Wilaya

(Elekezwa kutoka Kaunti)

Wilaya ni mgawanyo wa kiutawala au eneo lililotengwa kwa ajili ya utawala. Mikoa ya Tanzania na Kenya imegawiwa kwa wilaya.

Asili ya neno ni Kiarabu "ولاية" (wilaayatun - Kituruki: vilayet). Katika Dola la Osmani "vilayet" ilikuwa ngazi ya kwanza ya mgawanyo wa kiutawala ikimaanisha jimbo au mkoa. Mkuu wake au gavana alikuwa na cheo cha "Wali". Neno hili la "wilaya" limepatikana katika nchi nyingi zilizoathiriwa na utamaduni wa Uislamu au lugha ya Kiarabu kama vile Uturuki, Algeria, Tunisia, Oman, Mauritania, Sudan, Malaysia, Indonesia, Afghanistan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.

Katika Kiarabu cha Kisasa "wilaayatun" inamaanisha pia dola ndani ya shirikisho - kwa mfano madola kama vile Texas ndani ya Marekani.

Katika matumizi ya Kiswahili huko Kenya na Tanzania "wilaya" imekuwa mgawanyo wa ngazi ya pili yaani ni kitengo chini ya ngazi ya kwanza ya mikoa. Vitengo vya wilaya ni tarafa. Na vitengo vya tarafa ni kata zinazoitwa shehia katika Zanzibar na chini yake vijiji au mitaa.

Algeria ni nchi nyingine ambako wilaya inamaanisha ngazi ya pili ya kiutawala.