Nenda kwa yaliyomo

Wikichanzo:Historia ya Kanisa ikoll

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 07:07, 8 Machi 2022 na Kipala (majadiliano | michango) (1.2. UTAKATIFU NA KASORO ZA KANISA)
(tofauti) ← Pitio lililotangulia | Toleo la sasa (tofauti) | Pitio linalofuata → (tofauti)

HISTORIA YA KANISA

KITABU CHA WANAFUNZI

(kiliandikwa mwaka 1993 na Ingo Koll, Mbeya kwa matumizi ya Umoja wa Walimu wa Elimu ya Kikristo kwenye shule za sekondari mjini Mbeya)

YALIYOMO:

SURA YA KWANZA: UKRISTO KATIKA AFRIKA LEO

1. Faida ya Historia; 2. Utakatifu na kasoro za kanisa; 3. Ukristo katika Afrika leo

1.1.HISTORIA YA KANISA INA FAIDA GANI ?

Je, unapenda habari za historia ? Ikiwa unapenda utafurahia sana mhula huu wa pili katika Kidato cha III. Labda wewe ni mmojawapo wasiopenda habari za historia. Tutajitahidi kukuvuta kusafiri pamoja nasi katika safari iliyo mbele yetu. Kumbe tuulize watu kadhaa juu ya faida za kupeleleza historia:

Mama N.: Historia ? Siwezi kula historia wala kulisha watoto wangu kwa historia.

John D.: Historia inanipa mifano mizuri ya kuiga. Mimi si mtu wa kwanza duniani. Wengine wameshawahi kupambana na matatizo yanayofanana na matatizo yangu ya leo. Kwa nini nisijue na kutumia maarifa ya watu waliowahi kuishi zamani?

Fanny "Scud" T.: History ni somo linalonichosha kupita kiasi. Hawa wote wameshakufa ! Haina maana kwa vijana wa leo.

Sara F.: Kila mtu ni historia. Mimi ninayo historia yangu tangu kuzaliwa, wazazi wangu, ukoo wangu. Mimi nilivyo leo niko pamoja na historia yangu. Ningalizaliwa katika mwaka tofauti au katika nchi nyingine maisha yangu yangekuwa tofauti kabisa. Kumbe haya yote yalivyo ni sehemu ya historia yangu.

Juma S.: Historia inanisaidia kuelewa dunia vizuri zaidi. Angalia habari tunazozipata juu ya Afrika Kusini. Nani anaelewa habari hizo asipojua kidogo historia ile ya Ukoloni, Makaburu, ANC na Inkatha ?

Fila Z.: Lugha yetu ya Kiswahili ni ushahidi wa historia. Katika miaka mingi watu wa sehemu mbalimbali walichangia maneno yao katika lugha yetu. Kumbe nikifungua mdomo tu na kusema tayari natumia historia hai.

Padre N.: Imani yetu ni juu ya historia, - historia kati ya Mungu na binadamu. Historia ya kanisa ni sehemu muhimu sana ya historia iliyopo kati ya Mungu na sisi wanadamu.

Maswali na Maarifa (1.1.):

1.Je, Unaonaje mawazo haya ?

2. Fanyeni utafiti katika darasa. Hesabuni ni wanafunzi wangapi wanaotoka katika dhehebu mbalimbali. Je, ni wangapi Anglikana, Baptist, Inland Church, Lutheran, Moravian, Wakatoliki, Pentekoste n.k.?

3. Mwanafunzi kutoka kila dhehebu aombwe kueleza jina la dhehebu lake. Kwa nini anaitwa Mroma, Mlutheri, Mwanglikan, n.k.? Maana yake ni nini ? Jina linatokea wapi? - Kumbe: wakiwa na matatizo afadhali wafuate kiuangalifu muhtasari wetu !

TUKUMBUKE:

1. Historia si juu ya mambo yaliyopita tu. Historia ni sehemu ya hali halisi ya leo. Ni sehemu ya utu wetu. Asiyefahamu historia mara nyingi hushindwa kuelewa dunia yetu ilivyo.

2. Historia inatupa mifano mingi juu ya maisha ya kibinadamu. Mifano hii inaweza kutusaidia tukiiga mifano mizuri na kuepukana na mifano mibaya.


1.2. UTAKATIFU NA KASORO ZA KANISA

Kanisa ni kitu kizuri na muhimu sana. Ni chombo cha Mungu cha kuunganisha waumini wake. Linatangaza Habari Njema. Linaleta neno la faraja kwa watu wanaotaka kukata tamaa. Linaombea watu. Linasaidia wenye dhiki. Linatetea haki za binadamu. Limepewa wito wa Mungu kuwapelekea watu Neno lake.

Hii ndiyo sababu ya kusema : NAAMINI KANISA TAKATIFU KATHOLIKO.

(hayo ni maneno ya Waanglikana kwa Kiswahili; Wakatoliki hutumia lugha "Kanisa takatifu katoliki"; Waprotestanti wengine hupendelea kutafsiri neno "katholiko / katoliki": Waluteri wanasema "Kanisa takatifu la Kikristo lililo moja tu"; Wamoravian hutumia maneno "Kanisa takatifu lililopo popote")

Lakini kanisa lina upande mwingine vilevile. Tukisikia habari za siku zetu tunaweza kusikia juu ya magomvi ndani ya kanisa fulani. Viongozi wanaweza kushindana. Vikundi vinaweza kujitokeza na kujitenga na kanisa. Mambo ya hela yanaweza kupata uzito kuliko mambo ya kiroho. Masharti ya ajabu yasiyo na msingi katika Biblia au mafundisho ya mitume, yanaweza kusimamishwa kwa ghafla na kutangazwa kuwa kitu cha lazima mbele za Mungu.

Tukiingia katika historia ya kanisa kwa undani tunapata habari nyingi za kusikitisha. Kumbe kanisa lina upande mwingine pia. Wakristo ni wanadamu. Wamepokea wokovu katika Kristo wako njiani ya kwenda mbinguni. Lakini bado ni wanadamu wenye dhambi na wenye kasoro. Kasoro hizo za kibinadamu zinaonekana pia katika historia ya kanisa.

Maswali na Maarifa (1.2.):

1. Taja mifano jinsi utakatifu wa kanisa unavyoonekana katika kazi zake.

2. Taja mifano ya kasoro za kanisa unazoziona.

3. Soma Mt. 13., 24-30. Je, ukilinganisha mfano huo na hali ya kanisa - ngano na magugu ni picha au mifano ya hali zipi ?

TUKUMBUKE:

Kanisa lina pande mbili:

1. Kwa kuwa kanisa ni la Kristo na limepewa wito wa kuwapelekea watu neno lake - kanisa ni takatifu.

2. Kwa kuwa kanisa ni la wanadamu, kumbe kanisa ni lenye kasoro.


Dini kuu katika Afrika

1.3. HALI YA UKRISTO KATIKA AFRIKA LEO

Leo karibu nusu ya Waafrika wote ni Wakristo. Idadi yao inaongezeka haraka. Wataalamu wanakisia ya kwamba mnamo mwaka 2000 zaidi ya nusu ya Waafrika wote watakuwa Wakristo. Lakini asilimia ya wakristo inaweza kuwa ndogo katika nchi kadhaa na kubwa katika nchi zingine. Katika nchi za Afrika ya Kaskazini Wakristo ni wachache. Lakini ni wengi kwa theluthi mbili za bara kusini ya Sahara. Kwa jumla Wakristo wanaishi kati ya wafuasi wa dini zingine, hasa Uislamu na Dini za Kiasili.

Kuongezeka kwa Wakristo kunaendelea haraka sana. Kila nukta (sekondi) nne Mwafrika mmoja anaingia katika Ukristo. Wengine huzaliwa katika familia ikiwa mzazi mmoja au wote wawili ni Wakristo tayari. Katika sehemu kubwa ya Kanisa iko desturi ya kuwabatiza watoto wadogo wa wazazi Wakristo. Ubatizo huo unawafanya kuwa wanakanisa. Wakikua watafundishwa na kukaribishwa kwenye Kipa Imara. Katika ibada hiyo kijana atarudia ahadi ya ubatizo wake na kuwekwa mikono na mchungaji au askofu na kuombewa ili Roho Mtakatifu amsaidie katika maisha yake ya kikristo. Madhehebu mengine hayabatizi watoto wadogo. Yanaweza kuwapokea katika kanisa kwa ibada maalumu lakini yanasubiri mpaka mtoto atakapokuwa mtu mzima halafu anaweza kupokea ubatizo na kuwa mkristo rasmi.

Njia nyingine ya kukua kwa kanisa ni njia ya kuongoka. Maana yake mtu asiye Mkristo anasikia habari za imani na kuvutwa moyoni. Halafu anafika kwa kiongozi wa ushirika wa kikristo na kupata mafundisho juu ya imani na maisha ya kikristo. Halafu anaweza kubatizwa. Atakuwa mwanakanisa katika dhehebu fulani lakini ni vilevile Mkristo katika kanisa moja takatifu la Bwana Yesu lililopo popote duniani. Wakristo waafrika walio wengi kidogo ni watu walioongoka wamewahi kuwa wafuasi wa dini nyingine. Wakasikia Habari Njema wakaamua kumfuata Yesu. Wengi wameshawahi kuwa watu wenye imani ya kidini, hasa kutoka dini za kiasili, wengine wachache kutoka Uislamu.

Watu wa Ujerumani wa karne ya 13 walimkumbuka Mtakatifu Morisi (St Maurice) kama Mwafrika aliyeleta imani ya Kikristo katika nchi yao (sanamu katika kanisa kuu la Magdeburg, Ujerumani)

Wakati mwingine tunaweza kusikia wazo la kuwa Ukristo ni imani iliyoingizwa Afrika juzijuzi tu, na asili yake ni kutoka Ulaya. Wazo hili si kweli. Ni shabaha mojawapo ya Kitabu hiki tupate kujua historia kubwa ya Ukristo na Biblia katika bara letu. Kwa jumla Ukristo ni imani ya kale sana katika Afrika. Tangu mwanzo wa imani yetu Wakristo Waafrika walikuwepo. Lakini ni kweli vilevile ya kwamba petu Tanzania historia si ndefu sana. Kanisa la Kiroma-katoliki lilikuwa na kumbukumbu ya miaka 125, na Wamoravian pia Walutheri walikumbuka miaka 100 ya kuwepo kwa makanisa yao 1991. Mabadiliko yalikuwa ya haraka sana. Mnamo mwaka 1900 Wakristo hapa Tanzania walikuwa wachache, kama maelfu tu. Leo hii wako mamilioni. Wakati ule kati ya Watanganyika 100 walikuwa 2 walio Wakristo. Leo hii ni karibu 40 hadi 50 kati ya Watanzania 100 walio Wakristo.


Maswali na Maarifa (1.3.):

1. Taja njia tatu ambazo watu huingia katika Ukristo

2. Ni sehemu ipi ya Afrika yenye Wakristo wachache ?

3.Hapa Tanzania umri wa kanisa ni miaka mingapi ?

4. Ni asilimia ngapi ya Watanzania wanaokisiwa kuwa Wakristo ?

TUKUMBUKE:

1. Leo hii Ukristo ni imani yenye wafuasi wengi katika bara la Afrika, hasa kusini ya Sahara

2. Ukristo una historia ndefu tangu miaka 2000 hapa Afrika

3. Maongezeko yalikuwa ya haraka sana hasa katika karne ya 20.

4. Leo hii kama nusu ya Watanzania wote ni Wakristo.


SURA YA PILI: WAKATI WA MITUME

1. Kanisa lilipoanza; 2. Ushirika wa kwanza; 3. Mazingira ya Ukristo wa kwanza; 4. Kazi ya mitume; 5. Mashahidi wa Imani


2.1. KANISA LILIANZA YERUSALEMU

Siku ya Pentekoste, jinsi ilivyochorwa na Wakristo wa Kale huko Syria mnamo mwaka 586 (muswada ya injili ya Rabula)

Mwanzo wa Kanisa ni kule Yerusalemu. Ni mji mkuu katika nchi ile inayoitwa kwa majina mbalimbali katika historia yake ndefu, kama Kanaani, Israeli, Palestina au Uyahudi. Mnamo mwaka 30 B.K. Yesu wa Nazareti alikufa msalabani. Aliuawa na serikali ya kikoloni ya Kiroma. Liwali (gavana) Mroma kwa jina Pontio Pilato alitoa hukumu ya mauti kwa sababu ya maombi ya viongozi wa kiyahudi. Yesu akashtakiwa mbele yake kuwa anataka kujipatia cheo cha Mfalme wa Wayahudi yaani kupindua utawala wa kiroma. Viongozi wayahudi wenyewe wakaona kosa lake ni kwamba alijitangaza kwa uwongo kuwa Masiyah au mwana wa Mungu. Lakini hilo halikuwa kosa machoni pa Waroma (ambao walikuwa wapagani) hivyo wakatumia mashitaka yaliyoeleweka mbele za Pontio Pilato.

Biblia inatuambia jinsi wafuasi wa Yesu walivyoanza kukata tamaa lakini baadaye wakakutana na Yesu aliyefufuka. Akaonana nao na kuwafundisha katika kipindi cha siku arobaini baada ya Pasaka akapaa mbinguni. Siku ya hamsini baada ya Pasaka wanafunzi wa Yesu walipokea Roho Mtakatifu. Matokeo yake ni kwamba wafuasi na marifiki wa Yesu walitoka nje ya mkutano wao. Wakaanza kumshuhudia Bwana wao mbele ya watu wote. Wengi wakasikia na wengi wakaamini wakabatizwa. Hapo ndipo mwanzo wa ushirika wa kwanza wa kikristo. Siku ile inaitwa "Pentekoste" (pentekoste ni neno la kigiriki, maana yake ni "hamsini" yaani siku 50 baada ya Pasaka).

PENTEKOSTE NI SIKUKUU YA KUZALIWA KWA KANISA.

Siku ya Pentekoste ya mwaka 30 B.K. mji wa Yerusalemu ukajaa wageni kutoka sehemu nyingi za dunia. Wakawa Wayahudi waliofika kwenye sikukuu ya Pasaka ya kiyahudi. Hapa ndipo tunaposikia ushuhuda wa Luka aliyeandika katika "Matendo ya Mitume" mlango wa pili ya kwamba kati ya wasikilizaji wa mahubiri ya wafuasi wa Yesu walikuwa watu kutoka Asia, Ulaya na nchi za Afrika ya Kaskazini, wakabatizwa.


Maswali na Maarifa (2.1.):

Soma Matendo ya Mitume 2 (ukifupisha: 2,1-15 + 2,37-42):

1. Wangapi walibatizwa siku ile ?

2. Je, kupokea kwa Roho Mtakatifu kulileta mabadaliko gani kwa wanafunzi wa Yesu?

3. Je, unaona majina gani ya kiafrika kati ya wasikilizaji wa Pentekoste ?

TUKUMBUKE:

1. Yesu alisulibiwa mn. mw. 30 B.K. kule Yerusalemu katika nchi ya Israeli kwa amri ya gavana wa kiroma Pontio Pilato

2. Mwaka uleule siku 50 baada ya kifo na kufufuka kwake ndipo siku ya Pentekoste. Wanafunzi wa Yesu walipokea Roho Mtakatifu

3. Waliacha hofu yote wakahubiri waziwazi.Tangu siku ile watu wasiomfahamu Yesu ana kwa ana wakabatizwa wakawa Wakristo. Pentekoste ni siku ya kuzaliwa kwa kanisa.

4. Waafrika walikuwapo tangu mwanzo katika kanisa.

2.2. USHIRIKA WA KWANZA YERUSALEMU - MFANO WA KANISA LA POPOTE

Je, kanisa la kikristo la kweli liweje ? Tuulize wanafunzi wenzetu:

JOHN: Kanisa la kweli ndipo penye upendo

MARIAMU: Ushirika wa kweli - ni watu wanaokaa pamoja, kusali pamoja, kusikia neno la Mungu pamoja, wanaosaidiana.

TUMAINI: Penye Roho Mtakatifu

BONIFAS: Tunapopokea baraka za Mungu na sakramenti takatifu

Bila shaka kila mmoja amejibu vizuri. Lakini mawazo haya yanatoka wapi? Wametunga mawazo yao wenyewe ? Hapana. Picha hii ya Kanisa la Kweli linatokea katika Biblia. Luka hasa ndiye aliyetupa picha ya Ukristo wa kwanza akiwa mwandishi wa kitabu cha "Matendo ya Mitume". Katika maelezo yake anakazia hasa tabia kadhaa za jumuiya ya wafuasi wa Yesu zenye umuhimu popote.

2.2.1. Kanisa la kindugu

Wote waliobatizwa siku ya Pentekoste waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali.(Mdo. 2,42).

Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja.(Mdo.2,44)

Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho mmoja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kukabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. ( Mdo. 4, 32-35 ).

Je, tunashangaa tukiona ya kwamba ushirika wetu leo unaonekana tofauti katika mambo mbalimbali? Tusishangae. Picha hii hatujapewa kama sheria ili lazima tuifuate. Ni mfano bora. Kila mahali mazingira ya Wakristo ni tofauti. Tangu miaka 2000 Wakristo wamepata kusikia tena na tena habari hizo wakapata mawazo mazuri jinsi gani kujenga jumuiya ya kindugu na ya kusaidiana katika mazingira yao hapa duniani. Mtaalamu mmoja akasema: Si ajabu ya kwamba wafuasi wa Yesu wakimwangalia Bwana wao aliyeketi mkono wa kuume wa Mungu Baba - kumbe wanaanza kubadilisha hali ya dunia !

Mpaka leo tabia kadhaa zilizotajwa katika Biblia zinakubalika kuwa alama za kanisa:

  • a.Kujifunza toka mitume wa Bwana Yesu walioandika habari za Injili
  • b.kuishi pamoja kindugu, na kuwasaidia wanyonge
  • c. kumega mkate, yaani kuishi na sakramenti
  • d. kusali

Hali ya kushirikiana mali zote haikuendelea kama utaratibu wa kawaida wa Wakristo wote. Lakini kutokana na mfano huu zimejitokeza jumuiya mbalimbali katika maisha ya kanisa. Tutasikia juu ya mifano yao baadaye.


2.2.2. Kugawana kazi: madaraka mbalimbali

Kila jumuiya inatumia mbinu zake za uongozi. Mkuu wa jumuiya ya wanafunzi ndiye Bwana Yesu tangu mwanzo. Lakini kama kundi ni kubwa kazi ya uongozi ni tofauti. Haiwezekani kufanya kila kitu pamoja watu wakiwa wengi. Ipo lazima ya kugawana kazi na madaraka. Swali hili limekuwa muhimu sana katika historia ya Ukristo. Njia mbalimbali zilitafutwa na kujaribiwa. Njia hizo za uongozi ndiyo zinaonyehsa tofauti muhimu kati ya madhehebu yetu mbalimbali. Kwa jumla njia hizo zote zinajaribu kuiga mifano tunayopata katika Biblia juu ya ushirika wa kwanza.

Je, katika Biblia tunaona ugawaji upi wa madaraka? Katika nyaraka za Paulo (ambazo ni maandiko ya mapema katika Agano Jipya) tunaona hali ya Ukristo mwanzoni kabisa. Paulo anataja mitume, manabii, walimu , wenye vipawa mbalimbali (I.Kor 12,28 nk), au maaskofu na mashemasi, pia wazee. Kwa jumla hakuna picha kamili ya utaratibu mmoja uliokuwepo kila mahali.

Katika ushirika wa kwanza kule Yerusalemu ni Mitume yaani marafiki wa Yesu wa karibu waliotumwa naye na kupewa kazi ya kueneza Habari Njema ndio walikuwa viongozi. Lakini baada ya muda mfupi kazi zilikuwa nyingi hivyo wakaongeza "Wasaidizi saba" walioitwa mashemasi. Wale Saba walishughulika hasa kazi za upendo yaani kuwagawia wajane na wazee misaada. Kati ya mitume ndio hasa Yohane, Petro na Yakobo walioitwa "nguzo" za ushirika. Baada ya kuondoka kwake Petro Yerusalemu Yakobo ndiye aliyeongoza ushirika huo.

Vyeo na shughuli maalumu zilizopo katika Ukristo leo, vina asili na mwanzo katika ugawaji wa madaraka kama ilivyokuwa wakati wa mitume.

Baada ya karne ya kwanza cheo cha "Askofu" kiliimarika sana. Pamoja na Uaskofu kikundi cha Wakristo wenye vyeo maalumu vya utumishi kilianza kutokea.

Pamoja na Askofu vyeo vya Kasisi na Shemasi vilikuwa kawaida. Mashemasi wa kike walipatikana pia mwanzoni, lakini walipotea baadaye kutokana na utamaduni wa mazingira ya kanisa uliokazia kipaumbele cha wanaume.

Katika karne za baadaye vikundi mbalimbali vilianza kupinga kuwapo kwa vyeo maalumu vya utumishi. Walisisitiza zaidi "Ukuhani wa Wakristo wote" maana yake kila mkristo hushiriki katika utumishi ulio mmoja tu katika Kanisa.

Makanisa mengine ya kiprotestant yamekumbuka sana matatizo ya utaratibu wa kiaskofu wakati wa karne za katikati kumbe waliona afadhali kuendelea bila cheo hicho. Wakatoliki, Waorthodoksi pamoja na makanisa kama Moravian na Anglikana yamehifadhi ngazi za kale yaani Uaskofu, Ukasisi na Ushemasi. Kwetu Tanzania Waluteri pia Wabaptisti wa aina ya A.I.C. wanaheshimu cheo cha Uaskofu. Lakini kimataifa sehemu ya Walutheri, na hasa Wapresbiteri (Reformed) na Baptist hawana Askofu wakisisitiza zaidi uwezo na haki ya kila Mkristo kushiriki katika shughuli zote za utumishi akichaguliwa.

2.3. MAZINGIRA YA UKRISTO WA KWANZA

2.3.1. Wayahudi

Yesu na wanafunzi wake wa kwanza walikuwa Wayahudi. Yaani walizaliwa katika uzazi wa Abrahamu wakiwa watoto wa Agano lililofanywa kati ya Mungu na Taifa lake la Israeli zamani za Musa. Waisraeli hawa waliitwa kwa jina "Wayahudi". Wakati wa Yesu Wayahudi walio wengi waliishi nje ya nchi ya Israeli / Palestina, hali iliyotokana na vita vingi vya zamani vilivyosababisha wakimbizi kuhamia nchi penye usalama zaidi.

Kwa upande moja Wayahudi walitoka katika ukoo wa Ibrahimu, hasa waliokaa Israeli/Palestina. Lakini watu wengine wa asili ya mataifa waliwahi kujiunga na imani ya Wayahudi na kuchukua hatua ya kuongoka na kutahiriwa. Katika mazingira yao Wayahudi walikuwa watu wa pekee waliomshuhudia Mungu mmoja tu. Walikuwa tofauti na wengine kwani hawakushiriki katika ibada ya miungu ya serikali na kutunza utaratibu wa sabato yaani kutotenda kazi siku ya saba.

Jumuiya za wayahudi zilipatikana katika miji yote mikubwa ya Afrika ya Kaskazini (hasa Misri na Libia), Ulaya ya Kusini na Asia ya Magharibi mpaka Uajemi. Mitume walizunguka awali hasa katika jumuiya za wayahudi kila mahali walipokwenda. Mwanzoni Kanisa lilionekana kama dhehebu la kiyahudi tu.

Baada ya kupokea watu kutoka mataifa bila kuwatahiri hali ilibadilika. Hapo ndipo sababu ya Mtume Paulo kusema: Kanisa ni taifa la Mungu kutoka kwa Wayahudi na Mataifa.

2.3.2. Dola la Roma

Dola la Roma mnamo mwaka 100 BK ilikuwa milki kubwa kwenye mabara matatu

Mji wa Yerusalemu, pamoja na nchi ya Israeli/Palestina ilikuwa chini ya Dola la Roma. Dola la Roma lilitawala maeneo yote yanayozunguka bahari ya Mediteranea. Mkuu wa Dola alikuwa na cheo cha "Kaisari" akikaa mjini Roma (Italia). Waroma walidai utii na kodi za mataifa na makabila yote yaliyokuwa chini yao. Lakini hawakuwa na neno juu ya utamaduni na dini za nchi hizo. Utawala wa kiroma ulirahisisha biashara na uchumi pamoja na mawasiliano katika maeneo haya yote. Waroma hawakuwa na mitambo ya injini lakini walikuwa wataalamu wa uhandisi. Walikuwa hodari sana kujenga barabara na nyumba za ghorofa. Majengo kadhaa waliyoyajenga husimama mpaka leo. Magofu ya miji yao yanaonekana leo hii kuanzia Misri na Algeria hadi Ujerumani na Asia. Wasanii wao walichonga sanamu za mawe za kudumu. Unaweza kuziona katika picha mbalimbali za kitabu hiki.

  • Tazama ramani na kutaja nchi za leo zilizokuwa zamani chini ya Dola la Roma!

Israeli/Palestina ilikuwa na serikali yake ya kiyahudi lakini pia na liwali au gavana wa kiroma. Waroma walizima kwa ukali majaribio yote ya kupinda utawala wao. Wayahudi katika Israeli walijaribu mara mbili kuwafukuza Waroma nchini: mw. 70 na 135 B.K. Kila safari Waroma walilipiza kisasi, wakichoma moto miji na vijiji na kuwafanya wananchi kuwa watumwa (taz. chini).

2.3.3. Sehemu zingine za dunia

Miaka 2000 iliyopita mawasiliano kati ya nchi na nchi hayakuwa rahisi. Hapakuwa na redio wala simu wala ndege wala magari. Usafiri ulikuwa kwa miguu au kwa kutumia wanyama (k.v. farasi, ngamia, punda), halafu kwa meli za tanga. Meli hizo ziliweza kufuata pwani tu hazikuwa imara kutosha kuvuka Bahari kubwa. Lakini hata kwa vyombo hivi iliwezekana kufanya biashara kati ya Mediteranea na nchi za mbali kama Bara Hindi au Afrika ya Mashariki.

Tunafahamu kitabu kimoja kilichoandikwa mw. 100 B.K. na kueleza usafiri wa baharini kutoka Misri hadi pwani ya Afrika ya Mashariki. (iliyoitwa kwa jina "Azania" na Wagiriki). Lakini watu waliojua habari hizo walikuwa wachache.

Jangwa la Sahara lilikuwa kizuizi kikuu cha mawasiliano na usafiri kati ya sehemu kubwa ya Afrika na sehemu zingine. Mabara ya Marekani na Australia hayakujilikana kwa wataalamu wa Asia, Afrika na Ulaya. Watu wengi waliamini dunia kuwa tambarare yenye umbo la duara (kama sahani), ingawa wataalamu wengine katika Misri waliishagundua kwa njia ya kupima dunia kuwa na umbo la chungwa. Lakini si watu wengi walioamini wala kujali elimu hizo. Ilikuwa nje ya upeo wao.

Hali hii ilibadilika tu karne nyingi baadaye wakati meli za kuvuka hata bahari kubwa zilipopatikana.

Tukiona ya kwamba Asili ya Ukristo ni eneo la Yerusalemu tunaweza kuelewa jinsi gani mitume wa Kristo waliweza kutumia usafiri uliopatikana wakati ule na kufika nchi zilizojulikana katika mazingira yao lakini hawakufika mbali zaidi.


2.4. KAZI YA MITUME

Upendo alisali kanisani. Pamoja na waumini wote akasema maneno yafuatayo:

Naamini kanisa moja, takatifu, katholiko na la kimitume.

Maneno haya yamo katika "Imani ya Nikea" inayotumiwa katika makanisa mengi hasa wakati wa ibada za sikukuu. Nyumbani anamwuliza kaka : "Je, unaelewa wewe kwa nini sisi tunaendelea kuwakumbuka mitume wa Yesu? Mbona ni wanadamu tu waliokufa muda mrefu?"

Kaka akamjibu: "Upendo, imani yetu ni juu ya Yesu. Alikuja kwelikweli hapa duniani. Alichagua kuja katika nchi ile ya Israeli miaka 2000 iliyopita. Akawachagua wanafunzi wake ambao tunawaita "mitume". Nadhani alikuwa na maana kufanya hivyo. Basi ikiwa Biblia inatupa habari za aina hii hebu tuziangalie. Wale Mitume ni mifano ya Ukristo wetu katika nguvu au karama zao, lakini pia katika udhaifu wao."

Kumbe mitume ndio waliotekeleza maagizo ya Bwana Yesu "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyoamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dhahari." (Mt. 28,19.20)

2.4.1. Petro

Petro ni jina lenye maana ya "Jiwe" au "mwamba". Alikutana na Bwana Yesu akiwa mvuvi. Akaendelea kuwa rafiki yake wa karibu sana pamoja na Yohane. Yesu alipokamatwa Petro alitaka kutumia upanga wake ili amtetee. Lakini alipoulizwa baadaye kama yeye ni rafiki wa Yesu akaogopa akasema hamjui. Katika ushirika wa Yerusalemu alikuwa kiongozi muhimu ("nguzo za ushirika": Yohane, Petro, Yakobo). Alikuwa Mtume wa kwanza aliyempokea mtu asiye Myahudi katika kanisa. (Mdo.8 - taz. chini). Baadaye akaitwa katika mji mkubwa wa Antiokia akaongoza ushirika kule. Katika taarifa ya Luka (Kitabu cha matendo ya mitume) tunamwona tena Yerusalemu alivyokutana na Paulo na kushauriana juu ya kupokea wapagani katika Ukristo. Agano jipya inatupa nyaraka mbili zilizoandikwa katika jina lake. Kumbukumbu ya kale inasema ya kwamba alifika mpaka Roma. Hapo alikufa pamoja na Paulo katika mateso ya kwanza ya Wakristo chini ya serikali ya kiroma. Amesulubiwa kama Yesu.

Kanisa la Roma linamkumbuka kama askofu wake wa kwanza. Kila Papa wa kanisa la Katoliki huitwa "mfuasi wa Petro" kwani anashika cheo cha Askofu wa Roma kinachoaminika kuwa cheo cha kwanza kati ya maaskofu wote duniani.

Petro ni mfano mzuri kwa nguvu na udhaifu katika maisha ya kikristo.

  • Alikuwa na moyo kubwa kumtetea Bwana Yesu kwa upanga asikamatwe - lakini mpaka siku ile hakuelewa kwamba njia ya Yesu si njia ya silaha.
  • Alitaka kuwa karibu na Yesu - lakini kwa hofu akamkana.
  • Akamwingiza jemadari mpagani Mroma katika kanisa - lakini baadaye akanyamaza mbele ya mitume wengine wa Yerusalemu waliosema kwamba mpagani asiingie katika ushirika mpaka ametahiriwa na kuwa Myahudi kwanza halafu anaweza kumpokea Kristo.
  • Mwishoni mwa maisha yake Petro akawa shahidi wa damu kwa Bwana wake akafa msalabani kule Roma.

2.4.2. Paulo

Paulo hakuwa mfuasi wa Bwana Yesu alipotembea duniani. Alikuwa Myahudi mzaliwa wa Tarso (mji wa Asia Ndogo). Akaenda Palestina kwa masomo ya kidini. Akawa Mfarisayo. Tunasikia habari zake alivyotazama kifo cha Stefano (Mdo.6). Baadaye akatumwa na Baraza Kuu la Kiyahudi kuwatafuta Wayahudi waliojiunga na Ukristo na kuwakamata kama wakosaji. Aliposafiri Dameski (mji mkuu wa Siria) Bwana Yesu alimtokea katika ono akaongoka kuwa Mkristo. Mtesaji wa Wakristo akawa mhubiri wa Injili.

Hakuna mwingine aliyesafiri, kuhubiri na kuanzisha shirika kama Paulo kati ya mitume wote. Katika safari kubwa tatu alizunguka Asia na Ulaya ya Kusini. Akaendelea kufundisha shirika alipoondoka kwa njia ya barua (au nyaraka) zake. Nyaraka mbalimbali zimehifadhiwa katika Agano Jipya. Katika nyaraka hizo Paulo anaonekana kuwa mtaalamu wa Sheria ya Kiyahudi jinsi ilivyo katika Agano la Kale. (Labda hapo ndipo sababu moja ya kwamba wengine huona maandiko ya Paulo ni magumu). Akatetea kupokea wapagani katika Kanisa akafundisha jinsi gani uhuru katika Kristo unavyopita masharti ya sheria ya kale.

Mwishoni akakamatwa kule Yerusalemu akashtakiwa ya kuwa amehatarisha utawala wa kiroma. Kama mzaliwa wa Tarso alikuwa na uraia wa Roma akadai haki yake ya kuchukua rufaa kule Roma mbele ya Kaisari. Akapelekwa Roma (Mdo. 28).

Hatuna uhakika juu ya kesi yake. Labda alipata nafasi ya kusafiri tena na kuhubiri Injili mpaka Hispania. Lakini kumbukumbu ya kale inatuambia kwamba alisulubiwa katika mateso ya Wakristo ya kwanza pamoja na Petro mwaka 64 bK.

Paulo ni mfano mzuri jinsi gani mtu aliyepinga Injili vikali ameongozwa kuhubiri imani hiyo.

  • Nyaraka zake zinatuonyesha jinsi gani Mkristo anaweza kutumia akili zake pamoja na imani.
  • Katika maandishi yake tunapata mtu aliyebebwa na imani katika matatizo na mateso makubwa.
  • Anatufundisha kutoangalia imani kuwa kama sheria au amri tu (Fanya! Acha!) lakini kuwa jibu la upendo wa mtu aliyeelewa upendo wa Mungu kwanza.

2.4.3. Marko

Marko ndiye hasa mwinjilisti wa Afrika. Hakuwa mwanafunzi wa Bwana Yesu lakini aliandika Injili yaani taarifa juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Alikuwa mwandishi wa kwanza wa habari hizo. Mathayo na Luka walitumia taarifa ya Marko walipoandika injili zao. Wazazi wa Marko walitoka katika eneo la Kurene (Libia). Marko mwenyewe alisafiri pamoja na Petro alikuwa kama mwanafunzi wa Petro.

Wakristo wa Misri wanamkumbuka Marko kuwa ndiye aliyefika Aleksandria na kuhubiri Habari Njema. Hivyo akaanzisha Kanisa la Kristo kule Afrika. Anakumbukwa kama Askofu wa kwanza wa Aleksandria. Anasemekana alikufa akiwa shahidi wa imani. Mpaka leo Askofu Mkuu wa Aleksandria huitwa "Mfuasi wa Marko" .

2.4.4. Thoma

Mtume anayekumbukwa sana kule India ni Thoma (au: Tomaso) aliyefika mpaka Bara Hindi. Kaburi lake huonyeshwa katika mji wa Madras. Mpaka leo wako "Wakristo wa Thoma" kusini-magharibi mwa Bara Hindi. Kanisa hili kwa muda mrefu lilikosa mawasiliano na wakristo wengine waliokuwa mbali lakini siku hizi linashiriki katika umoja wa makanisa duniani.


Maswali na Maarifa (2.2 - 2.4.)

1. Nani anakumbukwa kuwa Askofu wa kwanza wa Roma ?

2. Nani alikuwa Mwinjilisti mkuu wa Afrika wakati wa mitume ya kwanza?

3. Nani alifungua milango ya kanisa hasa kwa ajili ya wapagani wasikuwa Wayahudi ?

4. Taja alama za Kanisa kufuatana na Luka.

5. Linganisha orodha ya yaliyomo na ramani za Biblia yako. Majina ya miji ipi yanapatikana katika majina ya nyaraka ?

TUKUMBUKE:

1. Ni mitume walioanza kueneza Injili mahali pengi wakitekeleza agizo la Bwana Yesu.

2. Mtume Paulo alianzisha shirika nyingi na kuwavuta waumini kutoka mataifa (wasio Wayahudi)


2.5. MASHAHIDI WA IMANI- MATESO KATIKA DOLA LA ROMA

2.5.1. Mashahidi leo

Askofu Janani Luwum

Mwaka 1977 Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda (Kianglikana) Janani Luwum aliuawa kwa amri ya Raisi wa Uganda, Idi Amin. Kosa lake lilikuwa ya kwamba hakunyamaza mbele ya maovu yaserikali akiandika barua pamoja na viongozi wengine wa kanisa kwa rais huyu kulaumu matendo mabaya ya wanajeshi wa serikali waliowatesa wananchi. Alijua hatari lakini aliona anawajibika kuwalinda Wakristo wake. Askofu Luwum anakumbukwa mpaka leo kama shahidi wa imani, yupo katika mfuatano wa mashahidi wengi tangu mwanzo wa Ukristo. Kifo chake kimesikitisha sana. Lakini vilevile kiliwapa Wakristo moyo kutonyamaza mbele ya uongo na maovu. Moyo huu umeonekana tangu mwanzo katika Ukristo. Kumbe tuangalie asili yake katika Ukristo wa kwanza.

2.5.2. Kristo na miungu mingi

Sanamu iliyohifadhiwa ya Kaisari Domitiano aliyeabudiwa kama mungu; sadaka zilichomwa mbele yake

Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika mabara matatu. Ni mataifa mengi walioishi chini ya utawala wake. Utawala huo katika nchi zinazozunguka Mediteranea ulianza kabla ya Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya tano baada ya Kristo. Kwa jumla serikali iliwaachia watu uhuru waendelee na desturi au mila zao ila tu lazima walipe kodi na kukubali utawala mkuu. Watu wengi sana walikuwa na imani ya miungu mingi. Waliabudu mahekaluni mbele ya sanamu za miungu ile. Walikuwa na imani ya kwamba miungu ilifanana kiasi na wanadamu ila tu miungu ni mikubwa na yenye nguvu zaidi na inaishi milele. Vinginevyo waliamini miungu kuwa na tabia nyingi zinazofanana na tabia za kibinadamu. Kwa upande mwingine waliamini ya kwamba hata mtu anaweza kupanda ngazi na kuwa kama Mungu akiwa na sifa za kutosha zinazokubalika mbele za miungu yote na hasa mungu mkuu. Hapa ndipo asili ya kumtangaza mtawala mkuu au Kaisari wa Roma kuwa na sifa za kimungu.

Katika karne ya kwanza B.K. Kaisari Domitiano alianza kudai ibada za kimungu kwake mwenyewe. Popote katika eneo kubwa la Dola la Roma watu waliitwa kusimamisha sanamu zake na kumwabudu. Kwa wakazi wengi jambo halikuwa geni sana maana yake jina moja liliongezeka katika orodha ya miungu iliyoabudiwa. Lakini kwa Wakristo tendo hili lilikuwa gumu mno. Imani ya kikristo hukataa kuwepo kwa miungu mingi vilevile hukataa kuiabudu.

Kumbe Wakristo walikataa kuabudu sanamu za Kaisari. Tendo hili lilionekana kama kusaliti serikali. Wakuu wa mikoa na majimbo walianza kuwaadhibu wale wanaokataa ibada hii. Lakini katika mwendo wa miaka ibada za sanamu za Kaisari zikaongezeka. Matatizo yakakua dolani. Vita vikaongezeka, uchumi na biashara vikashuka chini. Thamani ya fedha ikapungua. Watu wengi wakaanza kukata tamaa na kutafuta msaada katika dini mbalimbali. Kumbe mafundisho ya kidini yalizidi. Hapa ndipo wazo lilikua ya kuwa anayekana kuwepo kwa miungu ni hatari kwa umma. Ni mwasi atakayesababisha hasira ya miungu juu ya watu wote. Kumbe lazima aadhibiwe.

Mateso ya kwanza yalitokea mwaka 64 B.K., ya mwisho yalikwisha mw. 309 B.K. Katika kipindi hiki kirefu, vilirudia tena na tena vipindi vya mateso vilivyoongozana na vipindi vya starehe. Lakini miaka yote Ukristo ulikuwa dini isiyo halali. Kila mwezi mateso yaliweza kuanza upya.

Wakristo walifanya nini katika hali hiyo? Kwanza kabisa walijenga utaratibu mzuri wao kwa wao kufundishana na kusaidiana katika matatizo. Halafu wakakaza sana mafundisho ili waumini wasimame imara katika matatizo na madhulumu. Wakaendelea kuombea serikali na watu wote. Wakajitahidi kuonyesha kwa maisha na matendo yao ya kwamba Ukristo ni imani yenye amani na upendo isiyoharibu umma. Wakakutana katika nyumba za watu binafsi, au kule Roma pia kwenye "katakombi" yaani makaburini kwani polisi haikuruhusiwa kuingia makaburini.

(Taz. chini "Ukristo wa Afrika" mbele juu ya mateso ya Wakristo kule Roma.)


2.5.3. Mfano: Miungu ya kale katika lugha ya Kiingereza

Katika utamaduni wa kimila wa kibantu hakuna mawazo juu ya miungu mingi. Katika mapokeo ya babu zetu Mungu ni mmoja lakini kuwasiliana naye ilikuwa kwa njia ya mizimu hasa, sio moja kwa moja. Kumbe katika sehemu nyingi za dunia utamaduni wa kiasili ulikuwa na imani ya miungu mingi. Imani hizi zilipatikana katika mazingira ya Taifa la Israeli na pia wakati alipoishi Bwana Yesu. Dini za miungu mingi zilikuwa kawaida katika Afrika ya Kaskazini, Ulaya na sehemu nyingi za Asia kabla ya uenezaji wa Ukristo.

Lugha ya Kiingereza inatunza mpaka leo kumbukumbu ya miungu mingi iliyoabudiwa katika utamaduni wa Ulaya ya Kale kabla ya kuingia kwa Ukristo. Majina ya siku za juma mpaka leo ni majina ya miungu ambayo siku ziliaminiwa kuwa chini ya ulinzi wao hasa.

Siku

Mungu

(Kazi yake)

Sunday

Jua

(kutupa maisha: kutoa mwanga na joto – yote mbili muhimu hasa katika nchi baridi za Kaskazini )

Monday

Mwezi

"moon-day"

Tuesday

Tiu

(Mungu wa haki na sheria)

Wednesday

Wodan

(Mungu wa vita)

Thursday

Thor

(Mungu Mkuu, Bwana wa hali ya hewa <ngurumo>, mlinzi wa rutuba shambani)

Friday

Fria

(Mama wa Miungu, mlinzi wa unyumba na ndoa)

Saturday

Saturn

(Mungu wa kiroma wa mavuno, mlinzi wa kuzimu)

Kati ya miungu mingi iliyoabudiwa kila mmoja aliaminika kuwa na idara yake alipotawala hasa, kama vile Hali ya Hewa, vita, kifo, uponyaji, mavuno, mifugo, biashara , nguvu za kuzaa n.k.. Miungu iliyomaanisha nyota au sayari kama vile Jua, mwezi na Saturn (Zohali kwa Kiswahili) ilikuwa mapokeo ya kiroma, sio asili ya kiingereza.


