakili matini hizi. Walipatikana katika ofisi za serikali, ofisi za shirika za biashara, taasisi za elimu au pia kama waandishi waliojitegemea na kufanya kazi yao kibarua.

Kazi yao ilipotea kwa kiasi kikubwa tangu kupatikana kwa uchapaji. Hadi leo katika nchi zenye watu wengi wasiojua kusoma kuna waandishi wanaofanya kazi hii kwa wengine. Kazi yao ni zaidi kuandika barua za watu wasiojua kuandika.

Kaligrafia

[hariri | hariri chanzo]

Kaligrafia ni sanaa ya kuandika vizuri na kuremba maandishi. Hadi leo kuna waandishi wanaotekeleza kazi hii kama sanaa ama kwa kutunga kaligrafia za mapambo ya nyumba au kwa kutunga hati za pekee zinazotakwa kurembishwa.

Wengine wanajifunza kaligrafia kama burudani ya binafsi.

Katika utamaduni wa Uyahudi nakala za Torati kwa matumizi katika ibada ya sinagogi zinahitaji kuandikwa hadi leo kwa mkono: kuna waandishi walio mabingwa kwa shughuli hii.

Mengineyo

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1970 mwanamuziki wa jazz Herbie Hancock alianza kutumia jina "mwandishi" akaita bendi yake "Mwandishi" na kutoa albamu kwa jina hilo.[4]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  1. Åke W. Sjöberg, In Praise of the Scribal Art, Journal of Cuneiform Studies 24/4, 1972, 26-131
  2. Brian E. Colless, Divine Education. Numen 17/2, 1970, 120f.
  3. David McLain Carr, Writing on the Tablet of the Heart: Origins of Scripture and Literature, Oxford University Press 2005, ISBN 0-19-517297-3, p.66
  4. https://nickdimaria.wordpress.com/2014/05/16/my-masters-thesis-on-herbie-hancocks-mwandishi-band/