Kutoka (Biblia)

kitambo kitabu Biblia, mchanganyiko 40 sura ya

Kitabu cha Kutoka ni kitabu cha pili katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania), na kwa hiyo pia katika Agano la Kale (sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo); kitabu cha kwanza ni Mwanzo.

"Kuvuka Bahari ya Shamu" kadiri ya Nicholas Poussin.
Mose akishika mbao za Amri Kumi (mchoro wa Rembrandt, 1659).

Kwa asili kimeandikwa kwa Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa שמות, Shemot, maana yake “majina”, kutokana na neno lake la kwanza.

Wengine wanakiita Kitabu cha Pili cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa ndiye mwandishi wa kitabu hicho. Kwa lugha ya Kiyunani, kinaitwa ἔξοδος, Exodos, maana yake “kuondoka kwa watu wengi pamoja”.

Kitabu cha Kutoka kina sura arobaini.

  • Sura 1 hadi 18 zinasimulia Waisraeli walivyokombolewa na Mungu kutoka utumwani kule Misri na walivyosafiri mpaka Mlima Sinai.
  • Sura 19 hadi 24 zinasimulia Mungu alivyofanya nao agano pamoja na kuwapa mwongozo wa maisha (Amri Kumi na maagizo mengine).
  • Sura 25 hadi 31 zinaeleza utengenezaji wa hema takatifu (au hema la mkutano) na Sanduku la Agano.
  • Sura 32 hadi 34 zinahadithia Waisraeli walivyoasi na kuabudu sanamu ya ndama wakati Mose alipokuwa amekwenda kuzungumza na Mungu mlimani Sinai.
  • Hatimaye, sura 35 hadi 40 zinaeleza maagizo mengine kuhusu hema takatifu.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Utangulizi

hariri

Kama ilivyokuwa kwa kitabu cha Mwanzo, hata kitabu cha Kutoka kilipewa jina jipya na watafsiri wa kwanza wa Biblia ya Kiebrania (Agano la Kale) katika lugha ya Kiyunani (tafsiri ya Septuaginta). Maana ya jina hilo ni 'kutoka nje' au 'kuhama', kwa kuwa kitabu kinaeleza habari za kutoka au kuhama Misri.

Habari za kitabu cha Mwanzo zilimalizika kwa familia ya Yakobo-Israeli) kuhamia nchi ya Misri. Kitabu cha Kutoka kinaanza habari zake muda wa miaka kama 400 hivi baada ya hayo (Mwa 15:13; Kut 12:41).

Wakati huo wazao wa Israeli walikuwa wameongezeka sana, hata walikuwa taifa la maana, ingawa bado waliishi Misri. Kitabu hiki kinaonyesha jinsi Mungu alivyowaokoa katika utumwa wa Misri, akawapeleka mpaka karibu na Mlima Sinai, na huko alithibitisha rasmi agano alilolifanya na Ibrahimu, ili Israeli liwe kweli taifa na mali ya Mungu, nalo liishi kwa ajili yake. Kisha Mungu, kwa njia ya Musa, aliwapa watu hao kanuni zile ambazo kwa njia yake waishi, pia aliwapa sheria za dini walizotakiwa kuzitimiza ili kufurahia na kufaidi baraka za agano.

Ufunuo wa tabia ya Mungu

hariri

Licha ya thamani yake ya kutoa masimulizi ya matukio ya historia ambayo maisha ya kidini na ya kijamii ya Israeli yalijengwa juu yake, kitabu cha Kutoka pia kina thamani katika kudhihirisha sehemu kubwa ya tabia ya Mungu wa Israeli. Zaidi ya yote, alidhihirishwa kuwa Mungu aokoaye. Waisraeli walitakiwa wamkumbuke daima kuwa ndiye aliyewaokoa na kuwatoa 'katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa' (Kut 6:3-8; 20:2).

Waisraeli walitakiwa watambue historia yao si kama kusanyiko la masimulizi ya matukio, bali kama ufunuo wa tabia ya Mungu. Yeye kwao alikuwa nani, aliwafanyia nini, naye aliwatazamia wafanye mambo gani?

Mungu alishughulika na kila sehemu ya maisha wa Waisraeli. Matendo yake ya kuokoa yalikuwa yenye ushindi, na hukumu zake ziliangamiza. Kuhifadhiwa kwa taifa na kukua kwake kulikuwa kazi yake (Kut 1:21; 14:21-22:31; 32:35).

Mungu wa Israeli pia alikuwa Mtakatifu, maana yake watu wake pia wawe watakatifu. Walitakiwa wawekwe wakfu kwa Mungu, wakifuata kwa uangalifu sana matakwa yake kuhusu maisha ya maadili yaliyopangwa wazi naye (Kut 19:5).

Hata hivyo, Mungu huyo aliyetofautiana kabisa na wanadamu wenye dhambi (Kut 19:12-13), pia alitaka kuishi kati ya watu (Kut 25:8; 33:14). Yule ambaye utakatifu na [[haki] yake vilidai adhabu na hukumu kwa wenye dhambi (Kut 32:33), alikuwa yuleyule ambaye kwa huruma na neema yake aliandaa njia kwa wenye dhambi ili waweze kumkaribia tena, wasamehewe dhambi zao na kurudishwa tena katika ushirika hai na Mungu Mtakatifu (Kut 29:10-14; 34:6-7).

Muhtasari

hariri

1:1-4:31 Maandalizi ya Musa

5:1-15:21 Kuokolewa kutoka Misri

15:22-18:27 Safari ya kwenda Sinai

19:1-24:18 Kutolewa kwa agano

25:1-31:18 Hema la kukutania na ukuhani

32:1-34:35 Kuvunjwa kwa agano na matengenezo yake

35:1-40:38 Kuandaliwa na kujengwa kwa hema la kukutania

Marejeo

hariri

Vitabu vya ufafanuzi

hariri
  • Childs, Brevard S (1979). The book of Exodus. Eerdmans.
  • Fretheim, Terence E (1991). Exodus. Westminster John Knox Press.
  • Johnstone, William D (2003). "Exodus". Katika James D. G. Dunn, John William Rogerson (mhr.). Eerdmans Bible Commentary. Eerdmans.
  • Meyers, Carol B (2005). Exodus. Cambridge University Press.
  • Stuart, Douglas K (2006). Exodus. B&H Publishing Group.

Vingine

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.