Maswali na Maarifa (2.5.):

1. "Shahidi wa imani" ni Mkristo mwenye sifa gani?

2. Wakazi walio wengi katika Dola la Roma walikuwa na dini gani?

3. Kwa nini Wakristo waliteswa chini ya Dola la Roma?

4. Waliowatesa Wakristo waliogopa nini au walikuwa na sababu gani?

5. Kwa nini Janani Luwum huitwa "Shahidi wa Imani"?

TUKUMBUKE:

1. Katika karne tatu za kwanza Wakristo waliteswa sana katika Dola la Roma.

2. Mateso haya yalisaidia kuimarisha kanisa.

SURA YA TATU: MWANZO WA UKRISTO KATIKA AFRIKA

1. Afrika wakati wa Biblia 2. Mateso na kukua kwa kanisa katika Afrika 3.Misri: Elimu na Umonaki, Chuo cha Aleksandria 4. Agostino ; 5. Ethiopia na Nubia; 6. Kuja kwa Uislamu


Je, Baba . . .?

Tegemea anamwuliza baba yake ambaye ni mwalimu wa historia.

Tegemea:: Je, baba ni kweli ya kwamba Ukristo ni dini ya kizungu haifai kwetu Afrika ?

Baba:: Nani amesema ?

Tegemea:Juma amesoma katika kitabu.

Baba: Basi umwulize kama kitabu chake kinasema pia ya kwamba Injili iliwahi kufika Afrika kabla ya kuingia Ulaya.

Tegemea: Je, ni kweli baba? Ukristo uliwahi katika Afrika kuliko Ulaya ?

Baba:: Ndiyo ni kweli, kidogo iliwahi petu. Kule Misri na Ethiopia waliishajenga makanisa wakati Waingereza na Wajerumani bado waliabudu miungu yao chini ya miti.

Tegemea:: Lakini baba, mbona wengine wanasema wamisionari walitoka Ulaya ?

Baba:: Hicho ni kitu kingine kwa jinsi ilivyokuwa hapa kwetu Tanzania. Lakini juu ya asili ya imani yetu unaweza kujibu mwenyewe. Yesu aliishi wapi?

Tegemea:Kule Yerusalemu katika nchi ya Israeli.

Baba: Tazama ramani. Kutoka Israeli ni karibu kwenda wapi - Afrika au Ulaya ?

Tegemea: Kweli baba Afrika iko karibu sana kutoka Israel kushinda Ulaya.

3.1. AFRIKA WAKATI WA BIBLIA

Wakati wa Yesu Afrika ya Kaskazini ilikuwa chini ya utawala wa kiroma. Wakati ule wakazi hawakuwa Waarabu. Kiutamaduni palikuwa na sehemu mbili: Misri upande wa Mashariki na nchi za Waberiberi upande wa Magharibi. Nchi hizi za Waberiberi (Maroko, Algeria, Tunisia na Libia za leo) zilikuwa pia na miji mingi walipokaa wahamiaji kutoka Italia waliotumia lugha ya kilatini. Mji mkuu wa sehemu ile ni Karthago (leo: Tunis). Mji mwingine unaoonekana katika Biblia ni Kurene (kule Libia). Misri ilikuwa kitovu cha utamaduni wa juu tangu karne mingi. Mji mkuu wa Misri ulikuwa Aleksandria. Eneo la utawala wa kiroma lilifika mpakani mwa Sudani ya leo (eneo lililoitwa "Nubia").

Nchi hizo hazikuwa na mawasiliano mengi na nchi za kusini mwa jangwa kubwa la Sahara lililozuia usafiri. Lakini mawasiliano yalikuwepo na sehemu zingine za Ulaya ya Kusini na Asia, hasa kupitia Bahari ya Kati (Mediteranian). Kumbe ilikuwa rahisi kwa mitume wa Kristo kutumia mawasiliano haya yaliyokuwepo tayari. Hivyo imani ya kikristo ilifika haraka katika sehemu ya Kaskazini mwa Sahara lakini haikuvuka jangwa kubwa. Watu wa Mediteraneo walifanya tayari biashara kwa meli na pwani la Afrika ya Mashariki. Tunaweza kuwaza ya kwamba wafanyabiashara wakristo walitembelea mapema sehemu zetu lakini hakuna kumbukumbu yoyote kama walihubiri n.k.

Nchi hizi za Afrika ya Kaskazini zilikuwa tajiri. Hali ya hewa wakati ule ilikuwa afadhali kwa kilimo kuliko leo. Milima ya Atlas ilijaa misitu. Sehemu za Algeria na Tunisia ya leo ililimwa ngano kwa wingi na kuilisha Italia. Hata jina la "Afrika" lina asili yake katika kipindi cha kiroma. Nchi hizo kusini mwa Mediteranea zikaitwa kwa jumla "Ethiopia" au "Libia". "Afrika" ilikuwa jina la mkoa moja uitwao leo Tunisia. Kutoka kule jina hili lilitumika baadaye kwa sehemu zingine za bara letu.

Kwa jumla watu walifuata dini zao za asili za kuabudu miungu mingi. Palikuwa na mchanganyiko wa imani mbalimbali. Wanajeshi waroma waliokaa katika nchi nyingi walileta miungu yao na kuwajengea mahekalu pale walipokaa. Kule Misri na sehemu za Kurene waliishi pia Wayahudi wengi waliotumia hasa lugha ya kigiriki. Kwa njia ya Wayahudi hawa habari za Mungu mmoja zilikuwa zinasikika sehemu nyingi.

Watu wa Afrika ya Kaskazini walisafiri na kukaa pia katika miji ya Ulaya na Asia. Kutokana na mawasiliano mazuri tunaona Waafrika mbalimbali katika taarifa za Agano Jipya.

Tuangalie mifano

  • Yesu alipobeba msalaba wake kule Yerusalemu akaanguka chini. Maaskari wakamkamata mtu aliyepita mtaani jina lake ni Simeon Mkurene. Jina linaonyesha ya kwamba alikuwa mgeni kutoka Kurene (Libia). Lk. 23,26
  • wakati wa ushirika wa kwanza kule Yerusalemu Filipo alikutana na msafiri kutoka Kushi akambatiza. Kushi ni jina la kale la sehemu ya Sudan ya leo (matoleo mengine ya Biblia hutafsiri: Mhabeshi au Mwethopia). Mdo.8,26ff.
  • katika ushirika wa mji mkubwa wa Antiokia (Asia ya Magharibi) tunasikia juu ya watu wa asili ya kiafrika waliokuwa viongozi wa ushirika huu. Mmoja ni Lukio Mkurene (taz. juu). Mwingine ni "Simeoni aitwaye Nigeri". Neno "Nigeri" linatafsiriwa "Mweusi" katika toleo la Kiswahili cha Kisasa ndiyo maana yake. Kumbe hata huyu Simeoni anaonekana ametoka Afrika kutokana na rangi yake. Mdo. 13

Haya yote si ajabu. Nchi za Misri mpaka Sudan na Afrika ya Kaskazini-Magharibi zilikuwa sehemu ya dunia ya kiroma wakati ukristo ulipoanza kuenea .

Yesu mwenyewe alikaa miaka kadhaa Afrika. Alitoka nje ya Israeli-Palestina mara moja tu katika maisha yake wakati wazazi wake walipokimbilia pamoja naye Misri kwa sababu Mfalme mbaya Herode alitaka kumwua mtoto Yesu. Mpaka leo Wakristo wenyeji wa Misri wanatunza kumbukumbu ya Familia Takatifu katika nchi yao. Makanisa mbalimbali yapo mahali panapokumbukwa ya kwamba Yusefu, Maria na mtoto Yesu walipumzika.

Hatuna habari ndani ya Biblia juu ya shirika za kwanza zilizoundwa kule. Lakini Wakristo wa Misri wanamkumbuka Marko aliyefika Aleksandria na kuanzisha kanisa pale Misri. Anasemekana alikufa wakati wa mateso ya kwanza chini ya serikali ya kiroma.

Kule chini tutaangalia habari za kihistoria zinazojulikana juu ya nchi za Sudan na Ethiopia.

Maswali na Maarifa (3.1.):

1. Maisha ya Bwana Yesu yaligusana kivipi na Afrika?

2. Kaskazini ya Afrika ilihusiana kivipi na sehemu zingine za dunia ?

3. Nani alianzisha Ukristo kule Misri?

4. Kwa nini Ukristo wa Kale haukuenea katika Afrika yote?

5. Watu wengi katika Afrika ya Kaskazini walifuata dini gani?

6. Taja Waafrika waliokuwa viongozi katika kanisa wakati wa Biblia.

======
TUKUMBUKE: ====== 1. Ukristo una uhusiano wa karibu sana na Afrika tangu mwanzo.

2. Kaskazini ya Afrika ilikuwa sehemu ya Dola la Roma.

3. Waafrika walikuwapo kati ya viongozi wa kanisa la kwanza.


3.2. MATESO NA KUKUA KWA UKRISTO WA KALE AFRIKA

3.2.1. Je,Mkristo anaweza kuwa mdhaifu?

Tuntufye na Alex wanajadiliana juu ya udhaifu na dhambi.

Alex: Ukimpokea Kristo kweli huwezi kuwa na dhambi tena.

Tuntufye: Lakini udhaifu upo yaani Mkristo anaweza kushindwa na tamaa zake au hofu, sivyo?

Alex: Hapana, ukimpokea Kristo kweli udhaifu hautakushinda tena.

Tuntufye: Kumbe, unaona ni dhambi kumkana Kristo?

Alex: Ndiyo, ni dhambi kwani Biblia inatuambia "Ukimkiri Yesu kwa mdomo na kuamini moyoni utaokoka" (Rum 10:9) hivyo kukana ni dhidi ya amri hiyo.

Tuntufye: Lakini unaonaje ikiwa Mkristo anaficha imani yake hata kusema hamjui Kristo kwa sababu anaogopa hatari ? Kama vile pale Uchina wakati wa Mapinduzi ya Kiutamaduni walipobomoa makanisa na kuchoma Biblia motoni? Je walitenda dhambi walioficha Ukristo wao ? Au hawakuwa Wakristo wa kweli bali wale tu waliokuwa tayari kupigwa hata kukamatwa?

Alex: Kama alikuwa Mkristo kweli hawezi kuogopa kuonekana kama mtu wa Yesu.

Tuntufye: Mimi naona unaweka masharti makali sana. Mbona hata Yesu alionyesha huruma kwa Petro aliyemkana. Kama udhaifu ni dhambi basi Petro alikuwa na dhambi aliposema hamjui Yesu. Lakini Yesu alimwita mwanafunzi wake wakati anajua udhaifu wake. Na alimtuma kuhubiri Injili baada ya kukanwa naye Petro.

3.2.2. Mateso chini ya Roma

Wakati wa karne ya pili tunapata habari nyingi juu ya Wakristo kule Misri na Karthago vilevile. Habari zile zinaeleza mateso na maisha ya Wakristo wale.

Wakristo wa kwanza waliishi chini ya serikali ya Roma. Kwa jumla iliwaruhusu watu wote kuendelea na desturi na dini zao. Serikali iliona ni muhimu kuabudu miungu yote kwani ingekuwa hatari ikiwa mungu fulani anasahauliwa hata kusababisha akasirike. Soma Matendo ya Mitume 17, 16-23. Paulo alishangaa kuona sanamu nyingi za miungu kule Athene. Kati ya sanamu hizo aliona madhahabu (altare) yaliyotengwa kwa ajili ya "Mungu asiyejulikana". Kumbe serikali ya Athene iliogopa kumsahau mungu yoyote ikatoa sadaka za tahadhari.

Kaisari yaani Mfalme Mkuu wa Roma alipewa heshima ya kimungu naye. Raia walitakiwa kushiriki katika ibada za kumtolea sadaka mbele ya sanamu zake. Kwa watu wengi waliozoea kuabudu miungu mingi haikuwa vigumu sana kumwingiza Kaisari kama mungu wa nyongeza katika mawazo yao. Lakini kwa Wakristo haikuwezekana kushiriki katika ibada hizo. Kumbe walionekana kama maadui wa serikali. Walikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani.

Ukali wa mateso ulitegemea siasa ya wakuu wa mikoa ya kiroma. Wakati mwingine waliweza kujipatia sifa wakitoa taarifa ya kwamba wamekamata Wakristo wengi na kuwahukumu. Wakati mwingine waliona afadhali kuwaacha Wakristo na kutosababisha vurugu katika utaratibu wa mkoa. Nje ya swali la kidini Wakristo walikuwa raia wema.

3.2.3. Perpetua na Felista

Mnamo mwaka 203 B.K. aliishi mama kijana kwa jina Perpetua katika mji mkubwa wa Karthago (Tunis). Perpetua alikuwa mtoto wa familia tajiri mwenye miaka 22 alikuwa na mtoto wa kiume. Wazazi walikuwa wananchi walioheshimiwa sana. Kumbe Perpetua akashtakiwa kuwa mkristo akakamatwa. Baba akamwendea mkuu wa mkoa wakapatana Perpetua atoe sadaka mbele ya sanamu ya Kaisari na mashitaka yangefutwa. Kutoa sadaka maana yake ni kushika nafaka kidogo na kuitupa kwenye karai ya mkaa uliowaka mbele ya sanamu.

Baba akamweleza mtoto wake gerezani alivyopatana na mkuu wa mkoa. Perpetua akakataa. Baba akamsihi akamwomba asilete aibu juu ya wazazi wake amhurumie mtoto mdogo. Perpetua akamjibu Baba ya kuwa tendo hilo halipatani na imani yake. --

Felista alikuwa msichana mtumwa. Naye alikuwa mkristo na wanawake wote walikuwa marafiki ingawa Felista alikuwa mtumwa. Akafungwa ndani pamoja na Perpetua na vijana watatu. Walipokataa kutoa sadaka wakapewa wote hukumu ya mauti. Vijana Wakristo watano wakapelekwa katika uwanja wa michezo wa Karthago. Watu wengi wakatazama. Kuua wakosaji kulikuwa kama mchezo au burudani kwa wakazi wa miji. Walizoea kutazama maonyesho ya kuua wakosaji wenye hukumu ya mauti. Vijana Wakristo waliposimama uwanjani milango ya chini ikafunguka. Wanyamapori wakali waliokuwa wanahifadhiwa katika vyumba vya chini katika viwanja hivyo, wakiwekwa tayari ili kuwararua wakristo wakatokeza. Kuwatupa wakristo mbele ya wanyama hawa wakali ilifanywa kama onyesho la kuburudisha halaiki. Hawa vijana wakashambuliwa na wanyama; wengine wakawaua na wengine wakajeruhiwa vibaya. Mwishoni wote waliojeruhiwa waliuawa kwa upanga.

Maonyesho haya yalikusudiwa kutisha watu waogope kuwa Wakristo. Lakini yakageuka kuwa kama kampeni kwa ajili ya Ukristo. Watazamaji wakaanza kujiuliza: Je, watu wale wana kosa gani? Ni imani gani inayowapa nguvu ya kusimama mbele ya wanyama mwitu na kuuawa badala ya kutoa sadaka mbele ya sanamu? Kwa nini wale wanaokufa wanajulikana kuwa watu wasioiba wala kusema uongo lakini wengine wenye tabia mbaya hawana matatizo wakitoa sadaka tu mbele ya sanamu?

Kumbe damu ya mashahidi ilikuwa mbegu ya kukua kwa kanisa.

Katika karne ya tatu mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hii ilikuwa uasi. Wakaona lazima kuzima uasi huo. Kati ya miaka 302 na 308 B.K. maelfu wakauawa kule Aleksandria. Wakakatwa vichwa vyao na maaskari, wakapelekwa katika kiwanja cha michezo mbele ya wanyama mwitu, wakachomwa motoni. Lakini idadi ya Wakristo waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaaua. Kumbe mwaka 312 ilikuwa kama ukombozi kwa mji wa Aleksandria. Kaisari mpya kwa jina Konstantino akatangaza mwisho wa mateso. Akatoa sheria ya kuwa Ukristo ni dini halali katika Dola la Roma.

Kwa kweli si Wakristo wote waliosimama imara mbele ya vitisho. Wengi wakatoa sadaka mbele ya sanamu wakatubu baadaye na kuomba wasamehewe udhaifu huo. Wengine waliwahonga maafisa wa serikali wakanunua vyeti vilivyothibitisha ya kwamba walitoa sadaka zile ingawa si kweli. Katika eneo la Karthago jambo hili lilisababisha mfarakano ndani ya Kanisa.

3.2.4. Farakano la Donato

Katika mateso mw.303-308 Kaisari Diokletiano alijaribu kwa nguvu zote kuharibu kanisa na kufuta Ukristo. Mbinu moja ilikuwa kukusanya Biblia zote na kuzichoma moto. Katika miaka hii migumu walijitokeza hata maaskofu kadhaa na wachungaji walioona heri kuwakabidhi askari Biblia kuliko kufa.

Baada ya mwisho wa mateso haya na uhuru uliopatikana Wakristo walioasi au kukana imani walirudi. Hata wachungaji na maaskofu waliowahi kuwa wadhaifu walipokelewa tena baada ya kutubu.

Hapo ndipo Wakristo wa Karthago walio wengi walikataa kuwakubali tena. Wakiongozwa na Donato walimkataa aliyewahi kuwa Askofu lakini alitoa Biblia kwa serikali. Donato alisititiza ya kwamba aliyeasi hawezi kutoa sakramenti za kweli. Maana yake akibatiza, kusikia toba au kutoa ekaristia si sakramenti. Walitaka kuongozwa na wale tu waliosimama imara (au labda: waliokuwa na bahati kutokamatwa). Hapo ndipo sababu ya farakano kwani kanisa kubwa lilitetea mafundisho ya kuwa kila Mkristo anaweza kuteleza katika dhambi lakini toba inaponya makosa yote. Wafuasi wa Donato walijitenga wakijiona ndio kanisa la kweli lenye waumini na viongozi walio safi.

Farakano hilo la Donato lilidhoofisha kanisa la Afrika ya Kaskazini sana. Wadonato walijivuna kuwa Wakristo bora kuliko wengine. Viongozi wa Kanisa la Katholiko walikosa mara nyingi upendo wakiwashughulikia. Kanisa la Wadonato lilikuwa na maskofu hadi 200. Wakristo wengi hasa wa asili ya kiberiberi vijijini walifuata mafundisho ya Donato. Waberiberi walijisikia wananyonywa na serikali ya kiroma waliona Wadonato kama chombo cha upinzani. Kumbe matatizo ya kisiasa na kikabila yakaingilia kati.

Mafarakano haya yalikuwa jeraha kubwa katika Ukristo wa Afrika ya Kaskazini. Walipokuja Waarabu mnamo mwaka 670 walikuta Ukristo uliogawanyika na kudhoofishwa. Si ajabu ya kwamba katika sehemu hiyo ya Afrika Ukristo ulipotea baada ya miaka kadhaa ya Utawala wa Kiislamu. Pamoja na matatizo yaliyowapata Wakristo chini ya utawala wa kiislamu (taz. chini no.7) Wakristo wa sehemu za Karthago (Tunisia na Algeria) waliwahi kuona mfano mbaya wa Ukristo kwa muda mrefu mno.

Maswali na Maarifa (3.2.):

1. Kwa nini wakristo waliteswa chini ya serikali ya kiroma?

2. "Damu ya mashahidi ni mbegu ya kanisa" - eleza maneno haya.

3.Taja mbinu jinsi Wakristo walivyoteswa.

4. Taja mifano ya mateso makali ya Wakristo katika Afrika wakati wa karne za kwanza.

5. Eleza jinsi gani mateso yalisababisha mafarakano katika kanisa la Afrika.

TUKUMBUKE:

Wakati wa kiroma wakristo wengi waafrika walionyesha uhodari wasipokana imani yao na kufa kama mashahidi wa imani. Mfano huu ulisababisha wapagani wengi kuwa wakristo.

3.3. URITHI WA MISRI KATIKA UKRISTO MZIMA: ELIMU NA WAMONAKI

Je, Baba . . . . ?

Tegemea: Baba, kwa nini serikali iliomba kanisa kujenga shule ?

Baba: Naona inategemea msaada wa wananchi wote kuongeza elimu ya Taifa, hata jumuiya za kidini zisaidie.

Tegemea: Lakini mbona ni kazi ya kanisa kuhubiri neno la Mungu kwa nini watumie pesa za waumini kujenga shule ambako watasoma hata wasio wakristo?

Baba: Elimu ni muhimu sana katika Ukristo. Katika nchi nyingi shule zilianzishwa na kanisa. Miaka 20 iliyopita shule nyingi petu Tanzania zilikuwa shule za makanisa kabla ya kutaifishwa.

Tegemea: Kwa nini elimu ni muhimu hivi hasa katika Ukristo? Mbona wanafunzi wa Yesu walikuwa wavuvi na wakulima tu? Na ndio wasomi waliomkataa? Biblia husema "Hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele za Mungu" (Rum3,19). Rafiki yangu akasema mtu hawezi kuokoka kwa elimu yake hata asiyesoma anaweza kumpokea Kristo. Asema imani ni muhimu kuliko elimu.

Baba: Kiasi ni kweli anavyosema. Tukiwa na bahati ya kusoma tusidharau wengine ambao hawakuwa na nafasi hiyo. Lakini unaonaje: Kama hujajifunza kusoma - nani akusomee Biblia? Imani yetu haiendi bila Biblia - kumbe mkristo awe msomi. Kama Wakristo hawana elimu - nani atajibu maswali ya wasomi wanaopenda kumjua Yesu ? Halafu: Mungu ametupa amri ya kutawala dunia kwa niaba yake. Utatimizaje amri hiyo usipojua chochote juu ya dunia hiyo ?

Tegemea: Basi naona lazima nitafakari upya. Asante Baba.

3.3.1. Elimu ya kikristo: Chuo cha Aleksandria

Aleksandria ilikuwa mji mkubwa kwenye mdomo wa mto Naili nchini Misri. Ilikuwa mahali pa maktaba kubwa kuliko maktaba yote duniani. Wakati ule haikujulikana jinsi ya kupiga chapa vitabu. Kila kitabu kiliandikwa kwa mkono kikawa na bei kubwa sana. Kununua kitabu kulikuwa na gharama zinazofanana na gharama za kununua gari leo. Kumbe elimu ilikuwa na thamani kubwa, na maktaba kubwa ilikuwa na thamani kupita kiasi. Wataalamu toka pande zote za dunia walifika Aleksandria kusoma na kunakili vitabu. Aleksandria ilikuwa mji wa elimu. Si ajabu kwamba Agano la Kale lote lilitafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kigiriki pale Aleksandria miaka 150 K.K..

Kumbe Wakristo wa Aleksandria walijisikia hawana budi kuwa tayari kujadiliana na watu wenye elimu. Wawe tayari kujibu maswali na mashaka yao juu ya Injili. Wawe tayari kutetea imani kwenye ngazi inayolingana na elimu ya hali ya juu. Wakristo wenye elimu wakajitolea kuendesha mafundisho ya kuwaelimisha Wakristo wenzao. Katika masomo haya kilitokea chuo cha kwanza cha kikristo. Masomo yake yalifundisha imani na Biblia lakini vilevile elimu kwa jumla. Falsafa ilikuwa muhimu katika mawazo ya wataalamu hata katika mafundisho ya kidini ya wapagani na wayahudi. Kumbe mwalimu mkristo afadhali ajue falsafa na awe na msimamo wake juu ya uhusiano kati ya falsafa na imani ya kikristo.

Chuo cha Aleksandria kilipata sifa chini ya uongozi wa Panteno. Aliacha uongozi wa chuo mnamo mw. 200 B.K. akakubali kuwa Mmisionari akaenda Bara Hindi. Aliyemfuata alikuwa Klementi aliyefaulu sana kuwavuta wapagani wenye elimu kumpokea Kristo. Mwanafunzi wake mashuhuri alikuwa Origine baadaye akapewa uongozi wa chuo cha Aleksandria. Origine alikuwa mtaalamu wa pekee. Alikuwa mkristo wa kwanza aliyetumia njia ya kisayansi kuchunguza fasiri za Biblia. Alifanya kazi hii kwa muda wa miaka 25. Pamoja na karani wake akaandika maneno yote ya Kiebrania ya Biblia pamoja na fasiri zake katika nguzo sita kwenye karatasi kubwa. Njia hii ilisaidia kupima makosa au udhaifu katika fasiri hizo mara moja. Aliwafundisha vijana wengi kutumia akili yao katika kutafakari imani kwani akili ni kipawa cha Mungu.

Kwa njia hiyo Chuo cha Aleksandria kimekuwa mwanzo wa elimu ya juu katika Ukristo. Mpaka leo ni kawaida katika makanisa mengi ya kwamba mtumishi wa kanisa awe na elimu. Wachungaji, mapadre na masista wanasomeshwa katika vyuo mbalimbali hadi ngazi ya chuo kikuu. Ukristo umekuwa imani ya wasomi. Asili yake ni katika juhudi za babu zetu wa Misri.


3.3.2. Utawa na umonaki - maisha ya pekee

Bila shaka umewahi kumwona sista? Lakini si Wakristo wote wanaozoea kuwa na masista katika kanisa. Sista Maria ni kijana wa miaka 22. Aliwahi kusoma hadi "Form IV". Wakati bado anasoma aliomba kujiunga na ushirika wa masista wa dayosisi. Alipokelewa katika ngazi ya "unovisi" kwa mwaka mmoja. Aliishi pamoja na masista wengine vijana katika nyumba chini ya uongozi wa masista wengine waliowahi kujiunga tangu miaka mingi. Baadaye alitoa kiapo cha kwanza.

Karibuni atatoa kiapo cha pili atakapojiunga kwa muda wa maisha na shirika lake la masista. Kiapo kitakuwa na ahadi tatu: Sista Maria ataahidi kufuata maisha ya useja, umaskini na utii kwa kanuni za shirika lake. Je, atawezaje kufuata kwa miaka mingi ijayo masharti haya yanayoonekana kuwa magumu? Hana wasiwasi sana. Anasema : "Nilikuwa na muda wa kutosha wa kujipima na kuomba ushauri wa Mungu. Nategemea msaada wa Roho Mtakatifu katika maisha haya sina mashaka ya kwamba Bwana yu pamoja nami".

Masista na mapadre huitwa "Watawa". Wanajulikana ya kwamba ni Wakristo walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Mara nyingi tumezoea kuwaona katika Kanisa la Kiroma-Katoliki. Lakini watawa wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa sio wengi. Kule Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptist.

Mtawa ni nani? Ni mkristo aliyepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo:

Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo I.Kor7,8( yaani hajaoa mwenyewe).

Bwana Yesu mwenyewe alieleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila kuwa na familia au kuzaa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (MT.19,12 "wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni").

Kwa jumla watawa ni kikundi muhimu katika Ukristo. Makanisa yenye masista yanaona ya kwamba kweli wanasaidia sana kazi ya kiroho. Watawa ni watu ambao ni huru kuliko wakristo wengine kujitolea katika huduma ya kanisa. Kwani hawalazimishwi kutafakari maendeleo ya watoto wao. Watawa wa kike huitwa "masista". Watawa wa kiume wanaweza kuishi peke yao kama kwa mfano mapadre wa kikatoliki. Lakini mara nyingi wakijiunga na chama au jumuiya na kutoa nadhiri za Umaskini, Utii na Useja wanaitwa "Wamonaki".

3.3.3. Asili ya utawa katika Misri

Kumbe asili ya jumuiya hizo iko Misri. Katika karne ya tatu mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani waliogopa kulazimishwa kutoa sadaka mbele ya sananmu. Wengine waliona jinsi gani familia yao iliuawa katika mateso. Wengine karibu walikata tamaa wakiona jinsi gani Wakristo wengine walivyokana imani wakiogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya kawaida. Wengine wakajitenga na dunia ya kawaida wakaenda porini kuishi kule maisha ya kufunga na kusali.

Watawa hawa waliitwa kwa jina la kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake). Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala wa kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Walitumia muda mwingi wakisali na kusoma Biblia watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao katika mambo ya kiroho au ya maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k.. Wamonaki hawa wa kwanza walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana.

Antonio wa Misri alikuwa mmoja wao akaanza kuona umuhimu wa kuweka utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake. Wengine walianza kuzoea kupokea zawadi za wanavijiji wakaelekea kwenye maisha ya kuombaomba. Antonio alikusanya wamonaki majirani aliwaomba wafuate utaratibu wa pamoja. Hapo ndipo jumuiya ya kwanza ya watawa yenye utaratibu maalumu ikaanza. Mwanafunzi wake Pakomio aliendeleza mkazo wake akaitwa "Baba wa Wamonaki". Aliwaunganisha wamonaki mahali pamoja akawapa utaratibu wa kazi na sala ya pamoja. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1.Useja : atachagua maisha bila familia badala yake kujiunga na shirika la wenzake kama familia ya kiroho 2. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo (huitwa "Abba/Abbato" akichaguliwa kati yao) na kutii taratibu za ushirika wake 3. Umaskini: ataacha mali yake ya binafsi hatatafuta tena utajiri wa kidunia.

Utaratibu huu wa umonaki ulienea haraka watawa wakaanza kukaa pamoja na kufanya kazi pamoja ili kujipatia mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu ikiwa sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k. Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile huduma za upendo (hospitali, nyumba za yatima), huduma za kufundisha, uinjilisti, misioni, au maisha kimyakimya ya sala, kuombea n.k. Hivyo mmonaki au mtawa anaweza kuwa na maisha asipotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya wakristo au wasio wakristo akiwatolea huduma zake.

3.3.4. Wamisionari Waafrika katika mabara matatu

Panteno Mkuu wa Chuo cha Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri walijenga Kanisa kule Sudan na Ethiopia. Hata sehemu kubwa ya Ulaya inakumbuka wamisionari kutoka Afrika. Kule Ireland wamonaki wamisri waliunda monasteri mnamo mw. 500 na kufundisha Injili. Wanafunzi Waireland wa hawa waafrika ndio waliokuwa wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi. --

Waafrika wengine waliwahi kuhubiri Injili mara ya kwanza katika sehemu mablimbali za Ulaya wakati wa Waroma. Askari Wamisri na Wasudani katika jeshi la Roma walikaa kule Uswisi na penginepo. Kikosi kimoja kutoka Misri kimekuwa maarufu kwa kuwa na Wakristo wengi na kukataa sadaka mbele ya sanamu ya Kaisari. Wote waliuawa wakawa wafiadini Wakristo. Anayeheshimiwa hasa ni kiongozi wao Morisi Mtakatifu na miji mingi ya Ulaya inatunza kumbukumbu yake kwa kuonyesha picha ya mtu mweusi katika nembo.

TUKUMBUKE:

Misri ilikuwa kitovu muhimu katika Ukristo wa Kale. Uhodari wa Wakristo wake ulishinda mateso ya kiroma. Katika mapambano haya Wakristo Wamisri wakaunda silaha mbili ambazo zimekuwa muhimu katika kanisa zima mpaka leo:

1. Elimu ya Kikristo

2. Utaratibu wa Umonaki (Utawa).


3.4. AGOSTINO WA AFRIKA - MWALIMU WA KANISA ZIMA

3.4.1. Maisha yake

Agostino alizaliwa mw. 354 B.K. pale Numidia (leo: Algeria) yaani karne mbili baada ya Origine. Wakati ule Ukristo ulikuwa tayari dini iliyokubaliwa katika Dola la Roma. Mateso ya Wakristo yalikwisha. Mama yake alikuwa Mkristo, Baba mpagani aliyefuata dini ya zamani ya kuabudu miungu mingi. Alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Karthago (Tunis). Wakati ule palikuwa na tofauti kubwa kati ya utamaduni wa Misri na ule wa Afrika ya Kaskazini-Magharibi. Pale Misri ulikuwapo mchanganyiko wa utamaduni wa kikopti (yaani kiasili cha Misri) pamoja na kigi¬riki. Katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini watu wa asili ni Waberiberi, lakini watu wa mjini na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Kiulaya wakatumia hasa lugha ya Kilatini iliyokuwa lugha muhimu ya kimataifa pamoja na Kigiriki. Kwa jumla sehemu hii ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi, lakini Misri ilikuwa karibu na utamaduni wa Asia ya Magharibi na Ulaya ya Mashariki.

Agostino mwenyewe aliendelea kusoma pale Italia baada ya kumaliza masomo yake Karthago. Ndipo hapo akakutana na watu waliom¬vuta kuwa Mkristo. Akabatizwa akarudi Afrika akabarikiwa kuwa padre akachaguliwa kuwa askofu wa mji wa Hippo pale Numidia mw. 395 B.K.. Mpaka kifo chake aliendelea kueleza na kutetea imani kwa maandiko na vitabu vingi. Kwa njia hii amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo wa Magharibi (yaani Kanisa la Kiroma - Kato¬liki na pia katika makanisa yaliyo¬toka katika kanisa hilo.) Kwa mfano Martin Luther alimtaja Agostino kuwa baba yake wa kiroho pamoja na Mt. Paulo.

3.4.2. Kazi yake Agostino

Kazi kubwa ya Agostino si kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyo¬fanya Origine. Kazi yake kuu ilikuwa kutafsiri mafundisho ya Biblia katika mazingira ya kiroho, kijamii na kisiasa ya wakati wake. Hapa aliuliza maswali na kutoa majibu yenye umuhimu mpaka leo. Mafundisho yake yamesikika hasa juu ya swali la neema na dhambi halafu juu ya uhusiano wa Kanisa na Serikali.

Katika mafundisho yake juu ya neema na dhambi ni Agostino alitoa mafundisho ya kwamba ubinadamu umo katika dhambi ya asili tangu Adamu. Uhuru wa kibinadamu umepotea katika dhambi ya Adamu, hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwetu. Alisisitiza ya kwamba si mwanadamu anayemkuta Mungu lakini Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi.

Juu ya uhusiano kati ya serikali na kanisa aliandika kitabu chake "De civitate Dei" (mji wa Mungu). Badala ya "mji" tungeweza kutafsiri pia: "eneo au kikundi cha watu au utawala". Alieleza ya kwamba iko "miji" miwili: mji wa Mungu (yaani Yerusalemu wa mbinguni, au kanisa) na mji wa dunia hii, yaani taratibu za kisiasa. Katika "mji wa dunia hii" hali hubadilika. Hakuna taratibu za kudumu. Agostino alifahamu habari za taratibu za Waroma wa kipagani walio-angalia makaisari wao kuwa miungu, akafahamu habari za demokrasia ya kigiriki ya kale. Akafa¬hamu habari za mji mkubwa wa Roma ulioitwa "mji wa milele" lakini ulichomwo moto na maadui katika siku zake sawasawa jinsi ilivyoanguka zamani miji ya Babiloni au Yerusalemu. Lakini pamoja na "mji" huo upo "mji" wa pili ndio mji wa Mungu ambao ni mji wa upendo na undugu penye neema yake Mungu. Miji yote miwili iko pamoja mahali palepale ingawa taratibu zao ni tofauti. Mkristo ndiye raia ya miji yote miwili. Huitwa kuwa mwaminifu katika pande zote mbili. Lakini ajue ya kwamba mji wa dunia hii hauna shabaha ya kudumu. Umeingiliwa na dhambi. Lakini mji wa Mungu utadumu. Umepewa lengo la kudumu, unashirikiana katika enzi ya Mungu. Hapo ndipo sababu ya kwamba inafaa serikali isikie wazo la kanisa kwani ni kwa njia ya kanisa ya kwamba Mungu ameamua kufunua mapenzi yake. Mkristo anaweza kushiriki katika taratibu za kisiasa akijua ya kwamba mawazo na mipango yote ya siasa havidumu. Utakaodumu ni utaratibu wa Mungu.

Ni kutokana na mafundisho haya ya Agostino ya kwamba Kanisa la Magharibi (yaani Kanisa la Kiroma-katoliki na madhehebu yaliyotengwa naye) lilijifunza kuwa na msimamo mbele ya serikali mbalimbali zilizojitokeza katika historia ndefu ya kanisa. Agostino alikuwa kijana aliposhuhudia jinsi gani Mkuu wa Dola Kaisari Theodosio akatubu kanisani. Askofu Ambrosio wa Milan alikuwa amemtenga Kaisari kwani wana¬jeshi wa serikali waliua watu wengi sana ovyo walipo¬gandamiza fujo lililotokea katika mji wa Thesalonike. Kaisari alimpandisha cheo Mkuu wa jeshi hilo. Watu wengi pamoja na Askofu walisikitika na kuwa na huzuni juu ya tendo hilo. Theodosio alipotaka baadaye kuingia katika ibada Askofu alimtangaza ametengwa kwa sababu ya damu ya wananchi wa Thesalonike hawezi kushiriki meza ya Bwana. Kumbe Kaisari akakubali kosa mbele ya umati akatubu. Hata baadaye viongozi wa kanisa la magharibi wakafuata mara nyingi mfano wa Ambrosio na mafundisho ya Agostino.

Tunaweza kuona aina mbili za matokeo ya urithi huo:

Kwa upande mmoja kanisa lilijaribu kutawala juu ya jamii na serikali katika nchi za Ulaya. Lilidai sheria zote za serikali zifuate taratibu za kanisa. Viongozi wa serikali walitakiwa kusimikwa na kanisa. Hoja hili huitwa "Uklerikali" (clerica¬lism). Nguvu ya kisiasa ya kanisa lilipingwa na kupinduliwa katika mapinduzi mbalim¬bali ya Ulaya na Amerika (kuanzia mapinduzi ya Ufaransa 1789, katika mapinduzi ya Marekani ya Kusini karne ya 19 hadi mapigano mengi katika nchi kama Hispania na Austria wakati wa karne ya 20). Siku hizi wazo hili halipo tena lakini zamani lilileta matatizo mengi, kama vile ugandamizaji wa madhehebu mengine na hata vita.

Lakini sehemu nyingine ya urithi huo wa Agostino imebaki: kazi ya kanisa kuzitetea haki za kibinadamu, hata dhidi ya serikali inayoweza kugandamiza haki hizo. Kwa mfano ndiyo makanisa yaliyopinga sana siasa ya ubaguzi wa rangi pale Afrika ya Kusini na zamani pale Marikani, hata dhidi ya serikali iliyotetea utaratibu huo. Vilevile ni makanisa yanayotetea haki za wakimbizi katika nchi nyingi hata kama serikali zimeshachoka na mzigo wa kupokea wageni maskini kutoka nchi zingine.

3.4.3. Mfano wa siku hizi: Martin Luther King

Kiongozi mmoja mashuhuri wa kanisa la Kibaptist Marekani alikuwa mchungaji Martin Luther King. (Baba yake alimwita kwa jina la Martin Luther akimheshimu huyu mtaalamu Mjerumani wa karne ya 16.) Aliwaongoza Waamerika weusi kupinga ubaguzi wa rangi uliopatikana katika sehemu za USA mpaka miaka ya 1960. Katika mapambano haya alifuata mapokeo ya Mt. Agostino katika kanisa. Alieleza ya kuwa mtu amepewa heshima yake na Mungu na sheria za serikali zinazovunja heshima hii ni sheria bila haki. "Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu" (Mdo. 5,29). Aliwaita watu kupinga ubaguzi hata dhidi ya serikali na polisi lakini bila kutumia mabavu. Watu waliongozwa na M.L. King waliandamana mahali pengi wakanyamaza wakipigwa na kukamatwa. Wakaingia katika mahoteli, shule na vyombo vya usafiri vilivyotengwa kisheria kwa watu weupe. Wakasubiri mpaka polisi iliitwa na kuwakamata. Wakapokea adhabu na mapigo. Baada ya miaka kadhaa mapambano kwa silaha za amani yalishinda. Mahakama kuu ya Marekani na serikali kuu zilitangaza ya kuwa ubaguzi wa rangi katika mikoa mbalimbali hauruhusiwi kuendelea. Lakini M.L. King alikufa kama shahidi wa damu alipouawa na mteteaji wa ubaguzi wa rangi mwaka 1967.

3.4.4. Matatizo ya urithi wa Agostino

Mwishoni tusifiche sehemu ya urithi wa Agostino iliyokuwa ngumu mpaka leo. Katika mikoa ya Afrika ya Kaskazini walikuwepo wakristo wengi waliojitenga na kanisa kubwa na kuanzisha dhehebu la Wadonato. Agostino alijadiliana miaka mingi nao akajaribu kuwavuta warudi tena.

Mwaka 411 B.K. serikali ya kiroma ilitafuta shauri lake Agostino katika swali la Wadonato pale Karthago na Numidia (Tunisia na Algeria). Serikali ilitaka kuwa na umoja wa kidini kati ya wananchi. Pia wapinzani wa utawala wa kiroma pale Afrika ya Kaskazini walijiunga na kanisa la Wadonato. Basi Agostino aliona ya kwamba Wadonato walishika mafundisho ya uongo. Akaogopa wangewaongoza waumini wao jehenam. Akaona kanisa lisiache watu kufundisha uongo (alivyo¬elewa mwenyewe) akaona vema kutumia nguvu ya serikali kuzuia uongo huo. Agostino akaona vema walazimishwe kurudi katika kanisa kubwa. Mwenyewe hakukubali adhabu ya kifo kwa "wazushi" Wadonato. Lakini Serikali ilichukua kibali chake cha kuingia kati kama msingi wa kuwatesa Wadonato vikali na kuwaua wengi. Wadonato walipoteswa hivi na serikali ya kiroma Agostino akanyamaza hakupinga. Mateso haya ya wakristo Wadonato chini ya serikali ya kikristo mbele ya macho ya kanisa la kiroma-katoliki yalikuwa mwanzo wa mwisho wa Ukristo pale Afrika ya Kaskazini. Mateso haya yaliendelea muda mrefu. Miaka mia mbili baadaye wanajeshi wa waarabu waislamu wakaingia Afrika ya Kaskazini. Wakakuta Ukristo ulio¬dhoofishwa. Baada ya muda mfupi wenyeji wengi sana wa sehemu hizo wakaacha Ukristo wakajiunga na Uislamu. Basi tukiangalia hali ya Misri tunaona tofauti. Pale Misri wakristo wakashika imani yao katika karne zote ingawa kwa matatizo makubwa chini ya serikali ya kiislamu. Lakini katika sehemu ya Afrika ya Kaskazini-Magharibi nguvu za ndani za Ukristo zilivunjika wakati wa mateso haya makali ya wakristo Wadonato chini ya mikono ya wakristo wenzao. Tatizo halikuishi hapa Afrika ya Kaskazini. Agostino alitetea siasa ya ugandamizaji wa wazu¬shi katika kitabu kimoja, lakini bila kuruhusu wauawe. Katika karne zilizo¬fuata maandiko haya yaliongoza siasa ya kanisa la magharibi juu ya wazushi pote Ulaya. Kanisa lilikubali wazo la Agostino Mkuu ya kwamba wazushi wanapaswa kugandamizwa. Basi kwa karne nyingi kanisa la magharibi likaendelea kuwagandamiza na kuwatesa wakristo wasio-kubali mafundisho yake au hata uongozi wake. Watu wakateswa, kuchomwa motoni na kufungwa gerezani, yote haya kwa kibali na idhini ya kanisa . Hata madhehebu kama walutheri, waang¬likana na wareformed yalitenda hivihivi baada ya kuwa kanisa la serikali katika maeneo yao. Walifuata mfano uliowekwa wakati wa mgongano kati ya kanisa kubwa na Wadonato pale Afrika ya Kaskazini katika karne ya tano. Bila shaka Agostino hakutegemea matokeo haya lakini ni sehemu ya urithi wake.

