Alpi
Alpi (kwa Kijerumani: Alpen; kwa Kifaransa: Alpes; kwa Kiitalia: Alpi; kwa Kislovenia: Alpe) ni safu ya milima kunjamano katika Ulaya inayotenganisha Ulaya ya Kati na Ulaya ya Kusini, hususan rasi ya Italia.
Jina
haririAsili ya jina "Alpi" ni neno la Kilatini "Alpes". Mwandishi wa Roma ya Kale Maurus Servius Honoratus aliandika mnamo mwaka 400 BK ya kwamba Wakelti waliita milima mirefu yote "Alpi". Kuna pia jina "Alp" au "Alpe" katika lahaja za Kijerumani cha Kusini zinazomaanisha machungani ya mlimani.
Lina uhusiano na jina "Albania" kwa nchi za mlimani, kama nchi Albania ya leo au Albania ya nyakati za kale katika Kaukazi.
Hata nchi ya mlimani Uskoti iliwahi kuitwa "Albania" zamani.[1]
Jiografia
haririAlpi ni safu ya milima yenye umbo la hilali yenye urefu wa kilomita 800 na upana wa takriban kilomita 200. Alpi zinaanza upande wa mashariki katika Austria na Slovenia, zikipita Italia ya kaskazini, Uswisi, Liechtenstein na Ujerumani hadi ufuko wa bahari ya Mediteranea nchini Ufaransa upande wa magharibi. Katika Austria na Uswisi Alpi zinafunika sehemu kubwa ya eneo la nchi.
Nchi zenye maeneo makubwa ya Alpi ni Uswisi, Ufaransa, Austria na Italia. Pande za kati na magharibi zinafikia juu kuliko pande za mashariki. Kimo cha wastani ni mita 2500 juu ya UB.
Mlima wa juu kwa urefu ni Mont Blanc (kwa Kifaransa "mlima mweupe") mpakani mwa Ufaransa na Italia wenye kimo cha mita 4,808 juu ya UB.
Vilele vya juu vina theluji na barafu za kudumu yaani mwaka mzima, isipokuwa ukubwa wa barafuto za Alpi hupungua haraka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Alpi ni safu yenye umri mdogo kijiolojia wa miaka milioni 30-35. Safu ilijikunja na kupaaa juu kwa sababu bamba la Afrika linagongana na bamba la Ulaya, hivyo Alpi zaendelea kujikunja na kukua milimita 1-2 kila mwaka.
Safu hii inatenganisha tabianchi ya Mediteranea upande wa kusini na tabianchi ya kibara upande wa kaskazini.
Tazama pia
haririTanbihi
haririMakala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Alpi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |