Ufalme wa Kikatiba
Ufalme wa Kikatiba ni muundo wa serikali ambako kaisari, sultani, mfalme, malkia au mtemi ni mkuu wa nchi chini ya katiba yake. Hii inamaanisha ya kwamba madaraka ya mfalme yana mipaka yao katika masharti za katiba na sheria za nchi. Pale ambako hakuna katiba ya kimaandishi inayoratibu mambo mengi kuna kawaida inayoweka mipaka kwa madaraka ya mfalme jinsi ilivyo Uingereza.
Madaraka ya mfalme katika muundo huu yanatofautiana sana.
Zamani wafalme walikuwa mara nyingi viongozi wenye madaraka yote wasiobanwa na bunge au sheria. Aina hii ya ufalme umebaki mahali pachache tu kwa mfano Saudia.
Mfalme kama kiongozi wa heshima
haririKatika nchi kama Uingereza au Uswidi shughuli zote za serikali zinaendeshwa kwa jina la mfalme lakini mamlaka yapo mkononi mwa serikali inayochaguliwa na bunge ambalo limetoke katika kura ya wananchi wote. Hapo mfalme hana athira kubwa katika siasa. Nafasi yake iko hasa pale ambako vikundi vikundi ndani ya bunge havikubaliani kuhusu serikali mpya na hakuna upande mwenye kura nyingi kabisa. Hapo ni mfalme anayemteua mwanasiasa atakayejaribu kukusanya kura za kutosha kwa ajili ya serikali mpya. Kama chama fulani kina wabunge wa kutosha kitamtaja kiongozi wake na mfalme hana cha kufanya ila tu kumpa huyu wito wa kuunda serikali.
Mfalme kama kiongozi mkuu chini ya katiba
haririKatika nchi kadhaa nafasi ya mfalme inafanana na maraisi watendaji. Kwa mfano katika nchi kama Moroko au Yordani mfalme anaamua kama bunge linavunjwa au la na kumteua kiongozi wa serikali kwa hiari yake.