Hata habari hizi zinazohuzunisha ni sehemu ya urithi wa Agostino ambaye tunamkumbuka katika mengine kama mwalimu mkubwa wa Ukristo mzima.

===
3.5. ETHIOPIA NA NUBIA === Jangwa kubwa la Sahara lilifanya mawasiliano yote kuwa magumu kati ya Afrika ya Kaskazini na sehemu zingine za bara. Lakini njia ya mto wa Nile ilisaidia tangu zamani biashara na athari za kiutamaduni na kisiasa kuvuka kanda la jangwa. Hivyo upo uhusiano wa pekee kati ya Misri na eneo linaloitwa leo "Sudan". Zamani nchi kusini mwa Misri iliitwa kwa jumla "Nubia"; sehemu moja ilijulikana kwa miaka mingi kwa jina la "Kushi". Tunapata habari zake katika Biblia katika Mdo. 8. Filipo alimbatiza "Towashi wa Kushi" yaani afisa wa serikali ya malkia Kandake wa Kushi katika mji mkuu wa Meroe. (Agano Jipya toleo la Kiwahili la Kisasa linatumia hapa kwa kosa jina la "Ethiopia") Habari hii inaonyesha ya kwamba safari kati ya Kushi (Sudan) na Misri mpaka Yerusalemu zilikuwa kawaida. 3 Lakini hatuna habari zaidi kama huyu afisa alihubiri injili kwake nyumbani.

Kuanzia karne ya tatu athari za Ukristo zinajulikana katika Nubia. Wamonaki Wamisri walihubiri Injili. Kuanzia mw. 600 wakazi wengi wa Kushi walikuwa Wakristo. Makanisa mengi na makubwa yalijengwa na kupambwa katika miji mikubwa kama Dongola na Soba. Kwa miaka elfu moja utamaduni wa kikristo uliendelea. Kutoka kwa Dongola wamisionari walifika kusini mwa Sahara mpaka eneo la Tibesti (yaani Chad ya leo) jinsi inavyoonekana na maghofu yanayoonyesha alama za kikristo kule.

Kusini-Mashariki wa Kushi tunakuta eneo kubwa lenye milima mirefu inayosimama kama mnara katika tambarare ya nchi jirani. Ni nyanda za juu za Ethiopia au Uhabeshi. Mnamo mwaka 300 B.K. palikuwa na ufalme katika eneo la Aksum (Ethiopia ya leo). Wakati alipotawala Kaisari Konstantino kule Roma meli moja ilikuwa safarini kutoka Shamu kwenda Bara Hindi ikaharibika kwenye pwani ya Ethiopia. Vijana wawili waliokolewa wakapelekwa mbele ya mfalme kule Aksum. Mmoja wao kwa jina Frumentio alipata haraka sifa za kuwa mwenye elimu na hekima. Akapanda ngazi kuwa mshauri wa mfalme na mwalimu wa mwana wa mfalme aliyeitwa Ezana. Huyu Ezana akawa baadaye mfalme mwenyewe akiendelea kumtumia Frumentio kama mshauri wake. Kumbe Frumentio aliweza kuweka mbegu za imani moyoni mwa mfalme kijana.

Siku moja Frumentio aliomba ruhusa ya mfalme aende nyumbani kuangalia kama wazazi wake bado wanaishi. Mfalme akamruhusu akamwomba atafute pale walimu wanaoweza kufundisha elimu aliyokuwa nayo Frumentio pamoja na imani yake ya kikristo. Frumentio akamwendea Askofu Mkuu wa Misri aliyembariki kuwa askofu kwa ajili ya Waethiopia. Hivyo kanisa lilianza katika nyanda za juu za Ethiopia. Mfalme Ezana akabatizwa mwenyewe na watu wengi wa makao makuu wakamfuata.

Baadaye walifika wamonaki kutoka Misri na Shamu kule Ethiopia. Ndio wale walioanza kufundisha na kuwabatiza Wahabeshi wengi. Hapo ndipo mwanzo wa Taifa la Kikristo la Ethiopia. Wahabeshi wametunza urithi wao wa kikristo mpaka leo. Ukristo wao unafuata mapokeo ya kiorthodoksi (tazama chini) yalivyo hata kule Misri mpaka leo. Mpaka karne hii ya ishirini walipokea Maaskofu wao kutoka Kanisa la Kikopti la Misri.


3.6. MABADILIKO YA KARNE YA SABA: KUJA KWA UISLAMU

Tumesikia ya kwamba Afrika ya Kaskazini ilikuwa nchi ya Wakristo katika karne za kwanza. Labda tumeshangaa kusikia ya kwamba leo hii wako mamilioni ya Wakristo kule Misri kwa sababu tumesikia mara kwa mara ya kwamba wenyeji wa Misri ni Waarabu na Waislamu. Kumbe katika karne saba za kwanza baada ya Kristo hali ilikuwa tofauti kuliko leo. Lakini baadaye mageuzi makubwa yalitokea yaliyokuwa muhimu sana katika historia ya Afrika: Uenezaji wa Uislamu. Habari hizi tutaangalia kwa upana zaidi katika sura ya nne. Lakini ulisababisha mabadiliko gani katika Afrika?

Mnamo mwaka 610 B.K. sehemu kubwa ya Afrika ya Kaskazini iliunganika tena chini ya utawala wa Dola la Roma lililotawaliwa kutoka mji wa Bizanti (Roma ya mashariki). Lakini utawala ulikuwa hafifu kulingana na zamani za Roma ya kale. Wenyeji wa Misri na Mkoa wa "Afrika" (=Tunisia ya leo) walipinga utawala wa Bizanti. Wakristo wengi katika nchi hizi walikataa usimamizi wa Askofu Mkuu wa Bizanti wakiwafuata viongozi wao wa kitaifa. Viongozi wa Kanisa la Kikopti (Misri) waliteswa na serikali ya Bizanti. Dola la Roma ya Mashariki (=Bizanti) ilichosha nguvu zake vitani dhidi ya majirani ya Uajemi na makabila wakorofi kutoka kaskazini.

Hali hii ilibadilika ghafla mwaka 640 B.K. Habari za imani mpya kati ya Waarabu zilisikika tangu mw. 622 kutoka eneo la Maka na Madina. Kiongozi mpya aliyeitwa Muhamad aliunganisha makabila yote ya Waarabu katika jina la mungu mmoja "Allahu". Baada ya kifo cha Muhamad wafuasi wake walitoka nje ya jangwa la Arabuni na kushambulia maeneo jirani ya Bizanti na Uajemi. Kivita walipigana na majeshi ya nchi hizo na kushinda. Mwaka 640 waliingia Misri. Wenyeji Wakopti waliwapokea kwa matumaini ya kuwa watamaliza utawala wa Bizanti. Jeshi la Bizanti lilishindwa kwa kukosa msaada wa wazalendo. Kiongozi mwislamu aliahidi madhehebu yote yataheshimiwa. Alifanya mkataba wakristo waendelee na ibada zao, makanisa na desturi zao. Lakini baada ya muda Wamisri waliona ya kwamba wamekuwa watu wa ngazi ya chini. Mabwana wapya walianza kubadilisha utamaduni wa nchi. Aliyejiunga na Uislamu na kujifunza kiarabu alikubaliwa lakini wakristo wenyeji waliotunza urithi wao walibaguliwa. Majaribio yote ya kupambana uhuru yaligandamizwa vikali.

Miaka 100 baadaye waislamu waliteka sehemu iliyobaki ya Afrika ya kaskazini. Kule Tunisia na Algeria ukristo ulikuwa dhaifu kutokana na mafarakano mengi ya miaka ya nyuma. Katika nchi za jirani (Italia na Hispania) vita vilipigwa vikali kati ya waarabu walioshambulia na wakristo waliojitetea. Labda hali hii iliongezeka moyo wa kutovumilia kuwepo kwa wakristo. Kanisa lilipotea baada ya karne chache katika Afrika magharibi ya Misri.

Maswali na Maarifa (3.6.):

1. Kitu gani kulisababisha kurudi nyuma kwa Ukristo katika Afrika ya Kaskazini ?

2. Taja mwanzilishi wa dini ya Uislamu, mahali na wakati wa kuanzisha imani hiyo na vituo vikuu vya uenezaji wake hadi karne ya nane.

3. Jaribu kulinganisha jinsi gani Ukristo na Uislamu vilivyoenea katika vipindi baada ya kuundwa.

4. Je, Wakristo walilazimishwa kuacha imani yao chini ya Waarabu Waislamu ? Eleza utaratibu uliotumiwa.

5. Taja mambo yaliyosababisha Wakristo kupokea Uislamu.

6. Taja makosa kwa upande wa kanisa yaliyorahisisha uenezaji wa Uislamu.


SURA YA NNE : UKRISTO WA KWANZA KATIKA DUNIA

1. Injili katika mabara matatu; 2. Mageuzi ya Konstatino; 3. Mafarakano; 4. Uislamu; 5. Ulaya na Asia

4.1. INJILI KATIKA MABARA MATATU

Ukristo wa kwanza ulienea haraka katika mabara matatu:

  • Asia ya Magharibi,
  • Afrika ya Kaskazini,
  • Ulaya ya Kusini-Magharibi.

Siri ya uenezaji huo wa haraka ni kuwepo kwa Dola la Roma. Serikali yake ikatawala nchi nyingi kuanzia Misri na kando ya Sahara kusini mpaka Uholanzi na Uingereza Kaskazini, halafu kutoka milima ya Mesopotamia (Iraq) mashariki mpaka Hispania/ Moroko magharibi. Watu wa Roma walifaulu kujenga dola hilo kubwa katika muda wa karne nyingi. Kwa jumla wakatawala kwa hekima, hivyo wakafaulu kuendelea muda mrefu. Mwanzoni uraia ulikuwa kwa wakazi huru wa mji wa Roma tu, lakini polepole hata wakazi wa maeneo mengine chini ya Roma wakapewa haki za uraia.

Kuwepo kwa Dola hilo kulisaidia sana uenezaji wa Ukristo ingawa watawala wake walijaribu muda mrefu kupinga imani mpya -kama tulivyosoma tayari. Lakini kuwepo kwa utaratibu mmoja katika eneo kubwa kulisaidia kazi ya mitume na wahubiri wa Injili.

  • a. katika eneo kubwa hakuna mipaka inayoweza kuzuia usafiri na mawasiliano. Ukisafiri leo kutoka Maroko kuelekea Misri ungevuka mipaka mitano, ungehitaji paspoti na vibali vingi kila safari.
  • b. uchumi ukaendelea vizuri palikuwa na usafiri. Merikebu zilizunguka pote katika Mediteranea zikabeba mizigo na watu. Waroma pia walikuwa hodari kujenga barabara kwenye nchi kavu. Walihitaji barabara hizo kwa matumizi ya kijeshi lakini zilisaidia pia mawasiliano mengine ya kiuchumi na usafiri.
  • c. Walitumia popote hela moja, wakawasiliana katika lugha ileile ya kigiriki na kilatini. Kigiriki ilikuwa lugha ya elimu ya juu na ya biashara katika mashariki ya eneo lao. Katika sehemu za Magharibi walitumia zaidi lugha ya kilatini. Mpaka leo lugha hizo ni muhimu kama lugha za elimu. kwa mfano maneno mengi ya kisayansi ni ya asili ya kigiriki (biologia, geografia, fisikia, kemia, n.k.), yanatumiwa katika lugha mbalimbali lakini asili ni ileile.

Utawala wa kiroma ulileta kipindi kirefu cha amani na cha maendeleo ya kiuchumi. Lakini maendeleo haya yamejengwa juu ya utaratibu mkali wa unyonyaji wa nchi na mikoa ndani ya Dola. Kila sehemu wakazi walipaswa kulipa kodi. Idadi ya watumwa ilikuwa kubwa. Kama kabila fulani lilijaribu kupinga utawala wa Roma wanajeshi wake wakafika haraka na kuzima ghasia. Kwa mfano Wayahudi walipojaribu kujipatia uhuru tena mn. mwaka 70 B.K. mji wa Yerusalemu uliharibiwa kabisa na wakazi wote wakauzwa utumwani. Watoto wa watumwa wakawa watumwa tena. Njia nyingine ya kuwa mtumwa ni kwa njia ya madeni. Mtu mwenye madeni aliweza kushtakiwa na akishindwa kulipa aliuzwa mwenyewe kama malipo ya madeni yake. Katika mikoa kadhaa ya Dola la Roma asilimia ya watumwa ilikuwa kiasi cha 20 ya wakazi wote. Wengi wao walikuwa na maisha mabaya, lakini wengine waliweza kupata maendeleo na hata kupewa uhuru na mabwana wao.

Wale watumwa walifurahia sana kusikia mafundisho mapya ya kwamba kila mtu ni mtoto wa Mungu na anapendwa naye. Wakashangaa sana kusikia ya kwamba Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za watu wote, na Mungu hajali sifa au cheo. Wakiingia katika ushirika wa kikristo waliweza kushangaa kukutana na watu huru hata matajiri. Ibada za kipagani zilitenga tabaka za kijamii. Haikuwa kawaida kwa tajiri kusali pamoja na watumishi wake.

"Maana katika Roho mmoja tulibatizwa sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru"(Paulo katika IKor 12,13) Watumwa walisikia katika ibada za Wakristo nyaraka za Mtume Paulo zinazokazia usawa kati ya Wakristo wote, akisititiza ya kwamba Wakristo wote watazamane kama ndugu na viungo vya mwili mmoja.

Hapa ndipo sababu ya kwamba ujumbe wa kikristo ulienea hasa kati ya maskini na watumwa. Lakini hata watu wa tabaka za juu walivutwa na neno la Injili na mfano mzuri wa maisha ya Wakristo, uhodari wao katika mateso mbalimbali na utaratibu wao wa kusaidiana.

Maswali na Maarifa (4.1.):

1. Linganisha hoja zifuatazo:

a. Dola la Roma lilikuwa kizuizi cha uenezaji wa Ukristo kwani lilikuwa na serikali ya kipagani

b. Kuwepo kwa Dola la Roma lilisaidia uenezaji wa Ukristo Taja sababu zinazoweza kuimarisha hoja zote mbili ukieleza wazo lako.

2. Eleza jinsi gani hali ya kiuchumi na kisiasa wakati wa Roma ilivyosaidia uenezaji wa Ukristo

3. Kwa nini walikuwa hasa watumwa na maskini waliokuwa tayari kupokea Ukristo katika karne za kwanza ?

4.2. MAGEUZI YA KONSTANTINO

Mateso ya Wakristo yaliendelea mpaka mwaka 311. Lakini idadi yao iliendelea kuongezeka pote katika Dola la Roma. Mwaka 312 B.K. mtu kwa jina Konstantino alitafuta cheo cha ukaisari (cheo cha mtawala ). Siku moja aliposhindana kivita na mgombea mwenzake Konstantino aliota ndoto, akaona alama ya msalaba na akasikia sauti iliyosema: "Chini ya alama hiyo utashinda". Aliwaruhusu wanajeshi wake waliokuwa Wakristo kusali akamshinda mgombea mwenzake vita. Mwaka 313 B.K. Kaisari Konstantino akatangaza sheria iliyoruhusu Wakristo kuabudu kwa uhuru. Ukristo ukawa dini inayokubaliwa katika Dola la Roma.

Kwa Wakristo wengi hali mpya ilikuwa maajabu ya Mungu mwenyewe aliyemaliza matatizo yao, jinsi Biblia ilivyosema katika kitabu cha ufunuo. Kipindi kipya kikaanza katika historia ya Ukristo. Wakristo wakaanza kujenga makanisa. Maaskofu wao waliweza kukutana bila matatizo.

Mwaka 325 mkutano wa kwanza wa kanisa zima ukafanyika kule Nikea (Asia Ndogo). Wakristo wa nchi mbalimbali walitofautiana katika maelezo yao juu ya tabia za kiMungu na tabia za kibinadamu za Kristo. Yaani kiasi gani Yesu ni mwanadamu na kiasi gani yeye ni Mungu. Kama alikuwa Mwanadamu aliumbwa kama wanadamu wote? Lakini kama anaitwa Mungu ndiye Mwuumba mwenyewe. Kama yeye ni Mungu - aliweza kuumia msalabani? Au ni Mungu aliyejificha tu katika umbo la mwili kumbe hakuteswa kweli ilikuwa kama igizo tu. Maaskofu waliokutana kule Nikea wakapatana juu ya mafundisho ya "Imani ya Nikea" yanayosema "Twamwamini Bwana mmoja,Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, mwana wa azali wa Baba, yu Mungu kutoka kwa Mungu, yu nuru kutoka kwa nuru, yu Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, Mwana wa azali, asiyeumbwa; aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu wanadamu na kwa wokovu wetu; akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika Bikira Maria, akawa mwanadamu; akasulibiwa kwa ajili yetu zamani za Pontio Pilato; aliteswa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka kama yanenavyo maandiko matakatifu; akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Baba; kutoka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu walio hai na wafu; na ufalme wake hauna mwisho." Maneno haya hutumika mpaka leo katika ibada za kikristo (pamoja na "Imani ya Mitume").

Kanisa likaitwa "katholiko" maana yake kanisa moja kwa ajili ya nchi zote na watu wote. Kila mji ulikuwa na askofu wake aliyeongoza kanisa. Maaskofu wa eneo au mkoa mmoja walikuwa chini ya Askofu Mkuu. Maaskofu wa Aleksandria (Afrika), Antiokia (Asia), na Roma (Ulaya na Afrika ya Kaskazini-Magharibi) waliheshimiwa kuliko maaskofu wote wengine wakaitwa kwa cheo "Patriarka". Cheo cha Patriarka kilipatikana baadaye pia kwa Askofu wa Bizanti tangu makaisari wa Roma kuhamia kule. Mikutano ya maaskofu (mitaguso) iliamua juu ya maswali na matatizo yaliyojitokeza.

Baada ya Konstantino kanisa lilikua sana. Watu wengi waliosita zamani walianza kujiunga na Ukristo. Zamani ilikuwa hatari kuwa Mkristo. Sasa imekuwa faida kuwa Mkristo, kumbe hata watu wenye imani haba wakajiunga na kanisa.

Baada ya Konstantino makaisari wenyewe walikuwa Wakristo. Mnamo mwaka 400 mambo yaligeuka kinyume cha hali ya awali: serikali ya Kaisari ilitangaza Ukristo kuwa dini rasmi ya serikali. Kanisa lilipewa hela na serikali. Kaisari mpya aliwekwa wakfu katika ibada kanisani. Mwishoni serikali ilianza kufunga na kubomoa mahekalu ya wapagani. Asiyekuwa Mkristo alianza kupata matatizo. Ilitokea mara kadhaa ya kwamba walimu wapagani walipigwa na kuuawa na umati wa Wakristo. Katika miji mbalimbali watu walianza kuwatesa hata kuwaua Wayahudi wakiwashtaki ya kwamba ndio Wayahudi waliomwua Bwana Yesu. Sisi tunaweza kushangaa jinsi hali hii iliweza kutokea. Yesu mwenyewe alikuwa Myahudi na mpaka msalabani alifuata taratibu za taifa la Israeli. Mtume Paulo alifundisha ya kwamba Wayahudi hawawezi kutoka nje ya ahadi na agano lake Mungu hata wakimkataa Yesu Kristo. Bila shaka Yesu hakutaka ya kwamba watu wangelazimishwa kujiunga na kanisa lake. Lakini katika mawazo na uzoefu wa Waroma dini na serikali zilikuwa kitu kimoja. Ikiwa ya kwamba sasa Kaisari, wakubwa wa serikali na watu wengi walikuwa Wakristo walihisi ni kawaida kwa wote kufuata dini hii. Kumbe kanisa lilianza kutumika na siasa.

Maswali na Maarifa (4.2.):

1. Taja faida kwa ajili ya Kanisa kutokana na mageuzi ya Konstantino.

2. Unaona hatari gani kwa ajili ya Ukristo kutokana na mageuzi ya Konstantino ?

4.3. MAFARAKANO NA UTENGANO: WAKATOLIKI, WAORTHODOKSI NA WAKOPTI

Katika karne ya nne Dola kubwa la Roma lilianza kupata matatizo. Makabila kutoka kaskazini ya Ulaya yalianza kuhamia kusini. Hali ya hewa ilibadilika watu wakakosa chakula cha kutosha kule Kaskazini. Mwendo huu ulisababisha kipindi kirefu cha vita na vurugu. Waliohama wakawasukuma majirani wao walioanza kuhamahama wenyewe. Matembezi haya yalifika kwenye mipaka ya Dola la Roma. Waroma walishindwa kuwazuia na polepole mataifa yale makorofi yakaingia katika eneo la kiroma na kutwaa mikoa mbalimbali. Waroma wakatumia hela nyingi sana kwa ajili ya jeshi lao lakini bila kufanikiwa.

Mwaka 395 Kaisari akagawa eneo la Roma katika sehemu mbili yaani Magharibi (makao makuu Roma) na Mashariki (makao makuu Bizanti). Mpaka ulifuata tofauti ya kiutamaduni kati ya maeneo yaliyotumia zaidi lugha ya Kigiriki na maeneo yaliyotumia zaidi Kilatini. Ugawaji huu ulikuwa na kusudi la kurahisisha utawala na utetezi. Lakini mw. 410 makabila makorofi yaliteka na kuharibu mji wa Roma. Mw. 476 Kaisari wa mwisho wa Magharibi aliuawa. Makabila ya kijerumani yalichukua utawala katika sehemu zote za Ulaya mpaka Afrika ya Kaskazini. Dola la Roma la Magharibi likagawanywa katika nchi nyingi ndogondogo. Kila sehemu makabila toka Kaskazini yalitawala kama tabaka ndogo ya juu wakiwategemea wenyeji kuendelea kuzalisha mali na wenyewe kupokea kodi zao. Lakini utaratibu, mawasiliano na usalama viliharibika. Uchumi na utamaduni vilirudi nyuma. Umoja wa kisiasa uliharibika, badala yake yalitokea maeneo mengi madogo ya kikabila. Ulaya ya Magharibi palikuwa na chombo kimoja tu chenye umoja uliovuka mipaka: Kanisa la Katoliki chini ya uongozi wa Askofu wa Roma. Ndiye aliyetunza urithi wa jina kubwa la Roma akiheshimiwa pia kama mfuasi wa Mtume Petro. Kwa sababu elimu ilishuka chini popote Ulaya ya Magharibi ni ndani ya kanisa tu ya kwamba mapadre na wamonaki wakaendelea kusoma na kutunza elimu ya kale. Watu kutoka Ulaya ya kaskazini hawakuwa wasomi. Hivyo watawala wao walitegemea watu wa kanisa wakitaka kuandika au kusomewa barua au mikataba. Polepole watawala wapya wakapokea Ukristo wenyewe pamoja na makabila yao. Walifundishwa ya kwamba mfalme hupewa madaraka yake na Mungu hivi anapaswa kufuata shauri la kanisa ambalo linatangaza mapenzi ya Mungu. Kutokana na hali hii ya kiutamaduni na kiroho kanisa lilikuwa na athari kubwa sana.

Utamaduni na utaratibu wa kale viliendelea katika sehemu ya Mashariki. Mtawala wa Bizanti akaendelea kutumia cheo cha Kaisari wa Roma, Taratibu za siasa, serikali na uchumi ziliendelea. Makaisari wengine wa Mashariki walijaribu kutawala tena eneo lote la zamani lakini ilishindikana. Kanisa liliendelea kuwa dini rasmi ya serikali. Kwa sababu serikali ilikuwa yenye nguvu kanisa lilikuwa chini yake. Kaisari alikuwa mlezi mkuu wa kanisa. Ndiye aliyemthibitisha Askofu Mkuu wa Bizanti na maaskofu wa dayosisi.

Kwa sababu ya matatizo ya ndani ya Ufalme wa Mashariki (=Bizanti) mafarakano yalitokea katika nchi za Misri na Siria zilizokuwa chini ya Kaisari wa Bizanti. Katika nchi hizo sehemu kubwa ya Wakristo walijitenga na kuendelea kama kanisa la kitaifa. Kanisa la Misri linatumia tangu wakati ule jina la "Kanisa la kikopti-orthodoksi" (kopti = misri).5 Kanisa la Ethiopia na Nubia ilifuata njia ya Misri. Kwa namna hiyo makanisa ya kale ya Afrika yameendelea kwa namna ya pekee.

Kumbe kanisa lilianza kuendelea tofauti katika sehemu hizo za mashariki na magharibi. Wakristo wa Magharibi (nchi za Ulaya ya magharibi pamoja na Afrika ya Kaskazini) wakafuata uongozi wa Papa yaani Askofu wa Roma. Kanisani walitumia lugha ya kilatini. Wakristo wa Mashariki wakafuata maaskofu wao waliokuwa chini ya serikali ya Kaisari wa Bizanti. Katika lugha walitumia kigiriki. Tofauti hizi zilisababisha kutokea kwa desturi na mawazo yaliyotofautiana. Ziliweka msingi wa kutokea kwa madhehebu mawili makubwa yanayoendelea mpaka leo yaani Kanisa la Kiroma-Katoliki na Kanisa Kiorthodoksi. Mwaka 1054 wajumbe wa Askofu wa Roma walimtembelea Askofu Mkuu wa Bizanti. Walianza kupingana vikali na mwishoni wakalaaniana. Tangu mwaka ule farakano lilikuwa rasmi kati ya Ukristo wa Magharibi na Ukristo wa Mashariki. Ilichukua miaka mingi kuishinda laana ya zamani. Mw. 1967 Papa Paulo wa Roma alimtembelea Askofu Athenagoras wa Bizanti (leo: Istanbul) wakapatana tena na kusameheana makosa ya zamani.6

Uelewano umeanza kujengwa pia kati ya makanisa yaliyofarakana zamani na Bizanti kama vile Wakopti au Wasiria.

Maswali na maarifa:

1. Taja madhehebu (makanisa) mawili yaliyojitokeza mwaka 1054. 2. Eleza jinsi gani mapokeo yao hutofautiana kuhusu uhusiano kati ya kanisa na serikali.

TUKUMBUKE:

1. Miaka 500 baada ya Kristo farakano lilitokea kati ya Makanisa ya kitaifa ya Misri na Siria na kanisa rasmi ya Bizanti.

2. Farakano kubwa lilitokea kati ya Ukristo wa mashariki (kiorthodoksi) na Ukristo wa magharibi (kikatoliki) mw. 1054.

3. Katika karne hii ya 20 uelewano umeanza kupatikana tena.


4.4. UISLAMU

4.4.1. Mtume Muhamad

Mwaka 622 B.K. Mwarabu kwa jina Muhamad alikimbia kutoka mji wa Maka. Akisafiri pamoja na marafiki wachache akaelekea kwenye mji wa Jathrib (au: Madina). Wakazi wa Maka walimkasirikia Muhamad. Tangu miaka 12 aliwahi kuhubiri juu ya ufunuo alizopokea kutoka kwa malaika wa Mungu. Alipinga desturi na maadili ya watu wa mji wake. Akatangaza "Uislamu" yaani imani katika Mungu mmoja aliyetoa amri zake kwa wanadamu. Kumbe viongozi wa Maka waliona anaharibu dini ya asili ya kuabudu sanamu za miungu. Makabila ya Waarabu walikuja kila mwaka kuabudu sanamu za Maka katika jengo la Kaaba. Wakati wa ziara hizo biashara ya Maka ilistawi vizuri sana. Muhamad alionekana anaweza kuharibu biashara wakakasirika wakajaribu kumwua lakini akakimbia.

Pale Madina alipokelewa vizuri, na wenyeji wakamwamini. Habari zake zikaenea haraka pande zote za Uarabuni. Makabila mbalimbali ya Waarabu walimwunga mkono. Akawaongoza kama kiongozi wa kidini, kijeshi na kisiasa. Mwaka 630 akawashinda watu wa Maka kivita lakini alionyesha hekima kwa kuwahurumia wajiunge na Uislamu. Alipokufa mw. 632 B.K. karibu Waarabu wote waliunganishwa chini ya bendera ya imani mpya ya Uislamu. Katika jina la Mungu (kiarabu: Allah) wafuasi wake wakashambulia maeneo jirani ya Waroma wa Bizanti na ya Wajemi.

Dunia nzima ilishangaa kusikia habari ya kwamba Waarabu kutoka jangwani walifaulu kuwashinda wanajeshi hodari wa kiroma na kiajemi. Lakini katika miaka iliyotangulia dola hizi mbili kubwa ziliwahi kupingana katika vita virefu na vikali. Wananchi wote na wanajeshi wao walichoka. Wenyeji wa Misri na Shamu (Siria) walisikitika juu ya utawala wa Kaisari wa Bizanti. Walidai tangu muda mrefu uhuru wa kitaifa lakini wakagandamizwa. Uchumi ulidhoofishwa baada ya miaka 20 ya vita. Waarabu walikutana na maadui waliokosa nguvu. Mwaka 636 Waarabu wakawashinda Waroma wa Bizanti kule Shamu halafu wakateka Dameski na Yerusalemu. Mwaka uleule 636 wakawashinda Wajemi kule Mesopotamia (Iraq). Mw. 639 wakaingia Misri na kuteka Aleksandria miaka mitatu baadaye. 642 waliteka sehemu kubwa ya Uajemi yenyewe. Mw. 670/696 waliteka mkoa wa "Afrika" ya kiroma pamoja na Karthago (Tunisia leo). Mwaka 711 wakavuka Bahari na kuingia Hispania (Ulaya ya Kusini). Wakaenea pia Asia ya Kati. Mwaka 751 walipigana na jeshi la Uchina. Uenezaji wao ulikuwa wa haraka sana. Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na wenyeji mw. 732 lakini walitawala sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata. Walishindwa kuteka Bizanti yenyewe iliyoendelea kutawala Asia Ndogo. Na kule Mashariki wakasimama ana kwa ana mbele ya wanajeshi wa Wahindi na Wachina. Miaka mia moja baada ya kifo cha Muhamad sehemu kubwa ya dunia kati ya Maroko hadi Bonde la Indus ilikuwa chini ya bendera ya Uislamu.

4.4.2. Wakristo kuwa Waislamu

Utawala wa kiislamu ulifika nchi hizo kwa njia ya vita. Mwanzoni walikuwa Waarabu kadhaa tu walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na kuchukua nafasi ya kupata maisha nafuu. Walifundishwa ya kwamba ikiwa wanakufa vitani watapokelewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani wangekuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio waislamu. Imani ya aina hii kweli iliwapa nguvu na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao waliohamia Afrika ya Kaskazini na nchi za Asia ya Kati.

Chini ya utawala wa Waarabu waislamu wenyeji waliruhusiwa kuendelea na desturi zao lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio waislamu walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani. Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala. Vilevile kanisa lilidhoofishwa kule Afrika ya Kaskazini-Magharibi kutokana na farakano la Donato (III,3.4.). Baada ya karne za kulaumiana kati ya Wakristo wengine walikuwa na wasiwasi juu ya ukweli wa mafundisho ya kanisa. Masharti ya kujiunga na Uislamu yalikuwa rahisi sana. Hakuna masharti ya mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haikuwezekana kurudi katika Ukristo maana sheria ya kiislamu iliruhusu Mkristo kuwa Mwislamu lakini ilikataa kwa adhabu ya mauti Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.

Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa ya kwamba wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea.

Lakini vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha zaidi ustahimilivu kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi, Wafuasi wa dini ya Uajemi n.k.). Lakini Waturuki, Wajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali. Hasa vipindi vya vita kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu dhidi ya Wakristo chini ya utawala wa kiarabu. Katika vipindi hivi Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa, n.k..

4.4.3. Vita vya msalaba

Kuanzia mwaka 1095 Wakristo wakatoliki wa Ulaya walijaribu kuwaondoa Waislamu katika nchi za Mashariki ya Kati. Wakristo waliohiji Yerusalemu kutoka Ulaya walishambuliwa njiani mara kwa mara. Naye Kaisari wa Bizanti aliomba msaada wa Wakristo wa magharibi dhidi ya mashambulio ya Waturuki waislamu. Papa aliwaita mataifa ya Ulaya ya Katoliki kuikomboa nchi takatifu. Tangu mw. 1096 hadi mw. 1270 kempeni za kijeshi zilianzishwa Ulaya kuelekea Yerusalemu.

Kempeni hizi huitwa "Vita vya msalaba" kwani wanajeshi walipokea kanisani alama ya msalaba wa kitambaa waliobandika juu ya nguo zao. Walifundishwa kuwa vita hivi ni vita vitakatifu atakayekufa atafika mbinguni kwa hakika. Wataalamu wanahisi kama hapo athari za mafundisho ya kiislamu juu ya "jihadi" zimeingia katika Ukristo.

Mw. 1099 jeshi la Ulaya limefika mbele ya kuta za Yerusalemu. Baada ya mapigano mafupi jeshi la msalaba liliwashinda wateteaji waislamu. Katika hasira ya mapigano waliwaua ovyo wakazi wengi sana, wazee na watoto, Waislamu, Wakristo na Wayahudi. Mkabaila mfaransa alipokea cheo cha "Mfalme wa Yerusalemu".

Lakini miaka 100 baadaye Sultani Salah-ed-Din wa Misri aliwafukuza waMsalaba tena katika Yerusalemu. Miaka 40 baadaye alirudisha mji kwa hiari baada ya kupatana na Mfalme Mjerumani. Lakini muda wote waUlaya walitawala sehemu ya Palestina na Siria tu. Waislamu waliwaona kama maadui. Hata wakristo wenyeji waorthodoksi hawakuwakubali kuwa wakombozi kwani walijaribu kuwaunganisha wakristo wote chini ya kanisa la Kiroma-Katoliki. Safari moja iliyoondoka Ulaya mw. 1204 kuikomboa Yerusalemu ilifika mpaka Bizanti tu ambako wanajeshi wa msalaba waliteka mji, kupora utajiri na kumfukuza Kaisari wa Bizanti. Miaka 100 baadaye Kaisari alirudi na kuunda upya Ufalme wa Roma ya Mashariki.

Mwaka 1291 jeshi la kiislamu liliwafukuza wanajeshi wa msalaba kabisa katika nchi takatifu. Hawakurudi tena. Lakini waliwahi kuvunja nguvu ya Bizanti kiasi cha kutosha. Kumbe Ulaya ya Magharibi iliharibu ulinzi wake dhidi ya Waturuki waliofaulu baadaye kuingia Ulaya. Badala ya kufukuzwa jeshi la Waturuki lilianza kuishambulia Ulaya ya Kusini-Mashariki. Mw. 1453 ulianguka mji wa Bizanti, na mw. 1529 Waturuki walifika mpaka Vienna mji mkuu wa Mfalme wa Ujerumani. Hapo walirudishwa nyuma. Lakini nchi nyingi za Ulaya ya Kusini-Mashariki pamoja na Wakristo zao zilikaa chini ya Waturuki kwa karne zijazo.

Kwa ujumla majaribio ya "vita vya msalaba vya kuikomboa nchi takatifu" yalishindikana. Vita hivi vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya waarabu waislamu. Kipindi cha vita vya kidini kilisababisha mateso mengi ya wakristo waorthodoksi chini ya Waislamu.7 Walilipa madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya ya Magharibi.

Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengi wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya waislamu. Maisha haya yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza). Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile Kigiriki-Orthodoksi, Kikopti (Misri), Kisiria-Orthodoksi, Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Sababu kuu ni ya kwamba kama Mkristo amekuwa mwislamu - hakuweza kurudi tena. Sheria ya kiislamu inamruhusu mkristo kugeukia Uislamu, lakini mtu aliyekuwa mwislamu anastahili adhabu ya mauti akigeukia Ukristo au dini nyingine. pamoja na hayo wakristo walianza kuhamia nchi ambako wangekuwa raia huru bila kasoro.

Lakini Wakristo wengi wakati ule walikuwa na makosa yaleyale ya kukosa ustahimilivu kwa watu wenye imani tofauti. Hakuna mwislamu aliyeweza kubaki katika nchi za Hispania na Ureno baada ya kuvunjwa wa utawala wa kiarabu. Tukilinganisha hali ya Wakristo kule Misri na hali ya Waislamu kule Hispania hatuna budi kushukuru na kuwasifu Waislamu kwa kuwavumilia wakristo hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso. Lakini pia tusisahau ya kwamba ipo mifano mingine: wakristo wote walifyekwa katika Uarabuni penyewe - na waislamu walibaki chini ya utawala wa Waaustria wakristo walipotawala nchi za Ulaya ya Kusini-Mashariki. Kweli kati ya dini hizo mbili hakuna anayeweza kujisifu juu ya historia yake bila kukubali makosa na kasoro zake.


4.5. KANISA LILIVYOENDELEA ULAYA NA ASIA

Tumeshawahi kuangalia hali ya kanisa katika Afrika. Tangu kuja kwa Uislamu uenezaji wa Injili ulikwama na kurudi nyuma. Kusini mwa Sahara ilifika kupitia Nubia lakini baada ya Nubia kuwa ndani ya eneo la kiislamu athari hii haikuendelea. Kumbe uenezaji wa Ukristo katika kipindi kile ulipatikana Ulaya na Asia.

Kule Ulaya makabila mengi yaliendelea kupokea Ukristo. Wakati mwingine watu walivutwa na mahubiri kuacha upagani wa kale na kubatizwa. Mara nyingi waliona ya kwamba miungu ya kikabila ya kale hayana msaada tena katika mazingira iliyobadilika. Waliweza kuvutwa na mfano bora wa wamonaki walioishi kati yao, au kushangazwa na elimu au maendeleo yao. Wakati mwingine Wafalme wakaamua kwa sababu za kiroho au sababu za kisiasa kuwa Wakristo na kubatizwa pamoja na kabila au taifa zima. Katika mawazo ya waulaya wa kale dini haikuwa jambo la mtu binafsi lakini jambo la kijamii. Wakati mwingine washindi wa vita waliamua kuwabatiza maadui wa vita ili kujenga uhusiano wa kiroho nao. Hapo ndipo sababu ya ubatizo kwa mabavu ulioweza kutokea katika nchi kadhaa.

Mfano mojawapo ni ubatizo wa Wasaksoni. Wasaksoni walikuwa kabila kubwa katika eneo la Ujerumani ya kaskazini. Ni mababu yao waliovuka bahari na kuteka Uingereza (Anglo-Saxons). Wakati ule Wajerumani wengi walikuwa Wakristo lakini Wasaksoni waliendelea kutetea upagani wao. Mfalme wa eneo la Ufaransa na Ujerumani ya Magharibi aliyeitwa Karolo Mkuu alipigana nao mara kwa mara. Mwishowe aliona wakiwa ni wapagani hatawashinda. Mnamo mwaka 800 B.K. aliwapa chaguo: Upanga au ubatizo. Mwanzoni walikataa akawaua machifu 4000 wa wasaksoni katika siku moja. Waliobaki wakabatizwa wakawaamuru wenzao kubatizwa vilevile. Hivyo ndivyo eneo kubwa lilipokea Ukristo lakini sio kwa sababu ya imani lakini kwa sababu ya kulazimishwa. Si ajabu ya kwamba kwa muda mrefu Ukristo wa Ulaya katika nchi mbalimbali ulikuwa wa juujuu tu ukaonyesha dalili za mchanganyiko wa injili na desturi za upagani wa kale. Kumbe Ukristo ulikwenda njia ndefu sana tangu zamani za mashahidi wa Aleksandria na Karthago waliokufa badala ya kukana Ukristo wao mpaka wale Wakristo wapya wa Saksoni walioona heri wabatizwe kuliko kufa.

Maeneo mapya ya Ukristo yalifuata desturi za kule walikotoka wahubiri wao. Hivyo ndivyo makabila ya Ulaya ya kaskazini walivyojiunga na Kanisa la kiroma-katoliki. Makabila ya Mashariki wakawa Waorthodoksi wakipokea ubatizo kutoka kwa ya wajumbe wa Askofu wa Bizanti. Mpaka leo kule Ulaya mataifa ya Warusi, Wabulgaria, Waromania na Waserbia (Yugoslavia) pamoja na Wagiriki ni Waorthodoksi. (Kwetu Afrika ni hasa nchi za Misri na Ethiopia zinazofuata mapokeo ya Kikopti-Orthodoksi.) Mnamo mwaka 1000 karibu maeneo yote ya Ulaya yalikuwa na Wakristo ingawa mara nyingi kwa jina tu.

Kule Asia ni Ukristo wa Kiorthodoksi ulioendelea vizuri katika nchi nyingi. Waliotangulia walikuwa wamisionari toka Misri wakafika Bara Hindi. Mpaka leo lipo Kanisa la Bara Hindi Kusini (jimbo la Kerala). Wakristo walienea pia kule Uajemi na Asia ya Katikati. Wamisionari wa Kanisa la Uajemi walihubiri pote Asia ya Kati hadi Uchina. Lakini maendeleo haya yalirudishwa nyuma kutokana na mashindano kati ya Ukristo na Uislamu. Kiasili Uislamu ulikuwa na uvumilivu kwa dini za Wakristo na Wayahudi. Katika eneo la Waarabu kanisa liliendelea kupata ustahimilivu kama tulivyoona katika mifano ya kanisa kule Misri au Siria. Kule Wakristo waliweza kuendelea na ibada ya kikristo ingawa kwa matatizo. Lakini kule Asia makabila na mataifa mapya walipokea Uislamu, mara nyingi kwa njia ya vita. Makabila haya ya Waturuki na Wamongolia yalifuata imani ya kiislamu kwa ukali kuliko waarabu wenyewe. Waliwalazimisha wote waliokuwa na imani tofauti wawe Waislamu kama ni Wakristo, Wabuddha au wafuasi wa dini za asili. Mtawala mwislamu Tamerlan kiongozi wa Wamongolia aliua wakristo malakhi na kubomoa makanisa maelfu alipofanya vita vyake kule Asia ya Kati. Katika vita vingi Ukristo wa Asia ya Kati uliharibika. Maeneo makubwa yalichomwa moto, watu walilazimishwa kwa upanga kuwa waislamu, Wakristo waliuawa na makanisa yalibomolewa. Mnamo mwaka 1400 Ukristo wa Asia ulibaki katika Mashariki ya Kati tu (Asia ya Magharibi) pamoja na Bara Hindi Kusini. Kumbe uzito wa Ulaya uliongezeka katika kanisa kwani ni hapa tu ya kwamba Ukristo uliweza kuendelea bila maadui wa nje.

Maswali na Maarifa:

1. Taja mbinu mbalimbali yaliyotumika kueneza Ukristo katika Ulaya kabla ya mw. 1000. Taja angalau mbinu 3 tofauti. Unaonaje mbinu hizi?

2. Wamisionari wa Kanisa la Kale walifika katika sehemu zipi za Asia ? 3. Eleza sababu zilizofanya Ulaya kuwa kitovu cha Ukristo kuanzia mw. 1400.

SURA YA TANO : ULAYA KARNE ZA KATIKATI

1. Ukristo Ulaya, nguvu na shida za kanisa, 2. Majaribio ya matengenezo: Fransisko 2a. Farakano ktk. upapa 3. Hus/Wamoravia

5.1. MAENDELEO NA MATATIZO YA KANISA KULE ULAYA

Katika sura tatu zinazofuata tutaangalia zaidi habari za kanisa kule Ulaya. Tukiangalia hali yetu kama Wakristo wa Tanzania tunaona madhehebu mbalimbali. Madhehebu mengi yana asili yao kule Ulaya. Kumbe tukitaka kuelewa kwa nini tunaweza kuitwa Waroma (mji wa Italia), Walutheri (jina la Mjerumani), Wamoravian (mkoa wa Cekoslovakia), Waanglikana (jina la kale la "Uingereza") sio mbaya kujua historia yake. Labda elimu hii inaweza kutusababisha tushangae na kujiuliza: je, inafaa kwa Wakristo waafrika kuitwa kwa majina yanayotokana na matukio ya kale kule Ulaya? Je, inafaa kuangalia mpaka leo hii petu Tanzania tofauti zilizotokea karne nyingi zilizopita katika sehemu nyingine ya dunia ? Hatuna njia ya kujenga zaidi umoja wa Ukristo ?

Katika mwaka 1200 kwa ujumla Ulaya ilikuwa bara la Wakristo. Popote kanisa lilikuwa chini ya ulinzi wa serikali. Watu wote walipaswa kuonekana kuwa Wakristo. Watu wa pekee wenye tofauti walikuwa Wayahudi, lakini waliruhusiwa kuishi katika nchi kadhaa tu. Katika nchi zingine walifukuzwa. Kanisa la Kiroma-Katoliki (au: la Kiorthodoksi katika Mashariki) ilikuwa dini rasmi ya serikali. Katika mila na desturi za Ulaya zilizotangulia kuja kwa Ukristo umoja huo wa Dini na Kabila ulikuwa kawaida.

Kwa upande mmoja Ukristo ulikuwa na nguvu sana katika Ulaya wakati ule. Lakini kwa ndani ulikuwa na udhaifu wa aina mbalimbali. Wataalamu wengine huita kipindi hiki katika historia ya Ulaya "Karne za Katikati" au "Nyakati za Giza". Maana yake ni kipindi baada ya kuanguka kwa utamaduni na uchumi wa hali ya juu uliokuwapo wakati wa Dola la Roma na kipindi kuanzia mw. 1500 ambacho uchumi na elimu vilianza kusogea mbele tena. Kumbe tutajaribu kuangalia pande zote mbili yaani mafanyikio na matatizo.

5.1.1. Kuingiliana kwa dini na siasa

Sisi tumezoea ya kwamba serikali haina dini. Kila mwananchi ni huru kuchagua imani yake. Kumbe wazo hili si kawaida popote duniani. Mpaka leo tunasikia habari za nchi zinazoweka kipaumbele kwa dini au dhehebu fulani kwa upande wa serikali. Kule Uingereza mfalme au malkia anapaswa kuwa Mkristo wa Kianglikana na pia yeye ni mlezi mkuu wa Kanisa la Kianglikana. - Kule Denmark na Sweden wafalme wanapaswa kuwa Wakristo wa Kilutheri. - Katika nchi nyingi za Waarabu Raisi wa Taifa awe Mwislamu wa dhehebu wa Sunni. - Kule Uajemi (Iran) Raisi huchaguliwa kati ya wataalamu waislamu wa dhehebu la Shia. - Taratibu hizo ni mabaki ya utaratibu ambao miaka 200 iliyopita ulikuwa kawaida katika sehemu nyingi za dunia.

Zamani ilikuwa kawaida katika nchi nyingi duniani kuangalia mambo ya dini na mambo ya dola pamoja. Agano Jipya halina amri yoyote juu ya kuunda "serikali za kikristo". Kinyume chake Wakristo wanafundishwa na mtume Paulo kuiombea serikali ya kipagani ya Kaisari wa Roma. Lakini tangu viongozi wa mataifa waliokuwa Wakristo wenyewe waliona lazima kulitumia Kanisa kama chombo kinachoongeza umoja na nguvu ya nchi.

Katika Ulaya ya karne za katikati kanisa na serikali zilikwenda pamoja. Kule katika sehemu za Waorthodoksi kanisa lilikuwa chini ya wafalme waliokubaliwa kuwa walezi wakuu wa kanisa. Katika magharibi penye Wakristo wakatoliki kanisa lilikuwa na uhuru zaidi. Lakini hata hapa mambo yaliingiliana. Utaratibu wa utawala wakati ule ulikuwa wa kikabaila yaani machifu na watu wa familia za wakubwa walitawala maeneo chini ya serikali kuu ya mfalme.

  • a. Wafalme na watawala walikabidhiwa madaraka yao katika ibada kanisani.
  • b. Watawala walikabidhi madaraka mengi kwa maaskofu. Askofu aliweza kuunganisha uongozi wa kanisa katika eneo lake pamoja na wajibu wa kiserikali. Viongozi wa kanisa waliaminika kuliko machifu wa kawaida. Machifu wakikabidhiwa madaraka fulani kwa muda walijaribu mara nyingi kuyashika kama mali yao. Wakatafuta kuongeza mali yao kuwa urithi wa familia. Faida ya kutumia watu wa kanisa ilikuwa mapadre na maaskofu hawaoi hawana watoto hawana hamu ya kutafuta urithi kwa ajili ya watoto wao.
  • c. Watawala wakagandamiza wapinzani wote wa kanisa kwani wakaona wapinzani wale wangeleta vurugu hata kisiasa.
  • d. Maaskofu (na viongozi wengine wa kikanisa) walichaguliwa mara nyingi kutokana na sifa zao za kisiasa kuliko uwezo wa kuongoza kiroho. Kwa sababu cheo cha askofu kiliambatana na mapato makubwa ni familia za machifu zilizopeleka wana wao katika nafasi hizo. Kwa njia hii tabaka za kijamii zilionekana vilevile ndani ya kanisa: viongozi wa kanisa walitoka katika familia za wakubwa, nafasi za chini zilipewa watumishi kutoka familia za matabaka ya chini.

5.1.2. Utajiri wa Kanisa

Kanisa lilikuwa tajiri sana. Makanisa yalijengwa na wakubwa waliotoa baadaye shamba fulani kuwa mradi wa kanisa lile. Ilikuwa kawaida kwa kanisa kumiliki mashamba ya namna mbalimbali, moja kulipia matengenezo ya jengo, lingine kulipia gharama za mchungaji au padre kule, lingine kumlipa msaidizi wake n.k.. Kanisa kubwa lenye watumishi wengi lilikuwa na mapato makubwa. Watu wa vijiji kadhaa walitakiwa kuchanga sehemu ya mavuno yao na kufanyia kanisa kazi siku mbili kwa juma kama kodi kwa ajili ya gharama za jengo, mapadre kadhaa au askofu.

Mara nyingi zawadi hizo za mashamba au vijiji zilitolewa kama sadaka - ama kama alama ya toba au kama shukrani. Sadaka za makabaila ziliongeza utajiri wa kanisa. Familia za makabaila zilichagua nafasi za uaskofu kwa watoto wao. Mwana wa chifu aliyepokelewa katika upadre alizuiliwa kuunda familia na kurithi cheo cha baba - lakini alipanda ngazi ndani ya kanisa, kupata cheo cha heshima katika jamii na kuwa na mapato makubwa yaliyomwezesha kuishi maisha mazuri na tajiri kama familia yake.

Wakati wa njaa maskini waliweza kupata misaada kanisani hasa katika nyumba za watawa (wamonaki). Wamonaki waliweza kuuza hazina ya kanisa hata mapambo ya dhahabu yaliyopatikana wakati wa utajiri kuwasaidia maskini. Lakini mara nyingi maaskofu walijisikia kuwa wakubwa nao wengi hawakujali matatizo ya wadogo.

5.1.3. Ugandamizaji wa Wakristo "wazushi"

Serikali ziliona ni lazima kutetea umoja wa kanisa. Hapa ilikuwa majaribio kwa viongozi wa kanisa kutumia nguvu ya serikali kuhakikisha uongozi wao ufuatwe. Ikiwa Wakristo walijitokeza waliodai mabadiliko au kupinga uongozi wa kanisa serikali iliingilia kati na kuwagandamiza kama "wazushi". Ilikuwa hasa utajiri wa kanisa na wa maaskofu wengi uliosababisha ugomvi.

Kule Ufaransa alijitokeza mfanyabiashara mmoja kwa jina Petro Waldo. Katika karne ya 13. akasikia wito wa Kristo katika maisha yake. Aliwapa maskini mali yake yote akaanza maisha ya kuhubiri akijaribu kumwiga Bwana Yesu. Akafundisha ya kwamba mkristo wa kweli anapaswa kumfuata Yesu hata katika maisha ya umaskini. Akauliza: Je, mbona Kristo alikuwa maskini lakini maaskofu wa leo ni matajiri? - Wafuasi wake wakaanza kukutana nje ya makanisa. Kanisa liliwatangaza kuwa wazushi wakatafutwa na kukamatwa na serikali. Wengine wakafungwa gerezani wengine wakauawa. Baadaye ilikuwa kawaida kuweka "wazushi" mbele ya mahakama za pekee na kuwachoma moto. Papa Innosenti III akaunda idara ya pekee "Baraza la Ulinzi wa Imani". Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kuwatafuta "wazushi" na kuwahoji juu ya imani zao. Wakionekana kuwa na makosa walikabidhiwa mkononi mwa serikali iliyotoa adhabu ya mauti. Lakini hata hivyo mawazo yao yaliendelea kuzunguka kati ya watu wa kawaida. Wawaldo walihubiri kwa siri katika nchi nyingi.

5.1.4. Uhaba wa elimu

Karne za katikati kule Ulaya ilikuwa kipindi pasipo na elimu kwa watu wengi. Kwa jumla utamaduni wa juu wa kiroma ulianguka chini. Karibu watu wote hawakujua kusoma wala kuandika. Katika nchi nyingi ni watawa wa kanisa tu waliosoma. Tatizo mojawapo ni uhaba wa vitabu. Mashine za kupiga chapa vitabu hazikujulikana. Maana yake kila kitabu kiliandikwa kwa mkono. Nakala ya Biblia iliandikwa kwa muda wa mwaka au zaidi. Hivyo vitabu vilikuwa ghali sana. Mtu wa kawaida alishindwa kununua kitabu, hata kama angeweza kusoma. Kumbe Wakristo wengi sana hawakuwahi kusoma Biblia. Zaidi ya hapo kanisa katoliki lilitumia Biblia katika lugha moja tu popote yaani lugha ya kilatini. Kilatini ilikuwa pia lugha ya ibada zote kwa ajili ya nyimbo, masomo na sala. Kutumia lugha moja popote kulisaidia sana kutunza umoja wa kanisa. Lakini watu wa kawaida hawakuelewa kilatini, hata mapadre wengi hawakuelewa vizuri. Kidogo ingekuwa kama tungesoma Biblia na kuhubiri katika makanisa yetu hapa Tanzania kwa Kiingereza au Kifaransa tu. Hali hii ingesababisha elimu ya kikristo kuwa chini kati ya Wakristo wa kawaida. Badala yake walijali sana mambo ya pembeni. Watu wengi waliona muhimu sana kusafiri kwenye "mahali patakatifu" wakiamini ya kwamba safari za aina hii zinaleta sifa mbele za Mungu. Wengi walijali sana habari za masalio (taz. nyong.)8. Ilikuwa njema kusafiri na kusali kwenye kaburi la mtakatifu yaani shahidi wa imani aliyekufa kwa ajili ya imani yake zamani. (Tendo ambalo hata sisi wa leo tunaweza kuona vema likitusaidia kutafakari na kuiga mfano mwema lakini si kwa sababu ya hali ya mahali penyewe mbele za Mungu). Kumbe mifano inaonyesha jinsi gani imani ya kiasili ya ushirikina bado ilikuwa na nguvu baada ya kuenea kwa Ukristo.


5.2. MAJARIBIO YA MATENGENEZO I

5.2.1. Farakano ndani ya Upapa

Matatizo ya kanisa yalionekana mpaka ngazi ya upapa. Mara nyingi Papa mpya (Askofu wa Roma) alichaguliwa kufuatana na ukoo au sifa za kisiasa tu. Kumbe cheo cha Papa kiliingizwa katika siasa kubwa kati ya wafalme wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa. Mnamo mwaka 1300 Papa Bonifas VIII alidai kuwa na madaraka juu ya wafalme wote. Mfalme wa Ufaransa alikasirika akajaribu kulipiza kisasi. Migongano hii ilisababisha farakano ndani ya upapa. Sehemu ya maaskofu walimchagua papa kule Roma, wengine wakamchagua mwingine kuwa papa aliyekaa Ufaransa. Farakano hili liliendelea kwa muda wa karibu karne moja. Hali ilikuwa vibaya zaidi, mwaka 1409 walikuwepo watu watatu waliojiita "Papa" na kukubaliwa na sehemu ya maaskofu. 9

Maaskofu na wakristo walichoka sana na mfarakano huu. Mtaguso wa Maaskofu wote mwaka 1417 kule Konstanz (Ujerumani) uliondoa mapapa wote watatu na kumchagua Papa mmoja Martin V..

5.2.2. Fransisko na mwendo wa umaskini

Wakristo wengine walianza kukata tamaa juu ya hali ya kanisa. Katika matatizo haya Mungu aliwaita Wakristo wairudishe upya Roho ya Injili katika kanisa. Mmoja wao ni Fransisko wa Assisi. Alizaliwa katika familia tajiri akawa kijana aliyependa sana muziki, sherehe na divai. Vitani alifungwa mwaka mmoja akaanza kumtafuta Mungu. Siku mmoja aliposali akasikia sauti "nenda ukatengeneze kanisa langu lililobomolewa". Kumbe akachukua pesa akaanza kutengeneza kanisa dogo lililokuwa bovu sana. Baba yake akakasirika akiona kijana anapoteza mali ya familia. Kumbe Fransisko akakutana na Baba mbele ya Askofu uwanjani akavua nguo zake na kumrudishia baba pamoja na pesa zake. "Kuanzia sasa nitasema tu Baba yetu uliye mbinguni" Fransisko akaishi maisha kama mtawa akimwomba Mungu amwonyeshe njia. Siku moja alisikia somo la Matthayo 10, 7-20 kanisani. Sasa alijua: Hiyo ndiyo njia yangu! Alielewa maana yake "ukatengeneze kanisa langu" si jengo lile dogo alipoanza lakini Kanisa la Kristo lililobomolewa kwa sababu ujumbe wa Injili ulisahauliwa.

Alianza maisha ya umaskini akijaribu kuiga mfano wa Yesu. Akazunguka akivaa kanzu ya gunia na kuhubiri upendo wa Mungu. Vijana wengine wakamfuata wakaunda utaratibu wa maisha ya pamoja. Fransisko akaona ya kwamba nyumba za wamonaki zilikuwa tajiri sana. (ingawa mmonaki mwenyewe hakuwa na mali lakini jumuiya yake iliweza kuwa tajiri). Kwa wafuasi wake alikataa jumuiya isiwe na mali. Fransisko alipendwa sana kwani alionyesha imani ya furaha katika Kristo na upendo kwa watu wote. Mwenyewe alisafiri mpaka Afrika akahubiri mbele ya Sultani wa Misri. Ingawa wakati ule vita viliendelea kati ya jeshi la kikatoliki la Ulaya na Waislamu Sultani alimpokea kwa heshima akamsikiliza na kumruhusu kurudi kwake. Fransisko aliamini ya kwamba majaribio yote ya kuwashinda Waislamu kwa silaha ni ya bure. Kwa mkristo hakuna njia nyingine kuliko mfano wa Bwana Yesu yaani kwa upendo na unyenyekevu.

Mwendo wa Wafransisko ulienea haraka sana. Ndugu wafransisko walitembea popote wakivaa usiku na mchana kanzu ileile na kupewa chakula kutoka kwa Wakristo wa kawaida. Tofauti na wamonaki wengine wakaishi kati ya watu wa kawaida wakihubiri na kufundisha. Walikuwa mfano kwa kumtegemea Mungu kabisa katika umaskini kwani hawakuwa na mali wala mapato kuliko sadaka za hiari kutoka kwa wakristo. Katika maisha haya walifanana na vikundi kama Wawaldo (taz. juu 1.3.) lakini wakawafundisha Wakristo kufuata uongozi wa kanisa na maaskofu. Kumbe Wafransisko walikuwa silaha muhimu ya Kanisa la katoliki dhidi ya wapinzani waliopinga utajiri wa Kanisa.

Mahali pengi wakristo wa kawaida wakajiunga na jumuiya za kiroho zilizokuwa chini ya ulezi wa Wafransisko.

2.3. Kujenga maisha ya kiroho: shirika za watawa (Dominiko na wengine)

Muda uleule Mhispania kwa jina la Dominiko aliunda shirika la watawa. Kusudi la ushirika huu ilikuwa mahubiri. Kumbe shirika kama Wafransisko na Wadominiko zilinyosha kiasi kasoro za kukosa mahubiri katika misa ya kawaida. Walifanya kazi muhimu sana ya kuwafundisha watu wadogo waliokuwa maskini na bila elimu wala uwezo wa kusoma.

Wadominiko waliogopwa pia katika kazi ya kuwatafuta na kushtaki walioitwa "wazushi".

5.3. YOHANA HUS NA UMOJA WA NDUGU (WAMORAVIA)

5.3.1. Mwalimu Hus

Mwaka 1412 padre mmoja alihubiri kwa nguvu sana kule Prag (leo: nchi ya Ucheki). Yohana Hus alikuwa mwalimu wa Theologia kwenye Chuo Kikuu. Mwaka huo barua ya Papa wa Roma (walikuwepo mapapa wawili wakati ule) ilisomwa iliyowaomba Wakristo kuchanga hela ili kumsaidia kushinda "vita vitakatifu". Shabaha yake ilikuwa kumshinda Papa mwenzake. Maaskofu wa eneo la Prag walisambaza barua ile. Wakristo waliambiwa kununua vyeti vya rehema. Kiasi mkristo alivyotoa alipewa cheti kilichosema "Fulani asamehewa adhabu ya dhambi zake kwa muda wa miaka fulani katika moto wa toharani". Hus aliona ni hotuba ya uongo akapinga. Tena akafundisha ya kwamba mamlaka kuu kanisani ni katika Biblia si katika maazimio ya maaskofu au Papa.

Alishtakiwa mbele ya mfalme lakini wengi walimfuata. Maaskofu wakamtangaza kuwa ni mzushi. Akahifadhiwa na kufichwa na mkabaila katika boma lake. Mwaka 1415 palikuwa na mkutano mkuu wa maaskofu wote wa katoliki kule Konstanz/Ujerumani. Hus akaitwa kujitetea mbele ya mkutano huo. Akaahidiwa ulinzi wa mfalme yaani angeweza kurudi tena hata akionekana kuwa mzushi. Lakini kinyume cha ahadi alikamatwa akahukumiwa kuwa mwasi na mzushi. Akachomwa moto akiwa hai.

5.3.2. Wahus

Wafuasi wake kule katika mikoa ya Bohemia na Moravia (Chekoslovakia) wakasikitika mno. Wengine wakachukua silaha wakataka kutenga nchi yao kutoka uongozi wa kanisa lililomchoma Hus moto. Vita vya miaka mingi ilianza kati ya Wahus na askari wa mfalme na maaskofu. Alama ya Wahus ilikuwa kikombe cha Ekaristia (Chakula cha Bwana) kwani Hus alifundisha ya kwamba Wakristo wote wanapaswa kupokea kikombe kanisani. (Kanisa la Kikatoliki lilianza desturi ya kutoa kikombe kwa mapadre tu tangu mwaka 1200). Mwishoni Ukristo wa Bohemia na Moravia uligawanyika. Wahus wakali waliojaribu kuunda utaratibu wa kisiasa juu ya mahubiri ya Yesu na kuwalazimisha wote kuufuata kwa silaha wakashindwa. Wengine wakabaki ndani ya kanisa la Kiroma-katoliki. Wengine wakafuata Wahus wasio wakali waliopatana na wakubwa wa nchi. Wakapata ustahimilivu kuwa na ibada ya misa (chakula cha Bwana) wakipokea mkate na kikombe.

5.3.3. Umoja wa Ndugu - Wamoravian

Mwaka 1457 kikundi kidogo cha wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini walianzisha jumuiya ya kikristo iliyoitwa "Umoja wa Ndugu". Wakajaribu kuishi kama ndugu Wakristo wakikaa pamoja, kufanya kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao. Mbinu hii ilifanana na wamonaki wa aina ya Wafransisko lakini walikuwa jumuiya ya watu waliooana na kuwa na watoto. Wakaona muhimu wasiwe na taratibu za utawala katika kanisa lakini viongozi wawe kama ndugu na watumishi wa wengine. Hawakutaka kumlazimisha yeyote katika mambo ya imani kama ilivyokuwa katika maeneo ya Wakatoliki na ya Wahus wengine. Umoja huo ulienea katika mikoa ya Bohemia na Moravia ukawa mwanzo wa kanisa linaloitwa kwetu la "Moravian".

Mwanzoni walihudumiwa kiroho na mapadre wa Kanisa kubwa lakini mw. 1467 waliamua kuwachagua watumishi wao wenyewe. Askofu wa kwanza wa Ndugu alibarikiwa na Askofu wa Wawaldo (taz. 5.1.3.). Walitunza mpaka leo ngazi za mashemasi, makasisi na uaskofu.


SURA YA SITA: MATENGENEZO NA MAFARAKANO

1. Ukristo karne ya 16 2. M. Luther na vyeti vya rehema 3. Mafundisho na Kujenga kanisa jipya 4. Umuhimu wa Luther

6.1. UKRISTO WAKATI WA KARNE YA 16

Karne za 15/16 zilikuwa kipindi muhimu katika historia ya Ukristo. Petu Afrika mataifa ya kikristo ya Kushi (Sudan) yalishindwa vitani na Waarabu kutoka Misri wakati ule. Ukristo uligandamizwa katika eneo la Sudan. Ethiopia ikabaki kama kisiwa katika bahari ya Uislamu. Kule Asia ya Kati jeshi la Wamongolia Waislamu liliteka na kuharibu nchi nyingi chini ya kiongozi Timur. Makanisa yalichomwa moto popote Asia ya Kati na Uajemi mpaka Palestina. (Wakaharibu vilevile nyumba za dini zingine kama Wabudda au Wahindu). Mwaka 1452 mji mkubwa wa Bizanti ukatekwa na jeshi la Waturuki waislamu. Ilikuwa mwisho wa Dola la Roma lilivyoendelea katika eneo la Bizanti. Tangu muda ule Wakristo wote wa Mashariki ya Kati waliishi chini ya Waislamu. Waturuki wakaendelea kuingia Ulaya ya Kusini-Mashariki. Kwa muda wakatawala eneo la nchi za Bulgaria, Romania, Albania, Yugoslavia na Hungaria za leo. Ukristo wa kiorthodoksi ulikuwa na uhuru katika nchi za Urusi na Ethiopia tu. Lakini pale Hispania wafalme wakatoliki walifaulu mwishoni kuwafukuza Waarabu katika Hispania. Tangu mwaka 711 hadi 1491 sehemu za Hispania na Ureno zilikuwa chini ya Waarabu waislamu. Sehemu ya wenyeji wamekuwa waislamu. Kumbe 1491 mji wa mwisho uliotawaliwa na Waarabu ulitekwa na mfalme wake akakimbilia Maroko. Sasa wakristo wa nchi hizo walichukua nafasi ya kulipiza kisasi kwa mateso yote ya nyuma. Waarabu na wahispania waislamu waliobaki walilazimishwa kubatizwa, wengine kuuawa.

Lakini ingawa uhusiano kati ya mataifa ya waislamu na Wakristo ulikuwa mgumu waliendelea kufanya biashara. Kwa jumla Waarabu walikuwa na ujuzi zaidi katika mambo ya elimu na ufundi. Vilevile walifaulu sana katika biashara. Ni Waarabu walionunua bidhaa kule India na kuzipeleka mpaka Italia. Waulaya walisikitika sana bei kubwa ya bidhaa hizo na hasa faida kubwa ya wafanyabiashara waislamu lakini wakanunua kwani wenyewe walishindwa kuzitengeneza.

Katika Ulaya ya Kikatoliki farakano la Upapa liliisha. Mkutano wa Konstanz uliomchoma moto Y. Hus ukaangusha mapapa mawili na kumchagua papa mpya wa pamoja. Viongozi mbalimbali wakajitahidi kufuta maovu ndani ya kanisa lakini hawakufaulu sana. Walikuwepo watu wakubwa wengi mno waliofaidika na hali halisi ya kanisa. Nyumba za wamonaki zilienea sana. Ilikuwa kawaida kupeleka watoto wa nyongeza wasioweza kurithi katika nyumba hizo za wamonaki. Cheo cha uaskofu kilikuwa nafasi iliyotafutwa sana na familia za makabaila kwa ajili ya wana wao wasiorithi cheo cha baba. Uaskofu ulipatikana mara nyingi kwa njia ya kuwahonga wenye haki za kumchagua au kumthibitisha askofu. Viongozi wa kanisa katika eneo fulani walipokea hela kabla ya kumchagua askofu mpya. Papa wa Roma alidai hela kabla ya kumthibitisha askofu yeyote aliyechaguliwa. Mfalme alidai hela kabla ya kumkabidhi askofu madaraka ya kiserikali katika eneo lake. Lakini malipo haya yote yalifidiwa tena na watu wa kawaida, wakulima na wafanyabiashara wa eneo la huyu askofu waliopaswa kumlipa kodi zao kila mwaka. Maaskofu wengine walianguka kabisa wakitumia hela zao katika vita dhidi ya majirani wao, kwa ujenzi wa maboma na makanisa uliopita uwezo wao, au kwa maisha ya ulevi na uzinzi. Askofu alikataliwa kuoa lakini walikuwepo wengi waliokuwa na wapenzi wao na kuwajengea nyumba kubwa pamoja na watoto wao. Wakristo wengi wakasikitika juu ya hali hii. Mapapa mbalimbali walijaribu kusimamisha maovu haya lakini kwa jumla bila mafanikio makubwa.

Ni katika kipindi kilekile mawazo mapya yalienea duniani. Anguko la Bizanti mw. 1452 lilisababisha wataalamu wengi wa mashariki kukimbilia Ulaya ya Magharibi wakileta vitabu vyao. Elimu ilianza kusonga mbele. Hasa mjini shule ziliundwa. Mjerumani kwa jina la Gutenberg alitengeneza mashine ya kwanza ya kupiga chapa vitabu. Kumbe vitabu vilianza kupatikana kwa urahisi. Magazeti yalienea. Habari zikazunguka haraka kati ya nchi na nchi, hali isiyojulikana karne nyingi tangu anguko la Dola la Roma. Wataalamu walianza kusoma tena vitabu vya Wagiriki na Waroma wa kale. Wakaanza kusambaza tena mafundisho ya kale kuwa dunia si tambarare lakini mviringo kama chungwa. Na kule Hispania akajitokeza nahodha mmoja kwa jina Kristoforo Kolumbo aliyetaka kujaribisha mafundisho haya mapya. Ikiwa dunia kweli ina umbo la chungwa kumbe ingewezekana kusafiri kuelekea magharibi kutoka Hispania na mwishoni kufika mashariki katika Bara Hindi. Kwa njia hii ingewezekana kufanya biashara moja kwa moja na nchi tajiri za mashariki bila kulipa faida ya wafanyabiashara Waarabu. Mfalme wa Hispania akampa Kolumbo fedha za kuandaa meli tatu. Mwaka 1492 Kolumbo akatoka Hispania akakuta nchi mpya katika magharibi - Marekani. (Akafikiri ya kwamba amefika Bara Hindi hivyo akawaita wenyeji "Wahindi" na visiwa alipofika mwanzoni mpaka leo huitwa "Westindies" = India ya Magharibi). Wahispania walipora utajiri wa mataifa ya Marekani yaliyokosa silaha za kushindana nao. Utajiri huu mpya umesaidia maendeleo ya Ulaya iliyoanza kupita maendeleo ya mataifa ya Waislamu na ya Asia.

Maswali na maarifa (6.1.)

1. Taja mabadiliko makuu ya karne ya 15 kwa Ukristo katika mabara matatu ukitaja a) Afrika, b)Asia c) Ulaya

2. Taja sababu zilizosababisha kuongezeka kwa uzito wa Ulaya katika kanisa duniani. 3. Je, kabla ya Gutenberg vitabu vilitengenezwa namna gani?

6.2. MARTIN LUTHER

Katika miaka hii ya mabadiliko aliishi kule Ujerumani padre na mmonaki kwa jina Martin Luther (*1483 - +1546). Alizaliwa kama mtoto wa mchimba madini aliyemsomesha mtoto wake Martin mjini. Akaendelea kusoma sheria kwenye chuo kikuu. Siku moja alikuwa safarini alipatwa na mvua mkali. Katika hofu yake ya kupigwa na radi alimwomba Mungu akafanya ahadi atakuwa mmonaki akiokolewa. Akaacha masomo ya sheria akajiunga na chama cha wamonaki (watawa). Akatoa nadhiri za utawa akasomeshwa na chama chake elimu ya theologia. Akachukua digrii hata akawa dokta wa theologia. Akapadrishwa akafundisha theologia kwenye chuo kikuu cha Wittenberg /Ujerumani.

Katika mafundisho yake alianza kujiuliza maswali kuhusu kiini cha imani. Alipoingia katika utawa alitafuta amani ya kiroho kwa njia ya kujikana. Akasali akipiga magoti usiku kucha na kumwomba Mungu amhurumie. Akafunga kula chakula muda mrefu. Hata akajipiga kwa kiboko akitaka kuzuia mawazo yenye dhambi. Lakini alishindwa kupata amani moyoni. Hapa akasoma neno la Waroma 1,17: "Haki ya Mungu inadhihirishwa ndani ya injili , toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa: Mwenye haki ataishi kwa imani. (Kiswahili cha kisasa: Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu anavyowafanya watu wakubalike mbele yake; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: Mwenye kukubalika mbele yake Mungu kwa imani, ataishi)". Luther alianza kuelewa kwamba "Haki ya Mungu" si sheria ya Mungu inayomshtaki mwenye dhambi (alivyofundishwa mwenyewe). Akaelewa "haki ya Mungu" ni kipawa au zawadi toka kwa Mungu kwa mtu mwenye dhambi inayomwezesha kuishi katika imani na kwa neema. Zawadi hii tunapokea katika imani tu. Baada ya kuelewa haya akajisikia amezaliwa upya. Hakuweza tena kufundisha maadili mema ya kanisa kuwa njia ya kukubaliwa mbele ya Mungu. Hatuwezi kuhesabiwa haki tukiacha mabaya na kujaribu kutenda mema. Kwa sababu kila mkristo amekuwa mtu mpya kwa ndani lakini bado yumo katika mwili wenye dhambi. Anaweza kutambua hali hii na kupokea neema ya Mungu kama zawadi. Baada ya kuipokea ataishi maisha mapya akijaribu kumshukuru Mungu kwa maisha mazima, kwa maneno na mawazo na matendo yake. Msalabani pa Kristo tunapata neema hii. Tukianguka tena tunapokea msamaha wa dhambi upya kwa njia ya kutubu. Mawazo haya hayakuwa mapya. Ni mafundisho ya Mtume Paulo na vilevile ya Agostino. Maandiko yao yamekuwa mwongozo wa Luther. Lakini hayakufundishwa wakati ule na kanisa lililoorodhesha matendo yaliyohesabiwa kuwa yanaleta neema.

Mawazo haya yalimwongoza padre mkatoliki Luther kuanza kujiuliza polepole juu ya desturi nyingi za kanisa, na mafundisho mbalimbali.

Tatizo limejiweka wazi Luther alipokutana mara ya kwanza na vyeti vya rehema10. Papa Julius II. na Askofu mjerumani mmoja walipatana kuendesha kampeni ya kuuza vyeti vya rehema. Papa Julius alihitaji hela kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya la Mt. Petro kule Roma. Mpaka leo ni jengo kubwa kuliko makanisa yote duniani. Askofu alihitaji hela kulipia madeni yaliyobaki kutokana na kuwahonga waliomchagua kuwa askofu. Kumbe walipatana kumwita mhubiri kwa jina Tetzel aendeshe kempeni ya kuuza vyeti vya rehema wakigawana mapato. Mhubiri huyu alitangaza vyeti hivi bila wasiwasi akisema vitawasaidia hata wazee waliowahi kuaga dunia tayari. Mtoto akimnunulia marehemu cheti kitamtoa mara moja katika moto wa tohara na kumrusha mbinguni. Katika huduma yake ya upadre Luther alisikia Wakristo waliomwambia kwa furaha ya kwamba walisamehewa dhambi zao baada ya kulipia vyeti vya rehema. Luther akashtuka akapinga lakini akaona jinsi Wakristo wa kawaida walivyokimbia kununua vyeti hivi.

Tar. 31.10.1517 akaandika orodha ya hoja 97 alipopinga mafundisho juu ya vyeti hivi akaibandika kwenye mlango wa kanisa la Wittemberg. Akawakaribisha wataalamu wote Wakristo kujadiliana naye. Orodha hii ilipigwa chapa na kusambazwa pote Ujerumani. Katika mikoa yote Wakristo na mapadre wengi wenye elimu wakaelewa na kukubali hoja zake. Viongozi wa kanisa wakaona hatari kwa shughuli zao wakajaribu kumtisha anyamaze. Lakini alijitetea. Mjumbe wa Papa akafika kwake akamwonya aache mafundisho yake yaliyopinga azimio la kanisa. Luther akaendelea kufundisha. Alipopelekewa barua ya Papa iliyomtisha kuwa anaweza kutengwa katika kanisa akaichoma barua moto mbele ya wanafunzi wake. Kwa hiyo akatengwa katika kanisa la kiroma-katoliki akatangazwa kuwa mzushi. Maisha yake yalikuwa hatarini lakini mtawala wa eneo lake alimlinda. Mwaka 1521 Luther aliitwa mbele ya Bunge la Ujerumani ili ajitetee na kukana uzushi wake. Luther akasimama mbele ya Mfalme na wakubwa wote akasema: Nisipoonyeshwa katika Biblia na kwa sababu zinazoeleweka katika akili ya kwamba nimekosa sitakana. Akatangazwa kuwa adui wa kanisa na serikali lakini aliruhusiwa kurudi nyumbani. Mtawala wake akaendelea kumlinda.

Kumbe Luther alitengwa katika kanisa. Lakini watu wengi walimfuata. Katika miaka hii aliendelea kuandika vitabu vingi juu ya matengenezo ya kanisa. Alitaka kurudisha kanisa zima kwenye msingi wa mafundisho ya Biblia. Akaanza kupinga katika msingi huo utajiri wa kanisa na mamlaka ya Papa yalivyofundishwa wakati ule. Akapinga mafundisho ya utawa kuwa ni hali ya juu ya Ukristo. Akawaomba viongozi wa kiserikali kuunda popote shule na kuwafundisha vijana akiwa na matumaini ya kwamba watu wenye elimu hawatafuata imani isiyo na msingi kama vyeti vya rehema.

Kwa jumla mafundisho ya Luther yalikubalika katika sehemu kubwa ya Ujerumani na nchi za jirani. Serikali za nchi hizo ziliona sababu mbalimbali kufuata ushauri wake. Wengi wakaona nafasi ya kutoka katika madai ya utawala wa kanisa la kipapa yaliyoongozana na madai ya kifedha. Walichoka utawala wa Waitalia waliongoza kanisa. Wengine wakaona nafasi ya kuchukua mali za kanisa kwani ikiwa kanisa linatakiwa kuacha utajiri wake mali hiyo itapatikana kwa matumizi mengine. Wengine wakavutwa zaidi na mafundisho ya kiroho yenye nguvu kubwa. Kanisa katoliki pamoja na mfalme walijaribu kugandamiza mwendo wa wafuasi wa Luther. Lakini watawala wengi wa maeneo mbalimbali walisimama upande wake. Nguvu ya serikali kuu ilidhoofishwa pia kutokana na vita dhidi ya Waturuki waislamu walioshambulia mji wa Vienna makao makuu ya ufalme wa Ujerumani. Mfalme alihitaji msaada wa wakubwa wake wote pia msaada wa wale waliomfuata Luther.

Luther mwenyewe alitoka katika utawa akamwoa sista aliyekimbia utawa.11 Aliendelea kutoa mafundisho kwa ajili ya kanisa linalofuata maagizo ya mitume wa kwanza jinsi alivyoelewa. Alipokufa mwaka 1546 farakano lilikuwa limeshatokea tayari katika kanisa. Vitabu vyake viliendelea kuwa na athari kubwa. Kati ya maandiko haya muhimu ni hasa Katekesimo Ndogo yaani mafundisho kwa ajili ya vijana Wakristo wote na pia Katekesimo Kubwa kwa ajili ya wachungaji, pamoja na mengine mengi.

6.3. MAFUNDISHO YAKE NA KUJENGA KANISA UPYA

Luther hakutaka kuleta farakano katika kanisa. Alitaka kurudisha kanisa kwenye msingi wa mitume wa kwanza na maagizo ya Biblia. Muda mrefu alikuwa na tumaini la Mtaguso Mkuu (Mkutano wa Ukristo Mzima) utakaokubali mawazo yake. Alipoona ya kwamba matumaini haya yalishindikana alianza kutengeneza kanisa katika maeneo yaliyokubali mafundisho yake. Akatunza desturi zote za kale zilizopatana na Biblia akafuta zile tu zilizoonekana kuwa kinyume cha Biblia.

Kwanza akafuta kipaumbele kwa mapadre na watawa katika Ukristo. Akafundisha ya kwamba kila mkristo ameshakuwa kasisi wa Kristo katika ubatizo wake. Akafuta masharti ya wachungaji wa kanisa wasioe. Akafuta ibada zilizoendeshwa kwa ajili ya marehemu kwenye msingi wa kulipia - hivyo akaangusha nguzo muhimu ya kiuchumi ya kanisa la kale.


Akasisitiza Wakristo wote wapewe mafundisho juu ya imani akatunga Katekesimo. Akadai sharti wachungaji wawe wasomi waliopita Chuoni. Akadai ibada ziendeshwe katika lugha za watu sio tena katika kilatini na mahubiri ya Biblia yawepo katika kila ibada. Akapinga Chakula cha Bwana (Misa) kuwa sadaka.

Juu ya sakramenti aliweka mashariti mawili: kwanza sakramenti ni ibada ile tu inayotajwa katika Biblia, pili iwe iliamriwa na Yesu mwenyewe. Menginevyo alimfuata Mt. Agostino aliyeeleza Sakramenti kuwa Alama ya nje inayounganishwa na neno la Mungu (kama vile maji ya ubatizo, mkate na divai). Kwa sababu hii alifundisha idadi ya sakramenti kuwa mbili tu si saba tena (Ubatizo na ekaristia/chakula cha Bwana). Juu ya Toba kuwa sakramenti alihangaika, mwanzoni alikubali kwani imeamriwa na Bwana Yesu, baadaye alikataa kwani halina alama ya nje.

Juu ya muundo wa kanisa hakuwa na mawazo ya pekee. Kwake kanisa lilikuwa hasa mwili wa Kristo usioonekana mbele ya macho. Mwili huo wa Kristo umo ndani ya kanisa linavyoonekana mbele ya macho. Kwake utaratibu wa nje ulikuwa jambo la pembeni si lazima kwa wokovu. Akaona ni sawa kama wakristo katika serikali wakishika ulezi wa kanisa ambalo linajitawala chini ya usimamizi huo wa serikali. Kumbe bila kuwa na nia hiyo kweli Luther akaunda kanisa kuwa chombo cha serikali katika maeneo yaliyofuata ushauri wake. Pale mafundisho yake yalipofanywa kuwa mafundisho rasmi kanisa liliendeshwa kama idara ya serikali, hali inayopatikana mpaka leo katika nchi za Skandinavia. Aliona umuhimu wa wataalamu wa Biblia (walimu wa theologia) kuwa na neno katika uongozi wa kanisa12.


6.4. UMUHIMU WA LUTHER KAMA MWALIMU WA KANISA

Kwa jumla mafundisho ya Luther yamekuwa muhimu katika makanisa yote ya kiprotestant, sio tu katika makanisa yanayoitwa "kilutheri".

Kwanza kabisa ni Luther aliyefungua mlango walipopita wengine walioonekana baadaye kama Waanglikana, Wabaptist, Wareformed au Wapresbiterian. Aliweza kupinga vikali viongozi wengine waliotofautiana naye kama wale Wabaptist au Wareformed juu ya maswali kadhaa. Lakini wote walitegemea sehemu za mafundisho yake. Hata Umoja wa Ndugu (Wamoravian) waliotangulia kabla ya Luther walimfuata baadaye katika mambo ya mafundisho, kama juu ya sakramenti au juu ya neema ya Mungu.13

Siku hizi hata Wakatoliki walianza kumwangalia tofauti. Kwa kipindi kirefu cha maisha yake Luther alikuwa mkristo na padre wa Kanisa la Katoliki. Katika kitovu cha mafundisho yake alimfuata Mt. Agostino anayeheshimiwa mpaka leo kuwa mwalimu wa kanisa katoliki. Jinsi alivyopinga upapa na sakramenti saba hawezi kukubaliwa na kanisa katoliki lakini katika mambo mengi mafundisho yake yanaeleweka. Tatizo lililosababisha farakano lile yaani vyeti vya rehema liliondolewa miaka michache baadaye na kanisa katoliki lenyewe. Mtaalamu mmoja alisema: Luther asingetengwa katika Kanisa la Kiroma-katoliki la leo, na asingejitenga mwenyewe siku hizi.


SURA YA SABA : KUTOKEA KWA MADHEHEBU YA KIINJILI NA MATENGENEZO YA KANISA LA KATOLIKI

1. Wareformed (Zwingli/Calvin) 2. Waluther 3.Waanglikana 4. Wabaptist 5. Umoja wa Ndugu 6. Mtaguso wa Trento 7. Wayesu, shughuli zingine katika R.K. 8.Uhusiano wa madhehebu


Habari za Luther zilisikika kote Ulaya. Watu wengi walioochoka na hali mbaya ya kanisa walisoma maandiko yake na kuwa na tumaini la matengenezo ya kanisa zima. Wengine wakasita kuendelea ilipoonekana kwamba farakano litatokea wakaona afadhali kubaki ndani ya kanisa kubwa na kusubiri. Mmojawapo alikuwa mtaalamu mashuhuri Erasmo wa Rotterdam. Lakini penginepo viongozi mbalimbali wakaiga mfano wa Luther. Kwa sababu walikosa mawasiliano kati yao juhudi zikatofautiana katika nchi mbalimbali. Hapo ndipo mwanzo wa madhehebu haya yanayoitwa ya "kiinjili" au ya "kiprotestant".

Maana yake "kiinjili": walijiita hivyo wakitaka kusisitiza ya kwamba wanasimama kwenye msingi wa injili tu, kinyume cha kanisa la kikatoliki lililoona mafundisho yaliyopatikana katika mapokeo ya kanisa kuwa na umuhimu pamoja na Biblia. Maana yake "Kiprotestant" - hivyo ndivyo wafuasi wa Luther na wengine walivyoitwa na wakatoliki. Neno "protestanti" maana yake "wapinzani" (to protest - kupinga). Neno hili lilianza kutumika tangu viongozi wa wafuasi wa Luther walipopinga azimio la bunge lililotaka wajerumani wote warudi chini ya Papa wa Roma.

Neno "katoliki" tunaendelea kutumia hapa kwa maana ya kidhehebu. Kitheologia linamaanisha "kanisa lililopo popote, lililo moja tu kila mahali na kila wakati". Kwa namna hiyo kila mkristo yumo katika Ukatoliki kwani mbele ya kristo kanisa ni moja tu, kila mahali duniani. Waanglikana, Waluteri nao Wamoravian na wengine huamini kabisa ya kwamba wenyewe ni sehemu ya Kanisa lile moja la Bwana Yesu lililopo mahali popote, kwa lugha nyingine: Katoliki au "Katholiko" (umbo hili tunaona katika Liturgia ya Kianglikana au Liturgia ya Umoja wa Afrika ya mashariki) Vilevile hata kanisa la "Kiroma-katoliki" ni la "Kiinjili" kwani inakubali injili (=habari njema") ya Bwana Yesu Kristo. Dhehebu kubwa lenye wafuasi wengi hapa Tanzania na pia duniani ni "Kanisa la Kiroma-Katoliki" ambalo ni chini ya Uongozi wa Askofu wa Roma au Papa wa Roma. Zamani lilitumia zaidi jina la Roma na madhehebu mengine yamezoea kuliita hivyo lakini siku hizo jina la Roma halikazwi sana. 14


7.1. WAREFORMED (Wapresbiteri)

Kule Uswisi alikuwapo padre kwa jina Ulriko Zwingli (*1484 - +1531) aliyeiga mfano wa Luther. Aliwahi kuwa na mawazo yaliyofanana na Luther bila kumjua. Baada ya kupatikana kwa maandiko ya Luther akaongoza mwendo wa Waswisi kutengeneza kanisa. Akakubaliwa na viongozi wa serikali za miji na mikoa ya Uswisi iliyojitegemea. Kanisa la Katoliki likamtenga. Kwa jumla alishauri kama Luther kwamba Biblia iwe msingi wa imani, bila kuangalia desturi za kanisa zilizojitokeza katika historia. Wafuasi wake huitwa "Wareformed". (reform = kutengeneza upya). Mwalimu mwingine wa dhehebu hili alikuwa Yohane Kalvin (*1509 - +1564). Alikuwa mfaransa aliyeandika kitabu cha mafundisho yao. Aliweka mkazo kueleza jinsi gani mapenzi ya Mungu yanaamua juu ya maisha ya mwanadamu kabla ya mwanadamu kuamua mwenyewe.

Tofauti yao na Luther ilikuwa hasa kwamba walijaribu kujenga kanisa jipya moja kwa moja kwenye msingi wa Biblia jinsi walivyoielewa. Maana yake walikataa desturi zote wasizoziona katika Biblia - lakini Luther alikubali desturi zote alizoziona hazipingi Biblia. Katika ibada za wareformed wanakataa altari, picha za kupamba kanisa au kuimba Liturgia. Ibada ya kilutheri ni Misa ya Kikatoliki iliyosafishwa kufuatana na mawazo ya Luther. Wareformed hawakupenda kuchukua urithi wowote wa kanisa la kiroma-katoliki wakajaribu kuunda kila kitu upya kufuatana jinsi walivyoelewa Biblia.

Katika Utawala wa kanisa walikataa cheo cha uaskofu wakaona kanisa liongozwe na wazee waliochaguliwa. Kutokana na neno wazee katika lugha ya Biblia kigiriki "presbiteri" kanisa hili linaitwa pia la "kipresbiteri".


Tofauti nyingine ni katika mafundisho juu ya sakramenti. Zwingli alifundisha ubatizo na chakula cha Bwana kuwa matendo ya Wakristo tu yanayoiga mfano wa Yesu. Lakini Luther alitetea Chakula cha Bwana kuwa tendo la Kristo mwenyewe. Aliona Mkate ndio mwili wa Kristo wakati wa ibada hii kwani Kristo alisema "Huu ndio mwili wangu". Lakini Zwingli alisema ya kwamba mkate katika ibada ni ishara inayomaanisha mwili wa Kristo. Katika jambo hili hawakupatana na kwa sababu ya tofauti juu ya chakula cha Bwana Walutheri na Wareformed walishindwa kwa muda mrefu kuwa na ibada za pamoja. Lakini siku hizi wanaelewana vizuri.

Mafundisho kutoka Uswisi yalienea baadaye katika nchi kama Ufaransa, Uskoti na Uholanzi. Hata Wamoravia walichukua sehemu ya mafundisho ya Wareformed hasa juu ya chakula cha Bwana wakifuata katika mambo mengine mafundisho ya Luther. Petu Afrika ni wamisionari hawa kutoka Uswisi na Uskoti walioanzisha makanisa ya kipresbiteri kule Malawi, Kenya na Afrika ya Magharibi. Vilevile urithi wa kidini wa Makaburu wa Afrika ya Kusini ni ya Kireformed kwa sababu babu zao walitoka Uholanzi na Ufaransa.

===
7.2. WALUTHERI === Serikali za maeneo mengi ya Ujerumani ziliamua kutengeneza kanisa kwenye msingi wa mafundisho ya Martin Luther. Makanisa hayo huitwa ya kilutheri. Kwa jumla husisitiza sana mafundisho ya Katekesimo zilizotungwa na Luther. Ungamo la Augsburg ni mafundisho mengine yaliyotungwa mw. 1531 wafuasi wa Luther walipodaiwa kujieleza mbele ya Bunge. Katika Ujerumani makanisa ya kilutheri yaliendeshwa kama idara za kiserikali za sehemu za kilutheri chini ya uongozi wa wataalamu wa theologia. Lakini katika karne hii ya 20 kanisa na serikali zilitengwa.

Kule Skandinavia (Sweden, Norway na Denmark) wafalme waliamua kugeuza kanisa zima la kikatoliki kuwa kanisa la kiinjili-kilutheri. Katika Sweden Walutheri waliendelea na vyeo vya maaskofu na desturi nyingi za kanisa la kale. Ulutheri kule ulifanana zaidi na Uanglikana ya Uingereza (taz. chini). Baadaye dhehebu hili lilienea pale ambapo Wajerumani na Waskandinavia walihamia, kama Marekani. Petu Afrika Walutheri wako hasa katika nchi zilizokuwa makoloni ya Ujerumani, kama Tanzania, Namibia na Kamerun. Ni wamisionari kutoka Ujerumani walioweka msingi wa kanisa pamoja na kuleta dhehebu lao.


7.3. WAANGLIKANA

Mfalme Henriko alitawala Uingereza mw. 1509-1547 ni wakati wa Luther. Alikuwa mkristo mkatoliki aliyependa kanisa lake. Lakini alikuwa na matatizo mawili juu ya Papa kule Roma. Kwanza kabisa Uingereza ilikuwa na wajibu wa kumlipa Papa kila mwaka kodi ya pekee, tofauti na mataifa mengine ya Ulaya. Kwa upande mwingine huyu mfalme alikuwa na tatizo la kibinafsi. Alishindwa kuzaa na mke wake mtoto wa kiume atakayekuwa mrithi wake. Kumbe akamwomba Papa apate talaka amwoe mwingine. Lakini Papa alikataa. Henriko aliyekuwa mtu wa hasira aliita Bunge la Uingereza akawalazimisha wabunge kutangaza kwamba mfalme ndiye mkuu wa kanisa katika Uingereza. Halafu bunge lilikubali talaka yake. Azimio lingine lilikuwa kutolipa tena kodi hizo kule Roma zikaingia katika mfuko wa Mfalme mwenyewe. Lakini Mfalme Henriko hakupenda mabadiliko katika mafundisho au desturi. Baada ya kifo chake viongozi wa taifa waliona hawana budi kutengeneza kanisa kwa jumla. Askofu Mkuu Cranmer akachukua mafundisho mengi ya Luther na Kalvin lakini katika desturi za nje hakubadilisha taratibu isipokuwa chache. Hasa nyumba za wamonaki zilifungwa na mali zao zikachukuliwa na mfalme. Hivyo ndivyo Kanisa la Uingereza likajitokeza kuwa kanisa linaloendeleza ibada na desturi nyingi sana za kanisa la Katoliki lakini katika mafundisho yake linalingana na makanisa ya Kiinjili (kiprotestanti). Kwetu Afrika Waanglikana wako katika nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa kiingereza zamani kwani wamisionari wao waliweza kufanya kazi kwa urahisi.

Kwa jumla kanisa hili lipo katika hali mbili. Wale wanaokaza sana urithi wa kale pamoja na Liturgia ya kale (mavazi ya wachungaji/mapadre, kupiga magoti, kupiga alama ya msalaba kwa mkono wakati wa kusali, kutunza kumbukumbu ya watakatifu) wanaitwa "High Church (Kanisa la juu)". Waanglikana wengine waliovutwa zaidi na mambo ya uamsho na kutojali sana urithi wa kale wanaweza kuitwa "Low Church (kanisa la chini)". Kwa nje wale wa "juu" wanafanana na wakatoliki, na wale wa "chini" zaidi na Wareformed. Lakini Waanglikana hujisikia kuwa na umoja; kwa kweli walifaulu vizuri kuliko madhehebu mengine kuunganisha pande zote mbili ndani ya kanisa moja na kuepukana na hatari ya kufarakana kama ilivyotokea mahali penginepo. Waanglikana hujitegemea katika "majimbo" yao (Jimbo la Tanzania, Jimbo la Kenya, Jimbo la Uganda, kila jimbo lenye madayosisi mbalimbali) na kumkubali Askofu wa Canterbury (Uingereza) kuwa kiongozi wa kiroho akiwa kama mwenyekiti wa maaskofu wa Kianglikan lakini hana utawala.

Petu Afrika tunasikia hasa jina la Askofu Desmond Tutu kule Afrika ya Kusini ni Mwanglikana aliyetetea haki za Waafrika weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi. Siku hizi Waanglikana walikuwa kanisa la kwanza la kumbariki Askofu wa kike (Marekani - ni Mwamerika mweusi). Katika swali la kuwapokea wanawake katika ukasisi majimbo yao yanatofautiana.

===
7.4. WABATISTI === Wakatoliki, Walutheri, Wareformed na Waanglikana walikuwa madhehebu yaliyoendelea chini ya ulinzi wa serikali za maeneo yao. Wakati wa Luther lilianza dhehebu lingine ambalo lilikataliwa wakati ule na makanisa yote mengine: Wabatisti.

Wakati ule wa mabadiliko walijitokeza Wakristo waliopenda kuwa karibu zaidi na mfano wa Ukristo wa kwanza. Walitaka kujenga kanisa kuwa jumuiya ya watakatifu au Wakristo wa kweli tu. Katika kanisa kubwa waliona Wakristo wengi walionekana kuwa Wakristo kwa jina tu. Walivyoanza kujisomea Biblia walishindwa kuelewa desturi ya ubatizo wa watoto. Jinsi walivyoelewa Biblia watoto wadogo hawakubatizwa mwanzoni lakini watu wazima tu walioamini walibatizwa. Kwa jumla wakaona desturi ya kuwabatiza watoto wasiofahamu imani ni msingi wa kuwa na wanafiki na wakristo wa uongo ndani ya kanisa.

Mwaka 1525 ulitokea ubatizo wa mtu mzima kule Uswisi. Aliwahi kubatizwa kama mtoto lakini alianza kuelewa imani na kuongoka katika umri mkubwa tu. Akajisikia apokee "ubatizo wa imani". Habari hii na mafundisho yaliyolingana nayo vilienea haraka sana kule Uswisi na Ujerumani. Katika miji mbalimbali Wakristo walivutwa na aina mpya ya Ukristo, wakikutana katika vikundi vidogo nje ya makanisa, kusali pamoja na kuwa na chakula cha Bwana nyumbani mwao. Walioamini kwa njia hii walitafuta "ubatizo wa imani".

Viongozi wakatoliki na pia waprotestant wengine wakapinga mafundisho yao. Wakaona ni kudharau sakramenti ya ubatizo maana wale wote wameshawahi kubatizwa kama watoto wadogo. Tena walikuwa na mashaka juu ya mafundisho yao kanisa kuwa jumuiya ya "Wakristo wa kweli tu". Nani aamue juu ya ukweli kama si Mungu mwenyewe ? Jinsi wabatisti walivyojaribu kulinda utakatifu wao kwa kuweka masharti mbalimbali juu ya maadili na kuyatunza katika shirika zao wengine waliona kumbe wanaunda taratibu za kibinadamu. Luther aliyetoka katika jitihada za umonaki alipojaribu kujenga utakatifu wake kwa njia ya kutimiza mashariti mengi aliona kosa lilelile kwa "watakatifu" wale. Tatizo lingine lilikuwa uhusiano wao na serikali na dola. Wakaona katika Biblia mkristo asiape wala kutumia silaha, wala kushiriki katika mambo ya serikali. Kumbe wakaonekana ni maadui wa kila serikali. Jumuiya zao zilipokua baadaye mashariti mengine yaliachwa pembeni au kusahauliwa, kama vile kutoapa au kukataa matumizi ya silaha. Hali hiyo tumeshawahi kuona kati ya vikundi vingine. Jambo la kusikitisha sana ni kwamba madhehebu makubwa yalikuwa tayari kuwagandamiza Wabatisti kwa njia za kinyama. Waliobatiza watu wazima na kuhubiri imani hii wakatafutwa na kukamatwa, kufungwa gerezani na hata kuuawa. Katika matendo yale zilishirikiana serikali zote za Ulaya, kama za kiroma-katoliki, za kiluteri na pia za kireformed. Baada ya wengi kuuawa wabatisti wengine walianza kujificha au kuhama mahali walipopata ustahimilivu. Kikundi kimoja cha wabatisti waliweza kuishi kule Uholanzi na Ujerumani ya Kaskazini. Kiongozi wao alikuwa Menno Simoni. Wafuasi wake wakaitwa "Wamenno". Baadaye wakahamia mpaka Urusi kutafuta mahali penye uhuru wa kidini wasipolazimishwa kuwa wanajeshi au kuapa mahakamani. Kwetu Tanzania Wamenno wamefika hasa kule kaskazini. - "Kanisa la Uinjilisti" katika eneo la Mbeya limeundwa na wamisionari wa mapokeo ya karibu na Wamenno.

Ubatisti ulienea hasa kule Marekani walipokimbilia wafuasi wake kutoka sehemu mbalimbali za Ulaya. Katika karne zilizofuata wamisionari wa kibatisti walirudi tena Ulaya na sehemu zingine za dunia.

Wabatisti wanaangalia zaidi uhuru wa ushirika palepale wanaposali kuliko umoja wa kanisa hivyo wako duniani katika vikundi mbalimbali. Katika historia sehemu kubwa ya Wabatisti waliacha tena masharti ya kutotumia silaha au kukataa kiapo mahakamani.

Kwetu Tanzania kitovu cha Kanisa la Kibatisti lililoundwa na wamisionari waamerika liko katika Nyanda za Juu za Kusini. Kanisa la "African Inland Church - AIC" linafuata pia mapokeo ya kibatisti katika mengi lakini linatumia cheo cha Askofu.

Maswali na Maarifa (7.1. - 7.4.)

1. Taja tofauti mbili kati ya Wabatisti na madhehebu mengine.

2. Eleza tofauti kati ya Waluteri na Wapresbiteri (Wareformed)

  • a) juu ya ibada na mapokeo ya kanisa
  • b) juu ya sakramenti

3. Eleza Wakatoliki, Waanglikana na Wainjili wengine jinsi gani wanavyolingana na jinsi gani wanavyotofautiana.


7.5. UMOJA WA NDUGU (Wamoravia)

Kule Bohemia na Moravia wafuasi wa Hus walifurahia habari za Luther na wenzake. Hawakuwa tena wakristo wa pekee katika Ulaya walio nje ya Kanisa katoliki. Umoja wa Ndugu uliwahi kuanzisha mbinu mbalimbali zilizoigwa sasa na makanisa mapya ya kiinjili. Waliwahi kuendesha ibada zao katika lugha ya wananchi badala ya kilatini. Waliongozwa na wazee waliochaguliwa. Walipiga chapa vitabu vya nyimbo hivyo ushirika ulikuwa na kazi ya kutangaza neno la Mungu kwa njia ya uimbaji - tofauti na uzoefu wa kale ambako Wakristo ni wasikilizaji tu katika ibada inayoendeshwa na watumishi wa kanisa. Luther mwenyewe alisema "Sisi tunaanza petu Ujerumani mambo yaleyale yaliyowahi kufanywa na ndugu wa Bohemia na Moravia." Lakini katika mambo mengi ya mafundisho bado walifuata desturi za kale. Walizoea kuhesabu sakramenti saba kama kanisa la kikatoliki. Waliona Ukristo wa kweli upo katika matendo na utakatifu wa maisha.

Hapo ndipo walipokea mengi kutoka kwa mafundisho ya Luther na Kalvin. Lakini waliendelea kuwa kanisa lisilo chini ya usimamizi wa serikali yoyote. Wakaendelea kukua katika nchi za Bohemia na Moravia lakini kwa matatizo kutoka kwa serikali. Mnamo mwaka 1600 karibu theluthi moja ya wakazi wote wa nchi zao walijiunga na kanisa hilo kwa hiari. Tutaona chini jinsi gani kanisa hili lilivyoharibika shauri la vita na ugandamizaji. Liliendelea tu kwa njia ya wakimbizi ugenini. Ni kutokana na wakimbizi hawa ya kwamba misioni ilianzishwa iliyounda Kanisa la Moravian katika nchi za Afrika.


7.6. MTAGUSO WA TRENTO NA MATENGENEZO YA KIKATOLIKI

7.6.1. Matatizo ya Kisiasa

Viongozi wa kanisa la kikatoliki waliona kwa masikitiko kutokea kwa mfarakano. Mwanzoni walimwona Luther kuwa padre mdogo tu apaswaye kurudishwa kwenye njia iliyo halali. Papa Leo X. hakuona umuhimu mkubwa katika habari zake. Akamtenga Luther katika kanisa 1520 halafu akapokea habari za Bunge la Ujerumani lililomhukumu Luther kuwa mzushi na adui wa taifa. Baadaye alikufa. Mwaka 1522/23 akafuata Papa Adriano VI. Akiona uenezaji wa haraka wa mafundisho ya Luther kila mahali akakiri mwenyewe kuwa kanisa lilikuwa na makosa. Lakini uongozi wake ulidumu kifupi mno. Baada ya kifo chake akafuata Papa Klementi asiyekuwa na mawazo ya kiroho. Akashughulikia zaidi siasa akishindana kivita na Mfalme wa Ujerumani juu ya utawala katika mikoa mbalimbali ya Italia. Jeshi la Mfalme liliteka Roma mw. 1527. Papa akakimbia. Walipatana mw. 1529 lakini mwaka uleule Waturuki waislamu walifika mbele ya mji mkuu wa mfalme, Vienna. Kwa matatizo jeshi la Wakristo lilishinda. Kwa jumla viongozi wa kikatoliki yaani Papa na Mfalme walitumia nguvu zao kushindana kati yao.

Mfalme Karolo wa Ujerumani alikuwa pia Mfalme wa Hispania. Mwaka 1521 ukaona ushindi wa jeshi la Wahispania katika Mexiko, baadaye kule Peru katika Marekani ya Kusini. Dhahabu na fedha za mataifa ya Marekani zilianza kufika Hispania. Kumbe mawazo ya viongozi kwa upande wa kikatoliki yalikamatwa na shughuli nyingi za kisiasa na kivita. Mfalme Karolo V. hakuwa na muda wala nguvu kushindana na sehemu kubwa ya makabaila wa Ujerumani. Kivulini mwa matokeo haya mafundisho ya Wainjili yalienea haraka katika pande zote za Ulaya.


7.6.2. Ugandamizaji wa upinzani

Kuanzia mwaka 1530 ilikuwa wazi ya kwamba farakano limetokea. Sasa sauti ya wale waliodai mabadiliko ndani ya Kanisa katoliki ilisikika. Papa Paulo III. akachukua hatua mbili. Kwanza aliandaa mtaguso wa maaskofu wote halafu aliimarisha Baraza la Ulinzi wa Imani. Ofisi hii ilikuwa na kazi ya kufuatilia habari zote za upinzani dhidi ya kanisa katoliki na kuomba serikali zilizokuwa mkononi mwa Wakatoliki kugandamiza wote waliotaka kufuata mafundisho ya Luther na wenzake. Baraza lilikuwa chombo chenye nguvu sana. Kwa jumla lilifaulu kufuta vikundi vyote vya Wainjili katika nchi kama Italia, Ureno na Hispania. Lakini ugandamizaji huu uliongeza uchungu kati ya madhehebu ukasababisha ugandamizaji wa wakatoliki katika maeneo ya waluteri na ya wareformed. Chombo kingine kilikuwa "Orodha ya vitabu vilivyopigwa marufuku" vilivyokataliwa kwa kila Mkatoliki asivisome havikurusiwa katika nchi za kikatoliki. (Orodha ilifutwa na Papa rasmi katika karne hii ya ishirini)

7.6.3. Mtaguso wa Trento

Mwaka 1545 maaskofu wa Kanisa la kiroma-katoliki walikutana kule Trento/Italia. Wakajadiliana mafundisho na hali ya kanisa. Wakachukua hatua za kuondoa matatizo na kuimarisha mafundisho ya imani ya kikatoliki.

Maazimio makuu yalibaki muhimu mpaka karne hii ya 20.

  • a) Msingi wa imani ni Biblia pamoja na mapokeo ya kanisa.
  • b) Kanisa linakubali sakramenti saba
  • c) Juu ya kuhesabiwa haki (jinsi ya kupata wokovu) ni mafundisho ya kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa sababu ya matendo mema bali kwa neema ya Mungu lakini mwanadamu anashiriki katika kupokea na kutumia neema hiyo.
  • d) Kanisa peke yake lina mamlaka ya kueleza maana ya Biblia; Mkristo asijisomee bila mwongozo wa kanisa; toleo la pekee la Biblia linalofaa ni lile linalotolewa na Kanisa katoliki katika lugha ya kilatini (liliitwa "Vulgata"- pamoja na vitabu vya "Apokrifa" vilivyotengwa na Luther)
  • e) kufuta maovu katika kanisa: kempeni za kuuza vyeti vya rehema, malipo ya maaskofu kwa Papa ili wapate kuthibitishwa cheo, askofu kuwa na dayosisi zaidi ya moja (walivyofanya zamani kwa sababu ya mapato)
  • f) mapadre wawe na elimu, wote wapite kwenye masomo ya seminari, kila mmoja afuate utaratibu wa somo la Biblia la kila siku, mahubiri yawepo katika kila misa ya Jumapili
  • g) mtaguso uliagiza kutunga Katekesimo ya kwanza ya kanisa la Katoliki, pamoja na kitabu kipya cha liturgia

Kwa jumla Mtaguso wa Trento umeweka msingi wa matengenezo ya Kanisa la Kiroma-Katoliki. Katika nchi zilizobaki chini ya Roma kanisa lilipata nguvu tena. Lakini haikuwezekana kufuta farakano lililotokea tayari. Jitihada za kuwavuta Wainjili kurudi hazikuwa na nguvu sana. Badala yake Kanisa la Kiroma-Katoliki liliimarisha mafundisho ya kale pamoja na kuondoa kasoro mbalimbali.

7.7. WAYESU NA MISIONI YA KIKATOLIKI

7.7.1. Shirika la Yesu

Chombo muhimu sana cha matengenezo cha kanisa katoliki kilikuwa Shirika la Yesu. Kiliundwa na Mhispania kwa jina Ignatio Loyola. Ignatio alikuwa mwanajeshi. Mw. 1521 alijeruhiwa vibaya vitani. Alipokaa hospitalini muda mrefu akasikia wito wa Mungu uliobadilisha maisha yake. Akamtolea Bikira Maria upanga wake akaanza maisha kama "Mwanajeshi wa Kiroho". Akasoma theologia akapadrishwa. Akakusanya kikundi cha marafiki akiwaongoza kujenga maisha ya kiroho kwa njia ya mazoezi ya pekee. Kila mwaka walikutana kwa kipindi cha sala, kutafakari na kusoma kilichofuata hatua au mbinu maalumu. Akatumia nidhamu ya kijeshi katika maisha ya kiroho. Wengi walianza kumfuata na chama chake kikakubaliwa na Papa mwaka 1540. "Shirika la Yesu" lilikuwa jumuiya ya mapadre iliyoongozwa na "Jenerali" wake. Wote walifuata utaratibu uleule wa maisha ya kiroho. Shabaha kuu ilikuwa kutetea kanisa la kikatoliki. Kila mwanachama alitakiwa kuwa na elimu ya juu. Kumbe Kanisa la Katoliki liliimarika katika eneo la elimu la theologia, jambo lililowahi kukazwa zaidi na Wainjili. Mapadre wayesu walifanya hasa kazi ya ualimu wakiunda shule na kuwafundisha vijana elimu pamoja na upendo kwa kanisa katoliki. Mkazo mwingine ulikuwa kufufua utaratibu wa ungamo. Mapadre wayesu walikuwa popote Ulaya washauri hasa wa watawala wakatoliki. Waliposikiliza ungamo la dhambi walipata nafasi nzuri kuwapa mawazo. Kwa njia hizo walitumia athari yao kusababisha hatua za serikali za wakatoliki dhidi ya wananchi Waprotestant. Hivyo kulitokea kurudi nyuma kwa Uprotestanti katika nchi za Ulaya ambako wakazi wengi walianza kufuata mafundisho ya Luther na Kalvin lakini watawala bado walikuwa Wakatoliki.

Katika nchi hizo polepole shirika za wainjili ziligandamizwa kutokana na athari ya Wayesu katika watawala wakatoliki.

7.7.2. Misioni ya kikatoliki

Wakati wa matengenezo na farakano ulikuwa pia kipindi kilicholeta habari za nchi mpya kwa watu wa Ulaya. Mataifa ya Wahispania na Wareno yalijenga aina mpya za meli zilizoweza kusafiri pote duniani hata kuvuka bahari kubwa. Wafanyabiashara na wanajeshi wao walizunguka pande zote za dunia. Waliambatana na mapadre wao. Mapadre hawa walikutana na wenyeji wa nchi mbalimbali wasio Wakristo. Au hata kama walikuwa Wakristo kama Wahabeshi au Wahindi wa Kusini hawakuwa washiriki wa Kanisa Katoliki . Wakaanza kuwaeleza imani ya kikristo. Wahubiri wa kiroma-katoliki walifika mbele ya Mfalme wa Uchina na kwenye pwani za Afrika; mbele ya Negus Negesti wa Ethiopia na mbele ya watawala wa Marekani ya Kusini.

Tatizo la misioni hii ilikuwa kwamba iliambatana na uenezaji wa kijeshi wa Hispania na Ureno. Hasa kule Marekani wamisonari walijikuta kati ya mahitaji ya walowezi waliotaka kuhudumiwa kiroho na mahitaji ya wazalendo waliogandamizwa vibaya na walowezi walewale. Serikali ya kikoloni ilikuwa vilevile serikali ya mfalme mkatoliki. Haikuwa rahisi kwa wamisionari kutofautisha kati ya pande hizo mbili. Mara nyingi kanisa lilibariki tu utawala wa kikoloni uliomaanisha ugandamizaji wa wenyeji. Lakini mara kwa mara walijitokeza Wakristo wengine waliopinga unyama na kuleta taarifa za kweli kule Ulaya. Mmojawapo alikuwa Askofu Las Casas aliyewashtaki walowezi wahispania kwa sababu waliua wenyeji wengi wakiwalazimisha kufanya kazi zao migodini na mashambani bila kujali afya zao. Akafaulu kuleta sheria zilizolinda wenyeji wa Marekani na kupunguza ukali ulioruhusiwa dhidi ya watumwa lakini walowezi walijaribu kumwua. -- Mapadre wa Wayesu walijaribu kuwalinda wahindi wekundu wa Paraguay wakiwakusanya katika vijiji vya ujamaa vilivyojitegemea kiuchumi na hata kisiasa. Lakini walishtakiwa na walowezi majirani waliotaka kuwinda watumwa ati wanadhoofisha utawala wa kikoloni. Mwishoni Wayesu walifukuzwa na serikali katika Marekani na vijiji vya wakristo wenyeji waliharibiwa na wawindaji wa watumwa.

Kule Asia mapadre wa Shirika la Yesu walihubiri Injili mpaka Japani na Uchina wakafaulu kupanda mbegu ya Injili. Walijitahidi kupatanisha Injili na utamaduni wa nchi hizo. Lakini uongozi wa Kanisa kule Roma uliwakataa wasitumie mbinu zinazolingana na utamaduni wa Asia lakini ni tofauti na uzoefu wa Ulaya. Wakristo wa Japan walionekana wanafuata dini ya kigeni. Kanisa liligandamizwa katika vita vya ndani lakini wakristo wajapon wachache walishika imani yao kwa siri mpaka kutokea kwa uhuru wa kidini katika karne ya 19.


7.8. UHUSIANO WA MADHEHEBU - VITA NA AMANI

7.8.1. Dini ya serikali

Kwa jumla uhusiano kati ya madhehebu ya kikristo ulikuwa mbaya kwa muda mrefu. Karibu katika kila nchi Wakristo walilazimishwa kufuata dhehebu rasmi. Ikiwa mtawala fulani aliona vema kukubali mawazo ya Luther mapadre wote walipewa chaguo la kufuata Ulutheri au kutoka nchini. Vilevile ikiwa mtawala aliyemfuata baada ya kifo chake alibadilisha mawazo mapadre wakarudi na wachungaji wa kiinjili wakafukuzwa. Wakristo hawakuulizwa sana isipokuwa katika miji iliyojitawala na kuwa na utaratibu wa kidemokrasi. Lakini hata mjini haikuwa kawaida kuruhusu madhehebu mawili mahali pamoja.

Uhusiano mbaya ulikuwepo vilevile kati ya Wafuasi wa Luther na Wareformed. Katekesimo zao zilitumika kama bendera. Walishtakiana kuwa wazushi wasioelewa vizuri kiini cha imani. Kumbe mafundisho ambayo kwetu leo yanaonekana kuwa na tofauti ndogo yaliweza kumfikisha mtu gerezani au hata kifoni.

7.8.2. Vita vya kidini

Kilichofuata ni kipindi cha vita vya kidini kule Ulaya. Kilele ilikuwa Vita vya Miaka 30. Vilianza kule Bohemia na Moravia kwa sababu watawala wadogo waliokuwa karibu na Umoja wa Ndugu walijaribu kumpindua Mfalme wa kikatoliki. 1618 - 1648 nchi za Ulaya ya Kati ziliharibiwa na wanajeshi wa Mfalme, Papa, Wasweden, Wafaransa waliopingana kwa ukali. Theluthi moja ya wakazi wote walikufa. Mwishoni walipatana ya kuwa

  • 1. Madhehebu ya Wakatoliki, Waluteri na Wareformed ndiyo madhehebu halali, lakini vikundi vingine (kama Wabatisti na Umoja wa Ndugu) viliangaliwa kuwa wazushi popote
  • 2. Mtawala wa kila eneo ataamua ni dhehebu lipi litakalokubalika humo kati ya madhehebu matatu ambayo ni halali
  • 3. Katika maeneo kadhaa Wakristo wa dhehebu lingine walipewa ustahimilivu, lakini katika maeneno mengine walipaswa kuhamia katika nchi ya dhehebu lao au kufuata dhehebu la nchi.
  • 4. Ikiwa mtawala mkabaila angebadilisha dhehebu lake baadaye wananchi wangeruhusiwa kuendelea walivyozoea.

Kumbe mapatano haya yaliunda ramani ya kidhehebu kule Ulaya yenye maeneo ya Wakatoliki, Walutheri au Wareformed watupu. Jumuiya ndogo ziliendelea kugandamizwa wakapata ustahimilivu mahali pachache. Hivyo wafuasi wa madhehebu madogo (kama Wabatisti) walilazimishwa kuhamahama katika Ulaya au kuficha mapokeo yao. Wakati ule nafasi mpya ilitokea: Marekani! Mfalme wa Uingereza alikuwa na koloni la Marekani ya Kaskazini lakini alikosa watu. Akatafuta walowezi kwa ajili ya makoloni yake akiwaahidi wote watapata shamba pamoja na uhuru wa kidini. Hivyo watu kutoka nchi nyingi za Ulaya walianza kuhamia Marekani hasa wale waliokosa uhuru. Mpaka leo inaonekana kwamba nchi mbalimbali za Ulaya zinafuata hasa dhehebu moja, na Marekani ina madhehebu makubwa ambayo hayana wafuasi wengi kule Ulaya, k.m. Baptist.

7.8.3. Wamoravian (Umoja wa Ndugu)

Umoja wa Ndugu uliendelea kwa siri katika Bohemia na Moravia zilizotangazwa kuwa nchi za kikatoliki. Baadaye waumini wengi wakakimbilia maeneo jirani ya Waluteri au Wareformed waliobaki wakageukia Ukatoliki. Lakini katika kijiji kidogo cha Herrnhut Umoja wa Ndugu uliona ufufuo. Mkabaila mdogo kwa jina Zinzendorf aliwapokea wakimbizi kutoka Moravia katika eneo lake mw. 1722. Aliwaruhusu kuendeleza mapokeo yao ya kale akajiunga nao. Ndugu wa Herrnhut walikuwa na uamsho kati yao wakaanza kuhubiri furaha katika Bwana pote Ulaya lakini hawakupenda kuwavuta wakristo kutoka kwa madhehebu mengine kujiunga nao. Kwa namna hiyo Kanisa la Ndugu (walianza kuitwa sasa Wamoravia kwani wakimbizi walioanzisha Herrnhut walitoka Moravia) limebaki kwa kusudi kanisa dogo kule Ulaya. Kutokana na kazi kubwa ya misioni ya kanisa hili wakristo wamoravian walio wengi huishi Afrika na Marekani ni wengi zaidi kuliko katika nchi za asili ya Bohemia, Moravia na Ujerumani.

Maswali na Maarifa:

1. Kwa nini zipo nchi katika Ulaya zenye Wakatoliki/ Walutheri/ Wareformed wengi sana kuliko madhehebu yote mengine ?

2. Taja nchi za Ulaya zenye wafuasi wengi sana hasa wa madhehebu yafuatayo: a)Anglikana, b) Katoliki c)Lutheri, d)Reformed

3. Unaonaje mbinu za kutumia silaha katika juhudi ya kutetea imani ya kweli ?


SURA YA NANE : UKRISTO KATIKA AFRIKA 1500 - 1800

1.Ukristo wa Afrika mw. 1500 2. Uenezaji wa Wareno 3. Misioni kule Angola/Kongo 4. Afrika ya Mashariki


8.1. UKRISTO WA KIAFRIKA MNAMO MW. 1500

8.1.1. Afrika ya Kaskazini na Misri Mnamo mwaka 1500 (wakati wa Luther) Ukristo wa Kaskazini-Magharibi ulishapotea. Wakristo wa pekee walikuwa watumwa kutoka Ulaya waliofungwa katika nchi hizo. Waarabu wa kule walishindwa vitani katika Hispania. Wakimbizi Waarabu kutoka Hispania hawakuwa na moyo wa kustahimili Wakristo kati yao.

Katika Misri Ukristo uliendelea. Wakristo wakopti walishakuwa Waarabu kiutamaduni lakini bado waliendelea kuimba kwa lugha ya kikopti (kimisri cha kale) katika ibada zao. Katika miji mikubwa ya Kairo na Aleksandria vilevile katika vijiji vya Misri ya Kusini Wakristo walikuwa wengi kidogo. Hasa kule Aleksandria waliishi pia Wagiriki tangu karne nyingi.

8.1.2. Nubia

Nubia ni jina la kale ya Sudan ya kaskazini. Tangu karne ya sita wafalme wa Nubia walikuwa Wakristo. Mmisionari mkuu alikuwa Juliano wa Aleksandria aliyefika Nubia mw. 546. Baada ya kuingia kwa Uislamu kule Misri Wakristo wa Nubia walijitetea kwa silaha. Lakini polepole makabila ya Waarabu wahamiaji wakaelekea kusini. Baada ya mw. 1200 vita vikatokea tena na tena kati ya Waarabu waislamu na Wanubia wakristo. Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa sababu majaribio ya jeshi la msalaba toka Ulaya kuteka Palestina. Mtawala mwislamu wa Misri kwa jina Salah ed Din akalipa kisasi akishambulia madola ya Wakristo kusini mwa Misri. Mji mkuu wa Nubia ulikuwa Alodia (karibu na Khartoum ya leo). Mwaka 1504 jeshi la Waarabu iliteka Alodia. Kutokana na historia hii ya vita vikali watawala wapya hawakuonyesha ustahimilivu kwa Wakristo wa Nubia ilivyokuwa kule Misri. Ukristo uligandamizwa. Leo tunaweza kuona magofu tu ya makanisa ya kale yaliyohifadhiwa chini ya mchanga wa jangwa la Sudan.

====
8.1.3. Ethiopia ==== Kuenea kwa Uislamu katika Nubia na Pembe ya Afrika kulifanya mawasiliano ya Ethiopia na nchi za nje kuwa magumu. Taifa hili la kikristo lilijikuta kama kisiwa katika bahari ya kiislamu. Mawasiliano na Misri yaliendelea kwa shida. Kanisa la Ethiopia likakubali ulezi wa kiroho wa Askofu mkuu wa Aleksandria. Lakini kama kawaida katika mapokeo ya kiorthodoksi lilikuwa chini ya ulezi wa kisiasa wa Negus (Mfalme wa Ethiopia). Tangu mw. 1400 maNegus wakatambua kwamba msaada wa mataifa mengine ya Wakristo haupatikani mpaka Ulaya. Wakatuma wasafiri waliopeleka barua kwa watawala mbalimbali wa Ulaya, hasa mfalme wa Hispania na Papa wa Roma (mw. 1424 na 1441). Negus (Mfalme) Zara Yakubu akatuma ujumbe Italia kwa Papa akajaribu kujenga umoja wa kikanisa ila tu hayakutekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano. Safari kati ya Ulaya na Ethiopia kupitia maeneo ya nchi za Waislamu ilikuwa jambo la kubahatisha.

Mwaka 1493 mjumbe wa mfalme wa Ureno alifika katika mji mkuu wa Lalibela (karibu na ziwa Tana). Ziara hii ilianzisha kipindi cha mawasiliano kati ya Wareno na Ethiopia. Mwanzoni Wareno walisaidia Ethiopia kujitetea dhidi ya mashambulio ya Waarabu wa pwani. Waarabu walisaidiana na askari waturuki walioleta mara ya kwanza bunduki katika nchi hiyo. Walipoanza kushinda msaada wa wareno ulifika na Wahabeshi walipata pia bunduki. Mwaka 1543 Wahabeshi na wasaidizi wao Wareno wakawashinda Waarabu na Waturuki katika mapingano ya ziwa Tana.

Kipindi kilichofuata kilileta uhusiano mgumu. Wajumbe wareno wakaendelea kufika. Mapadre wa Shirika la Yesu wakaanza kuhubiri na kufundisha vijana. Wafalme wawili wakajiunga na Kanisa la Kiroma-Katoliki. Lakini majaribio ya kuunganisha Ukristo wa Ethiopia na Kanisa la Roma yalisababisha ghasia. Mapadre kutoka Ulaya waliona wasiwasi hawakuelewa desturi nyingi za kanisa la Uhabeshi. Ukristo wake ulionyesha uso uliolingana na utamaduni wa kiafrika. Katika misa ngoma hupigwa makasisi huchezacheza kiliturgia. Wavulana wakatahiriwa kama desturi ya kanisa. Kumbe Wayesu waliyaona mambo haya kama ni ya kipagani. Wakamshawishi Negus Sussenyos aliyekubali Ukatoliki "kutakasa" kanisa yaani kukataza desturi mbalimbali na kusoma misa kwa kufuata Liturgia ya Kiroma. Ghasia za wananchi zilifuata. Mw.1632 Negus Susneyos akajiuzuru. Wayesu wakafukuzwa. Wahabeshi waliokuwa Wakatoliki wakalazimishwa kurudi katika Ukopti. Kumbe kuingia kwa wageni kulisaidia kutetea taifa lakini kulileta vurugu ya ndani. Nafasi ya kuelewana tena haikupatikana kwa sababu Wareno walifukuzwa miaka ileile kwenye pwani za Uswahilini na Uarabuni. Ethiopia imekuwa tena kama kisiwa cha kikristo katika bahari ya Uislamu.

Maswali na Maarifa (8.1.):

1. Linganisha hali ya Ukristo wa Afrika katika mw. 600 na mw.1500 B.K. (ling. 3.7.) 2. Taja vitovu vya Ukristo wa Afrika vilivyobaki mw. 1500 3. Taja athari mbili toka nje ya Afrika zilizokuwa hatari na msaada kwa ajili ya Ukristo wa Ethiopia.


8.2. UENEZAJI WA WARENO

Ureno ni nchi ndogo jirani na Hispania. Kwa karne nyingi Wareno wakatoliki walishindana na Waarabu waliotawala kusini mwa Ureno na Hispania. Mw. 1492 Waarabu wa mwisho wakatoka katika Hispania. Mabaharia wareno wakaanza kufuata pwani za Afrika kuelekea kusini. Elimu mpya iliwasaidia. Mnamo 1450 vitabu vya kwanza vilianza kupatikana vilivyoeleza uhusiano kati ya nyota, majira ya mwaka na jiografia. Pamoja na chombo kipya cha "compass" vikawawezesha mabaharia kupiga hesabu juu ya safari zao baharini wakipima nyota hata bila kuona pwani. Mw. 1497 nahodha Vasco da Gama akazunguka Afrika ya Kusini akatembelea bandari za Uswahilini na kufika Bara Hindi. Katika bandari za Kilwa, Zanzibar na Mombasa Wareno wakashangaa kukutana tena na Waarabu waislamu waliozoea kuwa maadui tangu karne nyingi kule nyumbani kwao.

Shabaha ya safari za Wareno ilikuwa biashara na Bara Hindi. Kwa kutumia elimu mpya ya kijiografia wakaona ya kwamba inawezekana kuchukua bidhaa za mashariki kwa njia ya bahari badala ya kutegemea biashara mkononi mwa Waarabu kupitia Mashariki ya Kati. Katika njia hiyo walihitaji vituo kwa ajili ya meli zao katika pwani za Afrika. Walitumia vilevile nafasi ya kufanya biashara na Waafrika wa pwani.

Pamoja na hayo biashara nyingine ilianza kuongezeka: biashara ya watumwa. Wareno na Wahispania waliunda utawala wao kule Marekani ya Kusini katika karne ya 16. Walitafuta madini ya nchi hizo wakaanzisha mashamba makubwa. Lakini wakaona ugumu wa kutumia Wahindi wekundu kama wafanyakazi. Watu wa Marekani waliishi bila mawasiliano na watu wengine tangu miaka maelfu. Magonjwa yaliyokuwa kawaida katika Ulaya, Afrika na Asia (kwa sababu watu kule waliwahi kuambukizana tangu karne nyingi) yaliua wenyeji wengi wakiishi pamoja na Wazungu. Tena walowezi wazungu walikuwa wakali mno. Wahindi wekundu waliofanywa watumwa wakafa kwa mamilioni. Hapo ndipo wazo jipya lilijitokeza: kuchukua watumwa kutoka Afrika ili wafanye kazi Marekani! Waliopendekeza wazo hili walisema ya kuwa Waafrika wana nguvu na afya kuliko wenyeji wa Marekani. Kumbe hivyo ndivyo ilivyotokea. Msingi wa maendeleo ya Ulaya umewekwa kwa malighafi za Marekani zilizochimbwa na kulimwa na watumwa waafrika. Kwa karne tatu biashara ya watumwa ilikua na kuongezeka kwenye pwani za Afrika. Wareno walikuwa katika mstari wa mbele wa biashara hii ya aibu. Wakawauza watumwa popote. Baada ya kukomeshwa kwa biashara ya watumwa kimataifa waliendelea kuwapeleka katika koloni lao la Brasilia mpaka mw. 1850.


8.3. MISIONI YA KWANZA KATIKA KONGO NA AFRIKA YA MAGHARIBI

Wareno walipozunguka pwani za Afrika walikutana na jamii za wenyeji. Katika Afrika ya Mashariki na eneo la Kongo (Zaire/Angola) walijaribu kuunda vituo vya biashara. Wamisionari walichukua nafasi hizo kuhubiri Injili.

8.3.1. Afrika ya Magharibi

Hapa walikutana na watu walioiishi chini ya watawala wenye nguvu. Kwa jumla wamisionari walijaribu kuwasiliana na viongozi hawa kwa matumaini ya kwamba baadaye watu wa kawaida watafuata. Benin ilikuwa kitovu cha maendeleo ya kisiasa,kiuchumi na kisanii tangu mw. 900 B.K. . Mw. 1486 Mreno d`Aveira alimtembelea mara ya kwanza Mfalme wa Benin. Wakati wa Mfalme Esigie wamisionari wakaruhusiwa kuingia na kuanza kazi. Mfalme Orhogbua alikuwa mkristo mn. mw. 1550. Lakini chini ya wafuasi wake maendeleo ya Ukristo yalikwama na kuisha. Mifano ya aina hiyo inapatikana vilevile kutoka kwa Gambia, Sierra Leone au Ghana. Kutofanikiwa kwa majaribio haya kulitokana na

  • a) matatizo ya wamisionari wazungu katika hali ya hewa (iliyokuwa ngumu na hatari kwao - kabla ya kupatikana kwa dawa la "Kwinin" dhidi ya Malaria wazungu wengi katika nchi za joto walikufa shauri ya homa).
  • b) Wamisionari wakatoliki wa karne zile walifanya mara nyingi kosa la kutofundisha kiasi cha kutosha kabla ya kubatiza. Hivyo sehemu ya Wakristo wenyeji hawakuelewa imani mpya.
  • c) Kisiasa pwani ya Afrika ya Magharibi ilikuwa katika hali ya fujo. Kutokana na biashara ya dhahabu na watumwa mataifa ya Ulaya yalishindana kivita kati yao. Wareno, Wahispania, Wafaranasa, Waingereza, Waholanzi, Wasweden, Wadenmark na pia Wajerumani walipigana kati yao wakishirikiana pamoja au dhidi ya watawala wazalendo juu ya utawala wa biashara hiyo.
  • d) Wakristo wachanga wa Afrika ya Magharibi waliona kila siku mifano ya wakristo wabaya. Wanajeshi na wafanyabiashara wazungu mara nyingi hawakufurahia kupelekwa katika nchi zenye hatari za kiafya na tofauti kubwa na mazingira ya nyumbani kumbe wakaanguka katika ulevi na usherati, hali iliyokuwa vibaya zaidi kutokana na uharibifu wa kiroho uliosababishwa na biashara ya watumwa hata mioyoni mwa wakala wake.

8.3.2. Kongo

Kongo ilikuwa eneo kusini mwa mdomo wa mto Zaire. Tangu karne ya 14. Mfalme kwa cheo cha Manikongo alitawala nchi. Wakati wa Mfalme Nzinga Nkuwu Wareno wa kwanza walifika na kujenga ubalozi. Baada ya kusikia mahubiri ya wamisonari Mfalme akabatizwa akipokea jina la Yohane; Mji mkuu ukapewa jina la "San Salvador" (=Mtakatifu Mkombozi). Wakati wa Mfalme Affonso I. (1508-1545) kanisa lilikua sana. Mtoto wa Mfalme akasoma theologia kule Lisbon. Akasafiri Roma alipobarikiwa na Papa Leo X (aliyeshughulika baadaye mawazo ya Padre mjerumani kwa jina Luther) akarudi kama askofu wa kwanza mwafrika kusini mwa Sahara. Lakini pamoja na wamisionari wareno waliingia pia wafanyabiashara wa watumwa. Wakati uleule wamisionari walipofundisha injili na heshima ya binadamu kuwa kiumbe wa Mungu wale wafanyabiashara wa watumwa walivunja amani nchini. Walichukua watumwa kutoka jirani mwa Kongo lakini pia ndani ya Ufalme. Kumbe uhusiano kati ya serikali ya mfalme mkristo wa Kongo na wageni Wakristo wareno ulikuwa mbaya mpaka kupingana kwa silaha. Kwa jumla ndiyo biashara ya utumwa iliyoangusha ufalme huu wa kikristo. Mtaalamu wa historia ya kiafrika asema: "Biashara ya watumwa ilifanya vita kuwa hali ya kudumu kati ya makabila. Vita vilikuwa vikali zaidi. Watawala wa madola ya pwani wakauza watumwa. Watumwa waliouzwa wakawawezesha kununua bunduku nyingi. Bunduki nyingi ziliwawezesha kukamata watumwa wengi zaidi. Watawala wa pwani waliingia katika mzunguko wa kishetani wakipingana kivita kwa shabaha ya kupata wafungwa watakaouzwa kuwa watumwa. Watawala wakaanza kuwaangalia raia wao kuwa bidhaa tu zinazosaidia kujipatia yote wanayotamani" (Ki-Zerbo,231). Kumbe watu wakorofi hawakuwa tayari kuwatazama wenyeji wa Kongo tofauti kuliko waafrika wengine waliofaa machoni pao kuwa watumwa. Wafanyabiashara wale waliona mahubiri ya injili kuwa kizuizi cha biashara yao tu. Nia nzuri za Mfalme wa Ureno na vilevile wamisionari wenyewe hazikuwa na nguvu mbele ya uovo wa watu hawa na pesa zao. Mfalme Affonso alijitahidi sana kuwafukuza wafanyabiashara wareno. Lakini kufuatana na mkataba wake na Ureno alipaswa kuwarudisha ili waadhibiwe kule. Lakini walipokabidhiwa kwa maafisa wa kireno kwenye vituo vya pwani ya Afrika walitumia hela zao kuwalipa mahakimu wawekwe huru tena. Mara nyingi walitumia mapato ya biashara yao kuwahonga maafisa wa mfalme wa Kongo walioanza kumpinga.

Ufalme wa Kongo ulidhoofishwa ukaingia katika kipindi kirefu cha vita vya ndani, dhidi majirani wake na hata dhidi Wareno. Mwishoni uchumi na utaratibu pamoja na Ukristo viliharibika. Ureno ilishindwa kujenga taifa la marafiki wakristo kwa mkono mmoja na kwa mkono mwingine kuwaruhusu wafanyabiashara wake kuwafanya marafiki hawa kuwa watumwa wakati uleule.


8.4. MAJARIBIO YA MISIONI KATIKA AFRIKA YA MASHARIKI

Kati ya 1500 na 1800 wamisonari wakatoliki walihubiri kwenye pwani la Afrika ya Mashariki. Walifuata uenezaji wa Wareno waliojaribu kutawala pwani hiyo kama vituo vya biashara kati ya Ulaya na Bara Hindi. Kutoka kwa makao yao ya Sofala na Msumbiji walijaribu pia kutawala biashara ya dhahabu iliyochimbwa katika eneo la Mwene Mtapa (Zimbabwe).

Katika pwani za Uswahilini Wareno wakafika kuanzia mw. 1505 wakitafuta njia ya Bara Hindi. Waislamu wa pwani hawakufurahia sana kupokea Wakristo. Vilevile hawakuvutwa na picha ya kwanza waliyoipata juu ya Wareno kwa ujumla. Viongozi Wareno waliwaangalia Waislamu katika Afrika moja kwa moja kuwa maadui kama Waislamu kwao nyumbani walipowahi kupigana nao kivita tangu karne nyingi. Chini ya ulinzi wa kijeshi wa kireno wamisionari wakaanza kazi. Mapadre wa Shirika la Yesu wakaingia ndani la bara kuwahubiria wafuasi wa dini za asili. Mashirika mengine yalijaribu kujenga vituo kama hospitali na kuwasaidia maskini. Kazi iliendelea polepole kati ya waislamu. Lakini Pemba kisiwani na vilevile Mombasa Wakristo mamia wakabatizwa.

Mwaka 1630 Kijana kwa jina Jerome Chungulia akapokea cheo cha Mfalme wa Mombasa kwa msaada wa Wareno. Alikuwa mtoto wa Sultani mwislamu. Wareno walimwua baba vitani na kumlea mwanaye. Baada ya masomo kule Goa alirudi kama Mkristo. Lakini mw. 1631 alikumbuka jinsi gani Wareno walivyomua babake alilipiza kisasi. Akajitangaza kuwa Mwislamu tena akawaongoza Waislamu wa Mombasa kuwaua Wareno mjini. Waswahili wote waliopokea Ukristo waliauawa pia. Hukumbukwa kama "Mashahidi wa Mombasa".

Mnamo mw. 1560 mmisionari kwa jina Da Silveira akafika Msumbiji akaendelea kuhubiri sehemu za ndani akafika Manica (mji mkuu wa Mwene Mtapa). Baada ya kuhubiri kwa muda wa juma tatu Mwene Mutapa (cheo cha mfalme) alikuwa tayari kupokea ubatizo pamoja na wakubwa 300. Lakini washauri waislamu wa Mwene wakamshtaki Da Silveira kuwa mpelelezi na mchawi. Mwene akageuka akamwua Da Silveira alipolala usingiza. Maiti yake ikatupwa mtoni.

Wamisionari wengine walifaulu tena kufika Zimbabwe mwaka 1570. Walijifunza lugha ya nchi, walihubiri na kujenga makanisa. Katika karne ya 17 wafalme wa Mwene Mtapa walikuwa mara nyingi Wakristo wakatoliki. Watoto wa wakubwa walisomeshwa katika shule za misioni kule Tete (Msumbiji) au Goa (Bara Hindi). Mwana wa Mwene Kapararidze kwa jina Miguel (Michael) alichukua digri ya Daktari wa Theologia kule India mw. 1670. Baadaye alihudumia kanisa la Mt.Barbara katika Goa na kufundisha kama Profesa wa seminari. Mwaka 1983 maraisi wa Zimbabwe na Zambia, R. Mugabe na K. Kaunda walitembelea jengo la kanisa la Mt. Barbara wakimkumbuka mtaalamu wa kwanza wa kisasa Mzimbabwe.

Lakini maendeleo haya yote yaliingiliana na siasa ya kireno. Biashara ya dhahabu ilisababisha maafisa wa kireno kuhujumu utawala wa Mwene Mtapa kwani walipenda zaidi watawala wasio na nguvu waliowapa nafasi za kujitajirisha - na wakapindua watawala waliojaribu kujenga hali ya kujitegemea. Kumbe kati ya mashambulio ya makabila ya ndani (Rozwi, Zimba) na kuingilia kwa Wareno utaratibu wa Ufalme wa Mwene Mtapa ulianguka kabisa. Ukristo ulitegemea mno nguvu ya kifalme ukaanguka pamoja na utawala wake.

Kumbe tunaona jinsi gani mizizi ya kanisa ilikauka tena hapa Afrika mnamo karne za 16-18 kwa sababu ya kuingiliana kwa hotuba ya Injili na siasa ya ukoloni. Udhaifu wa kibinadamu uliongeza matatizo pamoja na ugumu wa mazingira na hali ya hewa kwa ajili ya wamisionari kutoka Ulaya.

Maswali na Maarifa (8.2.- 8.4.) 1. Taja vizuizi vya kazi ya misioni katika Afrika wakati wa karne 16. - 18. 2. Linganisha mbinu, mafanikio na matatizo ya misioni katika Afrika wakati wa kipindi cha kwanza (karne 1-5) na kipindi cha pili (karne 16.-18.) 3. Andika kifupi muhtasari inayoeleza misioni ya karne 16.-18. kwa ukitumia vipengele vifuatavyo: a) watu gani walifanya kazi hiyo, b)walitoka katika nchi zipi hasa c) kwa nini walizunguka pwani za Afrika (badala ya sehemu za ndani?) d)walitumia hasa mbinu zipi za kupata wakristo ? e)katika nchi zipi hasa walipata mafanikio f)ni matatizo gani yaliyowakabili na kuharibu mafanikio yao?




SURA YA TISA: UENEZAJI WA TATU WA UKRISTO KATIKA AFRIKA: KARNE YA 19


9.1. MAPINDUZI YA VIWANDANI

Uenezaji wa tatu wa Ukristo katika Afrika ulianzishwa na Wakristo kutoka nchi za Ulaya zilizoendelea. Mapinduzi ya viwandani yaliongeza sana uwezo wa kiuchumi wa mataifa haya kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Biashara ya kimataifa ilianza kuunganisha nchi za mbali sana. Vyombo vya usafiri kama vile meli na reli, baadaye hata ndege vilifikisha watu na bidhaa kila sehemu za dunia. Watu walianza kupata habari za nchi zisizojulikana kwao mpaka wakati ule.

Wakristo wa nchi za Ulaya walitumia mawasiliano haya. Labda tunaweza kulinganisha hali hiyo na sera zilizotumiwa na mitume wa kwanza. Nao hao walitumia njia zilizofunguliwa na biashara ya Kiroma katika karne za kwanza. Wengine waliona uwezo wao kama wito wa Mungu kwa Wakristo wa Ulaya katika karne ile hasa.

9.2. UAMSHO KATIKA ULAYA

Mahali pengi katika Ulaya wakristo hawakuridhika tena na hali ya kanisa. Ukristo ulishakuwa sehemu ya utamaduni na jambo la kawaida. Bila kutafakari sana mtoto alibatizwa, akafundishwa na kubarikiwa katika Kipa Imara, akafunga ndoa kanisani, akawabatiza watoto wake halafu akazikwa kwa ibada ya kanisa. Kanisa lilikuwa kama idara ya serikali ilisaidia taifa kuweka utaratibu wa kidini kwa manufaa ya maadili ya umma. Serikali zilihimiza watu washiriki na kuhudhuria ibada. Wasipofika kanisani waliweza kutozwa faini. Lakini mazingira na hali ya maisha vilibadilika. Watu walianza kuhamia mjini, jumuiya za vijiji zilianza kulegea na kuvunjika. Mahali pengi watumishi wa makanisa hawakujua kujibu maswali mapya ila tu kukumbusha juu ya uzoefu wa kale na mila nzuri tangu zamani. Hapo ndipo asili ya miendo ya uamsho iliyotokea kwa nguvu sana. Wasioridhika walikutana nje ya makanisa kusali katika nyumba za watu. Katika maeneo ya kiprotestant hali ilitegemea. Penye uongozi wenye busara walipewa nafasi zao shirikani. Watu waliguswa upya na neno la Mungu na Roho wake walitafuta njia mpya za kuishi na kuonyesha imani yao. Hivyo vilijitokeza vyama vya kuwasaidia wagonjwa, wajane na yatima, na maskini. Penye uongozi mkali uliokataa njia na mbinu mpya wakristo walikutana na kusali nje ya makanisa. Wengine walianzisha jumuiya na madhehebu ya pekee. Lakini sehemu kubwa ya wakristo walioangazwa na uamsho walielewa kazi yao ya kutengenezwa upya makanisa yao badala ya kuunda vikanisa vipya.

Katika maeneo ya wakatoliki miendo iliyofanana na uamsho ilisababisha mara nyingi kutokea kwa shirika mpya za watawa au za walei. Muundo wa kanisa la katoliki unasaidia kuwapa watu wenye wito au vipawa vya pekee nafasi zao katika shirika za watawa.

9.3. BIASHARA YA WATUMWA

16 Sababu moja iliyosababisha kuangalia hasa Afrika ni habari za biashara ya watumwa zilizopatikana sasa kwa watu wengi. Katika karne ya 18 na 19 mamilioni Waafrika walichukuliwa kama watumwa na kupelekwa hasa Marekani. Makanisa makubwa yalinyamaza au kufumba macho mbele ya mauovu haya. Wakristo wa madhehebu madogo ya kiprotestant kama "Makweka" au "Marafiki" na Wamethodist (baadaye pia sehemu ya wafuasi wa makanisa makubwa) katika Uingereza ndio walianza kupinga utumwa. Walifaulu kupata hukumu ya mahakama iliyosema ya kwamba si halali kuwa na watumwa katika Uingereza. Lakini bado utumwa uliendelea katika makoloni. Wakristo walimtumia Mbunge Wilberforce pamoja na wahubiri kanisani kukaza kempeni pote nchini. Mwaka 1807 walifaulu kupata sheria bungeni iliyopiga marufuku biashara ya watumwa kwa Waingereza na katika makoloni ya Uingereza (lakini watumwa waliokuwepo walibaki hivihivi). Waliendelea kudai matumizi ya meli za kijeshi za Uingereza dhidi ya biashara ya mataifa mengine kama vile Wafaransa, Wareno na Waarabu. Mwishoni baada ya mapambano marefu walipata sheria ilioweka watumwa wote huru katika makoloni yote ya Uingereza. Lakini bado nchi zingine ziliendelea na utumwa wa ndani. Kule Marekani (USA) swali hili lilisababisha farakano ya majimbo ya Kusini na vita vya ndani (1861-65). Majimbo ya Kaskazini yalishinda na kuwaweka watumwa huru. Kule Brasilia utumwa uliendelea karibu mpaka mwisho wa karne ya 19.

Hapa Afrika ya Mashariki biashara ya watumwa iliendelea hata baada ya Waingereza kumlazimisha Sultani wa Zanzibar mwaka 1874 kufunga soko la watumwa mjini Zanzibar. Mwingereza David Livingstone ndiye aliyetumia nguvu zake kupeleleza habari za biashara ya utumwa na kuzipeleka Uingereza. Alikuwa misionari na daktari alizunguka nchi zote za Afrika Kusini hadi Tanganyika. Akafa mw. 1873, moyo yake imezikwa kule Ujiji (Kigoma). Alifaulu kuwaamsha watu wengi juu ya biashara ya watumwa. Biashara ilikomeshwa tu baada ya kuundwa kwa utawala wa kikoloni. Lakini watu walishikwa kama watumwa mpaka mwanzo wa karne ya ishirini mpaka serikali za kikoloni walifanya taratibu za kuwaweka huru. Katika kampeni hizo wakristo ndio waliosukuma serikali zao na kuonyesha aibu kubwa juu ya ushirikiano wa mataifa ya kikristo ya Ulaya katika biashara ya watumwa wakati wa karne zilizopita.


9.4. SHIRIKA ZA MISIONI

Tumeshaona ya kwamba tangu mw. 1500 wamisionari wakatoliki walienda sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 17 na 18 waprotestant walianza kuiga mifano yao. Kanisa la Anglikana liliunda Kamati ya kupeleka injili katika nchi za ng'ambo lakini ilishughulikia hasa wahamiaji waingereza katika makoloni. Polepole wakristo wachache walianza kuwaendea pia wazalendo katika makoloni, jambo lililokuwa gumu kutokana na hali ya ukoloni mwenyewe. Kanisa la kwanza la Kiprotestant lililotuma wamisionari hasa kwa watu wasiomjua Kristo lilikuwa ni la Ndugu wa Herrnhut (Wamoravian) walituma wamisionari kule Carribbean, Greenland na Afrika ya Kusini kuanzia mwaka 1731.16 Wamoravian walihubiri mahali pengi Ulaya bila kuwashawishi wengine kujiunga nao lakini walisambaza sana habari za misioni kati ya wakristo wa madhehebu yote.

Wakiitikia mfano wa Ndugu wa Herrnhut wakristo kutoka vikundu mbalimbali vya uamsho walianza kuelewa wajibu wao kwa uenezi wa injili pote duniani. Mnamo mwaka 1800 wakristo Waingereza waliunda vyama mbalimbali vya misioni, kama Wabatisti 1792, Chama cha Misioni cha London 1795 na Chama cha Misioni cha Kanisa (la kianglikana = Church Missionary Society/CMS) 1799. Waprotestant wa nchi zingine za Ulaya walifuata. Wamisionari wa kwanza tangu zamani za Wareno waliofika Afrika ya Mashariki walikuwa ni Wajerumani waliotumwa na CMS. Majina yao ni Krapf na Rebmann. Wanakumbukwa pia kwa kutunga kamusi ya kwanza ya lugha ya Kiswahili.

Mara nyingi sio viongozi wa makanisa ya kiprotestant walioendesha kazi ya misioni. Viongozi wengi wa kiprotestant (isipokuwa kwa kiasi Waanglikana) wakati ule walijali maeneo yao tu wakikosa mtazamo wa dunia nzima kama wenzao wakatoliki. Kumbe walikuwa wakristo walei na wachungaji wa kawaida waliounda vyama vya misioni, kuombea kazi hii, kutafuta habari za nchi zingine na kuchanga pesa wakiandaa vijana watakaokuwa tayari kuacha ndugu zao wakielekea katika nchi za mbali zisizojulikana nao.

Katika kanisa la katoliki vyama vipya viliundwa hasa kwa ajili ya kazi ya Afrika. Cha kwanza kilichoingia Afrika ya mashariki walikuwa mapadre wa roho Mtakatifu. Anayekumbukwa sana ndiye askofu Mfaransa Lavigerie (tamka La-vi-je-ri). Mwaka 1868 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Afrika (linaloitwa "White Fathers") na mw. 1869 Shirika la Masista Wamisionari wa Afrika. Baadaye Lavigerie alipewa cheo cha Askofu Mkuu wa Algeria. Alijitahidi sana kukomesha biashara ya watumwa na kueneza Injili. Tofauti na shirika zingine za wakatoliki Mapadre Weupe waliwashambulia wafanyabiashara ya watumwa moja kwa moja na kuwpokea watumwa waliotoroka.

Wamisionari wa madhehebu mbalimbali waliunda vituo katika sehemu za pwani ya Afrika. Vituo hivi vilipokea watumwa waliochukuliwa na jeshi la Uingereza kwenye meli za wafanyabiashara. Walinunua pia watumwa na kuwapa uhuru. Wengine kati yao walipokea ubatizo na kuwa wakristo wa kwanza katika nchi zao. Vituo vya kwanza vya watumwa waliowekwa huru vilikuwa Freetown (= Mji wa watu huru) kule Sierra Leone , halafu Bagamoyo na Masasi petu Tanzania, au Freretown karibu na Mombasa.

9.5. KUELEKEA KWA KANISA LA KUJITEGEMEA KATIKA AFRIKA YA MAGHARIBI

Kwa namna hiyo uinjilisti ulianza kwanza Afrika ya Magharibi. Kazi ya kuhubiri Injili ilianzishwa na watu kutoka Ulaya lakini ikaendeshwa baadaye na wainjilisti au wachungaji waafrika. Samuel Crowther aliwahi kuwa mtumwa utotoni. Alinunuliwa na wamisionari waanglikana, akapewa uhuru, akasomeshwa theologia na kuwa padre wa Kanisa la Kianglikana. Mwaka 1864 alibarikiwa kule Nigeria kuwa Askofu wa kwanza wa Kianglikana katika Afrika. Msingi wa Kanisa la Kiafrika kusini mwa Sahara uliwekwa. Chama cha Misioni cha Kianglikana kiliona madhumuni yake kuwa kusaidia kutokea kwa "kanisa la kiafrika linalojitawala, linalojitegemea kiuchumi na linalojiendeleza".

9.6. MISIONI NA UKOLONI

Hali hiyo iligeuka kuwa tofauti baada ya mabadiliko ya kisiasa. Mwaka 1885 serikali za Ulaya ziligawanya Afrika kati yao. Kipindi kipya cha Ukoloni kilianza. Sehemu zote za Afrika ziliwekwa chini ya utawala wa kikoloni, (isipokuwa Ufalme wa Kikristo wa Ethiopia uliojitetea dhidi ya Waitalia - na Liberia iliyokuwa chini ya Ulinzi wa Marekani). Ukoloni ulileta mabadiliko gani kwa ajili ya kazi ya misioni katika Afrika ?

9.6.1. Faida na hasara kwa misioni

Serikali za kikoloni zilijiingiza katika kazi ya wamisionari. Mara nyingi ziliwategemea wamisionari kutoa huduma za elimu na afya. Mara nyingi wamisionari walifaidika na ulinzi wa serikali za kikoloni. Walipata msaada wa kumiliki ardhi na kukabidhiwa madaraka katika ustawi wa jamii. Lakini si kweli ya kwamba serikali za kikoloni ziliendesha misioni ya kikristo. Shabaha ya ukoloni ilikuwa kutawala bila matatizo. Katika sehemu nyingine hasa penye Waislamu wengi wamisionari walizuiliwa wasifanye kazi kwa sababu wakoloni walishirikiana na watawala (machifu) waislamu na kuogopa vurugu. Petu Tanzania makanisa yaliweza kuanza kazi sehemu nyingi za pwani baada ya uhuru tu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika nchi mbalimbali za Afrika ya Magharibi.

9.6.2. Athari za ubaguzi mpya katika misioni

Pale ambapo Kanisa la Kiafrika lilishaanza kujitawala kama katika Afrika ya Magharibi maendeleo yake yalikwama kwa muda mrefu. Ukoloni uliambatana na mawazo ya kibaguzi. Tangu watawala na walowezi kutoka Ulaya walipoingia itikadi ilienea ya kuwa mwafrika si mwanadamu kamili. Itikadi hiyo iliwasaidia wakoloni kujitetea mbele ya wananchi wenzao nyumbani kwao jinsi walivyoendesha ukoloni. Itikadi hiyo ikasababisha mageuzi ya mawazo. Wakristo wengi Ulaya walipewa mashaka kama inawezekana kweli kuwakabidhi Waafrika madaraka mara moja ndani ya kanisa. Askofu Crowther alishambuliwa sana na aliyemfuata alikuwa Mwingereza tena. Hata hivyo viongozi wengine wamisionari walilenga mapema kuwaandaa wenyeji kuwa viongozi baadaye, kama vile wamisionari waanglikana na wakatoliki kule Uganda.

9.6.3. Athari za siasa ya ukoloni

Mara nyingi serikali za kikoloni zilisisitiza kuwa na wamisionari kutoka kwa mataifa yao. Mfano ni Tanganyika ambako vituo vingine vya Waanglikana (Waingereza) vilifungwa baada ya kuingia kwa Wajerumani. Badala yake serikali ya Ujerumani iliomba makanisa ya kiluteri pamoja na Moravian (toka Ujerumani) kuanza kazi katika Tanganyika. Mara nyingi wamisionari walipokea kwa shukrani ulinzi huo wa pekee kutoka kwa serikali yenye uraia wao. Hii ilileta matatizo mara kadhaa ikiwa serikali ya kikoloni iligandamiza wenyeji na wamisionari walisita kuwatetea kwa sababu walikuwa karibu mno na serikali yao. Katika Tanganyika kuingiliana kwa namna hiyo kati ya kanisa na serikali ilisababisha kufukuzwa kwa wamisionari wajerumani wakati wa vita 1914-1918 nchi ilipotekwa na waingereza.

9.7. Wamisionari Wazungu na Wainjilisti Waafrika

Kazi ya kuhubiri kwetu Afrika ya Mashariki ilianzishwa katika sehemu nyingi na wamisionari wazungu. Lakini baada ya muda mfupi mzigo mkubwa wa kuhubiri injili ulibebwa tayari na wakristo wazalendo. Wamisionari walijitahidi zaidi kuendesha vituo kama shule, seminari na mahospitali. Pia walishika muda mrefu shughuli kama ubatizo, Chakula cha Bwana na sakramenti kwa jumla kwani hizo huhifadhiwa kwa wachungaji au mapadre vyeo ambavyo havikupatikana mwanzoni kwa wenyeji (tofauti kule Afrika ya Magharibi jinsi tulivyoona juu). Lakini kazi kubwa ya kuhubiri vijijini, ushuhuda wa moja kwa moja na hata kufundisha katika shule za msingi iliendeshwa baada ya muda mfupi wa mwanzo na wakristo waafrika. Wamisionari walikazia zaidi kuwaandaa hawa wainjilisti, makatekista na walimu. Hivyo tunaweza kusema ya kwamba kazi ya misioni tangu mwanzo ilikuwa kazi ya waafrika wenyewe, ingawa chini ya uongozi wa wamisionari wazungu.

9.8. MUHTASARI WA HISTORIA YA MISIONI KATIKA TANZANIA

Waliotangulia walikuwa wamisionari Krapf na Rebmann waliotumwa na chama cha C.M.S.; kutoka kwa kituo chao karibu na Mombasa walifika mpaka eneo la Tanzania leo. Kituo cha kwanza cha C.M.S. katika Tanganyika kilikuwa Mpapwa mw. 1876.

Katika mazingira ya Kanisa la Kianglikana chama cha Misioni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) kiliundwa kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika. Waliingia kule Zanzibar mw. 1864. Hapa walijenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa ikiwa altari imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na ubatizo kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.

Shirika la kwanza la katoliki lilikuwa la mapadre wa Roho Mtakatifu. Walianzisha kule Bagamoyo kituo cha kukalisha watumwa waliowanunua na kuwapa uhuru kuanzia mw. 1868. Walifuatwa na Mapadre Weupe walioanza mw. 1879 kule Ziwa Tanganyika. Baada ya kwanza ukoloni wa kijerumani serikali iliomba makanisa ya kijerumani kuchukua wajibu. Walutheri wa kwanza walianza Dar-es-salaam mw. 1887. Mw. 1889 walifika watawa wajerumani wa kwanza wa shirika la Mt. Benedikto waliounda baadaye monasteri za Peramiho na Ndanda na kushughulika uinjilisti katika Kusini.

Mw. 1891 walifika wamisionari Wajerumani Walutheri (Misioni ya Berlin) na Wamoravian kupitia Ziwa Nyassa wakipatana kugawa maeneo ya kazi; walijenga vituo katika Unyakyusa kule Rungwe na Manow. Waluteri wengine (misioni ya Leipzig) walianza kule Uchagga kituo cha Moshi. Wajerumani wengine waliofika mapema walikuwa Wasabato (Seventh Day Adventists). Kutoka Kenya ilianzishwa kazi ya A.I.M. (Africa Inland Mission) katika mkoa wa Mwanza - chama hiki kiliundwa kule Marekani kama misioni ya kimadhehebu lenye athari kubwa ya kibatisti.

Karne hii ya ishirini iliona wamisionari wengi kutoka makanisa mbalimbali ya Ulaya na Marekani. Baada ya vita vya pili vya dunia Wamarekani walijenga Kanisa la Kibatisti Kusini-Magharibi mwa Tanzania. Walifika pia wamsionari kutoka makanisa mbalimbali ya kipentekoste kama vile Swedish Pentecostals, Assemblies of God n.k. Tofauti na nchi za Afrika Kusini na Magharibi wamisionari ya makanisa ya wamarekani weusi hawakuwa na athari kubwa. Pia makanisa ya kiorthodoksi hawakuanza kuenea tofauti na Kenya ambako Kanisa la Kiorthodoksi la Kiafrika (linaloshirikiana na Patriarka ya Kigiriki-orthodoksi wa Aleksandria-Misri) ni kubwa.16

9.9. MASHAHIDI WA UGANDA

Hatuna budi kukumbuka kilichotokea mwanzoni mwa hiostoria ya kanisa katika Afrika ya Mashariki huko Uganda.

Kule Buganda palikuwepo ufalme mkubwa. Mtawala wake kwa cheo cha Kabaka aliyeitwa Mutesa aliwakaribisha wageni. Katika miaka 1877 hadi 1879 walifika wamisionari wazungu kule Buganda, wakitangulia Waanglikana wa C.M.S. waliofuatwa na Wakatoliki wa shirika la Mapadre Weupe.

Mara moja Waingereza wa C.M.S. na Wafaransa wa Mapadre Weupe walianza kushindana mbele ya mfalme na wakubwa wake. Mashindano haya yalidhoofisha sifa za wamisionari mbele za Kabaka. Zaidi ya hapo washauri waislamu walimweleza Kabaka ya kwamba wageni wale walitaka tu kuangusha ufalme wake. Mfalme na wakubwa walisita kukaribia zaidi mahubiri mapya.

Lakini makao makuu yalijaa vijana kutoka kwa familia za machifu waliofanya kazi ya kumhudumia mfalme. Wamisionari walitafsiri Biblia katika Kiganda wakafundisha kusoma. Ilikuwa mara ya kwanza ya kwamba lugha ya kiganda iliandikwa. Vijana wengi walivutwa na mahubiri ya kikristo pamoja na elimu mpya. Kuanzia mw. 1882 Waanglikana walianza kubatiza. Kwa namna hiyo Kanisa la Uganda lilianza kwa njia ya vijana.

Baada ya kifo cha Mutesa alifuatwa na Kabaka Mwanga aliyekuwa na wasiwasi juu ya wamisionari. Mw. 1885 watumishi watatu wa mmisionari Mackay waliuawa kwa amri ya mfalme walipomsindikiza dhidi ya amri ya mfalme.

Waziri wa Mfalme aliyefuata imani za jadi na aliyekuwa pia na mipango ya kumwangusha mfalme na kuwafukuza wageni wote aliendelea kumshawishi. Tar. 25. Mai 1886 hasira ya Kabaka iliwaka. Aliamua kuwaondoa wakristo wote katika mazingira yake. Vijana wote waliitwa mbele yake wakaulizwa kama wako tayari kuacha Ukristo. Walio wengi walikataa. Tar. 3.Juni 1886 zaidi ya vijana wakristo 30 walichomwa moto wakiwa hai kwa amri ya Mfalme. Mahali pa vifo paliitwa Namugongo. Inajulikana ya kwamba wamisionari waanglikana na wakatoliki waliendelea kuvutana juu ya matatizo mpaka dakika la mwiosho. Lakini pale Namugongo wakristo walikufa pamoja, wakatoliki 12 na waprotestant 9 wanjulikana; juu ya wengine hakuna uhakika. wengine hawakubatizwa bado walikuwa wanafunzi wa ubatizo.


SURA YA KUMI: KARNE YA 20

1. vita vya Ulaya/kujitegema 2. African Independent Churches 3. Viongozi wazalendo 4. Kukua kwa Kanisa 5. Madhehebu mengi 6. Ekumene na ushirikiano 7. Kanisa na serikali 8. Uhusiano na dini zingine

Leo hii tuko katika awamu ya nne ya uenezaji wa Ukristo katika bara ya Afrika. Leo hii ni Waafrika wenyewe bila uongozi wa nje ambao wanahubiri neno la Mungu kwa wenzao. Kanisa katika Afrika inakua haraka kuliko katika mabara yote mengine. Wataalamu wa takwimu wakristo na waislamu wanashindana ni nani mwenye waumini zaidi lakini zipo alama ya kwamba katika mwaka 2000 idadi kubwa ya waafrika watakuwa wakristo ya madhehebu mbalimbali.

Tangu mwanzo wa karne hii mpaka sasa kanisa katika Bara la Afrika limeshuhudia mabadiliko makubwa. Mabadiliko haya ndiyo yaliyosababisha jinsi Ukristo unavyoonekana leo. Mwanzoni mwa Karne makanisa yalikuwa bado chini ya uongozi wa wamisionari wazungu. Sababu zifuatazo zilisababisha mabadiliko:

10.1. Vita vya Ulaya vilisaidia kukomaa kwa kanisa la Afrika

Mahali pengi Tanzania makanisa yalianzishwa hasa na wamisionari wajerumani, ama waluteri au wakatoliki au wamoravian, wasabato, n.k. Katika vita vikuu vya kwanza (mw. 1914-18) jeshi la Kiingereza liliingia na kuteka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika). Raia wa Ujerumani walifukuzwa pamoja na wamisionari. Kwa muda wa miaka saba wakristo waafrika walibaki peke yao mpaka wamisionari wajerumani waliruhusiwa tena kurudi. Bila maandalizi makubwa wainjilisti, makatekista na walimu waafrika walipaswa kuongoza kanisa changa. Wengi walihofu ya kw amba kanisa litarudi nyuma. Lakini mahali pengi idadi ya wakristo imeongezeka mpaka wamisionari waliporudi.17 Hali hiyohiyo imerudi wakati wa vita vya pili 1939-45. Safari hii wamisionari wajerumani waliwabariki wainjilisti waafrika kuwa wachungaji kabla ya kufukuzwa wenyewe katika Tanganyika na serikali ya kiingereza.

10.2. "Makanisa ya kiafrika yanayojitegema"

Katika nchi mbalimbali ukali wa ukoloni ulisababisha mafarakano katika makanisa yaliyoongozwa na wamisionari halafu kutokea kwa makanisa yanayoitwa "African Independent Churches". Mifano hii ipo Kenya, Zaire, Afrika ya Kusini na penginepo. -- Katika Kenya wenyeji walishtushwa sana na tendo la kuchukuliwa ardhi yao iliyotolewa kwa walowezi wazungu. Uchungu mkubwa ukajengwa ulioonekana pia katika mashaka dhidi ya wamisionari wazungu. Wakikuyu walipoanza kupinga siasa hiyo wamisionari waliwashauri wakristo watulie (wakijaribu wenyewe kutetea haki za wenyeji mbele ya serikali ya kikoloni). Kumbe wainjilisti na walimu pamoja na wakristo wengi walianza kujitenga katika makanisa yaliyoongozwa na wamsionari wakaanzisha makanisa yao. Makanisa haya yalikuwa mara nyingi ya kikabila yakiendelea kufarakana kati yao. Lakini yalifaulu sana kuunganisha utamaduni wa kiasili na imani ya kikristo kwa namna yao.

Katika nchi ya Kongo (Zaire) mwinjilisti Simon Kimbangu alionekana kuwa na kipawa cha uponyaji. Watu wengi walimwendea wakitafuta nafuu wakasikia mahubiri yake. Serikali ya kikoloni ya Ubelgiji iliogopa mikutano hii mikubwa ya Waafrika bila usimamizi wa wazungu au machifu. Kimbangu akaagizwa na wamisionari kwa amri ya serikali kuacha mahubiri na uponyaji hakuweza kutii. Wabelgiji wakamkamata wakamfunga gerezani miaka mingi mpaka kifo. Wafuasi wake wakamwamini kuwa ni nabii wa Mungu wengine walisema ndiye Yesu aliyerudi wakatoka katika uongozi wa wamisionari walionyamaza mbele ya tendo la serikali kumfunga Kibangu bila kosa. Kati ya wafuasi wake limetokea "Kanisa la Kristo kwa Mtume wake Simon Kimbangu" ni kanisa kubwa katika Zaire lenye waumini mamilioni. -- Kule Afrika ya Kusini milioni za Wakristo ni wafuasi wa makanisa yanayoitwa "Ki-Zayuni" au "Ki-Ethiopia".

Kwa jumla kutokea kwa makanisa haya ya "African Independent Churches" kumeonekana penye ukoloni mkali, ugandamizaji kupita kiasi au kuingia kwa walowezi waliochukua ardhi ya wenyeji ikiwa wamisionari wazungu waliomba wakristo wao kutulia na kutii serikali. Siasa kali ya kikoloni iliunda uchungu mkubwa ulioweza kusababisha farakano. -- Jina la "African Independent Churches" lina ugumu siku hizi kwa sababu hata makanisa mengine kama RC, Anglikana au Walutheri yameshakuwa makanisa ya kiafrika yanayojitawala tena tangu miaka mingi. Lakini kwa uzoefu jina hili la heshima limebaki kwa makanisa haya yaliyoanzishwa wakati wa ukoloni kama alama ya Waafrika kuchukua Injili mikononi mwao hata bila kibali cha wamisionari au serikali ya kikoloni.

10.3. Viongozi wazalendo

Katika Afrika ya Mashariki walikuwa hasa wamisionari katika Uganda waliofanya mapema maandalizi ya kuwa na mapadre na wachungaji waafrika. Kazi kubwa ilikuwa kuunda taasisi zilizoweza kutosheleza madai kwa ajili ya elimu ya juu ya vijana waliotoka katika mazingira bila vitabu wala shule. Ingawa mazingira ya kikoloni yalikuwa na ubaguzi mkali bado viongozi wengine walitunza msimamo wa kueleleka kwenye kanisa la kiafrika litakalojitawala na kujitegemea. Mwanglikana Tucker, Askofu wa Uganda aliwahi kuwabariki mapadre wa kwanza mnamo mw. 1893, akifuatwa na Wakatoliki mw. 1913. Lakini Wakatoliki walisogea mbele walipombariki askofu mwafrika Kiwanuka mw. 1939. Baada ya vita vya pili duniani makanisa mengi yaliyoongozwa na wamisionari yalianza kuwaandaa viongozi wenyeji kushika madaraka. Mapambano wa kupata uhuru wa kisiasa yaliharakisha mwendo huu hata ndani ya makanisa yaliyowahi kuchelewa kufanya maandalizi haya mapema. Makanisa yanayolingana na "African Independent Churches" hayakuwa na wakristo wengi sana katika Tanzania ingawa yapo hasa katika maeneo karibu na mipaka kwa mfano kule Mara (Maria Legio Church kutoka Kenya) au katika Mbeya.

Kiongozi Mtanzania wa kwanza aliyepata cheo cha kimataifa alikuwa Askofu Laurian Rugambwa aliyebarikiwa mw. 1952. Miaka minane baadye alipewa cheo cha "Kardinali" alikuwa kardinali ya kwanza mwafrika. Kardinali ni cheo cha askofu mkatoliki anayepewa pia kanisa moja kule Roma pamoja na haki ya kumchagua papa. Halmashauri ya makardinali inakaa pamoja na Papa na kushauriana juu ya uongozi wa kanisa. Papa akifa ndio makardinali tu wanaokutana kumchagua papa mpya.

10.4. Kukua kwa Kanisa

Tangu Uhuru wa kisiasa idadi ya Wakristo imeongezeka sana katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara. Hakuna bara nyingine ambako idadi ya Wakristo inaongezeka haraka kama kwetu Afrika. Sababu ziko nyingi, kwa mfano:

  • a) imani za kiasili zimefifia kwani si rahisi kuzifuata nje ya mazingira ya kijadi yanayoendelea kubadilika.
  • b) Ukristo umeambatana tangu mwanzo na elimu. Elimu inaonekana kuwa mlango wa maendeleo hivyo machoni pa watu wengi Ukristo na maendeleo vimekwenda sambamba. Karibu shule zote zilianzishwa na wamisionari au makanisa. Viongozi walio wengi wa Afrika huru (Wakristo na waislamu) walipita katika shule za misioni (hata wale waliotaifisha baadaye shule za makanisa).
  • c) Kanisa lilijitahidi sana kutumia utamaduni wa kiafrika pamoja na Injili. Chombo kikuu kilikuwa Biblia yenyewe. Ni kweli ya kwamba wamisionari wengi hawakuelewa rahisi pande zote za utamaduni wa kiafrika. Sababu moja ya farakano kubwa kati ya wamisionari na wakristo Wakikuyu kule Kenya ilikuwa kutoelewana juu ya kutahiriwa kwa wasichana. Lakini lugha nyingi za kiafrika ziliandikwa mara ya kwanza wakati wamisionari wageni walipojitahidi kujifunza lugha hizo na kutafsiri Biblia. Leo hii Biblia nzima au angalau Agano Jipya vimepatikana katika lugha mamia ya kiafrika, vilevile nyimbo za kikristo. Siku hizi hata nyimbo za kikristo zinazidi kutumia tuni za kiafrika, ingawa bado ziko tofauti kubwa kati ya madhehebu mbalimbali juu ya uzoefu wa kutumia zaidi tuni za kale za Ulaya au zile za kienyeji.
  • d) Sababu muhimu ya kukua kwa kanisa katika Afrika ni bila shaka ushuhuda na mfano wa wakristo wenyewe unavyotolewa mbele ya majirani wao. Kiasi jinsi maisha ya watu wanaoitwa "Wakristo" kwa jina la Kristo yanavyolingana na upendo na amani vinavyotoka katika Injili ujumbe huo hueleweka vizuri.
Maswali na Maarifa:

Fanya utafiti katika vitabu vya nyimbo vya makanisa mbalimbali. Tazama maelezo juu ya watungaji wa tuni au maneno. Je, asilimia gani ina asili ya kiafrika, au asili ya ng'ambo?

10.5. Madhehebu mengi

Kanisa la Afrika hupatikana katika madhehebu mamia. Hali hii kiasi ni tokeo la urithi wa wamisionari walioleta mafarakano yao ya kale kutoka Ulaya au Marekani mpaka Afrika. Kweli vijana wa leo wangeuliza swali kama sababu zilizosababisha mafarakano kule Ulaya miaka 500 iliyopita bado zina nguvu leo hii kwa vijana waafrika. Lakini idadi kubwa ya madhehebu yametokea kutokana na mafarakano ndani ya makanisa yaliyokuwepo tayari. Pia hali ya kiuchumi ina uzito wake - siku hizi vikundi vingi vya kikristo kutoka nchi tajiri zinaendelea kufika hapa na kuwavuta wafuasi kwa uwezo wao wa kutoa misaada mbalimbali. Wakati mwingine madhehebu yanajitahidi zaidi kuwavuta wakristo watoke katika dhehebu lao la asili kuingia lingine kuliko kuwatafuta wasio Wakristo.

10.6. Uekumene na ushirikiano: kwa bahati nzuri ushirikiano upo pia si mafarakano tu. Hasa karne hii ya 20 imekuwa karne ya kujenga ushirikiano. Wakristo wa madhehebu mbalimbali yanashirikiana kirahisi katika shughuli mbalimbali. Wamisionari wenyewe hasa kwa upande wa kiprotestant waliona tayari umuhimu wa ushirikiano. Kwa mfano Waluteri waliwaomba Wamoravia kuanzisha kazi pamoja katika Tanganyika Kusini-Magharibi. Wamisionari wao walifika mwaka uleule wa 1891 wakitumia njia ya Ziwa Nyasa wakagawana maeneo yao kama walivyogawana wachungaji wa Ibrahimu na Lutu. Baadaye walichapisha hata kitabu cha pamoja cha nyimbo za kikristo.

Mw. 1936 viongozi wa madhehebu kama Waluteri, Waanglikana, Wabatisti na Wamoravian waliunda "Baraza la Misioni Tanzania". Baraza hili lilikuwa utangulizi wa CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania / Christian Council of Tanzania). Katika miaka ya 1960 viongozi wa makanisa ya kiprotestant waliongea juu ya kuunda Kanisa la Muungano katika Afrika ya Mashariki. Kwa bahati mbaya wafadhili wengine kutoka ng'ambo waliona hawawezi kusaidia kanisa la muungano kama si tena kanisa la dhehebu lao. Kumbe hatari ilionekana kwa kazi kama mahospitali na shule zilizotegemea msaada kutoka ng'ambo hivyo muungano ulisimamishwa. Lakini makanisa yaliyoongea wakati ule yanaendelea kushirikiana katika vyombo vya pamoja kama vile CCT. Wanachama wa CCT ni kama wafuatao: Kanisa la Kiinjili-Kiluteri, CPT/ Kanisa la Jimbo la Tanzania (Anglikana), Majimbo ya Kanisa la Moravian, Africa Inland Church, Kanisa la kibatisti, Presbyterian Church, Jeshi la Wokovu, Kanisa la Uinjilisti (Mbalizi), pia vyama kama TCRS/Huduma ya kikristo ya wakimbizi Tanzania.

Ushirikiano umejengwa pia kati ya makanisa ya CCT na Kanisa la Katoliki. Zamani za wamisionari uhusiano huo ulikuwa mara nyingi mgumu. Lakini katika karne hii mabadiliko mengi yamejenga msingi wa uelewano na hali ya kuheshimiana. Hatua muhimu sana ilikuwa Mkutano Mkuu wa Kanisa la Katoliki duniani ulioitwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano mw. 1962 hadi 1965. Hapo maaskofu wote chini ya uongozi wa Papa Yohane XXIII walitamka ya kuwa Kristo yupo katika makanisa yote ya kikristo na ya kwamba kujenga umoja wa kanisa ni wajibu wa wakristo wote. Leo hii makanisa ya CCT na Baraza la Maaskofu wakatoliki hushirikiana katika shughuli mbalimbali kama vile Baraza la kikristo la Afya Tanzania (Tanzania Christian Medical Board) au katika kuandaa mafundisho ya pamoja katika elimu ya kikristo mashuleni. Kitabu hiki unachosoma sasa hivi ni tokeo la ushirikiano huo.

Chama cha Biblia ni chombo kingine cha ushirikiano wa kimadhehebu. Chama hicho kina kazi ya kutoa Biblia kwa bei nafuu kwa watu wengi. Kinasimamia utafsiri wa Biblia katika Kiswahili cha kisasa. Kinaandaa matoleo mapya ya Biblia na misaada kama ile "Itifaki ya Biblia".

10.7. Wajibu wa kinabii

Katika nchi nyingi kanisa limekuwa nguvu ya kutetea haki za binadamu. Tumesikia habari za Askofu Desmond Tutu kule Afrika ya Kusini au za Askofu Luwum katika Uganda jinsi walivyojaribu kutetea haki za wananchi dhidi ya utawala mbaya. Labda tunamkumbuka Askofu Ambrosio wa Milano (aliyemvuta kijana Agostino kuwa Mkristo) alivyomtenga Kaisari katika kanisa kwa sababu ya uuaji wa wananchi wengi wasio na kosa uliofanywa na wanajeshi wa serikali. Ikiwa wakristo wanajisikia wito wa kusimama na kusema mbele ya wakubwa hukumbuka manabii wa Agano la Kale hadi Yohane Mbatizaji. Wanakumbuka pia wakristo wengi katika historia walioweza kusimama mbele ya wafalme au wakubwa na kutetea haki za watu. Msingi wake ni katika mafundisho juu ya kazi ya uumbaji. Mbele ya Mungu tuko sawa - kumbe kuna msingi gani tukiona ya kwamba wengine ni sawa zaidi?

Lakini si wakristo wote wanaokubali na kufurahia msimamo wa aina hiyo. Wengine huona ya kwamba Imani ya Kikristo haina shughuli na taratibu za dunia hiyo. Wengine huona ya kwamba ni wajibu wa Mkristo kutii serikali yoyote wakikumbuka maneno ya Mtume Paulo katika Rum 13. Pamoja na haya yapo mapokeo katika Ukristo kutoshindana na wenye mamalaka bali kuwavumilia katika yote. Wengine labda huona hofu ya kuwa dini inaingizwa mno katika siasa.

TUJADILI:

je, ni sawa kwa wakristo kushiriki katika mambo ya siasa. Taja sababu zinazosaidia na kupinga wazo hili. Je, Mkristo anapaswa kusaidia serikali katika mambo yote?

10.8. Dini zingine

Siku hizi Wakristo pote duniani huishi pamoja na watu wa dini zingine. Kwetu Tanzania ni hasa watu kutoka vikundi viwili: Waislamu na wafuasi wa dini za asili. Hasa uhusiano wetu na ndugu zetu Waislamu ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Katika sehemu mbalimbali za Afrika uhusiano huo ulianza kuwa mgumu. Sababu moja ni mzigo wa historia tunaoubeba mara nyingi bila kujua. Kumbe Waislamu wanaweza kutumia neno "jihadi" wakiongea juu ya jitihada za pekee kuimarisha jumuiya yao au kueneza imani yao - lakini wakristo walio wengi wanasikia neno hilo "Jihad" vibaya. "Vita vitakatifu" vya Waarabu waislamu viliitwa kwa neno "jihadi" vilileta mateso mengi juu ya Wakristo katika nchi mbalimbali. Kumbe neno halimaanishi vita hasa - lakini liliwahi kutumika hivyo tangu muda mrefu.

Wakristo wengi hawana tatizo kutumia neno "Crusade" kwa ajili ya mikutano ya kiroho. Lakini Waislamu wanaweza kuchukua neno hili vibaya pia kwani kiasili "Crusade" maana yake "Vita vya Msalaba" linamaanisha hasa kipindi cha miaka 800 iliyopita. Wakati ule Wakristo wa Ulaya ya Magharibi walijaribu kuwafukuza Waislamu katika nchi za Mashariki ya Kati kwa vita vilivyoendelea muda wa miaka 200.

Itakuwa kazi muhimu sana kwa vijana wa leo kushindana na ule mzigo wa historia na kuvumiliana. Mzigo huo ni hasa urithi wa historia ngumu kati ya Waislamu na Wakristo kule Ulaya na Asia. Lakini mwanzoni mwa Uislamu alikuwapo Mfalme Mkristo wa Ethiopia aliyewapokea na kuhifadhi wakimbizi waislamu kutoka Maka.18 Katika Misri Wakristo wengi walifurahia kuja kwa Waarabu waliopunguza ugandamizaji kutoka kwa Wafalme wakristo wa Bizanti. Hapa Tanzania Wakristo na Waislamu walishirikiana vema katika mambo mengi ya kijamii.

Kwa Wakristo wengi ni siri kwanini Mungu alikubali kutokea kwa dini hiyo mpya. Ukristo na Uislamu ni karibu katika mambo mengi lakini hutumia mafundisho yanayogongana katika sehemu zingine. Mpaka leo hii Waislamu walikuwa wagumu sana kupokea Injili. Lakini kwa ujumla sisi Wakristo hatuna sababu ya kujivuna kuhusu sifa zetu kuwa bora kuliko waislamu. Anayesoma "Historia ya Kanisa" ataona mifano mingi jinsi gani Wakristo walivyosahau mafundisho ya Bwana Yesu na kutendeana kwa unyama. Kwa hiyo tusijivune ya kwamba Ukristo ni dini ya upendo au imani yenye maendeleo - kama sisi wenyewe si mifano ya upendo huo na maendeleo haya.

Mt. Fransisko aliona wakati wa "Crusades" (vita vya msalaba) ya kwamba hakuna njia kuwavuta Waislamu kwa njia ya mabavu au kushindana nao. Mashindano ya pekee yanayoruhusiwa kwa mkristo ni yale ya upendo ya kumfuata Bwana Yesu. Kwa jumla mawazo ya Mt. Fransisko yamethebitishwa na historia. Kwa hiyo si vibaya tukianza kujiandaa kushirikiana na wenzetu waislamu kwa njia ya kikristo tukifahamu kidogo imani yao , na tukiwa na uwezo kutambua pia sifa nzuri zilizopo katika maisha na mafundisho yao.

Kuhusu ndugu zetu zinazofuata imani za asili tunapaswa pia kukumbuka mashariti ya upendo. Tusisahau ya kwamba wanatunza katika mila na desturi zao urithi wa utamaduni. Hata maadili mengine yanayofundishwa kwao yanalingana na sehemu za Biblia. Hakika si vema kama vijana wakristo wanawacheka na kuwaita kwa majina kama "pagani". Hata juu ya imani hizo za jadi ni kweli ya kwamba zilimjua Mungu kwa namna fulani kutokana na uumbaji wake jinsi alivyoandika Mtume Paulo katika Rom.


Maelezo juu ya tahijia ya majina (namna ya kuandika maneno)

1. Kwa ujumla kitabu kinajaribu kufuata kawaida ya Kamusi za Kiswahili. Wakati mwingine mazoea yanatofautiana kutumia neno la asili ya Kiarabu (kama mara nyingi katika Kiswahili cha urasimu) au maneno mapya ya asili ya Kiingereza. Kwa sababu mapokeo ya waandishi wa habari za kitheologia yanaelekea zaidi kwenye Kiswahili cha urasimu lakini wanafunzi siku hizi hawafahamu tena maneno haya azimio letu lilikuwa la mara kwa mara. (Kwa mfano: "Iskenderia" - "Aleksandria"; "Bahari ya Kati" - "Mediteranea"- kwa bahati mbaya hata vitabu mbalimbali vya shule vinachanganya Kiswahili na Kiingereza)

2. Juu ya maneno na majina yanayotumika hasa katika Historia ya Kanisa kitabu kinafuata mara nyingi ushauri wa "Msamiati wa Maneno ya Kitheologia"; pale ambako hautoi mifano tumejaribu kuunda maneno yanayolingana na utaratibu wa lugha ya Kiswahili, tukiepukana na kuchukua vivumishi vya sifa kutoka kwa Kiingereza. (Mfano: Wakopti badala ya Koptiki, Wadonato badala ya Wadonatist, Wahus badala ya Wahussite, kwa ujumla kuepukana na viambishi tamati vya kiingereza visivyolingana na lugha za asili -kwani hata Kiingereza hakitumii hapo maneno ya asili bali imepokea maneno haya kutoka kwa malugha mengine kama kigiriki na kilatini.) Menginevyo tumejitahidi kufuata kawaida ya wenye mapokeo fulani; kwa mfano waandishi waprotestant huzoea kuandika "Chama cha Yesu" wakati wenyewe hujiita "Shirika". Vilevile hutafsiri Indulgences kuwa "msamaha" wakati kanisa katoliki hutumia "rehema".

3. Juu ya Majina ya Kibiblia kitabu kimejitahidi kuitikia ushauri wa Kamati ya Umoja wa Makanisa katika Mkoa wa Mbeya unaosema: "Tukitaja majina ya Kibiblia tufuate utaratibu wa Agano Jipya/ Kiswahili cha Kisasa." Hivyo wasomaji kutoka kwa makanisa mbalimbali wataona umbo lililo tofauti na uzoefu wao: Roma badala ya Rumi, Kristo badala ya Kristu, Yohane badala ya Yohana, Maria badala ya Mariamu, n.k. .

Kuhusu kitabu hiki: Dibaji ya mwaka 1993

Maandishi yafuatayo ni matokeo ya kazi ya siku nyingi kama Mchungaji wa Wanafunzi na Mwalimu wa Elimu ya Kikristo katika shule za sekondari Mbeya. Tumefuata muhtasari uliokubalika na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (T.E.C.) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (C.C.T.). Muhtasari wetu unaweka uzito fulani katika Historia ya Kanisa lakini wanafunzi wetu hawaandaliwi vizuri sana kwa upande wa somo la "History". Bila kitabu, mafundisho haya ni magumu sana tulihangaika mara kwa mara.

Kitabu hiki kisingetokea bila Kamati ya Walimu wa Dini (Elimu ya Kikristo) Mbeya. Kamati hii inaunganisha walimu kutoka makanisa ya CCT (Anglikana, Lutheri, Moraviani na Kanisa la Uinjilisti) pamoja na Kanisa la Katoliki (RC) wanaohudumia shule za sekondari katika eneo la Mbeya. Kamati hii inatekeleza nia ya TEC na CCT kuwa na utaratibu mmoja shuleni jinsi inavyoonekana katika muhtasari ya pamoja kwa ajili ya shule za sekondari. Kwa bahati mbaya utekelezaji wa nia hiyo si kawaida katika Tanzania. Inawezekana ya kwamba Mbeya ni eneo la pekee ambapo wanafunzi wa kikristo hawatengwi kidhehebu wakati wa somo la dini. Kwa sababu hii sina budi kutoa shukrani za pekee kwa viongozi waliowezesha ushirikiano huu ndio hasa Askofu Sanga wa Kanisa la Katoliki pamoja na Askofu Wawenza na Uongozi wa Kanisa la Moravian. Waliteua mara kwa mara masista, mapadre na wachungaji kwa ajili ya kazi hii inayoendelea kupanuka, na kuwaruhusu washirikiane.

Yafuatayo ni mawazo machache yaliyoongoza kazi ya utungaji. (Maelezo zaidi katika Nyongeza (1).

1. Kitabu kiwe kifupi - kwa matumizi katika shule za sekondari na kwenye ngazi ya vyuo vya Biblia / Makatekista na kwa Wakristo wetu wanaopenda kujielimisha. Shuleni kitasaidia wakati wa mhula wa pili Kidato cha Tatu na kwa marudio wakati wa Kidato cha Tano au Sita. Lugha yake inajaribu kuwa rahisi. 2. Kinatumia lugha ya Kiswahili kwani somo la dini hufundishwa kwa Kiswahili- . 3. Ni kwa ajili ya wanafunzi na kwa ajili ya matumizi katika Tanzania hivyo kinakazia sehemu za kiafrika za Historia ya Ukristo pamoja na kuweka msingi kwa ajili ya kuelewa asili ya madhehebu yetu yalivyo Tanzania. Habari nyingi za kihistoria zimepangwa kufuatana na uhusiano wao na Historia ya Afrika. Habari hizo zinaweza kurudia kwa upana zaidi katika vifungo zinazoeleza historia ya kanisa kwa ujumla. Mwalimu akitaka kufupisha anaweza kutumia hasa sura zinazoeleza habari za Ukristo katika Afrika kwa kuchagua vipande tu vya sura zingine. 4. ni kwa ajili ya matumizi ya Kiekumene (kimadhehebu) - kimejaribu kutunza mizani na kuheshimu mapokeo ya makanisa mbalimbali bila kuacha kabisa msingi wa historia ya kisayansi. Kwa sababu madhehebu yetu ya Tanzania yana asili yao nje ya Afrika ilikuwa lazima kueleza pia habari za matengenezo na mafarakano ya kanisa kule Ulaya.

Siwezi kuficha kasoro mbalimbali: Maandishi haya ni kazi ya mwandishi mmoja tu -tumaini langu mwanzoni lilikuwa kutunga kurasa hizo pamoja na wengine. Ingekuwa lazima kwangu kama Protestant kushirikiana na mkatoliki, na ingekuwa lazima kwangu kama mtu kutoka Ulaya kukamilisha kazi hiyo pamoja na Watanzania. Pia ingelikuwa vizuri zaidi kama muswada ungeandaliwa tangu mwanzo na wasemaji wa Kiswahili, hata hivyo ndugu mbalimbali walijitolea kusahihisha lugha. Tatizo lingine ni Kiswahili chetu cha kidhehebu katika msamiati wa kidini yaani tumezoea kutumia maneno mbalimbali kwa namna tofauti kati ya madhehebu yetu.

Sina budi kutoa shukrani mbalimbali. Mch. Jaeschke (Chuo cha Biblia Kidugala KKKT) alinipa wazo na moyo kutafakari kazi hii. Masista na mapadre wenzangu wakatoliki katika Umoja wa Walimu wa Dini wa Mbeya walinisaidia sana kuelewa mapokeo ya kanisa lao. Mch. Sichone, Ndiwela Sichone, Mch. Buyah na Mwal. Mwaisumu walinisaidia kwenye ngazi mbalimbali masahihisho ya Kiswahili. Makosa yaliyobaki ni makosa yangu, si ya kwao. Anayefahamu Kitabu cha "Christian Living Today" atatambua ya kwamba nilichota mawazo mengi mle.

Nashukuru sana Motheco Publishers (Idara ya maandiko ya Chuo cha Theologia cha Moravian Mbeya) waliopima na kukubali muswada na kuitoa kama kitabu. Kuwepo kwa picha kumewezekana kwa sababu ya msaada wa Herder Publishers (Freiburg/Ujerumani) walioturuhusu kutumia picha zao bila malipo. Ofisi ya Bildarchiv ya Wamisionari wa Afrika (Cologne/Ujerumani) ilisaidia pia picha mbalimbali.

Mbeya, Julai 1994 Ingo Koll (Mchungaji wa Wanafunzi Kanisa la Moravian Mbeya 1987 - 1993)


Maelezo ya Nyongeza

Kuhusu (2.3.3.) Mazingira ya Ukristo katika sehemu zingine za dunia

Lakini hata zamani ile watu waliweza kufanya safari za ajabu. Miaka 600 k.K. Mfalme wa Misri alituma meli kuzunguka bara la Afrika. WAlirudi baada ya miaka mitatu na kuandika taarifa. Lakini haikuwezekana kurudia safari ile iliyokuwa na hatari mno. -- Babu za makabila mbalimbali ya Madagaska wametoka Indonesia wakivuka Bahari lakini mawasiliano haya yamekatika baadaye. Asili yao inaonekana tu kutokana na lugha yao na mila zao zinazolingana na lugha na desturi za watu wa Indonesia. Wenyewe hawana kumbukumbu. -- Makabila ya Norway walifaulu kufika Greenland na Kanada mn. mw. 900 b.K. lakini hata mawasiliano haya yamevunjika na kusahauliwa baadaye.

Wenyeji wote wa Marekani ("Wahindi Wekundu") ni watoto wa makabila waliohama kwa miguu kutoka Asia. Lakini mawasiliano haya hayakujulikana kwa watu wengine, na hata yalisahauliwa baadaye mara kwa mara.

Kuhusu (3.5.) Ethiopia na Nubia

Wahariri wa Agano Jipya (Toleo la Kiswahili cha kisasa) walitafsiri "Ethiopia" badala ya Kushi. Wamefuata mfano wa tafsiri mbalimbali katika Ulaya waliotumia jina linalojulikana yaani Ethiopia badala ya jina lisilojulikana yaani Kushi. Lakini kihistoria ni kosa kwani Kushi na Ethiopia (au Uhabeshi) zilikuwa nchi mbili jirani.

Kuhusu (4.1.) MAISHA BAADA YA KIFO: mawazo ya kipagani na imani ya kikristo

Karibu imani zote za kimila zinategemea aina fulani ya maisha baada ya kifo. Wamisri wa Kale waliamini ya kwamba maisha baada ya kifo italingana na maisha ya sasa. Hapo ndipo sababu za kujenga makaburi makubwa walipoweka akiba za chakula, nguo, silaha na vifaa ili marehemu apate haya yote anayostahili kutokana na cheo chake. -- Katika imani za makabila mbalimbali ya kiafrika (lakini pia watu wa kale wa Ulaya) mkubwa alipaswa kwenda na watumishi au wake hivyo waliuawa na kuzikwa pamoja na chifu (au mfalme). Wanyiha wa eneo la Mbozi walisema "Chifu anahitaji kiti kaburini" walimzika kijana naye. -- Kiini cha imani hizo ni ya kwamba hakuna tofauti ya kimsingi ya hali ya mtu kabla na baada ya kifo. Kumbe katika jamii zilizobagua sana tabaka mbalimbali ndani ya umma imani za kijadi hazikuwa na faraja sana kwa watu wa chini kwani wangeendelea kuwa wakulima au labda watumwa hata baada ya kifo. Hapo ndipo sababu muhimu ya kwamba mafundisho ya Ukristo yaliwavuta hasa watumwa na maskini. Matumaini ya kikristo yaliwapa faraja kubwa ya kwamba hata kama maisha haya ni mabaya yatakuwa tofauti kwa Mungu katika maisha ya milele.

Kuhusu (4.3.) MAGAWANYIKO NDANI YA KANISA LA ORTHODOKSI

(Kutokea kwa makanisa ya kitaifa ya Misri, Siria na Uajemi)

Kanisa la Kiorthodoksi katika Mashariki lilikuwa chini ya ulezi wa serikali ya Bizanti. Hali hiyo ilisababisha mafarakano hasa katika nchi za Shamu (Siria) na Misri.

Katika vitabu vya historia vya Ulaya mafarakano haya mara nyingi huitwa "Ki-monofisiti" au "Ki-nestorio". Lakini makanisa yaliyotokana na matukio haya yenyewe hayakubali majina haya wala hayakubali maelezo yaliyotolewa na makanisa ya Kiorthodoksi au Kikatoliki (pamoja na wanahistoria wengi wa kiprotestant wanaofuata maelezo ya babu zao wakatoliki). Maelezo yafuatayo yanaeleza mafarakano haya kihistoria bila kuweka mkazo mkubwa kwenye tofauti za mafundisho yaliyochukuliwa zamani kueleza tofauti zilizopo. Makanisa yaliyotokea katika mafarakano ya karne ya tano yataitwa makanisa ya "kitaifa" (Oriental National Churches) na siku hizi mabingwa walio wengi hukubali ya kwamba tofauti za kiutamaduni na kitaifa zilikuwa za kimsingi. Maswali ya mafundisho yaliyojadiliwa ni muhimu mpaka leo hii lakini hayakuwa sababu kuu ya farakano.

Nchi hizo zilikuwa na mchanganyiko wa watu. Kiasili kila nchi ilikuwa na utamaduni wake tangu muda mrefu. Wakazi wa miji walitumia lugha ya kigiriki wakijisikia kama raia ya Dola la Roma, lakini watu wadogo vijijini walio wengi walijisikia kama Wamisri au Wasiria wakitumia lugha zao za asili. Wakati Dola la Roma liligawanyika matatizo ya kiuchumi na kisiasa yaliongezeka. Vita vingi vikasababisha kukua kwa mzigo wa kodi hasa kwa ajili ya wakulima. Wenyeji walianza kujisikia vibaya kuwa wanagandamizwa na kunyonywa. Wakaanza kuangalia serikali kuu kama utawala wa mabavu wa kikoloni wakaanza kupinga. Mara nyingi maaskofu wa nchi hizo walisimama upande wa wananchi wao. Kwa sababu kanisa rasmi lilikuwa chini ya usimamizi wa serikali ya Kaisari kule Bizanti heshima aliyopewa Patriarka (Askofu Mkuu wa Bizanti) ilipungua machoni pa Wamisri.

Matatizo haya ya kisiasa yalichanganywa na matatizo ya kutoelewana juu ya maswali ya mafundisho ya imani. Katika karne ya nne na tano Kanisa lilijitahidi sana kueleza vema tabia ya kimungu na tabia ya kibinadamu ndani ya Yesu Kristo. Jitihada hizo zinaonekana za ajabu machoni petu leo hii. Lakini zilikuwa muhimu kwa sababu dini mbalimbali katika mazingira ya Ukristo ziliweza kutumia maneno na mafundisho yaliyofanana kiasi na maelezo ya Biblia lakini kwa maana nyingine. Kumbe wakristo wengine walianza kuchanganya dini hizo. Katika mitaguso (mikutano ya maaskofu) kanisa lilifanya maazimio jinsi gani kufundisha sawa.

Katika Mtaguso wa Kalsedoni mw. 451 maaskofu walijadili mafundisho juu ya swali jinsi gani Kristo alikuwa Mungu na mwanadamu wakati uleule. Labda tunaweza kushangaa jinsi gani katika swali la aina hiyo wakristo wanaweza kugongana vibaya mpaka kuuana. Lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa. Juu ya matumizi ya maneno ya maelezo haya farakano lilitokea. Likawa vibaya zaidi kwani serikali ilidai mkutano utamke kwa namna fulani. Azimio hilo likatumika kumpindua Askofu Mkuu wa Alexandria ikiwa Mtaguso ulimwondoa madarakani. Tukio hili liliwasha moto katika Misri, pamoja na Siria, hasa kwa sababu Kaisari mwenyewe alijiingiza katika majadiliano. Maazimio ya mtaguso yalikataliwa katika sehemu kubwa ya makanisa ya Misri na Siria, pia kule Armenia.

Kumbe matokeo yake ni farakano kati ya Kanisa la Kiorthodoksi linaloitwa pia "Kigiriki" na makanisa ya kitaifa ya Misri, Siria na Armenia. Matatizo ya aina hiyo yalisukuma pia kutengana kati ya Kanisa la Uajemi na Kanisa la Kiorthodoks. Kumbe tangu wakati ule wamisri wenyeji wa Misri huitwa "Monofisiti" walitetea "fisia" au "maumbile moja" katika Kristo. Lakini tatizo kubwa lilikuwa kutokea kwa tofauti zilizotajwa tayari.

Kuhusu (4.3.) FARAKANO MASHARIKI - MAGHARIBI NA SWALI LA KIPAUMBELE KATI YA MAKANISA

Swali la kipaumbele kati ya maaskofu lilileta matatizo kwa muda mrefu.. Kanisa la Kale lilikuwa mwanzoni na majimbo makuu matatu: Alexandria (Afrika) Antiokia (Asia), Roma (Ulaya); tangu 381 Bizanti iliongezeka ambayo ilikuwa tangu Konstantino makao makuu ya Dola la Roma lilipoanza kutawaliwa na makaisari wakristo. Maaskofu wa miji hii waliitwa "Patriarka" walikuwa kama viongozi wa maaskofu katika maeneo yao. Baadaye Askofu wa Yerusalemu alipewa cheo hiki kwa heshima ya kumbukumbu ya mahali alipoiishi Bw. Yesu. Kumbe hawa ndio mapatriarka watano wa Kanisa la Kale. Walioshindana hasa walikuwa maaskofu wa Roma na Bizanti. Roma iliheshimiwa kama mji mkuu wa Dola la Roma na mahali walipokufa mitume Petro na Paulo. Bizanti (Konstantinopoli) iliheshimiwa kama "Roma mpya" kwa sababu makaisari kuanzia Konstantino. Mtawala wa Bizanti alikuwa peke yake na Cheo cha "Kaisari wa Roma" baada ya mwisho wa Ukaisari kule Roma mw. 476.

Kumbe Mtaguso wa Chalcedon mw. 451 ulitamka ya kuwa mapatriarka wa Bizanti na Roma wanastahili kupewa heshima ileile kwa sababu wako ngazi moja. --Baadaye maaskofu wa Bizanti na Roma waliendelea mara kwa mara kuvutana juu ya kipaumbele. Farakano la 1054 lilitokea juu ya kuvutana nani atawale kikanisa maeneo ya Italia ya Kusini. Lakini kabla ya farakano kutokea sehemu zote mbili zilikwisha kuwa na maendeleo ya karne nyingi iliyoongeza tofauti za kiutamaduni kati ya Mashariki na Magharibi. Kidogo tunapata picha ya nguvu za tofauti hizo tukisikia habari za siku hizi juu ya kupasuliwa kwa Yugoslavia. Mstari wa ugawaji wa nchi hiyo inafuata mstari wa ugawaji uliotolewa miaka 1500 kati ya Roma ya Magharibi na Mashariki. Majimbo ya Wasloveni na Wakroati mpaka leo ni kikatoliki, maeneo ya Waserbia ni ya kiorthodoksi. Kumbe mstari uliochorwa muda mrefu uliopita umesababisha kutokea kwa tofauti zinazoweza kupasua nchi ya siku zetu. Sababu zilizotajwa wakati ule zilihusu kwa jumla mambo ambayo hayaeleweki kwetu rahisi siku hizi, kama vile tofauti juu ya siku za kufunga, swali la kutumia mikate iliyochachuka au isiyochachuka wakati wa Ekaristia, utaratibu wa kuimba Halleluja, ndoa ya mapadre, na swali moja la imani yaani kama Roho Mtakatifu anatoka kwa Mungu Baba au kama anatoka pamoja kutoka kwa Baba na Mwana.

Kuhusu (4.4.) Uislamu

Uislamu ulienea haraka sana kwa njia ya nguvu ya kijeshi katika nchi zilizokuwa na wakristo wengi. Sababu muhimu ya udhaifu wa Wakristo hawa Waorthodoksi ilikuwa mafarakano kati yao, na hasa majaribio ya serikali ya Bizanti kuwalazimisha wakristo wote kufuata uongozi wake. Kwa upande wa serikali ilikuwa majaribio ya kuitumia na kuitawala dini kama nguzo ya siasa yake. Lakini mambo ya imani hayafai kulazimishwa.

Hivyo wakristo katika nchi kama Misri waliotafuta uhuru wa kisiasa walilazimishwa chini ya Askofu wa Bizanti, wakajisikia wanagandamizwa kidini pia si kisiasa tu. Walipofika Waarabu Waislamu walikaribishwa mahali pengi kuwa wakombozi wanaomaliza utawala wa kidikteta. Waliwaahidi vikundi vyote vya wakristo uhuru wa kidini.

Ahadi hii ilitimizwa kwa namna tofauti. Kwa upande mmoja wakristo wote waliona ubaguzi mbele ya waislamu, wakilazimishwa kulipa kodi za nyongeza, wakikataliwa kujitetea mahakamani dhidi ya mwaislamu n.k. Mara kwa mara yalijitokeza matendo mabaya kwa upande wa watawala na wakubwa; makanisa yalibomolewa, wakristo kutozwa kodi kali za nyongeza n.k. Kwa mfano misikiti kuu ya Dameski (Siria) ilikuwa zamani kanisa la Mt. Yohane. Mwanzoni waarabu waliahidi kuiheshimu, lakini mtawala alifuata alitaka jengo kubwa lililopatikana mjini kwa ajili ya ibada yake. Hivyo ndivyo ilivyotokea Waturuki walipoteka Konstantinopoli. Kanisa Kuu la Hagia Sofia (Hekima Mtakatifu) limegeuka kuwa misikiti.

Lakini waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi zilivunjika, lakini mahali pengi wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya waislamu. Maisha haya yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza). Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile Kigiriki-Orthodoksi, Kikopti (Misri), Kisiria-Orthodoksi, Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Sababu kuu ni ya kwamba kama Mkristo amekuwa mwislamu - hakuweza kurudi tena. Sheria ya kiislamu inamruhusu mkristo kugeuka kuwa mwislamu, lakini mtu aliyekuwa mwislamu anastahili ahdabu ya mauti akigeukia Ukristo au dini nyingine. pamoja na hayo wakristo walianza kuhamia nchi ambako wangekuwa raia huru bila kasoro.

Lakini kwa namna fulani Uislamu unastahili sifa. Inatosha kulinganisha hali ya Waislamu kule Hispania. Sehemu kubwa ya Hispania ilikuwa miaka mamia chini ya utawala wa Waarabu waislamu. Katika vita vingi Wahispania waliteka nchi tena. Mwaka 1492 mfalme wa mwisho mwislamu alishindwa. Waislamu wakaishi chini ya utawala wa Wahispania wakatoliki. Lakini miaka michache baadaye waislamu wote walilazimishwa wapokee ubatizo, wengine waliuawa au kufukuzwa. Bila shaka haya ni matokeo ya hali ya vita kati ya Waislamu na Wakristo. Wahispania walionyesha tabia zinazofanana na zile za Wamongolia waislamu walioharibu makanisa yote ya Asia ya kati. Kumbe historia inaonyesha ya kwamba giza ipo hata kwa upande wa Wakristo. Hakuna sababu ya kujisifu kuliko wenzetu waislamu.

Kuhusu (5.1.4.) MASALIO

Tokeo mojawapo la uhaba huu wa elimu katika Ulaya ya Karne za Kati lilikuwa kutathmini sana masalio (=mabaki ya maiti ya watakatifu). Ilikuwa desturi tangu kale kukumbuka makaburi wa Wakristo wale wa kwanza waliokufa kwa ajili ya imani yao. Makanisa mengi yalijengwa penye makaburi haya. Baadaye ilikuwa desturi kuchukua kipande cha maiti ya Mtakatifu na kuiweka chini ya altari ya kanisa jipya pasipo na kaburi la aina hii. Desturi hii ilisaidia kutunza kumbukumbu ya mfano mzuri aliounyesha. Lakini ilisababisha pia Wakristo wasio na elimu kufikiri ya kwamba nguvu ya ibada inategemea idadi ya masalio mahali pa kanisa. Imani hii ilisababisha hata biashara ya masalio. Askofu na Wakristo wa sehemu moja waliona afadhali wapate masalio ya Mtakatifu hasa mwenye sifa nyingi. Askofu wa sehemu nyingine aliweza kuwasaidia ikiwa alikuwa na kaburi la Mtakatifu, kwa mfano kwa njia ya kutenga mkono, mguu au kidole na kuvitoa viungu hivi. Kutokana na desturi hii walijitokeza wafanyabiashara wa masalio. Baada ya muda fulani vipande vyovyote vya maiti ya watakatifu viliuzwa na kununuliwa. Matajiri walianza kukusanya masalio kibinafsi. Si ajabu ya kwamba baadaye masalio ya uongo yalipatikana. Wakati wa karne ya 16. biashara ya masalio imekuwa tayari kichekesho kwa wenye elimu. Lakini wakristo wa kawaida waliamini wakanunua. Kumbe uliweza kuona vidole vya Mtakatifu fulani mahali ishirini ingawa hata huyu alikuwa na vidole kumi tu. Uliweza kuona mahali panne mguu wa mtume fulani. Walionyesha vipande vya msalaba wa Yesu lakini wataalamu walipiga hesabu ya kwamba ukijumlisha vipande vyote hata umeshapata msitu si msalaba mmoja tu. Kumbe watapeli walichukua kipande chochote cha kuni na kukitangaza kimetoka Yerusalemu na kukiuza ndicho kipande cha msalaba wa Yesu. Waliweza kuiba kipande cha maiti yoyote makaburini halafu kukikausha na kukiuza kuwa ni kipande cha maiti ya Mtume Petro au Luka. Mtawala mmoja mjerumani aliyeishi mnamo mwaka 1520 alikuwa na masalio ya aina hii 25.000 aliyoyanunua akiamini yote ni ya kweli ! (Mkusanyiko mkubwa ulikuwa na thamani sana kifedha maana yake ilikuwa ghali kuyanunua masalia mengi hivi. Kumbe mtawala huyu alikuwa mkabaila wa jimbo la Saksonia aliyekuwa mwajiri wa Martin Luther kama profesa wa Chuo Kikuu cha Wittemberg. Jinsi alivyomlinda Profesa yake Luther dhidi ya mashambulio ya Papa na Mfalme alipaswa kuona jinsi gani thamani ya mkusanyiko wake ilivyoshuka chini kwani watu wengi hawakuamini tena ukweli wa masalio haya.)

Watu walikuwa tayari kuamini mengi sana mpaka kupokea nywele za Bwana Yesu (zilizokatwa akiwa mtoto mdogo), au neppi zake; hata vipande vilionyeshwa vilivyokatwa kwenye kucha zake. Kilele ni kipande cha ngozi cha uume wa mtoto Yesu kilichokatwa wakati wa tohara yake. Kipande hiki kilionyeshwa mahali patano. Imani ya masalio ilikuwa na nguvu sana tangu karne nyingi. Wafanyabiashara kutoka Venice (Italia) waliiba Kichwa cha maiti ya Marko katika kaburi lake kule Alexandria na kukipeleka kwao. Pale Kanisa kubwa la Marko Mtakatifu lilijengwa linasimama mpaka leo. Wenyeji waliamini ya kwamba ulinzi wa Mt. Marko ulitegemea sana kuwepo kwa kichwa chake.

Wataalamu wanaona ya kwamba imani hizo ni alama ya kuingiliana kwa Ukristo na mawazo ya kipagani ya kale.

Lakini hata leo "masalia" ya namna fulani yanajitokeza. Magazeti yatoa wakati mwingine taarifa ya kuwa pale London au Marekani suruali, viatu, gita, nguo au kiti alipokalia "star" (mbingwa) mrehemu fulani wa sinema au musiki vimeuzwa kwa bei kubwa sana. Wanaonunua ndio watu waliompenda mbingwa huyu sasa wako tayari kutoa pesa nyingi kuwa na kumbukumbu ya mali yake.

Kuhusu (5.1.1.) MADAI YA KISIASA YA MAPAPA

Mafundisho ya Papa Gregorio VII mw. 1075:

1. Ndiye Mungu peke yake aliyeunda kanisa la kiroma

2. Papa wa Roma peke yake ana haki kuitwa Papa wa dunia

3. Yeye peke yake ana haki ya kuteua maaskofu na kuwaondoa madrakani ......

9. Watawala wote hupaswa kubusu miguu ya Papa tu.

12. Papa anaweza kumwondoa Kaisari madarakani.

19. Hakuna mtu anayeweza kumhukumu.

(SSO I, 107)

Papa Innosenti III (barua)

Jinsi Mungu alivyoumba mianga miwili, ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawala usiku , vivyo hivyo alivyoteua watawala wawili wakuu katika Kanisa la Katoliki. Mmoja mkubwa juu ya roho na mmoja wa chini juu ya miili vinavyohusiana kama mchana na usiku. Haya ndiyo mamalaka za Papa na Mfalme. Jinsi gani mwezi unavyopokea mwanga wake kutoka kwa jua vivyo hivyo mamlaka ya Mfalme yanapokea mn'garo wake kutoka kwa mamlaka ya Papa. (SSO I, 109)

Kuhusu (6.2.) Martin Luther

Vyeti vya rehema

Waandishi wa kiprotestant wamezoea mara nyingi lugha "Vyeti vya msamaha". Lakini theologia ya kikatoliki inatumia kwa Kiswahili neno "rehema" badala ya "msamaha". Hatuna budi kufuata uzoefu wa mwenye mafundisho haya.

Asili ya uzoefu unaotofautiana kati ya waandishi waprotestant ni bila shaka juhudi la kutafsiri neno la "Indulgences / Ablaß" bila kufahamu jinsi kanisa la katoliki lenyewe lilivyotafsiri katika Kiswahili. --

Inafaa kukumbuka hapa ya kwamba leo hii mafundisho ya "rehema (=indulgences)" hayapewi uzito sana katika theologia ya kikatoliki. Katika Kiswahili zipo nakala za katekesimo mbalimbali zinazorudia mafundisho juu ya rehema lakini ni tafsiri za matoleo ya miaka ya nyuma. Kwa bahati mbaya Katekesimo mpya iliyotolewa Roma 1992 haikupatikana bado kwetu ili tuweze kuona kama mafundisho haya yaliyogawa Ukristo karne 4 zilizopita yameonekana tena na kwa namna gani.

Kuhusu (6.2.) Ndoa ya Luther

Alizaa watoto na mke wake. - Tukisikia vijana wengine wanaodai eti hawawezi kusubiri mpaka kuoa wakiogopa ya kwamba nguvu za kuzaa zitakauka - basi Martin Luther ni mfano mmoja tu wa kihistoria (wasipopenda kusikia sayansi) ya kwamba mtu aliyeishi maisha ya utawa anaanza kuzaa hata katika umri wa miaka zaidi ya arobaini.

Kuhusu (6.3.) Mafundisho ya Martin Luther na kutengeneza kanisa upya

Wengine husema ya kwamba Luther aliangusha uaskofu katika kanisa badala yake aliunda utawala wa wataalamu.

Tukiona leo hii katika makanisa yanayoitwa "kiluteri" ya mazingira yetu ya kwamba cheo cha Askofu kina uzito mkubwa si mapokeo ya "kiluteri", angalau si ya Martin Luther. Yeye mwenyewe hakujali vyeo.

Sababu yake ni kihistoria: makanisa ya kiluteri ya Tanzania yalianzishwa na wamisionari kutoka Ujerumani ambao hawakufahamu cheo cha Askofu kutoka kwao nyumbani. Hivyo makanisa ya Waluteri yalianzishwa katika muundo ya "Sinodi", yaani kanisa linaloongozwa na wawakilishi wa shirika zake (wachungaji na walei) chini ya mwenyekiti anayechaguliwa. --

Kutokana na kufukuzwa kwa wamisionari wajerumani wakati wa vita 1914/18 na 1939/45 wamisionari waluteri kutoka Sweden na Marekani walifika kusaidia. Kumbe katika Sweden Kanisa la Kiluteri lilitunza cheo cha Askofu (taz.7.2.). Vilevile mafundisho ya "mfuatano wa mitume" yaliweza kuingia katika kanisa la kiluteri la Sweden na warithi wake katika Marekani. Sehemu kubwa ya wataalamu wa kiprotestant (nje ya mapokeo ya "High Church" ya kianglikana na kiluteri) haiamini kuwepo kwa kitu kama hicho tangu siku za mitume wa Yesu. --

Kama mgeni anaweza kuruhusiwa kutaja yale yanayoonekana kwake: sehemu hiyo ya mapokeo ya Uluteri ya "High Church" ilikuwa na nguvu katika mazingira ya Tanzania. Matokeo yake ni kugeuka kwa masinodi kuwa madaiosisi, kutumia alama za nje kama vile Kofia na nguo ya pekee, fimbo n.k. ---

Hata maaskofu wa Kimoravian wameanza katika mazingira yetu kutumia mapambo kama msalaba kuwa alama ya cheo cha uaskofu --

Kwa bahati mbaya mwandishi hana ujuzi wa kutosha kufanya utathmini wa kutokea kwa cheo cha Askofu kati ya madhehebu kama vile Pentekoste, Baptist n.k. ambayo kiasili hayana kitu hicho. --

Bila shaka waandishi wenyeji watatoa maelezo jinsi gani mabadiliko haya yanaongozana labda na utamaduni na mazingira kwa upande mmoja, na pia jinsi gani mabadiliko haya yanaweza kupatanishwa na urithi wa kiprotestant.

Kuhusu (7 sura ya saba mwanzoni) - neno "katoliki"

Tukitaka kutumia maneno haya kikamilifu sana tunapaswa kukumbuka ya kuwa: Kiroma-Katholiki humaanisha sehemu tu ya kanisa chini ya Papa inayotumia utaratibu wa kiroma kwa ajili ya ibada zake; yapo makanisa ambayo hukubali pia uongozi wa Papa au Askofu wa Roma lakini hutumia taratibu za mapokeo ya kiorthodoksi, kama vile kikopti-katoliki, kigiriki-katoliki, kiethiopia-katoliki. Mapadre wa makanisa haya wanaweza kuoa kama mapadre waorthodoksi (lakini si maaskofu wao). Asili ya makanisa haya ni katika majaribio ya kuunganisha makanisa ya kiorthodoksi na Roma; kwa kawaida majaribio hayakufaulu yaliwavuta maaskofu wachache pamoja na wakristo wachache. Maaskofu hawa walipewa na Roma cheo cha Patriarka cha Aleksandria au Antiokia n.k. kwa kushindana na Mapatriarka wa makanisa ya kale. Lakini zipo nchi kadhaa ambako wakristo wengi kidogo wa mapokeo ya kiorthodoksi hufuata uongozi wa Papa kama kule Lebanon, pia Wakristo wengi kule Iraq na wengi kidogo katika nchi ya Ukraine. Katika nchi hizo yapo makanisa mbalimbali ya katoliki kandokando, kwa mfano Misri Kanisa la Kikopti-Katoliki, kigiriki-katoliki na Kiroma-Katoliki (wanoitwa pia: kilatini). Mapadre wakatoliki wa mapokeo ya kikopti na kigiriki wanaweza kuoa na huendesha misa katika taratibu zao za kale; mapadre waroma-katoliki hawawezi kuoa na hufuata liturgia ya kiroma. Wote hukubali uongozi wa papa hawashindani yaani wengine wanahudumia wakristo wa mapokeo ya kikopti, wengine wa mapokeo ya kigiriki na waroma-katoliki wanaangalia mara nyingi wakristo wakatoliki kutoka kwa nchi zingine wanaokaa kule Misri.

Kuhusu (7.4.) Umoja wa Ndugu (Wamoravian)

Katekesimo ya Martin Luther inakubaliwa katika Kanisa la Moravian kuwa kitabu cha mafundisho halali.

Kuhusu Milango ya tisa na ya kumi kwa jumla

sura hizi mbili ziko katika umbo fupi tu kutokana na matatizo yaliyoelezwa awali. Lakini sehemu ya Sura ya Tisa kwa kirefu inafuata katika nyongeza kuhusu utumwa

Kuhusu (9. 3.) Utumwa na kanisa kabla ya karne ya 19

Tangu muda mrefu utumwa ulikuwa utaratibu wa kijamii katika sehemu nyingi za dunia. Habari za kwanza za kimaandishi juu ya Afrika ya Mashariki karne 2 k.K. zilisema: "wanaleta kutoka pwani lile ndovu, dhahabu na watumwa". Kule Ulaya kipo kikundi cha mataifa kinachoitwa tangu zamani "Waslavi" (Slavonic Nations), kama vile Warusi, Wapoland, Wayugoslavia. Kumbe neno "slavi" kiasili linamaanisha "watumwa" : watu wa mataifa yale walikamatwa zamani na kuuzwa kama watumwa katika sehemu nyingine za Ulaya na Asia (na pia Afrika ya Kaskazini).

Sisi tumejifunza ya kwamba ni hali mbaya sana hailingani kabisa na utu na heshima ya kibinadamu. Utumwa haupatani na Ukristo. Lakini watu walioishi zamani katika mazingira penye utumwa waliozoea hali hiyo. Mara nyingi mtu aliweza kuwa mtumwa akiwa na madeni makubwa na hawezi kulipa.

BIBLIA NA UTUMWA

Habari za watumwa tunaweza kusoma hata katika Biblia. Ilikuwa jambo la kawaida katika mazingira ya Israeli ya Kale. Mtu aliweza kukamatwa na kuuzwa utumwani ili kulipia madeni yake. Mara nyingi watumwa walikuwa watu waliokamatwa vitani. Kwa mfano wakazi wote wa Yerusalemu walifanywa watumwa baada ya mji huu kutekwa na wanajeshi Waroma mwaka 70 b.K.. Wakati wa Biblia asilimia mn. 20 za wakazi wa Dola la Roma walikuwa watumwa. Lakini katika nchi ya Israeli hali ilikuwa tofauti. Sheria ya Musa ilimwacha mtumwa awe huru baada ya miaka 7 (Kut. 21.2). Kwa sababu hiyo hawakuwapo watumwa wengi katika Israeli. Labda hapo ndipo sababu ya kwamba Yesu hakufundisha juu ya utumwa kwani walikuwa wachache sana katika mazingira yake.

Mtume Paulo aliishi nje ya eneo la Israeli. Katika miji mikubwa kama Korintho, Antiokia, Efeso au Roma watumwa walikuwa wengi. Paulo alifundisha kuwa ni wajibu wa mabwana wakristo kuwatendea watumwa wao vizuri. Kwa nini hajapinga utumwa ? Wataalamu wengi huona ya kwamba Paulo alitegemea kurudi kwake Yesu na mwisho wa dunia karibuni sana hivyo hakuona umuhimu kubadilisha utaratibu wa kijamii. Lakini alisititiza ya kwamba ndani ya kanisa ni marufuku kutofautisha kati ya watumwa na walio huru.Ukristo uliweza kuwavuta watumwa wengi, kwani hapa walikubaliwa kuwa watu wenye utu na heshima kamili. Wapinzani wa Ukristo waliuita kuwa "Dini ya watumwa". Mtumwa mmoja alichaguliwa kuwa Askofu wa Roma. Kanisa la Katoliki linamkumbuka kama Papa Silvesta.

Baada ya uenezaji wa Ukristo utumwa ulipungua sana katika Ulaya. Mabadiliko ya uchumi yaliondoa faida ya kutumia watumwa. Vilevile walimu wengi wakristo walipinga utumwa wenyewe.

Katika Asia na Afrika ya Kaskazini utumwa uliendelea kwa jumla mpaka karne iliyopita au mwanzo wa karne hii ya 20. Uislamu ulikubali utumwa. Lakini waislamu walifundishwa mashariti fulani kama kuwatendea watumwa vizuri. Walifundishwa pia ya kwamba ni tendo njema mbele ya Mungu (Allah) kumwacha mtumwa awe huru.

UKOLONI WA MAREKANI NA KUTOKEA KWA UTUMWA MPYA

Hali hii ilibadilika baada ya kuanzishwa kwa ukoloni kule Marekani. Wareno na Wahispania walioteka nchi hizo walivutwa na tamaa ya dhahabu. Mataifa ya Ualya yalipeleka mara kwa mara wakazi wa magereza yao ng'ambo kwa nia ya kusafisha jamii zao na kupunguza gharama za magereza. Watu waliona kule mbali hawawezi kusababisha hasara. Kumbe hawakujali hali ya wenyeji walioteswa na wale wakorofi walioona nafasi ya kujitayarisha. Hata maafisa wa serikali za kikoloni walishindwa kuwatawala vizuri kwani waliwategemea katika kuwatawala wenyeji ambao hawakunyamaza kwa hiari. Hapo ndipo wamisionari wa kanisa walijitahidi kupakana ukorofi uliokuwepo. lakini kiasi jinsi mapato kutoka makoloni yalivyokuwa muhimu kwa ajili ya makisio ya serikali za Ulaya haikuwa rahisi kupakana unyonyaji kule katika makoloni ya mbali.

Rasmi kanisa la kikatoliki wakati ule halikukubali biashara ya watumwa. Lakini Mapapa waliona hawana nguvu ya kuzuia biashara hiyo. Walijaribu zaidi kuweka mashariti jinsi ya kuwatendea watumwa. Mataifa kadhaa yalifuata mafundisho ya kanisa. Kwa mfano Hispania na Ufaransa vilikataa kuwepo kwa soko la watumwa katika nchi hizo lakini walifunga macho ikiwa raia wao wakiendesha biashara ya watumwa nje ya mipaka yao. Wengine kama Wareno hawakuona tatizo la kufanya biashara ya watumwa. Watumwa wa kwanza kutoka Afrika waliingia Ureno wakati Mfalme wa Ureno alipokubali kupokea idadi ya watumwa kama malipo ya madeni kutoka waarabu wa Morocco. Wapelelezi wareno walioanza kuzunguka pwani za Afrika walileta tena na tena wafungwa kama watumwa. Lakini mpaka wakati ule walikuwa wachache kwani soko kule Ulaya lilikuwa dogo. Lakini baada ya kuanzishwa kwa ukoloni kule Marekani watumwa walitafutwa sana kwa ajili ya mashamba makubwa na kuchimba madini pale. Kumbe ukoloni kule Marekani ulisababisha kukua kwa mahitaji ya watumwa. Hapo ndipo utaratibu wa kale wa utumwa ulipanuka kuwa mbaya sana kuliko nyakati zote za kabla. Mamilioni mengi ya Waafrika waliuawa katika vita vya kukamata watumwa na mamilioni wakapelekwa kama wafungwa kule Marekani.

Kumbe ulikuwa mvurugo uleule ulioharibu jamii nyingi za kiafrika uliosababisha vilevile uharibifu wa misioni ya kikristo katika karne za 16 - 18. Si ajabu ya kwamba Waafrika walishindwa kutambua tofauti kati ya wamsionari wareno au wahispania upande mmoja na wafanyabiashara wa watumwa kutoka mataifa yaleyale. Uharibifu wa taratibu za kijamii ulikuwa mbaya zaidi katika eneo la pwani yaani kulekule walipoingia wamisionari. Tena hali ilikuwa vibaya zaidi kutokana na wamisonari wale waliojiingiza katika mambo ya utumwa walivyofanya wengine.

Kuhusu (9.3.) Wakristo walianza kupinga utumwa

Mwanzoni awamu jipya la utumwa halikuonekana kwa watu wengi kule Ulaya maana uliendeshwa kule Afrika na Marekani hasa. Lakini habari zake zilienea. Mara walijitokeza wengine waliopinga utumwa au waliojaribu kupakana nguvu yake. Lakini wakati ule hata wakulima wengi katika nchi mbalimbali za Ulaya hawakuwa watu huru.(ingawa sio watumwa). Katika karne ya 17 dhehebu la kikristo la "Marafiki" (waliitwa pia "Quaker") kule Uingereza waliamua ya kwamba haipatani na Ukristo kuwa na watumwa na mwenye watumwa anajitenga katika dhehebu lao. Wakitangulia hivyo baadaye Wakristo wengine wakajiunga nao polepole. Kule Uingereza ulijitokeza mwendo wa kuondoa utumwa ("to abolish - The Abolitionist movement) Mwaka 17... wakristo wa mwendo huo walimshtaki mlowezi mmoja mwingereza kutoka Visiwa vya Caribbean aliyetembelea Uingereza pamoja na mtumwa. Hakimu aliamuru ya kwamba si halali kuwa na watumwa katika eneo la Uingereza. Wapinzani wa utumwa wakaendelea kusukuma katika Bunge la Uingereza. Lakini matajiri wa Liverpool (waliofaidika na utumwa kama wenye meli au kwa sababu waliendesha biashara ya watumwa wenyewe) walitetea vikali hali halisi. Katika karne ya 19 polepole utumwa na biashara ya watumwa vilikomeshwa. Kwa jumla ni aibu kubwa katika Ukristo ya kwamba wakristo wengi walitumia muda mrefu mno kutambua ya kwamba Kristo na utumwa havipatani.

Tuliona ya kwamba magawanyiko ndani ya kanisa ilikuwa jambo la kusikitika sana. Kumbe hapa tumepata mfano jinsi Mungu alivyotumia kutokea kwa vikundi vidogo vidogo ndani ya Kanisa kuwa njia ya kuwaelimisha Wakristo wote. Maana makanisa makubwa yalikuwa karibu mno na serikali na matajiri yalikosa nguvu ya kupinga utumwa kikali. Ni Wakristo wa makanisa madogo kama Marafiki (Quaker) au Wamethodist waliotangulia na kuwasaidia Wakatoliki, Waanglikana na Wareformed kutambua ukweli.

Hali nyingine iliyosaidia kukomeshwa kwa utumwa ni mabadiliko ya kiuchumi. Uchumi mpya wa ubepari ulibadilisha mkazo ndani ya jamii mbalimbali. Kumbe sio tena wafanyabiashara wa "Biashara kati ya Marekani, Ulaya na Africa"[?] (Triangular trade) waliokuwa na pesa nyingi (na hivyo na athari) katika jamii ya Uingereza. Ni mabepari walioendesha viwanda wakitumia wafanyakazi huru na wasiotegemea watumwa ambao walipata uzito zaidi katika jamii. Umuhimu wa kazi ya watumwa ulipungua sana kutokana na njia mpya za kuzalisha mali.

Kuhusu (9.4.) Mwanzo wa Misioni ya Kiprotestant

Katika kijiji kidogo cha Herrnhut kule Ujerumani waliishi wakimbizi wamoravia waliopewa ustahimilivu kuanzisha upya ushirikia wa Umoja wa Ndugu kufuatana na urithi wao kutoka Moravia / Cekoslovakia. Walikuwa watu wa kawaida kama wakulima na mafundi. Siku moja katika mwaka 1732 walikutana na mgeni kutoka Denmark. Huyu mgeni kwa jina Anton alikuwa mtumishi wa Bwana Mkubwa Mdenmark aliyemtembelea Mkuu wa Herrnhut, Ludwig von Zinzendorf. Anton alikuwa mtumwa wa asili ya kiafrika aliyenunuliwa kule Visiwa vya Westindies na Bwana wake. Baadaye akapewa uhuru wake akasafiri pamoja na Bwana wake kule Denmark. Kutoka Anton Ndugu wa Herrnhut wakasikia mara ya kwanza habari za hali mbaya ya watumwa waafrika kule Westindies, na jinsi gani walivyozuiliwa kusikia neno la Mungu pamoja na mateso yao mengine. Kumbe katika usiku ule ndugu wawili wakasali pamoja na asubuhi yake wakamwendea Mkuu wa Herrnhut wakamwomba wapewe rukhsa kusafiri kule St. THOMAS/Westindies ili wahubirie wale watumwa. Katika sala hiyo ya waseremala wawili ilianza kazi ya misioni ya Kanisa la Umoja wa Ndugu (Moravian) iliyokuwa kanisa la kwanza la kiinjili (kiprotestant) kupokea wajibu wa kuhubiri injili kwa wasio wakristo hasa. Baadaye Ndugu Wamoravia waliendelea kuhubiri kule Greenland, Urusi, Nicareagua, Afrika ya Kusini na kati ya Wahindi wekundu wa Marekani. Kumbe mawasiliano mapya yakaleta habari katika kila pembe ya dunia zisizosikika zamani kwa watu wengi.

Kuhusu (9.8.) Misioni katika Tanzania - Waorthodoksi

isipokuwa Wagiriki waliohamia Tanzania walijenga makanisa machache ya kiorthodoksi kule Daressalaam, Iringa, Arusha n.k..

Kuhusu ( 10.1.) Vita vya Ulaya vilisaidia kukomaa kwa kanisa la Afrika

Katika vipindi vya kufukuzwa kwa Wajerumani katika Tanganyika ieleweke ya kwamba wamisionari wachache wa mataifa mengine au madhehebu mengine walisaidia, kama vile walutheri kutoka Marekani na Skandinavia, au Wapresbiteri kutoka Malawi katika eneo la Wamoravia.

Kuhusu (10.8.) Dini zingine - Mfalme wa Ethiopia kuwasaidia Waislamu wa kwanza

Mapokeo ya kiislamu yanasema kwamba mfalme huyu aliyekuwa na jina "Negasi" aligeukia Uislamu baadaye. Lakini "Negasi" si jina, ni cheo cha wafalme wote wa Ethiopia hadi mw. 1974 (kwa kawaida huandikwa "Negus"). Halafu hakuna habari wala kumbukumbu kule Ethiopia ya kwamba mfalme yeyote wa karne zile aliacha Ukristo wake.

"Maelezo ya Dibaji" - juu ya misingi ya kitabu hicho

a. kitabu kifupi - kwa ajili ya shule za sekondari (labda itasaidia hata kwenye ngazi ya vyuo vya Biblia / Makatekista). Lugha yake inajaribu kuwa rahisi. Kwa bahati mbaya muhtasari ya Historia shuleni si pana sana, hivyo wanafunzi wetu wa sekondari hawana picha ya Historia nje ya Afrika; hata historia ya Afrika ya Kale kaskazini mwa Sahara karibu inakosekana. Kumbe Kitabu hicho kinajitahidi kutoa maelezo yasiyodai elimu ya awali. Lakini kama muhtasari wa History shuleni haibadilishwi ingekuwa afadhali kutafakari upya sehemu ya historia ya kanisa ndani ya somo la Elimu ya kikristo kwani mzigo ni mkubwa kujaza mapengo ambako hatuna msingi uliowekwa na somo la General History. Gregoire/Mcgrath ni kitabu kifupi kwa Kiswahili lakini si rahisi kukitumia nje ya Kanisa la Katoliki. Kinaweka mkazo wake hasa katika Kanisa la Kale.

b. kinatumia lugha ya Kiswahili kwani somo la dini hufundishwa kwa Kiswahili- tatizo la toleo hilo la jaribio ni ya kwamba muda haukutosha kupata ushauri wa mtaalamu wa Kiswahili. Tatizo lingine ni Kiswahili chetu cha kidhehebu katika msamiati wa kidini. Kwa jumla nilijaribu kufuata mapatano ya msamiati wa Agano Jipya (Kiswahili cha kisasa) ambacho ni kazi ya pamoja kati ya madhehebu, k.m. Wakatoliki walitoa sadaka ya "Kristu", Waprotestant walikubali "Yohane", "Roma" n.k. Mapatano haya hayakuingia bado katika uzoefu wa kila siku. Katika kutafsiri majina ya vikundi nilijitahidi kuepukana na uzoefu wa kilatini au kigiriki uliyofika katika Kiswahili kupitia Kiingereza, Kifaransa au Kiitalia cha watafsiri. Kwa mfano: Fransisko - Wafransisko (siyo Wafransiskani); Kalvin (Calvin) - kikalvin (siyo kikalvinisti); Hus - Wahus (siyo Wahusiti) . "Yohane " Hus - siyo John Hus kwani jina lake halisi ilikuwa "Jan" . Hivyo "John" ni tafsiri yake katika Kiingereza siyo katika Kiswahili ambapo umbo lake ni "Yohane". Maneno mengine yameshaingia kabisa katika Kiswahili ingawa umbo lake haliridhishi kisarufi, kwa mfano "Moravian" (Moravia - ingekuwa Wamoravia/kimoravia). Katika mifano mingine waandishi wa kitheologia wanapenda kutumia maneno ya Kiswahili cha zamani kidogo. Lakini sioni faida kuwafundisha wanafunzi wetu maneno kama "Iskenderia" au "Uhabeshi" wakitumia tayari katika shule ya msingi "Alexandria" na "Ethiopia". Kwa bahati mbaya neno zuri "Dachi" limesahauliwa (linachanganywa na "kiholanzi" /kiing. "dutch") ambalo lingesaidia sana katika historia ya mwisho wa Dola la Roma (tofauti kati ya "Wadachi" wa leo na makabila ya "Wajerumani" wa zamani - kiing. "German"-"Germanic")

Historia ya D.A. Peterson mpaka sasa ni kazi bora inayopatikana kwa Kiswahili lakini ina kasoro zake, hasa amebaki sana katika mfumo wa mapokeo ya Ulaya akipita harakaharaka kwenye historia ya Ukristo katika Misri na Uhabeshi, bila kutaja Sudan.

  • Tena inaonyesha ya kwamba imeandikwa na Mwingereza (bila shaka kurasa hizo zitamwonyesha Mjerumani hata akijaribu kujificha)

c. kwa ajili ya wanafunzi waafrika na kwa ajili ya matumizi katika Tanzania - kasoro yake bila shaka kitabu kimeandikwa na mgeni kutoka Ujerumani.

(kitabu bora kwenye soko la Tanzania ni L. Malishi lakini ameandika kwa kiingereza, tena amechukua "Ukristo katika Afrika" tu kuwa kichwa chake. Vinginevyo ameandika katika msimamo wa kiekumene ingawa zaidi kwa ajili ya wasomaji wakatoliki lakini kwenye msingi wa elimu bora juu ya misioni ya kiprotestant katika Afrika. Anastahili sifa kwa kuwa hana matatizo ya ubaguzi wa kidhehebu. Kutokana na mkazo wake hajadili matengenezo na mafarakano ya Kanisa kule Ulaya katika karne za 15/16. Kitabu hiki ambacho kinajaribu kuwasaidia wanafunzi wa madhehebu mbalimbali kujielewa katika historia yao kinajaribu kutoa muhtasari wa mazingira ya mafarakano ya kidhehebu.

d. kwa ajili ya matumizi ya Kiekumene (kimadhehebu) -

hapa ni jaribio ambalo halitaridhisha sana. Kasoro yake ilishindikana kumpata hapa mwenzangu mkatoliki aliyekuwa na nafasi kutunga kitabu chenyewe pamoja nami. Lakini kwa jumla nashukuru sana mawazo mengi niliyoyapata kutoka kwa walimu wenzangu masista na mapadre katika umoja wa walimu wa dini hapa Mbeya, hasa maneno ya Pd. Rudi Wigger juu ya muhtasari ya kwanza. Pia nilitegemea muundo wa "Christian Living Today" ambayo ni mfano bora wa ushirikiano wa kidhehebu kule Kenya/Uganda.

Azimio lingine nililofuata kutokana na msingi huo wa ekumene lilikuwa kuepukana na maneno kama "wazushi, heretiki" n.k. katika Historia ya Ukristo wa Kale Leo hii Wadonato, Wanestorio na Wamonofisiti wangeitwa "madhehebu" si "wazushi". Kwa bahati nzuri Kanisa la Katoliki limeacha kubandika majina ya aina hii tangu Vatikano II, na kati ya Wainjili desturi hiyo imeaga dunia bila kelele kubwa karne iliyopita (Katika Ungamo la Augsburg hawakusita kulani akina Donato na wengine). Lakini kwa ajabu majina haya (na labda mawazo yanayaoambatana nao) yamepata hifadhi zao katika Historia ya Kanisa la Kale (pamoja na Idara ya Historia ya Mafundisho ya Kikristo /History of Dogmatics). Natumaini ya kwamba inalingana zaidi na makumbusho kule Daressalaam tunapoonyeshwa mifupa na picha kuliko Ngorongoro ambako wanyama hutembea hai. Lakini bila shaka ina faida yake: anayependa kuchapa kiboko "wazushi" au kuwavinda anapata nafasi katika Historia ya Kale (afadhali kuliko leo hii).

Maelezo na Dibaji ya toleo la 1993

Maelezo juu ya tahijia ya majina

1. "Dibaji" - juu ya misingi ya kitabu hicho

1. kitabu kifupi - kwa ajili ya shule za sekondari (labda itasaidia hata kwenye ngazi ya vyuo vya Biblia / Makatekista). Lugha yake inajaribu kuwa rahisi. Kwa bahati mbaya muhtasari ya Historia shuleni si pana sana, hivyo wanafunzi wetu wa sekondari hawana picha ya Historia nje ya Afrika; hata historia ya Afrika ya Kale kaskazini mwa Sahara karibu inakosekana. Kumbe Kitabu hicho kinajitahidi kutoa maelezo yasiyodai elimu ya awali. Lakini kama muhtasari wa History shuleni haibadilishwi ingekuwa afadhali kutafakari upya sehemu ya historia ya kanisa ndani ya somo la Elimu ya kikristo kwani mzigo ni mkubwa kujaza mapengo ambako hatuna msingi uliowekwa na somo la General History.

Gregoire/Mcgrath ni kitabu kifupi kwa Kiswahili lakini si rahisi kukitumia nje ya Kanisa la Katoliki. Kinaweka mkazo wake hasa katika Kanisa la Kale.

2. kinatumia lugha ya Kiswahili kwani somo la dini hufundishwa kwa Kiswahili- tatizo la toleo hilo la jaribio ni ya kwamba muda haukutosha kupata ushauri wa mtaalamu wa Kiswahili. Tatizo lingine ni Kiswahili chetu cha kidhehebu katika msamiati wa kidini. Kwa jumla nilijaribu kufuata mapatano ya msamiati wa Agano Jipya (Kiswahili cha kisasa) ambacho ni kazi ya pamoja kati ya madhehebu, k.m. Wakatoliki walitoa sadaka ya "Kristu", Waprotestant walikubali "Yohane", "Roma" n.k. Mapatano haya hayakuingia bado katika uzoefu wa kila siku. Katika kutafsiri majina ya vikundi nilijitahidi kuepukana na uzoefu wa kilatini au kigiriki uliyofika katika Kiswahili kupitia Kiingereza, Kifaransa au Kiitalia cha watafsiri. Kwa mfano: Fransisko - Wafransisko (siyo Wafransiskani); Kalvin (Calvin) - kikalvin (siyo kikalvinisti); Hus - Wahus (siyo Wahusiti) . "Yohane " Hus - siyo John Hus kwani jina lake halisi ilikuwa "Jan" . Hivyo "John" ni tafsiri yake katika Kiingereza siyo katika Kiswahili ambapo umbo lake ni "Yohane". Maneno mengine yameshaingia kabisa katika Kiswahili ingawa umbo lake haliridhishi kisarufi, kwa mfano "Moravian" (Moravia - ingekuwa Wamoravia/kimoravia). Katika mifano mingine waandishi wa kitheologia wanapenda kutumia maneno ya Kiswahili cha zamani kidogo. Lakini sioni faida kuwafundisha wanafunzi wetu maneno kama "Iskenderia" au "Uhabeshi" wakitumia tayari katika shule ya msingi "Alexandria" na "Ethiopia". Kwa bahati mbaya neno zuri "Dachi" limesahauliwa (linachanganywa na "kiholanzi" /kiing. "dutch") ambalo lingesaidia sana katika historia ya mwisho wa Dola la Roma (tofauti kati ya "Wadachi" wa leo na makabila ya "Wajerumani" wa zamani - kiing. "German"-"Germanic")

Historia ya D.A. Peterson mpaka sasa ni kazi bora inayopatikana kwa Kiswahili lakini ina kasoro zake, hasa amebaki sana katika mfumo wa mapokeo ya Ulaya akipita harakaharaka kwenye historia ya Ukristo katika Misri na Uhabeshi, bila kutaja Sudan. * Tena inaonyesha ya kwamba imeandikwa na Mwingereza (bila shaka kurasa hizo zitamwonyesha Mjerumani hata akijaribu kujificha)

3. kwa ajili ya wanafunzi waafrika na kwa ajili ya matumizi katika Tanzania - kasoro yake bila shaka kitabu kimeandikwa na mgeni kutoka Ujerumani.

(kitabu bora kwenye soko la Tanzania ni L. Malishi lakini ameandika kwa kiingereza, tena amechukua "Ukristo katika Afrika" tu kuwa kichwa chake. Vinginevyo ameandika katika msimamo wa kiekumene ingawa zaidi kwa ajili ya wasomaji wakatoliki lakini kwenye msingi wa elimu bora juu ya misioni ya kiprotestant katika Afrika. Anastahili sifa kwa kuwa hana matatizo ya ubaguzi wa kidhehebu. Kutokana na mkazo wake hajadili matengenezo na mafarakano ya Kanisa kule Ulaya katika karne za 15/16.

Kitabu hiki ambacho kinajaribu kuwasaidia wanafunzi wa madhehebu mbalimbali kujielewa katika historia yao kinajaribu kutoa muhtasari wa mazingira ya mafarakano ya kidhehebu.

4. kwa ajili ya matumizi ya Kiekumene (kimadhehebu) -

hapa ni jaribio ambalo halitaridhisha sana. Kasoro yake ilishindikana kumpata hapa mwenzangu mkatoliki aliyekuwa na nafasi kutunga kitabu chenyewe pamoja nami. Lakini kwa jumla nashukuru sana mawazo mengi niliyoyapata kutoka kwa walimu wenzangu masista na mapadre katika umoja wa walimu wa dini hapa Mbeya, hasa maneno makali ya Pd. Rudi juu ya muhtasari ya kwanza. Pia nilitegemea muundo wa "Christian Living Today" ambayo ni mfano bora wa ushirikiano wa kidhehebu kule Kenya/Uganda.

Azimio lingine nililofuata kutokana na msingi huo wa ekumene lilikuwa kuepukana na maneno kama "wazushi, heretiki" n.k. katika Historia ya Ukristo wa Kale Leo hii Wadonato, Wanestorio na Wamonofisiti wangeitwa "madhehebu" si "wazushi". Kwa bahati nzuri Kanisa la Katoliki limeacha kubandika majina ya aina hii tangu Vatikano II, na kati ya Wainjili desturi hiyo imeaga dunia bila kelele kubwa karne iliyopita (Katika Ungamo la Augsburg hawakusita kulani akina Donato na wengine). Lakini kwa ajabu majina haya (na labda mawazo yanayaoambatana nao) yamepata hifadhi zao katika Historia ya Kanisa la Kale (pamoja na Idara ya Historia ya Mafundisho ya Kikristo /History of Dogmatics). Natumaini ya kwamba inalingana zaidi na makumbusho kule Daressalaam tunapoonyeshwa mifupa na picha kuliko Ngorongoro ambako wanyama hutembea hai. Lakini bila shaka ina faida yake: anayependa kuchapa kiboko "wazushi" au kuwavinda anapata nafasi katika Historia ya Kale (afadhali kuliko leo hii).]

   1 (namna ya kuandika maneno)

1. Kwa ujumla kitabu kinajaribu kufuata kawaida ya Kamusi za Kiswahili. Wakati mwingine mazoea yanatofautiana kutumia neno la asili ya Kiarabu (kama mara nyingi katika Kiswahili cha urasimu) au maneno mapya ya asili ya Kiingereza. Kwa sababu mapokeo ya waandishi wa habari za kitheologia yanaelekea zaidi kwenye Kiswahili cha urasimu lakini wanafunzi siku hizi hawafahamu tena maneno haya azimio letu lilikuwa la mara kwa mara. (Kwa mfano: "Iskenderia" - "Aleksandria"; "Bahari ya Kati" - "Mediteranea"- kwa bahati mbaya hata vitabu mbalimbali vya shule vinachanganya Kiswahili na Kiingereza)

2. Juu ya maneno na majina yanayotumika hasa katika Historia ya Kanisa kitabu kinafuata mara nyingi ushauri wa "Msamiati wa Maneno ya Kitheologia"; pale ambako hautoi mifano tumejaribu kuunda maneno yanayolingana na utaratibu wa lugha ya Kiswahili, tukiepukana na kuchukua vivumishi vya sifa kutoka kwa Kiingereza. (Mfano: Wakopti badala ya Koptiki, Wadonato badala ya Wadonatist, Wahus badala ya Wahussite, kwa ujumla kuepukana na viambishi tamati vya kiingereza visivyolingana na lugha za asili -kwani hata Kiingereza hakitumii hapo maneno ya asili bali imepokea maneno haya kutoka kwa malugha mengine kama kigiriki na kilatini.)

Menginevyo tumejitahidi kufuata kawaida ya wenye mapokeo fulani; kwa mfano waandishi waprotestant huzoea kuandika "Chama cha Yesu" wakati wenyewe hujiita "Shirika". Vilevile hutafsiri Indulgences kuwa "msamaha" wakati kanisa katoliki hutumia "rehema".

3. Juu ya Majina ya Kibiblia kitabu kimejitahidi kuitikia ushauri wa Kamati ya Umoja wa Makanisa katika Mkoa wa Mbeya unaosema: "Tukitaja majina ya Kibiblia tufuate utaratibu wa Agano Jipya/ Kiswahili cha Kisasa." Hivyo wasomaji kutoka kwa makanisa mbalimbali wataona umbo lililo tofauti na uzoefu wao: Roma badala ya Rumi, Kristo badala ya Kristu, Yohane badala ya Yohana, Maria badala ya Mariamu, n.k. .


DIBAJI

Maandishi yafuatayo ni matokeo ya kazi ya siku nyingi kama Mchungaji wa Wanafunzi na Mwalimu wa Elimu ya Kikristo katika shule za sekondari Mbeya. Tumefuata muhtasari uliokubalika na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (T.E.C.) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (C.C.T.). Muhtasari wetu unaweka uzito fulani katika Historia ya Kanisa lakini wanafunzi wetu hawaandaliwi vizuri sana kwa upande wa somo la "History". Bila kitabu, mafundisho haya ni magumu sana tulihangaika mara kwa mara.

Kitabu hiki kisingetokea bila Kamati ya Walimu wa Dini (Elimu ya Kikristo) Mbeya. Kamati hii inaunganisha walimu kutoka makanisa ya CCT (Anglikana, Lutheri, Moraviani na Kanisa la Uinjilisti) pamoja na Kanisa la Katoliki (RC) wanaohudumia shule za sekondari katika eneo la Mbeya. Kamati hii inatekeleza nia ya TEC na CCT kuwa na utaratibu mmoja shuleni jinsi inavyoonekana katika muhtasari ya pamoja kwa ajili ya shule za sekondari. Kwa bahati mbaya utekelezaji wa nia hiyo si kawaida katika Tanzania. Inawezekana ya kwamba Mbeya ni eneo la pekee ambapo wanafunzi wa kikristo hawatengwi kidhehebu wakati wa somo la dini. Kwa sababu hii sina budi kutoa shukrani za pekee kwa viongozi waliowezesha ushirikiano huu ndio hasa Askofu Sanga wa Kanisa la Katoliki pamoja na Askofu Wawenza na Uongozi wa Kanisa la Moravian. Waliteua mara kwa mara masista, mapadre na wachungaji kwa ajili ya kazi hii inayoendelea kupanuka, na kuwaruhusu washirikiane.

Yafuatayo ni mawazo machache yaliyoongoza kazi ya utungaji. (Maelezo zaidi katika Nyongeza (1).

1. Kitabu kiwe kifupi - kwa matumizi katika shule za sekondari na kwenye ngazi ya vyuo vya Biblia / Makatekista na kwa Wakristo wetu wanaopenda kujielimisha. Shuleni kitasaidia wakati wa mhula wa pili Kidato cha Tatu na kwa marudio wakati wa Kidato cha Tano au Sita. Lugha yake inajaribu kuwa rahisi. 2. Kinatumia lugha ya Kiswahili kwani somo la dini hufundishwa kwa Kiswahili- . 3. Ni kwa ajili ya wanafunzi na kwa ajili ya matumizi katika Tanzania hivyo kinakazia sehemu za kiafrika za Historia ya Ukristo pamoja na kuweka msingi kwa ajili ya kuelewa asili ya madhehebu yetu yalivyo Tanzania. Habari nyingi za kihistoria zimepangwa kufuatana na uhusiano wao na Historia ya Afrika. Habari hizo zinaweza kurudia kwa upana zaidi katika vifungo zinazoeleza historia ya kanisa kwa ujumla. Mwalimu akitaka kufupisha anaweza kutumia hasa sura zinazoeleza habari za Ukristo katika Afrika kwa kuchagua vipande tu vya sura zingine. 4. ni kwa ajili ya matumizi ya Kiekumene (kimadhehebu) - kimejaribu kutunza mizani na kuheshimu mapokeo ya makanisa mbalimbali bila kuacha kabisa msingi wa historia ya kisayansi. Kwa sababu madhehebu yetu ya Tanzania yana asili yao nje ya Afrika ilikuwa lazima kueleza pia habari za matengenezo na mafarakano ya kanisa kule Ulaya.

Siwezi kuficha kasoro mbalimbali: Maandishi haya ni kazi ya mwandishi mmoja tu -tumaini langu mwanzoni lilikuwa kutunga kurasa hizo pamoja na wengine. Ingekuwa lazima kwangu kama Protestant kushirikiana na mkatoliki, na ingekuwa lazima kwangu kama mtu kutoka Ulaya kukamilisha kazi hiyo pamoja na Watanzania. Pia ingelikuwa vizuri zaidi kama muswada ungeandaliwa tangu mwanzo na wasemaji wa Kiswahili, hata hivyo ndugu mbalimbali walijitolea kusahihisha lugha. Tatizo lingine ni Kiswahili chetu cha kidhehebu katika msamiati wa kidini yaani tumezoea kutumia maneno mbalimbali kwa namna tofauti kati ya madhehebu yetu.

Sina budi kutoa shukrani mbalimbali. Mch. Jaeschke (Chuo cha Biblia Kidugala KKKT) alinipa wazo na moyo kutafakari kazi hii. Masista na mapadre wenzangu wakatoliki katika Umoja wa Walimu wa Dini wa Mbeya walinisaidia sana kuelewa mapokeo ya kanisa lao. Mch. Sichone, Ndiwela Sichone, Mch. Buyah na Mwal. Mwaisumu walinisaidia kwenye ngazi mbalimbali masahihisho ya Kiswahili. Makosa yaliyobaki ni makosa yangu, si ya kwao. Anayefahamu Kitabu cha "Christian Living Today" atatambua ya kwamba nilichota mawazo mengi mle.

Nashukuru sana Motheco Publishers (Idara ya maandiko ya Chuo cha Theologia cha Moravian Mbeya) waliopima na kukubali muswada na kuitoa kama kitabu. Kuwepo kwa picha kumewezekana kwa sababu ya msaada wa Herder Publishers (Freiburg/Ujerumani) walioturuhusu kutumia picha zao bila malipo. Ofisi ya Bildarchiv ya Wamisionari wa Afrika (Cologne/Ujerumani) ilisaidia pia picha mbalimbali.

Mbeya, Julai 1994

Ingo Koll

(Mchungaji wa Wanafunzi Kanisa la Moravian Mbeya 1987 - 1993) s:Category:Kiswahili